KUNYAKULIWA KWA KANISA

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

Somo:  Kunyakuliwa kwa kanisa

Mpendwa msomaji, ninatanguliza shukrani zangu za dhati kwako, kwa jinsi ulivyoamua kuisoma “note” hii.  Nasema tena, asante sana.  Sasa basi ninakusihi uisome “note” hii hadi mwisho, ili uchote baraka zote za Mungu zilizokusudiwa kwako.

Somo hili, tunaligawa katika vipengele sita kama ifuatavyo:-

(i).  Dalili ya mwisho wa dunia.

(ii). Maana ya kanisa

(iii) Kunyakuliwa kwa kanisa.

(iv) Mifano ya kibiblia iliyokuwa  kivuli cha kunyakuliwa kwa kanisa.

(v)  Jinsi kunyakuliwa kwa kanisa kutakavyokuwa.

(vi) Sifa za wale watakaonyakuliwa.

 ( I ). DALILI ZA MWISHO WA DUNIA.

Kama wanafunzi wa biblia tutaweza kuona dalili za kunyakuliwa kwa kanisa zikiwa zimetajwa katika biblia zetu. Maandiko yafuatayo ni mfano wa maandiko hayo. ( MATHAYO 24:3-14; 1TIMOTHEO 4:1-5; 2TIMOTHEO 3:1-5; UFUNUO 22:6-7, 10-12 ).

Katika (  MATHAYO 24:3-14 )tunaona mengi yaliyotajwa  yamekwisha kutukia. Wameshatokea watu wengi wakijiita kuwa wao ni Makristo  ( Yesu ). Makristo wengi sana, mamia kwa mamia wamekwisha kutokea duniani tangu haya kutajwa.. Wamekuja kwa sura mbalimbali kwa kuwa walikuwa makristo wa uongo na imesha dhihirika kuwa walikuwa wa uongo. Watu wengi walijitokeza hata katika nchi zinazotuzunguka kwa mfano Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kenya na hata katika nchi nyingine nyingi za dunia. Pia katika nchi yetu Tanzania, kuna mtu aliyejitokeza katika wilaya ya Sumbawanga akijiita Kristo. Wamekuwepo makristo wa uongo wengi ili kutimiza hilo andiko. Vita vya kila namna vimeweza kutokea duniani. Vita ya kwanza ya dunia, vita ya pili ya dunia, taifa  kupigana na taifa na ufalme kupigana na ufalme. Taifa kupigana na taifa inazungumzia vita ya kikabila. Vita vya wenyewe kwa wenyewe ndani ya nchi moja (MWANZO 25:21-24). Yakobo na Esau watoto wa tumbo moja, mama mmoja wanaitwa mataifa mawili. Ufalme kupigana na ufalme hapa ndipo vinazungumziwa vita vya mataifa, nchi moja ikipigana na nyingine. Katika bara letu la Afrika na duniani kote tumeshuhudia vita nyingi za kikabila na vita za mataifa yakipigana. Hii ni dalili ya mwisho wa dunia. Dalili nyingine ni njaa ya kutisha ambayo imekuwepo duniani katika baadhi ya nchi mfano Ethiopia na Somalia. Imekuwepo njaa ya kutisha katika baadhi ya nchi kiasi kwamba watu wakiuona hata mjusi wanatamani kuurukia iliwaweze kuula lakini kwasababu ya njaa kali wanakosa hata nguvu ya kuurukia mjusi. Dalili nyingine ni ya matetemeko mahali mahali. Tumeshuhudia matetemeko makubwa katika baadhi ya nchi ambayo yalisababisha maafa makubwa sana. Siku za mwishoinatajwa kuwa watoto watakuwa wakaidi, upendo wa wengi utapoa, watatokea mafundisho ya kuwazuia watu kula baadhi ya vyakula na wenguine kuwakataza watu kuoa (1TIMOTHEO 4:1-5; 2TIMOTHEO 3:1-5).

Tuchukue nafasi ya kujifunza dalili za mwishomwisho kabisa kabla ya kunyakuliwa kwa kanisa:-

( i ). Magonjwa ya kuambukiza yasiyokuwa na dawa wala tiba.

Watu waliotafsiri biblia zetu za Kiswahili waliruka kitu cha muhimu ambacho hakitajwi katika biblia zetu za Kiswahili. Katika MATHAYO 24:7 kuna kitu hakikutajwa katika biblia za Kiswahili lakini kimetajwa katika biblia ya asili ya kiyunani iliyotumika kuleta biblia kwetu. Tunaweza kuona katika biblia ya kiingereza ya tafsiri ya King James Vision likitajwa hilo lililoachwa katika biblia za Kiswahili. Kuna neno linatajwa “pestilences” likiwa na maana ya magonjwa ya kuambukiza yenye uwezo wa kuua kwa haraka, yasiyoweza kuwa na tiba au dawa. Magonjwa haya yana lengo la kuwafanya watu waliokuwa mbali na Mungu kumtafuta Mungu zaidi kuliko mwanzo. Ili watu waache kutumaini akili tu na maarifa ya kisayansi ambayo mengi yamewapotosha  na kumsahau Mungu wao. Baada ya kukwama kila mahali, pesa wanazo lakini wanakufa kwa magonjwa , watakumbuka maneno ya Yesu aliyesema “niangalieni mimi mkaokolewe”. Kama vile wana wa Israeli  Jangwani  walipokuwa wanatewa na nyoka za moto na kuuawa na ndipo walipolazimika  kumuangalia nyoka wa shaba aliyekuwa ametundikwa juu ya mti. Nyoka wa shaba alikuwa  amesimama badala ya Yesu Kristo ambaye baadaye  alitundikwa  msalabani. Magonjwa haya ya kuambukiza yasiyokuwa na dawa yanayotajwa kutokea siku za mwisho ni pamoja na ukimwi.. Kila dawa inayojitokeza  inaonekana si dawa, si chochote si lolote na watu watazitumia lakini bado tu wataendelea kufa.

( ii ). Habari njema ya ufalme kuhubiriwa  kwa mataifa yote.

Katika  ( MATHAYO 24:14 ) tunaona kuwa habari za ufalme zitahubiriwa ulimwenguni mwote kuwa ushuhuda kwa mataifa yote. Mungu anataka injili ifike kila mahali, pande zote za dunia na kila mtu asikie tu ili siku ile ya hukumu asiwepo mtu wa kujitetea kuwa hakuisikia injili. Leo hii tunaona injli ikihubiriwa kona zote za dunia kwa teknolojia tulionayo sasa. Injili inahubiriwa kupitia radio, luninga (television), internet na njia nyingine nyingi. Injili kwa njia hizo haina mipaka, inafika kila mahali duniani. Tunapoyaona hayo tunapaswa kutambua kuwa tupo ukingoni kabisa mwa siku za mwisho. Mungu hakutuacha bila kutupa dalili au alama za siku za mwisho (MATHAYO 16:3). Kama vile tunapoona mawingu tunatambua  kuwa  ni dalili ya mvua  na ndipo tunapoanza kuanua nguo ili kuiwahi mvua isizinyeshee. Hivyo hatuna budi kuhakikisha tunakaa katika utakatifu tukijua kuwa saa tusiyodhani  Bwana yuaja. Hakuna ajuaye siku wala saa Atakayokuja Bwana Yesu.

( iii ) Wachafu watazidi kuwa wachafu na watakatifu watazidi kutakaswa

Katika  (UFUNUO 22;11 ) tunaona kuwa wachafu watazidi kuwa wachafu na kuongezeka kwa namna ya kutisha. Maasi yataongezeka hivyo kufanya watu wengi kuwa wachafu (MATHAYO 24:12). Uchafu unaozungumziwa hapa ni urawiti na unajisi. Urawiti na unajisi kwa namna ile ya Sodoma na Gomora vitaongezeka kwa namna ya kutisha ili kuonesha kuwa ni siku za mwisho.Siku hizi tunasikia ripoti za kutisha za urawiti . Watu wanarawiti vitoto vidogo, ubakaji wa watoto wadogo, kufanya uchafu na wazazi wao, wengine wakifanya unajisi na maiti. Wengine wakifanya unajisi na  wanyama kama vile kondoo, ng’ombe,  mbuzi kwa namna ya kutisha kuliko wakati wowote.

( II ). MAANA YA KANISA.

Kanisa maana yake ni nini?

Neno kanisa linatokana na neno la asili katika lugha ya kiyunani linaloitwa “ECLESIA” lenye maana  “walioitwa na kutoka miongoni mwao”. Kanisa linafananishwa na wana wa Israeli walioitwa na kutoka katika utumwa wa Farao kule Misri na kuanza kwenda Kanaan kupitia jangwani.. Walipokuwa jangwani waliitwa kanisa la jangwani (MATENDO 7:38). Kwa msingi huu kanisa leo ni wale wote walioitwa na kutoka katika utumwa wa dhambi.Kama vile wana wa Israeli walivyokuwa watumwa wa Farao vivyo hivyo na watenda dhambi ni watumwa wa Shetani. Watu wote wote waliookoka kwa kutoka katika utumwa wa Shetani koye duniani bila kujali dhehebu lake la dini , wote kwa pamoja wanaitwa kanisa. Watu  wote  ambao majina yao yamefutwa katika kitabu cha hukumu yakaandikwa katika kitabu cha uzima mbinguni  hao ndiyo kanisa.. Hilo kanisa ndilo linatajwa kwamba litanyakuliwa  kama tukio la kwanza katika matukio ya mwisho  ambayo hayako mbali sasa.

( III ).KUNYAKULIWA KWA KANISA

Hatuna budi kufahamu kwanza maana ya kunyakuliwa.                                                   (1 WATHESALONIKE 4:17; 1 WAKORINTHO 4:15-17 ).

Kunyakuliwa ni tendo la kuchukuliwa kwa kitu ghafla kwa kasi kubwa na kuondolewa pale kilipokuwa  katika hali ya kuwaacha watu wakiwa wamepigwa butwaa kwa jinsi wasivyoweza kukipata kitu hicho tena.Tunaweza kulifananisha tendo hilo na jinsi mwewe anavyovinyakua vifaranga vya kuku na kumwacha  kuku amepigwa butwaa juu ya jinsi ya kuwapata watoto wake (vifaranga) tena. Kwa namna hi ndivyo kutatokea kunyakuliwa kwa kanisa. Watu wote waliookolewa muda ambao siyo mrefu ujaowatanyakuliwa, watatolewa  kwenye uso wa dunia hii.Wale ambao watakuwa wamebaki duniani watakuwa ni wenye dhambi tu. Baada ya kanisa kunyakuliwa kutoka duniani kwa wale ambao watabaki duniani watabaki katika wakati au kipindi kibaya sana cha dhiki kubwa ya miaka saba ambayo haijawahi kutokea tangu kuumbwa kwa dunia na wala haitatokea tena (MATHAYO 24:21). Ukitaka kujua mengi kuhusiana na dhiki kubwa huna budi kufatilia somo la dhiki kubwa.    Jambo la muhimu kufahamu ni kwamba, kanisa litakuwa limenyakuliwa kabla ya dhiki hiyo kubwa  kinyume na mafundisho ya  walimu wa uongo wanaosema kanisa litakuwepo wakati huo wa dhiki kubwa. Ili kupata ufafanuzi zaidi hilo linatuleta kwenye kipengele cha nne sasa.

( IV ). MIFANO YA KIBIBLIA ILIYOKUWA  KIVULI CHA KUNYAKULIWA KWA KANISA.

Mungu katika hekima yake hakutuacha bila kutupa mifano inayoonesha jinsi kunyakuliwa kwa kanisa kutakavyokuwa ili tusiweze kudanganywa na walimu wa uongo. Katika mifano hii tunajifunza na kufahamu kuwa watu waliookolewa au kanisa wataondolewa kabla ya hasira ya Mungu kushuka juu ya uso wa dunia.Watu wake Mungu wataondolewa kwanza. Na mifano hii inathibitisha  waziwazi kwamba unyakuo wa kanisa utatokea  mapema kabla ya kuanza kwa dhiki hiyo kubwa.

( i ). Nuhu na wenziwe saba

( MWANZO 7:11-18 ). Tunaona kuwa Nuhu na wenziwe saba walitolewa  kwanza na kuwekwa safinani kabla ya kuanza kwa gharika juu ya wenye dhambi.Nuhu na wenziwe saba wanatajwa kuwa ni wenye haki. Hao ndio waliotolewa kwanza kabla ya gharika kuja ambayo dhiki kubwa inafananishwa na gharika itakayokuja. Kwa hiyo, kanisa ambalo ni Nuhu na wenziwe saba watakuwa wamekwisha tolewa kwanza kabla ya gharika au dhiki hiyo kubwa.

( ii ). Ruthu alishikwa mkono na kutolewa nje ya mji wa Sodoma. na Gomora  kabla ya Bwana kuleta uharibifu  juu ya nchi..

(MWANZO 19:12-16, 23-24) Tunaona Ruthu na wenziwe watatu  walitolewa kwanza  kabla ya Mungu  kushusha moto na kiberiti juu ya  Sodoma na Gomora. Dhiki kubwa ambayo itakuwa imejaa mateso makubwa kwa wenye dhambi  walioukataa wokovu, haitalihusu kanisa (watu waliokolewa).Baada ya kulizwa parapanda kanisa litanyakuliwa na kuruhusu kuanza kwa dhiki kubwa katika uso wa dunia kwa wenye dhambi wote walioachwa.

( iii ). Kabla ya Bwana kuwaangamiza wana wa Kola alihitaji kuwaona Musa, Haruni na wengine  wasio waasi  wametengwa mbali nao.

(HESABU 16:20-21, 23-27, 31-35) Ukisoma hapo uaona jinsi watu wasio waasi  walitengwa na waasi na ndipo waasi walipoadhibiwa. Dhiki kubwa  ni adhabu ya mateso ambayo hailihusu kanisa.. Kama vile Henoko na Eliya walivyotwaliwa na kwenda mbinguni bila kufa ndivyo watakatifu  waliohai  watakavyonyakuliwa  bila kufa (MWANZO 5:24 ) Henoko na (2WAFALME 2:1-12) Eliya. Sisi tuliookoka tutakaosalia bila kufa tutaweza kunyakuliwa bila kufa kama Henoko na Eliya na kuwaacha wenye dhambi wakiteseka  katika dhiki hiyo kubwa itakayokuja

( V ). JINSI KUNYAKULIWA KWA KANISA KUTAKAVYOKUWA.

Wakati usio mrefu ujao tukio la kunyakuliwa kwa kanisa linaweza kutokea . Nani ajuaye? Huenda ni leo au kesho. Yesu alisema “siku au saa  ile hakuna mtu aijuaye ila Baba peke yake” (MATHAYO 24:32-33). Hakuna aijuaye siku wala saa lakini yeye ajaye anakuja  wala hatakawia (WAEBRANIA 10:37). Katika kipindi hiki kifupi, yatatokea mambo kufumba na kufumbua. Sehemu nyingine za dunia zinatofautiana majira kijeografia. Kuna sehemu zinakuwa katika majira ya mchana wakati huohuo sehemu zingine zinakuwa wakati wa usiku.  Unyakuo wa kanisa ukitokea usiku itatisha sana na vilevile ukitokea mchana itatisha pia. Kitakachotokea ni kwamba, wale walioopo mbinguni watakatifu watarudi tena  katika miili yao ya asili na ghafla watatokea katika uso wa dunia.. Kufumba na kufumbua watakatifu waliokuwepo duniani ambao hawakufa  yaani kanisa nao watabadilishwa miili yao kwa kuvikwa miili isiyoharibika na kuanza kupaishwa kwenda juu. Kitakachotokea ni kwamba malaika mkuu atapiga parapanda na Yesu atakuja mawinguni na watu waliokolewa yaani kanisa watadakwa kama ni kwa sumaku na kumlaki Yesu mawinguni. Tumeona kuwa Yesu hatakuja duniani mara ya pili wakati wa unyakuo bali atakuja mara ya pili duniani baada ya miaka saba kuanzia hapo alipowachukua watu wake. Wakati wa kunyakuliwa kwa kanisa Yesu anakuwa mawinguni lakini wakati wa kuja mara ya pili duniani kutawala, atatua katika uso wa dunia katika mlima mzeituni alipopaa akiwa na wanafunzi wake.. Kwa hiyo watakatifu waliokufa watarudi katika miili yao ya zamani na sisi tutabadilishwa miili yetu na pamoja nao tutamlaki Bwana mawinguni. (MATHAYO  24:40-41).Watu wawili watakuwa wakilima pamoja shambani lakini parapanda itakapolia mmoja atatwaliwa n mmoja kuachwa. Wengine watakuwa wamelel katika kitanda kimoja na baada ya parapanda kulia mmoja atatwaliwa na mmoja ataachwa. Wengine watakuwa wakisaga pamoja , yule aliyeokoka atatwaliwa na kumuacha mwenye dhambi.  Kama ni usiku itatisha sana maana watu wote waliookoka watatwaliwa na ndugu zao, wazazi, wake, watoto watahangaika kuwatafuta watu waliopotea. Vyombo vya habari vikitumiwa na watu wenye dhambi walioachwa navyo vitatoa habari za tukio kubwa la kupotelewa na watu kila upande wa dunia. Polisi nao ambao walikutwa bado hawajaokoka watapokea taarifa za kupotea kwa watu na zitawachanganya sana kutokana na wingi wa watu walioopotea. Baada ya muda itathibitika kuwa waliopotea ni watu waliookoka (walokole). Parapanda itakapolia mtu aliyeokolewa atanyakuliwa palepale alipo. Kama utakuwa ndani ya gari, treni, ndege, meli na vyombo vingine vingi, utanyakuliwa humo humo.  (1 WAKORITHO 15:52). Huuni wakati wa kuutunza utakatifu kuliko mwanzo. Huu ni wakati wa kuilinda imani kwa kila hali. Mmeo au wazazi wakikupiga kwasababu ya wokovu wewe songa mbele katika jina la Yesu.

( VI ).  SIFA ZA WATAKAONYAKULIWA.

1.  Ni wale tu walioziungama dhambi zao na kuziacha. Afichaye dhambi zake hatafanikiwa bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema (MITHALI 28:13).

2.. Wale tu waliomfanya Yesu Kristo Bwana na mtawala  wa maisha yao yote na kutii kila neno  analotuagiza katika maandiko bila kuchagua la  la kufanya.. Huu ni  (ZABURI 119:6,9 ). Huu sio wakati  wa kufuata mapokeo ya wanadamu . Kama biblia inasema tubatizwe katika maji tele wewe usimletee ubishi Mungu. Tusichezee nafasi hii tuliyopewa maana hakuna nafasi tena kwa mataifa kuokoka. Huu wakati tulionao unaitwa wakati wa majira ya mataifa. Lolote tunaloagizwa kulitenda tulifanya bila mjadala mwisho unakuja.

Tunasoma haya katika LUKA 1:77, “Uwajulishe watu wake wokovu, katika kusamehewa dhambi zao”.   Hii ina maana kwamba ukiisha kutubu dhambi zako leo utasamehewa kwa hakika, na hivyo kupata wokovu mara moja.  Je, kweli utasamehewa?  Jibu ni Ndiyo!  Yesu mwenyewe anasema katika YOHANA 6:37, “……….Wala yeyote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe”.  Hivyo kwa dhahiri, leo hii, dakika hii hii, utasamehewa na kupata wokovu.  Je, uko tayari kuokoka sasa na kuhesabiwa miongoni mwa wale watakaoingia mbinguni na kuishi na Mungu milele, hata wakiiaga dunia sasa hivi?  Ukiwa tayari kuifuatisha sala ifuatayo ya toba, mara tu baada ya sala hii, nitakuombea na kwa ghafla utawezeshwa kushinda dhambi.  Je, uko tayari kuifuatisha sala hii sasa?  Najua uko tayari.  Basi sema maneno haya,  “Mungu Baba, natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Naomba unisamehe na kuniosha dhambi zangu kwa damu ya Yesu iliyomwagika msalabani.  Niwezeshe kushinda dhambi kuanzia sasa.  Liandike sasa jina langu katika kitabu cha uzima mbinguni.  Asante kwa kuniokoa, katika Jina la Yesu, Amen”.  Sasa ninaomba kwa ajili yako, “Mungu Baba msamehe kiumbe wako huyu dhambi zake zote, na mpe uwezo wa kushinda dhambi kuanzia sasa na kumuokoa. Mbariki kwa baraka zote katika Jina la Yesu, Amen”.  Tayari umeokoka.  Ili uzidi kuukulia wokovu, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI!!!

            Masomo ya matukio ya mwisho wa Dunia. Unaweza kuingia kwenye link ya kila somo.
1. KUNYAKULIWA KWA KANISA
https://davidcarol719.wordpress.com/2013/01/02/kunyakuliwa-kwa-kanisa/
2. DHIKI KUBWA
https://davidcarol719.wordpress.com/dhiki-kubwa/
3. TAJI KWA WATAKATIFU NA HARUSI YA MWANAKONDOO
https://davidcarol719.wordpress.com/2013/02/10/taji-kwa-watakatifu-na-harusi– ya-mwanakondoo/
4. KUJA KWA YESU KRISTO MARA YA PILI DUNIANI NA VITA VYA HAR-MAGEDONI
https://davidcarol719.wordpress.com/2013/02/10/kuja-kwa-yesu-kristo-mara-ya-pili-duniani-na-vita-ya-har-magedoni/
5. MIAKA 1,000 YA UTAWALA WA YESU KRISTO DUNIANI NA VITA VYA GOGU NA MAGOGU
https://davidcarol719.wordpress.com/miaka-1000-ya-utawala-wa-yesu-kristo-duniani-na-vita-vya-gogu-na-magogu/
6. UFUFU WA WAFU
https://davidcarol719.wordpress.com/187-2/
7. JEHANUM YA MOTO
https://davidcarol719.wordpress.com/jehanum-ya-moto/
8. KITI CHA ENZI KIKUBWA CHEUPE CHA HUKUMU
https://davidcarol719.wordpress.com/231-2/
9. MBINGU MPYA NA NCHI MPYA
https://davidcarol719.wordpress.com/mbingu-mpya-na-nchi-mpya/

                                                          . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .         

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “note” hii, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.

                                                         UBARIKIWE NA BWANA YESU

Advertisements
By neno la uzima

2 comments on “KUNYAKULIWA KWA KANISA

  1. Rutu na Nuhu hawakunyakuliwa, kwa hiyo hawawezi kuwa kivuli, bali walikuwa ni mfano wa mtu mwenye haki, ambaye ni mfano sawa na kanisa lililoukataa ubatizo wa kwa jina la Bwana Yesu Kristo ili liondolewe dhambi zake, kwa hiyo halikujazwa Roho Mt, limeishia kwenye vipawa vyake tu, ambavyo lilijiridhisha kuwa ndiye Roho Mt; basi hilo kanisa litalazimika kupita katika Dhiki Kuu likiwa limeukosa Unyakuo, kama wale wanawali watano ambao taa zao hazikuwa na mafuta! walio kivuli cha Unyakuo ni Henoko na Eliya, na watakatifu wooote wa Agano la Kale alioondoka nao Kristo!!!!
    Ubarikiwe mtumishi!

    • @ Lwembe
      Kanisa la leo ni wenye haki wa Mungu kama ilivyokuwa kwa Nuhu na wenzie saba pia Ruthu na wenzie 2 Mungu aliwaepusha na hukumu yake. Wakati wa Nuhu aliwaingiza safinani kwanza kabla ya gharika kushuka na wakati wa Ruthu aliwashika mkono kupitia Malaika na kuwatoa nje ya miji ile aliyoiteketeza. Mapigo ambayo Mungu atashusha juu ya wanadamu waliokataa wokovu hayatalikuta kanisa ( UFUNUO 16:1-). Ni muhimu kufahamu kuwa Mpinga Kristo hawezi kufunuliwa yeye na wakati wake ( Dhiki Kubwa 0 ni mpaka yeye azuaye ( kanisa ) aondolewe kwa kunyakuliwa ( 2 WATHESALONIKE 2:7-12 ). Kuja kwa Yesu mara ya pili duniani ni tofauti na tukio la kunyakuliwa kwa kanisa. Wakati wa kunyakuliwa kwa kanisa, watakatifu waliokufa watafufuliwa kwanza baada ya parapanda kulia na wataungana na watakatifu waliokuwepo duniani ambao nao watabadilishwa miili yao na kwa pamoja watamlaki Bwana Yesu mawinguni. Lakini tukio la kuja kwake ni miaka saba baada ya kunyakuliwa kwa kanisa na muda huo tunaujua kuwa utakuwa baada ya miaka saba ya Dhiki. Kuja kwa Yesu mawinguni kwa ajili ya unyakuo saa wala muda hakuna aijuaye ila Baba peke yake. Yesu atakuja mara ya pili Duniani akiwa na Malaika wake na Watakatifu wake yaani kanisa na wote watatua katika mlima Mzeituni alipoondokea wakati wa kurudi mbinguni baada ya kufufuka. Mlima utapasuka mara pande mbili na atakuwa na utiisho mkuu kama Mfalme wa Wafalme na Bwana wa mabwana. Kila goti litapigwa na kila ulimi utakiri ya kwamba Yesu ni Bwana. Watakaookolewa kutoka katika dhiki kubwa ni Waisraeli pekee kama maandiko yanavyosema ( WARUMI 11:25-32 ). Wakati huu tulionao unaitwa wakati wa majira ya mataifa ( wakati wa neema ya wokovu kwa mataifa ) Parapanda ikilia wakati huo utakuwa umeisha na neema itawarudia Waisraeli ambao tulipata Neema kwa Kuasikwao. Kumbuka alikuja kwa waliowake lakini waliowake hawakumpokea, yaani Waisraeli. Kama nilivyoeleza kuhusiana na Agano la Mungu na Waisreli katika somo la DHIKI KUBWA , kwa hiyo Mungu atalitimiza agano lake la kuwaokoa waisraeli siku ya huku yake kwa wanadamu. Ndiyo maana Yesu anasema,”ndipo waliopo Uyahudi na wakimbilie mlimani”. Wanatajwa Wayahudi tu na siyo wWatanzania wala Mataifa yoyote. Wakikimbia na kuwa mbali na mpinga Kristo na kuepuka kumsujudia ( namba 666 ) ndipo Yesu ataagiza Malaika kuwakusanya atakapokuja mara ya pili duniani. Nakuomba usome somo la Dhiki Kubwa ili kuongeza Maarifa.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s