SAUTI YA MUNGU

NenZACHARY KAKOBEo la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

SOMO:   SAUTI YA MUNGU

K

una mengi sana ya kujifunza katika Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu.  Leo, tutatafakari kwa makini YOHANA 12:27-36.  Katika mistari hii, pamoja na mambo mengine, tutajifunza juu ya “SAUTI YA MUNGU“.  Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika mistari hii, katika vipengele saba:-

(1)      SAUTI YA MUNGU (MST. 27-30)

(2)      HUKUMU YA ULIMWENGU MSALABANI (MST. 31);

(3)      HUKUMU YA MKUU WA ULIMWENGU MSALABANI (MST. 31);

(4)      NIKIINULIWA NITAWAVUTA WATU WOTE KWANGU (MST. 32-33);

(5)      CHANZO KIKUU CHA TAFSIRI POTOFU YA MAANDIKO (MST. 34);

(6)      UMUHIMU WA UVUMILIVU KWA MWALIMU WA BIBLIA (MST. 35-36);

(7)      MATOKEO YA KUBISHANA NA NENO LA MUNGU (MST. 36).

 

(1)      SAUTI YA MUNGU (MST. 27-30)

            Sauti ya Mungu ilikuja kutoka mbinguni ikisema, “Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena“.  Mkutano, yaani watu wengi, waliosimama karibu, wakasikia.  Wengine walisema ya kwamba kumekuwa ngurumo, wengine walisema, Malaika amesema naye.  Sauti ya Mungu, ina nguvu na uawezo wa kipekee, ni kama ngurumo (AYUBU 37:5).  Hata kama sauti ya Mungu ikisikika kupitia kwa Wajumbe wake, bado pia inakuwa na uawezo wa kipekee kama ngurumo (UFUNUO 10:1-4).  Baada ya sauti hii kusikika, Yesu alisema kwamba sauti hii ilikuja maalum kwa ajili yao, ili wapate kitu cha ziada.  Hapa tunajifunza jambo la umuhimu mkubwa.  Kama wahubiri wa Neno la Mungu, hatuna budi kuutafuta uso wa Mungu KABLA ya kulihubiri au kulifundisha neno la Mungu; na kuhakikisha kwamba katika mahubiri yetu, kunakuwa na SAUTI YA  MUNGU, akisema na watu wake.  Ikiwa ni sauti yetu tu, wanadamu, mioyo ya wale tunaowahubiria, haiwezi kubadilishwa.  Tutasema mameno mengi na misari mingi, kwa ufundi mkubwa wa kibinadamu, kwa kutumia akili na maarifa yetu; lakini maneno hayo hayawezi kuwa na uwezo wa kubadili maisha ya watu.  Maneno machache yanayotokana na SAUTI YA MUNGU, yanakuwa na utukufu mkubwa, na uwezo wa kubadilisha kabisa maisha ya watu, tunaowahubiri au kuwafundisha (ZABURI 29:4-9), kuliko maneno mengi ya kibinadamu.  Kwa sababu hii, hatuwezi kuwa Waalimu au Wahubiri wenye uwezo mkubwa, ikiwa hatuzungumzi na Mungu kwanza kabla ya kuzungumza na watu; tukimwaomba Mungu kwamba yeye mwenyewe azungumze na watu wake KWA SAUTI YAKE!  Hata hivyo, kuna jambo jingine la kuzingatia hapa.  Ni hatari kubwa kwa yeyote kati yetu, kutafuta kuongozwa  “Sauti ya Mungu“ iliyo mbali na Neno la Mungu.  Wengine wanaweka uzito katika kutafuta jumbe za Mungu kuliko Neno la Mungu.  Wanataka kusikia sauti halisi ya Mungu akisema nao!  Jambo hili linahitaji tahadhari kubwa.  Ziko sauti za namna nyingi duniani (1 WAKORINTHO 14:10).  Shetani, kwa kutumia pepo wa uongo, huwa mwepesi sana kusema na watu wanaotaka kuongozwa na sauti halisi ya Mungu, na kuwatia katika hatari kubwa (2 NYAKATI 18:19-21).  Tusitafute, “kuwa wa kiroho sana“ kwa kutafuta sauti halisi ya Mungu na kutaka aseme nasi kwa jinsi hiyo, na kujiingiza mtegoni bali turidhike na SAUTI YA NENO LAKE katika Biblia! (ZABURI9 103:20).  Kwa mfano, hatuna haja ya kungojea sauti halisi ya Mungu kutufahamisha kwamba Yesu yu karibu kuja wakati neno la Mungu limekwisha kueleza hivyo waziwazi (UFUNUO 22:7; 3:11; WAEBRANIA 10:37).  Vivyo hivyo, sauti yoyote tunayoisikia katika ulimwengu wa roho, hatupaswi kukubaliana nayo tu kwamba ni sauti ya Mungu.  Tunapaswa kuijaribu kwa kuipima na Neno la Mungu katika Biblia (1 YOHANA 4:1; ZABURI 119:9).

(2)         HUKUMU YA ULIMWENGU MSALABANI (MST. 31)

         “Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo?“  Yesu aliyasema maneno haya muda mfupi kabla ya kusulubishwa.  Hukumu ya Ulimwengu wote, iko MSALABANI.  Mtu yeyote anahukumiwa kutokana na jinsi anavyoliona kulielewa NENO LA MSALABA.  Kwa wengine neno la msalaba, ni UPUUZI, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu.  Kwa Wayahudi, watu wanaojihesabia haki, MSALABA ni kikwazo na kwa Wayunani wanaotumia akili, ni upuuzi (1 WAKORINTHO 1:18, 23-24).  Msalabani, kulikuwa na picha ya jambo hili.  Kulikuwa na wahalifu WAWILI msalabani.  Mmoja alimpuuza Yesu alipomwona msalabani na mwingine akamwona Yesu, Mungu; ingawa alikuwa msalabani.  Huyu wa pili, alihesabiwa haki ya kuingia mbinguni (LUKA 23:39-43).  Hata leo, ni vivyo hivyo.  Mtu atakayeingia mbinguni, ni yule anayeiamini kazi iliyomalizika msalabani.  Yesu akafa kwa niaba yetu na kwa ajili yetu.

(3)     HUKUMU YA MKUU WA ULIMWENGU MSALABANI (MST. 31)

            Hapo mwanzo Mkuu wa Ulimwengu, alikuwa Adamu.  Aliumbwa na kupewa Utawala wa Ulimwengu na vyote vilivyomo (MWANZO 1:26-28).  Adamu alipomtii Shetani pale alipofanya dhambi, Shetani alichukua utawala wa ulimwengu, maana yeye anayekushinda, ndiye anayechukua utawala (LUKA 4:5-7).  Hata hivyo, mapema kabisa Mungu alisema, utatokea uzao wa mwanamke utakaomponda kichwa nyoka (MWANZO 3:15).  Uzao huu wa mwanamke, ni Yesu Kristo, alizaliwa na mwanamke tu, bila mbegu ya mwanamume kuwa na sehemu.  Sasa, pale msalabani, Yesu Kristo, alimponda kichwa Shetani, na Shetani aliambulia tu kumponda kisigino!  Pale msalabani, Shetani alihukumiwa na kutupwa nje ya Utawala! (YOHANA 16:11).  Kabla ya msalaba, Yesu aliyonyesha jambo hili kwa kutoa pepo na kuwaweka huru maelfu walioonewa na Ibilisi.  Leo, Shetani hana mamlaka ya kututawala.  Anamtawala tu yeye asiyeijua Kweli (YOHANA 8:32).

(4)      NIKIINULIWA NITAWAVUTA WATU WOTE KWANGU (MST. 32-33)

             Yeye aliyesulibishwa, alipigiliwa kwanza msalabani, msalaba huo ukiwa juu ya ardhi, kisha uliinuliwa na kuchimbiwa chini, hivyo aliyesulibishwa ALIINULIWA JUU.  Yesu alipoinuliwa hivi, aliweka mikono yake katika hali ya kumkaribisha, kumpokea na kumkumbatia kila atakayemfuata msalabani!  Aliinuliwa ili awavute Watu wote kwake na siyo Wayahudi peke yao!  Hapa pia tunaona kwamba Yesu na Baba ni Umoja.  Baba huwavuta watu pia (YOHANA 6:44).  Ni muhimu kufahamu kwamba mtu hawezi kuokolewa asipovutwa na Baba na Mwana, Kwa Roho Mtakatifu, ndiyo maana, kuhubiri bila maombi kwanza, hakuna maana yoyote.  Vivyo hivyo, sisi kama Wakristo, tunapokufa, NDIPO tunapoinuliwa kwenda juu kwa Baba!

(5)      CHANZO KIKUU CHA TAFSIRI POTOFU YA MAANDIKO (MST. 34)

            Ni muhimu kufahamu kwamba maandiko yanatafsiriwa kwa kuoanishwa na kulinganishwa.  Ukichukua andiko moja au mawili, na kuyatafsiri peke yake, bila kuyaoanisha na maandiko mengine, kunakuwa na hatari ya kuambulia TAFSIRI POTOFU!  Hapa, mkutano walisema Kristo adumu hata milele kwa kuangalia (ZABURI 110:4; 21:4; 61:6).  Hawakuoanisha maandiko haya, bna kukatiliwa mbali kwa Masihi (DANIELI 9:26), kumwaga nafsi yake hata kufa (ISAYA 53:12), wamenizua (Kiingereza KJV Bible, “They Pierced“) yaani wamenichoma mikono na miguu (ZABURI 22:16-18) n.k.  Kwa kuangalia upande mmoja tu wa sarafu ya maandiko, wakaona kwamba Yesu siye Mwana awa Adamu yaani siyo Masihi; na kukosea vibaya.  Hata leo, chanzo kikuu cha tafsiri potufu ya maandiko ni kuangalia upande mmoja tu wa saafu ya maandiko.  Kwa misingi hii, wengi wamesema Mungu anaangalia ndani ya tu tu na siyo nje, kwa kukosa kuoanisha KUSAFISHA KWANZA NDANI ILI NJE YAKE NAYO IWE SAFI (MATHAYO 23:25-26) na kuangalia andiko la kuwa watakatifu MWILI na ROHO (1 WAKORINTHO 7:34; 2 WAKORINTHO 7:1).  Wengine wanasema hatuko chini ya Sheria, kwa kuzingatia WAGALATIA 5:18; bila kuzingaia kwamba tuko chini ya Sheria ya Kristo (WAGALATIA 6:2).  Wengine wanasema tuko “HURU“ kwa kuzingatia 2 WAKORINTHO 3:17; bila kuzingatia kwamba tuko HURU MBALI NA DHAMBI (WARUMI 6:22).  Hiki ndicho chanzo kikuu cha Tafsiri potofu ya maandiko.  Hatuna budi kuwa na tahadhari.

(6)      UMUHIMU WA UVUMILIVU KWA MWALIMU WA BIBLIA (MST. 35-36)

             Pamoja na watu hawa kumwona Yesu hajui maandiko, na kubishana naye.  Yesu kama Mwalimu wetu wa Biblia wa mfano, anaonyesha uvumilivu, na kutaka kuwavuta, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli (2 TIMOTHEO 2:24-26; 4:2).  Yesu anawajibu kwa kujitaja kuwa ni NURU.  Ufalme wa Kristo, unafananishwa na JUA na MWEZI ambavyo huleta nuru (ZABURI 72:17; 89:36-38).  Jua linapotua, au mwezi unapotoweka, haina maana kwamba havipo tena.  Hatuvioni sisi, lakini wengine upande mwingine wa ulimwengu, wanaviona!  Na yesu kama Jula la haki (MALAKI 4:2), pale msalabani, alitua tu, lakini adumu hata milele!  Maadamu tunayo NURU ni muhimu kutembea kwa kasi ili tufike tunakokwenda kama wasafiri.  Likija giza, tutashindwa kusafiri salama.  Wakati tunayo nuru, yaani wakati tun uhai, wakati tuna nafasi ya kuokoka, tusicheze na nafasi hii kwa kubishana na maandiko, halafu giza likaja, tukafa!  Tutajuta!

(7)      MATOKEO YA KUBISHANA NA NENO LA MUNGU (MST. 36)

             “Akajificha wasimwone“.  Tukizidi kubishana na Neno la Mungu, Yesu huuficha uso kwetu tusimwone tena (KUMBUKUMBU 32:20).  Hatuna budi kulisikia neno, na kulitendea kazi mara moja. …………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoniMungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . ……………………………………………………………….

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements
By neno la uzima

One comment on “SAUTI YA MUNGU

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s