MALIPIZO YA NDOA

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SOMO:    MALIPIZO YA NDOA

Baada ya kuokoka, ni muhimu kuangalia kwa makini kama mume  wetu au mke wetu tuliye naye niwa kwetu kumbe siyo sahihi ( YOHANA 4:18 ).Hili linaweza kutughalimu kwenda Jehanamu ya moto pamoja na pambio zetu, kusali kwetu na kushuhudia kwetu ( LIKA 16:18; 1WAKORINTHO 6:9 ). Je tufahamu namna gain kuwa huyu ni mume au mke wetu na baada ya kufahamu tufanyeje? Ni kwa sababu hii, leo tunajifunza somo, “ Malipizo ya ndoa “, na tutaligawa somo hili katika vipengele sita:-

( 1 ). NINI MAANA YA MALIPIZO?

( 2 ). NINI MAANA YA NDOA?

( 3 ). NDOA  BAADA YA MTU KUOKOKA.

( 4 ). NDOA NI YA WATU WANGAPI?

( 5 ). TALAKA KATIKA UKRISTO

( 6 ). KUHESABU GHARAMA

( 1 ).  NINI MAANA YA MALIPIZO?

Neno “Malipizo” au kiingereza  “ Restitution ‘ tunaliona katika KUTOKA 22:2-3. Malipizo ni kufanya masahihisho ya kosa au kuzaa matunda yapasayo toba. Inatupasa baada ya kuokolewa, kufanya masahihisho ya makosa tuliyowafanyia watu, kurudisha kwa wenyewe vitu vilivyoibiwa, kulipa madeni, kulipa pale tulipodhurumu, kukiri makosa na kuomba msamaha kwa watu tuliowasingizia, kuwatukana, kuwasengenya, kuwaambia uongo n.k, ili asije akatulaumu kwa habari ya wokovu tulioupokea. Tukitangulia kufikiri yaliyo mema, si mbele za Bwana tu, hata mbele za wanadamu ( 1 SAMWELI 12:1-5 ; 2 SAMWELI 12:1-7; EZEKIELI 33:14-16; MATHAYO 3:8; 5:23-24; LUKA 17:3-4; 19:8-9; MATENDO 23:1-5; 24:16; 2 WAKORINTHO 8:20-21; YAKOBO 4:17; 5:1-4; FILIMONI 1:18-19 ). Kwa misingi hiyohiyo, malipizo ya ndoa ni kumrudisha au kumuacha mume au mke ambaye siyo wa kwetu kindoa mbele za Mungu ( MWANZO 20:1-7, 14-18; EZRA 10:2, 10-12 ).

( 2 ). NINI MAANA YA NDOA?

Kwa kukosa ufahamu, wako watu wanadhani ndoa harali ni pale mwanaume anapovaa suti na mwanamke kuvaa shera  na Padre au Mchungaji  akawafungisha ndoa hiyo. Wengine wamedhani kwamba ndoa  zinazofungwa kwa Kamishna wa Wilaya au Bomani siyo ndoa harali. Wengine wamedhani kwamba ili iitwe ndoa, ni lazima kiwepo cheti cha ndoa. Wengine wamedhani kwamba ndoa zinazofungwa na Mashehe wa Kiislamu siyo ndoa. Wengine wamedhani kuwa ndoa zinazofungwa na Wahindu, Wabudha, Mashahidi wa Yehova n.k, siyo ndoa harali. Wengine wanadhani ndoa harali ni zile zinazofungwa  Roman Catholic,  Lutheran Church, Anglikana, Assemblies of God, Pentecoste au A.I.C  n.k. Wengine wanadhani ndoa za kimila siyo ndoa. Tushike lipi basi? Inatubidi  tuangalie Biblia! Kwa watu ambao hawajaokoka, yafuatayo yakitimia, hiyo ni ndoa tayari mbele za Mungu:-

  1. Mume na mke wawe wote hawajawahi kuoa au kuolewa, au mmoja wapo au wote wamefiwa na mke au mume aliye harali ( 1 WAKORINTHO 7:8-9, 38-39; WARUMI 7:2-3 ).
  2. Ruhusa ya mwanamke kwa kuwa radhi kuolewa na mume huyo                    ( MWANZO 24:57-58 ).
  3. Mume lazima apate ruhusa ya wazazi wa mwanamke katika vikao vya majadiliano ya mahali. Ikiwa wazazi wa mwanamke wataruhusu waishi pamoja na mahali ifuate baadaye au vinginevyo, la msingi ni ruhusa ya mzazi ( MWANZO 34:8, 11-12; 1 WAKORINTHO 7:36 ).
  4. Mume na mwanamke baada ya ruhusa ya wazazi wa mwanamke, wakiwaacha wazazi na kuambatana pamoja na kuishi pamoja na kutambulika hivyo katika jamii, basi hao wamekuwa si wawili tena, bali mmoja na hawawezi kutenganishwa, wameunganishwa na Mungu               ( MATAHYO  19:5-6 ). Sala zozote au Baraka wanazofanyiwa baada ya hapo na watu ambao hawajaokoka, wawe na majina ya Mapadri, Wachungaji, Maaskofu, Mashehe, Wazee wa kimira, Msajiri wa ndoa wa Bomani n.k.haziongezi wala kupunguza chochote biblia inasema wazi kwamba sala yoyote ya mtu ambaye hajaokoka ni chukizo mbele za Mungu wala haisikiwi.sala ya jinsi hii haiongezi chochote mbele za Mungu (MITHALI 15:19; 28:9.YOHANA 9:31) Mungu haihesabu kuwa ni ndoa kwa sababu ya cheti cha ndoa au kufungwa kwa ndoa hiyo na” kubarikiwa ”na mtu ambaye sala yake ni chukizo Mungu anahesabu kuwa ni ndoa baada ya vipengele hivyo vinne tu kutimia.

( 3 ). NDOA BAADA YA MTU KUOKOKA

Mtu akitaka kuoa au kuolewa baada ya kuokolewa, anapaswa kutimiza kwanza vipengele hivyo vine lakini kuna jambo la ziada la kufanyika kama mwana wa nuru kabla ya kuambatana na kuishi na mwanamke kama mke  na mume. Mungu aliwabariki Adamu na Hawa kabla hawajaanza kuishi pamoja                        ( MWANZO 1:27-28 ). Hatimaye Mungu aliwachagua watumishi wake, Haruni na wanawe  na kuwaagiza wabariki watu kwa niaba yake na kwamba yeyote atakayembariki atakuwa ameberikiwa ( HESABU 6:22-27 ). Leo hii watumishi wa Mungu kwa mfano wa Haruni na wanawe, ni Wachungaji na watumishi wengi waliookoka. Hivyo basi kama ilivyokuwa kwa Adamu na Hawa walipokuwa na mfano wa sura ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli             ( WAEFESO 4:24 ),  mtu mpya yaani aliyezaliwa mara ya pili au kuokoka, anatakiwa kwanza apate baraka za Mungu kupitia kwa Mchungaji kabla ya kuishi na mwenzi wake. Watu waliokwisha kuoana katika giza kabla ya kuokoka, hawana haja tena ya kufunga ndoa kanisani. Kufanya hivyo ni taratibu za kibinadamu na za unafiki-mtu anamuoa mke wake huku watoto wakishangilia na kusema ‘ baba na mama wanaoana!”.

( 4  ).  NDOA NI YA WATU WANGAPI?

Mume mmoja, mke mmoja ( MATHAYO  19:4-5; 1 WAKORINTHO 7:2 ; WAEFESO 5:25-28 ). Popote Biblia ikisema “ mume” inafuata “mke”.Ikisema “waume” inafuata “wake”. Mtu wa kwanza kuoa wake zaidi ya mmoja alikuwa Lameki ambaye pia alikuwa muuaji ( MWANZO 4:19,23-24 ). Wote waliofuata tabia yake waliangamizwa kwa gharika na walioingia safinani walikuwa waume wanne, wake wanne kila mmoja na mkewe mmoja tu                      ( MWANZO 7:13 ). Huu ndio mpango wa Mungu tangu mwanzo. Yeyote aliye na mke zaidi ya mmoja au mume zaidi ya mmoja ataangamizwa. Inampasa kufanya malipizo ya ndoa na kubaki na yule wa kwanza tu.

( 5 ).  TALAKA KATIKA UKRISTO.

Hakuna kabisa talaka katika Ukristo. Mungu anachukia kuachana. Ni mume mmoja, mke mmoja hadi kifo kiwatenganishe ( MALAKI 2:13-16 ; 1 WAKORINTHO 7:39; WARUMI 7:2-3 ; LUKA 16:18 ).

  1. VISINGIZIO VYA WATU KUACHANA.

( a ). Kwa sababu ya uasherati ( MATHAYO 19:9 ). Uasherati unafanywa  kati ya msichana na mvulana siyo kwa yeyote aliyekwisha kuoa au kuolewa. Huyu anafanya uzinzi ( LUKA 16:18 ). Nyakati za Biblia, mtu akitoa posa kwa mchumba wake hata kabla ya kuoana waliitwa mtu na mkewe. Katika uchumba huu, ikithibitishwa kwamba msichana amefanya uasherati kwa mfano kuwa na mamba, mwanaume hapo anakuwa huru kumuacha maana amekuwa dhahiri kuwa dada huyo hakuwa mwaminifu, hajaokoka. Hata leo ndivyo inavyopasa kuwa ( MATAHYO 1;18-20; KUMBUKUMBU LA TORATI 20:23-24 ).

(  b ). Kwa kuwa mwenzi ambaye hajaokoka ameondoka, mtu hafungiki ( 1 WAKORINTHO 7:12-15 ). Kinachosomwa katika mistari hii ni kwamba Mungu ametuita katika AMANI. Yeye ambaye hajaokoka akisema hataki kuishi na ambaye ameokoka na kukazania kwamba aondoke, mwache aondoke, usimfunge kamba na kumuweka stoo! Baada ya kumuacha hutafungika kanisani kwa maana kwamba hutatengwa kwa kuonekana kuwa ni mzinzi ( 1WAKORINTHO 5:9-11 ). Tutaomba na atatapikwa kama Yona. Mtu akitengana na mkewe anapaswa kukaa bila kuoa au kuolewa tena au wapatane ( 1 WAKORINTHO 7:10-11 ). Mmeo aliyekuacha hata kwa talaka potea, mtarudiana kwa maombi na unapaswa kukaa hivyo bila kuolewa.

( 6 ).  KUHESABU GHARAMA.

Biblia inasema tuhesabu gharama kabla ya kujenga mnara ili tusije tukadhihakiwa kwa wokovu wetu wa bandia ( LUKA 14;28-32 ). Ni gharama zaidi kwenda motoni kuliko kumuacha mume au mke na kubaki na shida. Ni afadhali kuingia uzimani ukiwa kigutu, kiwete au chongo kwa kumkosa mume au muke wako asiye harali ( MARKO 9:43-47 ). Linalotupasa tufanya ni kumwomba Mungu atupe Neema ya kutuwezesha kufanya mapenzi yake, maana Neema na kweli vilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo ( YOHANA 1:17 ).

……………………………………………………………………………………………………….

JE UNAPENDA UISHI NA MUNGU MILELE?

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook ,Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “note” hii, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.

                                                         UBARIKIWE NA BWANA YESU!!!

Advertisements
By neno la uzima

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s