MAARIFA YA MSINGI BAADA YA KUOKOKA

ZACHARY KAKOBE

Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

Somo: Maarifa ya Msingi Baada ya Kuokoka                                                                       Mpendwa Ubarikiwe!  Bwana Asifiwe!  Itika, “Amen”, neno lenye maana “Na iwe hivyo”.  Mpendwa, umepata neema kubwa kuipata “note” hii.  Katika “note” hii kuna mafundisho muhimu sana, ambayo yatakufanya uchote baraka zote za rohoni ambazo Mungu amekusudia kukupa.  Hata hivyo, ili ufuatilie vizuri mafundisho haya, itakuwa vema uwe na Biblia yako karibu, ili ufungue na kusoma mistari inayotajwa, ili upate kuelewa vizuri.  Kama umepata “note” hii mbali na mahali Biblia yako ilipo, basi kwanza usiendelee kuisoma, hakikisha unaipata kwanza Biblia yako, halafu ndipo uisome “note” hii, ukiwa mahali penye utulivu; iwe ni nyumbani, ofisini,au popote pengine penye utulivu.  Je, uko tayari sasa?  Najua uko tayari.  Vema sasa, sasa tuendelee.

Kwanza kabisa, hongera sana kwa kuokoka.  Je ninajuaje, au wewe utajuaje kwamba kweli umeokoka?  Jibu, ni kwamba, tunajua kwamba kweli tumeokoka, kutokana na jinsi Neno la Mungu linavyotuambia.  Wakati ulipotubu dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha, kwa dhahiri Yesu Kristo alikusamehe dhambi zako, maana Neno la Mungu linasema katika YOHANA 6:37, “……Wala yeyote ajaye kwangu, sitamtupa nje kamwe”.  Hakuna mtu yeyote anakwenda kwa

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

                                      Kwanza kabisa hongera sana kwa kuokoka

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Yesu na kutubu dhambi zake, akiwa anamaanisha kuziacha ambaye anatubu dhambi kisha Yesu akamtupa nje na kuacha kumsamehe.  Hivyo, ni dhahiri kwamba ulipotubu dhambi zako ulisamehewa dhambi.  Dhambi zako zote zimesamehewa na Mungu hazikumbuki tena (ZABURI 103:12;  ISAYA 43:25).  Sasa baada ya kujua kwamba umesamehewa dhambi zako, ni muhimu kufahamu pia kwamba kupewa msamaha kunaambatana na kupewa wokovu, maana Biblia inasema katika LUKA 1:77, “Uwajulishe watu wake wokovu, katika kusamehewa dhambi zao”.

Hivyo basi, kwa hakika umeokoka, na jina lako limefutwa katika kitabu cha hukumu na kuandikwa katika kitabu cha uzima wa milele mbinguni.  Kuna furaha na shangwe kubwa mbele za Mungu na malaika zake, kutokana na uamuzi wako (LUKA 15:7, 10).  Hivyo tangu leo huna budi kuwa na hakika ya wokovu wako, ili Shetani asikudanganye kwamba hujaokoka.  Shetani huweza kutudanganya kwamba hatujaokoka kwa kutumia hisia zetu, na wakati wote tukawa ni watu wa kufuatisha tu sala ya toba na kutaka kuokoka, tena na tena.  Hatupaswi kuwa hivyo.  Hatuenendi kwa kuona, bali kwa imani (2 WAKORINTHO 5:7).  Na imani, ni kuliamini Neno la Mungu, na kulichukua kama lilivyo.

Sasa je, ina maana kwamba huwezi kabisa kufanya dhambi yoyote kabisa kuanzia pale ulipookoka?  Na kama je, ukifanya dhambi moja baada ya kuokoka, ndiyo wokovu wako umeishia hapo?  Ni muhimu sana kufahamu majibu ya maswali haya au siyo ni rahisi kudanganywa na shetani na kujikuta tumeacha wokovu.  Mara tunapookoka halafu tukajikuta tumekasirika au tumesema uongo n.k., Shetani upesi hutudanganya na kutuambia, “Wewe bado hujaokoka.  Kama umeokoka mbona asubuhi hii umekasirika na kufanya jambo baya?”   Inakupasa kuwa na maarifa haya muhimu ili tusiangamizwe (HOSEA 4:6).

Ni kweli, ni mapenzi ya Mungu kabisa kwamba baada ya kuokoka tusitende dhambi tena.  Hata hivyo tunapokuwa bado watoto wachanga kiroho,  bado tunaweza tukajikuta tunafanya dhambi hapa na pale.  La msingi ni kwamba, mara unapojikuta umetenda dhambi, unatakiwa utubu mara  moja kwa nia ya kuacha dhambi hiyo na utasamehewa palepale, na wokovu wako unaendelea nao.  Biblia inasema katika 1 YOHANA 2:1-2 , ”Watoto wangu wadogo nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote”.  Hata hivyo, mtu aliyeokoka hawezi kutenda dhambi kwa makusudi, yaani anajua kwamba kufanya hili ni dhambi, halafu yeye analifanya kwa kusudi kabisa eti atatubu!  Mtu anayetenda dhambi kwa kukusudia hivyo, huyo bado hajaokoka maana kufanya hivyo, Biblia inasema ni kumtukana Mungu (HESABU 15:30-31).  Mtu aliyeokoka anaweza kujikuta amefanya dhambi bila kukusudia na hilo litamkosesha amani sana, na vilevile anaweza kufanya dhambi fulani kwa sababu ni mtoto mchanga kiroho, hivyo hajajua sana neno la haki; yaani hajajifunza sana Neno la Mungu, na kuyafahamu mapenzi ya Mungu kuhusu jambo hilo (WAEBRANIA 5:12-13).

              Baada ya kupata maarifa haya, sasa tupige hatua zaidi katika mafundisho yetu.  Baada ya kuwa umeokoka sasa, hupaswi kuona haya au aibu kuwaambia ndugu na marafiki zako kwamba umeokoka.  Ukiona haya, Yesu Kristo atakuonea haya katika utukufu wa Baba yake (MARKO 8:38), yaani hatakubali uingie mbinguni.  Mtu anayemuonea haya mtu mwingine anakuwa kama hamjui kabisa, na anakuwa hataki hata kumtazama, ili asije kushawishika kumwonyesha upendo au huruma.

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

                        Mtu aliyeokoka hawezi kutenda dhambi kwa kukusudia     

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Vivyo hivyo, sisi nasi kama tunaona haya kuwaeleza watu wengine kwamba tumeokoka, siku ya mwisho Yesu atakuwa kama hatujui kabisa.  Tukumbuke kwamba tunapookoka na kuwahi kuwaeleza watu wanaotufahamu kwamba tumeokoka, hilo linatupunguzia hatari ya kuvutwa dhambini.  Mapema kabisa, mwanzoni tu mwa mazungumzo yetu, na marafiki wa kiume au wa kike wa zamani katika uasherati na uzinzi, ulevi, dansi, ushirikina n.k.; hatuna budi kusema, “Je unajua, mimi nimeokoka, hivyo siwezi tena kufanya mambo yale ya kale tuliyokuwa tunayafanya pamoja”.

Vilevile hatuna budi kuvunja urafiki wa  pete na kidole na watu wale tulikuwa tunafanya dhambi pamoja, maana kama tutaambatana nao kwa karibu sana, kama mwanzo; wataturudisha tena dhambini.  Ni vema sasa kuwa na urafiki wa pete na kidole na wenzetu waliokoka (ZABARI 119:63;  MITHALI 22:24-25).  Hata hivyo hatupaswi kuwachukia au kuwadharau, bali tunapaswa kuwapenda, kuwaombea na kuwaalika kusikia mahubiri, ili wao nao waokoke kama sisi.  Bado tutashirikiana nao vizuri ofisini n.k.  Ila, wale tulikuwa tunafanya nao uasherati au uzinzi, tujiepushe nao kabisa maana ni rahisi sana kurudia uchafu wa mwanzo.

Ni muhimu pia kukumbuka kwamba tukiwaambia ndugu na marafiki kwamba tumeokoka, upesi watasema kwamba tumepotea.  Tusijali maneno hayo. Hawajui walisemalo.  Kabla ya kuokoka, ndiyo tulikuwa tumepotea, lakini sasa tumepatikana, maana Yesu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichokuwa kimepotea (LUKA 19:10).  Furaha  na shangwe zilifanyika baada ya mwana mpotevu kurudi kwa babaye, na inatajwa kwamba alikuwa amepotea, lakini sasa ameonekana (LUKA 15:32).  Hivyo waliopotea yaani wana wapotevu ni watu ambao hawajaokoka, siyo sisi tuliookoka!

Tuendelee tena sasa.  Ni muhimu tena wakati huu wa mapema, baada ya kuokoka, kufahamu jinsi ya kuukulia wokovu.  Maneno mengine yanayotumika badala ya kuokoka, ni kuzaliwa mara ya pili (YOHANA 3:3).  Hivyo kwa maneno mengine, umezaliwa mara ya pili, kwa Roho.  Ulizaliwa mara ya kwanza, pale ulipozaliwa kwa njia ya kawaida ya kimwili.  Wakati huo ulizaliwa kwa mwili, lakini sasa umezaliwa kwa Roho, kama Yesu alivyozaliwa, kutokana na mimba iliyopatikana kwa uwezo wa Roho Mtakatifu (YOHANA 3:6-7;  MATHAYO 1:20-21).  Wewe sasa ni mtoto mchanga wa kiroho.  Sasa basi, hebu tafakari jambo hili.  Je mtoto mchanga anapozaliwa katika hali ya kawaida ya kimwili,

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

                          Mtoto mchanga anapozaliwa ataishi bila kunyonya

                                                                maziwa?                                                      . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

anaweza kuendelea kuishi bila kunyonya maziwa?  Jibu ni kwamba atakufa baada ya muda mfupi kwa sababu ya kukosa chakula.  Vivyo hivyo hakuna mtoto mchanga wa kiroho anayeweza kuendelea katika wokovu kama hapati maziwa  yasiyoghoshiwa yaani yasiyochanganywa na maji.  Tunasoma katika 1 PETRO 2:2, “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu”. Maziwa haya yasiyoghoshiwa ni nini?  Ni mafundisho ya Neno la Mungu yanayofundishwa kwa kuzingatia Biblia inavyosema, bila kuchanganya na taratibu tu za kibinadamu.  Neno la Mungu ni chakula cha roho zetu (MATHAYO 4:4;  KUMBUKUMBU LA TORATI 8:3;  YEREMIA 15:16).

Baada ya kuokoka, haikupasi kuzungukazunguka huko na huko kwenye mahubiri yanayozungumzia tu kutubu dhambi na kuokoka.  Hayo pamoja ni jinsi yalivyo mazuri, umekwisha yasikia, na tayari umekwisha okoka.  Unachokihitaji sasa ni mafundisho ya kina ya neno la Mungu ya kukuwezesha kufahamu yanayokupasa kufanya na yale yasiyokupasa kufanya, na hatimaye wewe nawe uwe mwalimu wa wengine (MITHALI 12:1;  HOSEA 4:6;  MAMBO YA WALAWI 5:17;  MATHAYO 22:29;  WAEBRANIA 5:11-14).  Kabla ya kuokoka, tulikuwa katika mafundisho manyonge yenye upungufu, ndiyo maana hayakutufanya tuokoke.  Baada ya kuokoka, Neno la Mungu linatuonya kutoyarejea mafundisho hayo manyonge, kama tunataka kuukulia wokovu.  Tuwe tayari hata kuwaacha ndugu zetu huko na kutafuta kanisa lenye watu wenye imani moja na sisi yaani waliokoka kama sisi, ambapo mafundisho yote ni ya wokovu (Soma WAGALATIA 4:9;  HOSEA 4:17;  2 PETRO 1:1).  Vilevile, kama tunataka kuukulia wokovu, tusitosheke na ibada moja tu ya Jumapili kwa wiki, au kwa mwezi.  Miili yetu inakula mara mbili au tatu kwa siku.  Roho zetu ni za thamani zaidi, hivyo hatuna budi kuhudhuria ibada zote za kanisa kwa gharama yoyote, ili tuukulie wokovu, hata kama kanisa tuliloliona linatufaa, liko mbali kiasi gani! (Soma MATHAYO 12:42;  MITHALI 2:3-5;  AYUBU 23:12;  ZABURI 119:72).

Tukiwa ukingoni sasa mwa somo letu, hatuna budi pia kufahamu juu ya shetani.  Neno  “Shetani”, kwa lugha ya asili, maana yake Adui, Mshindani, Mpinzani, na pia Yeye aletaye vizuizi kwa watu wa Mungu au watu waliokoka katika hali ya uadui kabisa, ili ikiwezekana, waiache njia ya kweli ya wokovu  ya kumfikisha mtu mbinguni.  Shetani atatumia mawazo yako mwenyewe, ndugu zako wa kimwili, na hata watu wengine waliokoka wasio wakamilifu, kukuvunja moyo na kukukatisha tamaa kuendelea na kweli yote ya wokovu uliyoipokea.  Utashangaa siku ya ibada ndiyo magonjwa yanaanza, ndiyo wageni wanakuja kukutembelea n.k., ujue vyote hivyo ni vizuizi vya Shetani, mpinge kwa kutokuruhusu lolote lile kukutoa katika ibada (YAKOBO 4:7).  Mateso na maudhi mbalimbali kwa mume, wazazi, ndugu n.k; yanaweza kuja kwako baada ya kuokoka.  Hii si ajabu, ni kazi za upinzani za shetani.  Yalimpata Yesu.  Wewe songa mbele tu bila kujali yatakayokupata (WAFILIPI 1:29-30;  1 WATHESALONIKE 3:3;  1 PETRO 3:14;  MATHAYO 5:1-12;   YOHANA 5:16;  YOHANA 7:19-20;  YOHANA 8:48;  YOHANA 15:24-25;  MARKO 3:21;  2 TIMOTHEO 3:12;  WAGALATIA 4:29;  1 PETRO 4:12-16).  Kwa vyovyote vile, usigeuke nyuma na kuacha wokovu.  Vipige vita vizuri vya imani, imani uilinde (WAEBRANIA 3:14;  2 PETRO 2:20-22;  2 TIMOTHEO 4:7).  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook, Twitter, n.k,  kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “note” hii, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.

     UBARIKIWE NA BWANA YESU!!!

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s