AMANI YA KRISTO IAMUE MIOYONI MWENU

Neno lZACHARY KAKOBEa Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SOMO LA KANISA LA NYUMBANI

SOMO LA 16

AMANI YA KRISTO IAMUE MIOYONI MWENU

NENO LA MSINGI:

WAKOLOSAI 3:15:

“Na AMANI YA KRISTO IAMUE MIOYONI MWENU; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani.”

<><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><>< 

M

ara nyingi utamsikia mtu anaulizwa “Mbona wewe umeokoka na unafanya kazi kiwanda cha sigara?”  “Mbona wewe unakunywa divai inayolevya katika ushirika “mtakatifu?”  Utasikia mtu anayeulizwa akijibu “Mimi ninasikia amani ndani yangu, sihukumiwi”.  Maneno haya ni mtego mkubwa wa shetani.  Ni makusudi basi ya somo la leo la Kanisa la Nyumbani kujifunza juu ya “AMANI” na “KUHUKUMIWA” ili baada ya kuifahamu kweli ituweke huru wakati wote na kuishindania.

MAKUNDI MAWILI YA AMANI

1.         AMANI INAYOTOKANA NA ULIMWENGU.

2.        AMANI INAYOTOKANA NA KRISTO (Hii ndiyo inaitwa AMANI YA KRISTO).

Katika msitari ufuatao, tunaona makundi hayo mawili ya amani:-

YOHANA 14:27

“Amani nawaachieni, AMANI YANGU NAWAPA, niwapayo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo.”

Ukiuangalia kwa makini msitari huu, utaona kwamba Yesu anatoa Amani, na ulimwengu pia unatoa amani; na amani hizi ni tofauti kabisa.  Atupavyo Yesu, SIVYO KAMA ulimwengu utoavyo.  Maana yake ni kwamba, amani aitoayo Yesu siyo amani inayotolewa na ulimwengu.  Ili basi tuelewe amani ipi inatoka wapi, ebu tuangalie tofauti ya makundi haya mawili ya amani.

(1)       AMANI INAYOTOKANA NA ULIMWENGU:

            Kuna aina mbili za amani zitokanazo na ulimwengu:-

            (a)       AMANI YA KIBINADAMU ILIYO SAWA NA NJIA ZA ULIMWENGU;

            (b)       AMANI YA SHETANI MKUU WA ULIMWENGU;

(A)       AMANI YA KIBINADAMU ILIYO SAWA NA NJIA ZA ULIMWENGU

Biblia inatuagiza kwamba, hatupaswi kuitafuta amani ya namna hii ya kibinadamu:

KUMBUKUMBU 23:6

“USITAFUTE AMANI YAO wala heri yao siku zako zote, milele”.

Amani hii ya kibinadamu, ni amani anayokuwa nayo mtu kutokana na kukipenda kitu kile anachochagua kukifanya kutokana na njia za kawaida za Ulimwengu.  Mtu yeyote hata kama hajaokoka anaweza kuwa na amani ya namna hii.

Kwa mfano mtu amekaa muda mrefu bila kazi, na akaletewa taarifa ya nafasi ya kazi mahali fulani; mtu yeyote katika mazingira haya anaweza kuwa na amani ya kwenda haraka kwenye kazi hiyo.  Hii ni amani ya kawaida ya kila mtu wa ulimwengu.  Hana kitu kabisa, akipata kitu chochote kitampa amani.  Mtu wa ulimwengu anaweza akawa hana sigara na akakosa amani.  Akipata mtu wa kumpa sigara, anapata amani.  Mtu mwingine ambaye ametafuta sukari kila duka na kukata tamaa, anapopata sukari mahali fulani inayouzwa kwa magendo, na ana fedha mfukoni; ataona ni amani kuipata sukari hiyo.

Mtu mwingine aliyeokoka ambaye amekaa muda mrefu bila kupata mchumba anapomuona mtu yeyote anamwijia na kutaka awe mchumba wake anaweza kuona na akajibu haraka kukubali lakini ikawa ni amani tu ya kibinadamu.

Kwa ufupi, amani ya kibinadamu inakuwa inatokana na  sababu au njia za kawaida za ulimwengu.  Kwa mfano:-

  • Kwa sababu nina fedha, mradi tu nipate ninachokihitaji;
  • Kwa sababu chumba hiki kodi yake ni ndogo sana basi kinafaa;
  • Kwa sababu kazi hiyo ina mshahara mkubwa kuliko hii ninayoifanya, basi naacha hii mara moja na kwenda huko kuanza kazi;
  • Kwa sababu nimechelewa sana kupata mchumba, basi yeyote wa kwanza atakayenitaka niwe mchumba wake, huyo simwachi nisije nikafa bila kuolewa;
  • Ni vigumu sana kupata leseni kwa njia halali.  Kuna mizunguko mingi sana.  Ni heri kutoa chochote tu kwa maofisa wanaohusika.  Fedha utakayowapa itakupunguzia muda wa usumbufu na fedha utakazotumia katika “Nenda rudi”.  Mpe fedha hiyo mara moja.  Kesho tu utapata leseni.  Hiyo ndiyo njia ya mkato.

Hizi zote ni njia au sababu za kibinadamu zinazotokana na jumla ya fikra ya mwanadamu tu.  Njia ya Mungu, inaweza ikawa tofauti kabisa na njia inayotokana na jumla ya fikra za kibinadamu.

Wana wa Israeli walipotoka Misri kwenda Kanaani, AMANI YA KIBINADAMU ILIYO SAWA NA NJIA ZA ULIMWENGU, ingekuwa ni kutumia njia fupi ambayo ingetumia chini ya wiki mbili kufika Kanaani.  Katika jumla ya fikra ya mwanadamu, kwa nini tupite njia ndefu ya mzunguko wakati iko njia fupi rahisi ya kufika Kanaani?  Haya ni mawazo au njia ya kibinadamu.  AMANI YA KRISTO katika safari hiyo, ilikuwa ni kupita njia ndefu ya miaka 40 iliyohitaji miujiza mikubwa kama kuigawanya Bahari ya Shamu n.k. Unaona?  Amani ya Kristo inakuwa katika njia ndefu tofauti kabisa na njia fupi inayokubalika haraka katika fikra za mwanadamu [SOMA KUTOKA 13:17-18].

Njia za Kibinadamu zinaweza kuwa potofu mbali kabisa na zile za Mungu zilizo juu sana.  Amani inayopatikana kutokana na hisia, na njia na sababu za kawaida za ulimwengu, hiyo ni amani ya kibinadamu tu inayotokana na ulimwengu.  Hiyo siyo Amani ya Kristo.  Utamsikia mtu akisema “Msichana huyu ana umbo zuri sana linalonivutia.  Kila nikimuona ninakosa amani.  Amani nitaipata tu nikimuoa”.  Mtu huyu hatafuti Amani ya Kristo.  Anatafuta amani ya kibinadamu inayotokana na njia za kawaida za ulimwengu “Kupendeza kwa macho”.  Hii siyo njia ya Amani ya Kristo.

ISAYA 59:8

“Njia ya amani hawaijui, wala hapana hukumu ya haki katika mienendo yao, wamejifanyizia njia zilizopotoka; kila apitaye katika NJIA HIZO HAJUI AMANI.”

(B)       AMANI YA SHETANI, MKUU WA ULIMWENGU

Hii ni amani inayokuwa juu ya mtu anayeishi katika dhambi.  Anafanya dhambi yaani kinyume na Neno la Mungu lakini yeye anaitetea dhambi hiyo na kusema yeye ANA AMANI katika kufanya anayoyafanya.  Hii siyo AMANI YA KRISTO.

2 WAFALME 9:22

“Ikawa, Yoramu alipomwona Yehu, akasema, Je! ni amani, Yehu?  Akajibu AMANI GANI MAADAMU UZINZI WA MAMA YAKO YEZEBELI NA UCHAWI WAKE NI MWINGI?”

Mtu akiwa katika uasi na ukaidi na akawa anafanya jambo lililo kinyume na Neno la Mungu na akasema yeye ana amani, asifikiri amani hiyo itamsaidia.  Ataendelea kujibariki hivyo lakini hasira ya BWANA itamkalia na ataangamizwa pamoja na Amani yake ya Shetani.  Angalia maandiko:-

KUMBUKUMBU 29:19-20

“Ikawa asikiapo maneno ya laana hii, ajibarikie mtu huyo moyoni mwake, na kusema, Nitakuwa katika amani, nijapotembea katika upotoe wa moyo wangu, kwa kuangamiza mbichi na kavu; (kwa kwenda kinyume na Neno la Mungu)  BWANA hatamsamehe mtu huyo, lakini wakati huo hasira ya BWANA na wivu wake vitafuka moshi juu ya mtu yule, na laana yote iliyoandikwa katika kitabu hiki itamkalia juu yake, na BWANA atalifuta jina lake chini ya mbingu.”

Amani ya Shetani, mkuu wa ulimwengu ikimkalia mtu, ataona kana kwamba mambo yake yanakwenda vizuri katika dhambi na kumbe hizo ni kama jeraha zilizoponywa juujuu tu.  Kwa amani hiyo ya Shetani, atatenda yaliyo machukizo mbele za Mungu bila haya usoni, lakini hatimaye amani hiyo itamuangamiza.

YEREMIA 6:14-15

“Wameiponya jeraha ya watu wangu kwa juu juu tu wakisema, Amani, Amani wala hapana amani. Je! walitahayarika walipokuwa wametenda machukizo? la, hawakutahayarika hata kidogo, wala hawakuweza kuona haya usoni, basi wataanguka miongoni mwa hao waangukao; wakati nitakapowajilia wataangushwa chini asema BWANA”.

Ukimsikia mtu anasema “Sishuhudiwi kubatizwa katika maji tele baada ya kuamini.  Ubatizo ule wa utotoni unatosha.  Nina amani tele moyoni mwangu”.  Amani hii ni ya Shetani mkuu wa ulimwengu.  Mtu huyu anasema Amani, Amani, wala hapana Amani.  Ataanguka miongoni mwao hao waangukao.  Jeraha zake zimeponywa kwa juu juu tu na Shetani na anasema anaona amani.  Hii siyo amani ya Kristo.

Mtu ambaye anafanya kazi yoyote kiwanda cha bia au cha sigara, na akasema ana amani kwa sababu yeye hanywi pombe wala havuti sigara; hii ni amani ya shetani mkuu wa ulimwengu.  Kufanya kazi yoyote kiwanda cha sigara au cha bia, ni sawa na kusema umeokoka halafu ukauza pombe au sigara katika duka lako.  Biblia inasema ole wake yeye ampaye jirani yake kileo au sumu yoyote na kumlevya.  Mtu huyu amejaa aibu badala ya utukufu na ni heri kwake anywe na yeye pombe hiyo au avute sigara hizo kuliko kujidanganya nafsi yake. [SOMA HABAKUKI 2:15-16]Amani yoyote inayopatikana nje ya Neno la Mungu, ni amani ya shetani mkuu wa ulimwengu.  Amani hiyo, mwisho wake ni maangamizo.  Mtu anapokunywa “Dodoma Wine” ambayo inayolevya katika ushirika unaoitwa mtakatifu na akasema anaona amani moyoni mwake, wakati Neno linasema katika MITHALI 23:20, “Usiwe miongoni mwao WANYWAO mvinyo,” amani hiyo ni amani ya Shetani, mkuu wa ulimwengu.  Mtu yeyote ajibarikiaye moyoni mwake na kusema atakuwa katika amani, ajapotembea katika upotovu wa moyo kwa kwenda kinyume na Neno la Mungu; mtu huyo anaitafuta hasira ya BWANA ifukayo kama moshi.

(2)   AMANI YA KRISTO

Amani ya Kristo inayoamua mioyoni mwetu, hupatikana ndani ya Kristo!  Maana yake ni kwamba Amani ya Kristo hupatikana katika Utakatifu wa Kristo, katika mapenzi yake, katika Neno lake, katika mpango wa Mungu.

YOHANA 16:33a

“Hayo nimewaambieni mpate kuwa na AMANI NDANI YANGU…………”.

Amani yoyote ambayo siyo Amani ndani ya Yesu, ni amani ya ulimwengu.  Amani ndani ya Yesu ni AMANI NDANI YA NENO LA MUNGU.  Yesu Kristo ni NENO LA MUNGU. 

[UFUNUO 19:13, YOHANA 1:1].

Ni amani ndani ya Neno la Mungu na siyo nje ya Neno la Mungu.  Amani yoyote iliyo nje ya Neno la Mungu, ni amani ya shetani, mkuu wa ulimwengu.

Amani ya Kristo ni ile tu ambayo inapatikana baada ya kumwomba Mungu juu ya jambo sawasawa na mpango wa Mungu juu ya jambo lile.  Kwa kuwa Kristo ni Neno la Mungu, amani ya Kristo inapatikana baada ya kulipima jambo kwa Neno la Mungu.  Neno la Mungu likitupa amani kulifanya jambo fulani, basi hiyo ni amani ya Kristo.  Roho wa Mungu ambaye anashuhudia ndani yetu, yeye pia ni ROHO WA KWELI na wakati wote maongozi yake hutuongoza na kututia katika KWELI YOTE [YOHANA 16:13].  Hatuongozi kufanya kinyume na Neno.  Tunapokuwa tumeomba juu ya jambo fulani sawa na Neno la Mungu, na kufuata njia za Mungu anazozitumia kutuongoza kufahamu jibu, na tukawa na amani kufanya jambo sawa na jibu hilo; amani hiyo ni amani ya Kristo.  Ni amani iliyo ndani ya Neno la Mungu, ndani ya mapenzi yake, ndani ya mpango wake.

KUHUKUMIWA MOYONI

1 YOHANA 3:21

“Wapenzi, MIOYO YETU ISIPOTUHUKUMU, tuna ujasiri kwa Mungu.”

“Wapenzi”  wanaozungumzwa katika sura yote ya tatu ya Waraka wa Kwanza wa Yohana, ni WANA WA MUNGU [1 YOHANA 3:1-2].  Katika sura hii tunaelezwa kwamba kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu. [1 YOHANA 3:9]  Tunazidi kuelezwa kwamba mtu yeyote asiyetenda haki, ni mtoto wa Ibilisi na siyo mtoto wa Mungu au Mwana wa Mungu [1 YOHANA 3:10].  Maana yake ni kwamba, yeyote yule ambaye kweli ni mtoto au mwana wa Mungu, anapofahamu jambo fulani ni dhambi, kamwe hawezi kuendelea kulitenda.  Biblia inasema dhambi ni uasi [1 YOHANA 3:4] na tena ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi [YAKOBO 4:17]

Aliye mtoto wa Mungu au mwana wa Mungu kweli, akiwa alikuwa amefanya jambo lililo kinyume na Neno la Mungu na akafahamu hivyo, mara ileile ATAHUKUMIWA MOYONI na hawezi kuendelea kufanya dhambi au kuliasi Neno la Mungu.  Dalili ya kwamba mtu fulani ni mtoto wa Ibilisi na siyo mtoto wa Mungu, ni jinsi ambavyo hahukumiwi moyoni anapofahamu kuwa jambo lile alitendalo siyo sawa na Neno la Mungu.

Mtu ambaye hajazaliwa mara ya pili au hajazaliwa na Mungu, hata akijua kwamba wizi, uongo, uasherati, matusi, kunywa pombe, yote ni dhambi; bado ataendelea kuyafanya na asihukumiwe moyoni na wakati mwingine ataitetea dhambi na kujisifia kuifanya.  Kwa mfano atasema “Wezi wengine watashikwa wote kwa sababu hawajui kupanga mipango yao vizuri, lakini mimi hawaniwezi.”  “Furaha yangu hutimilika pale ninapotembea na wake za watu.  Kijiji hiki, wote nitawamaliza.”  Lugha zote hizi ni za mtu ambaye hajazaliwa na Mungu.  Nuru inapokuja ndani ya mtu humumulika na ndipo hujiona mwenye dhambi na kuhukumiwa hadi toba, na akazaliwa mara ya pili.

Ukimsikia mtu anasema kwamba hahukumiwi moyoni wakati anafahamu kwamba anatenda jambo ambalo ni kinyume na Neno la Mungu, hiyo ni dalili kwamba mtu huyo hajazaliwa na Mungu.  Siyo mtoto wake Mungu.  Uasi bado uko kwake na anaufurahia.  Watoto wa Ibilisi tu ndiyo wako hivyo.  Mtoto wa Mungu, dhambi itamhukumu na kuwa mzigo mzito mno kwake [ZABURI 38:4].  Amani itakuja kwake pale tu atakaporekebisha mambo yake na Mungu kwa kutubu na kuyaacha.

DHAMIRI HAINISHUHUDII KUWA NI DHAMBI

Utamsikia mwingine akisema, “Dhamiri hainishuhudii kwamba kufanya jambo hili ni dhambi.  Kwa hiyo mimi ninaendelea kulifanya ingawa mnasema kwamba liko kinyume na Neno la Mungu.”  Huu tena ni mtego mkubwa.  Jambo la kukumbuka hapa ni kwamba DHAMIRI INAFUNDISHIKA.  Unaweza ukashuhudiwa na dhamiri yako kwamba jambo hili ni sawa kulifanya lakini baada ya kukubali kufundishwa Neno la Mungu na ukawa tayari kubadilika, kuanzia hapo dhamiri yako itakushuhudia kinyume na mwanzo.  Dhamiri yako sasa itakushuhudia kulingana na ulivyojifunza.

Utaona basi kuwa, siyo kwamba kwa sababu dhamiri yako haikushuhudii kuwa kufanya jambo hilo ni dhambi, ndiyo tuseme kwamba siyo dhambi hata kama Neno la Mungu linasema kuwa ni dhambi.  Kila afanyaye uasi wa sheria, afanya dhambi hata kama dhamiri yake dhaifu inamshuhudia kwamba siyo dhambi.

Tunafahamu kwamba kufanya jambo fulani ni dhambi kutokana na Neno la Mungu linavyotuambia, na siyo kutokana na dhamiri zetu zinavyotuambia.  Dhamiri zetu zinaweza kutukosesha kabisa, zikiwa zinashuhudia ndani yetu jambo lililo kinyume na Neno la Mungu.  Biblia inasema, “Neno lako ni taa ya miguu yangu na mwanga wa njia yangu.”[SOMA ZABURI 119:105].  Biblia haisemi, “Dhamiri yangu ni taa ya miguu yangu na mwanga wa njia yangu.”

M A S W A L I

(1)       Taja makundi mawili ya amani:

            (a)————————————————————————————————————

            (b)————————————————————————————————————-

(2)       Taja aina mbili za amani zitokanazo na ulimwengu au zitolewazo na ulimwengu:

            (a)————————————————————————————————————-       

           (b)————————————————————————————————————-

(3)       Ni nini maana ya Amani ya Shetani, Mkuu wa Ulimwengu?

            —————————————————————————————————————-

            —————————————————————————————————————-

(4)       Je, mtu akijibariki moyoni kwamba anaona amani, wakati anakwenda kinyume na Neno la Mungu; mtu huyu atasalimika wakati wa hasira ya BWANA, asipotubu?  Lithibitishe jibu lako kwa andiko.

            —————————————————————————————————————-

            —————————————————————————————————————-

            —————————————————————————————————————-

(5)       Nini maana ya Amani ya Kristo?  Eleza kwa ufupi ukitumia maandiko:

            —————————————————————————————————————-

              —————————————————————————————————————-

            —————————————————————————————————————- 

             —————————————————————————————————————

(6)      Je, mtu anaweza asihukumiwe moyoni au dhamiri yake isimshuhudie kwamba anafanya dhambi,  lakini  bado ikawa ni kweli anafanya dhambi?  Tunajuaje kwamba kufanya jambo fulani ni dhambi?  Eleza kwa ufupi.

            —————————————————————————————————————-

            —————————————————————————————————————-

            —————————————————————————————————————-

            —————————————————————————————————————-

            —————————————————————————————————————-

<><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><>< 

         Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements
By neno la uzima

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s