KUONGOZWA NA NENO LA MUNGU

ZACHARY KAKOBE

Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SOMO:   KUONGOZWA NA NENO LA MUNGU

Maisha ya milele ya kila mmoja wetu, yatategemeana  sana na jinsi tutakavyoishi kila siku hapa duniani, baada ya kujifunza somo hili “KUONGOZWA NA NENO LA MUNGU”.Ikiwa kuanzia  leo tutaishi sawasawa na somo hili, maisha ya milele yatakuwa katika mbingu mpya na nchi mpya, Yerusalemu mpya, mahali ambapo hakuna maombolezo, kilio, wala maumivu, bali ni furaha tu daima. Tukiishi duniani pasipo kuzingatia mafundisho ya somo hili, basi maisha yetu ya milele yatajaa mateso na huzuni kuu katika ziwa la moto liwakalo moto na kiberiti. Bwana ampe kila mmoja neema ya kuishi sawasawa na mafundisho haya katika jina la Yesu. Tutajifunza somo hili kwa kuligawa katika vipengele vine:-

       ( 1 ).  KUONGOZWA NA NENO LA MUNGU

       ( 2 ).  MADHARA YA KUONGOZWA NA MAMBO MENGINE

       ( 3 ).  NENO LA MUNGU, MAMLAKA YA MWISHO

       ( 4 )   JINSI YA KUFANYA KIVITENDO ILI TUINGIE     MBINGUNI

( 1 ). KUONGOZWA NA NENO LA MUNGU.

Watu wote tunapenda sana kuishi maisha ya raha peponi au mbinguni na hakuna apendaye kwenda motoni milele. Ndugu, marafiki au jamaa zetu wakifa, wengine huandika magazeti wakisema, “Mungu muweke Fulani mahali pema peponi”. Hata hivyo, hatuna budi kufahamu kwamba tunaweza kuingia mbinguni, ikiwa tutakuwa tayari kuongozwa na neon la Mungu katika maisha yetu na siyo vinginevyo. Tukiongozwa na Neno la Mungu katika kila jambo tunalolifanya duniani, iwe ni kutafuta kazi ya kufanya, kufanya biashara zetu, kuishi na majirani au ndugu n.k., ndipo tunapoweza kumwona Mungu. Maandiko yanaeleza waziwazi jambo hili kwa kulifananisha Neoi la Mungu na:-

  1. TAA AU MWANGA (ZABURI 119:105)

Njia ya kuingia mbinguni, ni nyembamba sana, imesonga (MATHAYO 7:14), na pia wanadamu wenye dhambi, tumezungukwa na giza (AYUBU 10:22, 1YOHANA 2:11). Hatuwezi kamwe kuiona njia nyembamba iendayo mbinguni, bila kuongozwa na taa au mwanga. Taa au mwanga huu, ni Neno la Mungu. Wana wa Israeli katika safari yao kwenda Kanaani waliongozwa na nguzo ya moto usiku (KUTOKA 13:21). Neno la Mungu leo, ndiyo nguzo hii ya moto ya kutuangazia, tupate kuiona njia ya kwenda Kaanani yaani mbinguni. Mamajusi, waliongozwa na nyota iliyowatangulia, wakaifuata hadi pale alipokuwapo mtoto Yesu (MATHAYO 2:9). Sisi nasi tunahitaji kuongozwa na nyota au mwanga, yaani Neno la Mungu. Neno hili la Mungu  ndilo litakalotuongoza mpaka pale alipo Yesu yaani mbinguni. Pasipo kuongozwa na Neno la Mungu, kwa msingi huu, hatuwezi kamwe kuingia mbinguni.

2.RAMANI AU DIRA.

Wanadamu hapa duniani, ni wpitaji na wasafiri, hapa hatuna makao ya kudumu    (1 NYAKATI  29:15, ZABURI 39:12; WAEBRANIA 11:13 1 PETRO 2:11). Msafiri yeyote anayekwenda mahali asipopajua, sharti awe na ramani au dira ya kumwongoza aendako, au siyo ni rahisi sana kupotea na kwenda mbali kwingineko. Dira hutumiwa na wasafiri wa jangwani na baharini, kuongozwa waendako, au siyo ni rahisi sana kupotea na kwenda mbali kwingineko. Watalii sharti wawe na ramani ya kuwaongoza waendako. Vivyo hivyo, sisi kama wasafiri  jangwani tukitaka kufika kanaani,  tunahitaji kuwa na dira au ramani. Dira hii au ramani yetu, ni Neno la Mungu. Neno la Mungu, ndiyo dira au ramani ya kutuongoza hadi kutufikisha mbinguni. Mtu anayeishi maisha yasiyoongozwa na Neno la Mungu, huyu ni msafiri asiyekuwa na  dira au ramani. Kwa hakika mtu huyu anakwenda UPOTEVUNI. Hawezi kufika mbinguni.

  1. 3.      NJIA

Neno la Mungu, linaitwa pia NJIA YA BWANA (MATENDO18;24-26). Yesu Kristo anaitwa  Neno la Mungu (UFUNUO 19:13), Yesu Kristo pia ni Neno anayetajwa katika YOHANA 1:1. Yesu aliye Neno anasema yeye ni NJIA na kwamba mtu hawezi kufika kwa Baba yaani mbinguni isipokuwa kwa njia yake (YOHANA 14:6) Hivyo basi tunaona kwamba Neno la Mungu ndiyo njia  ya kutufikisha mbinguni. Tukikengeuka na kuiacha Njia hii ya Bwana na kwenda kusho au kulia, yaani kuacha kuongozwa na Neno la Mungu,basi tujue tayari tumeiacha Njia ya kwenda uzimani.

  1. ALAMA ZA BARABARANI.

Alama za  barabarani, ni maonyo yanayotufanya wasafiri tuepuke ajali au mauti. Mapema  kabisa, alama hizi hutuongoza au kutuelekeza kwamba  kuna kona kali au mtelemko mkali mbele . Alama hizi huweza tena kutuashiria  kwamba kuna daraja bovu mbele n.k. Tukikubali kuongozwa na alama hizi, ndipo tutakapoepuka mauti, lakini sisi kama wasafiri,  tukipuuza maonyo haya, tunajipeleka wenyewe katika mauti. Sasa basi Neno la Mungu ni maonyo ya jinsi hii(1 WAKORINTHO 10:5-11), Tukikubali kuongozwa na maonyo haya, ndipo tunapoepuka mauti ya milele au kwenda Jehanum. Kufanya uzinzi au uasherati, kusema uongo, kusengenya,  kuiba, kunywa pombe,  au kuvuta sigara n.k, …ni kusafiri  kwenye daraja bovu au kusafiri kwenye mtelemko mkali bila breki. Ni kutafuta mauti, naam mauti ya milele.

  1. MKONO WA BWANA WA KUTUONGOZA.

Kipofu anahitaji mtu mwenye macho mazima kumwongoza. Kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, anatafuta madhara (MATHAYO 15:14). Wanadamu tusiofanya mapenzi ya Mungu, tunafananishwa na vipofu mbele za Mungu (YOHANA 9:39-41). Kila mmoja wetu kwa namna moja au nyingine, hajui neno lolote  bado kama impasavyo kujua (1 WAKORINTHO  8;2). Hivyo kila mmoja wetu ana upofu wa  namna mota au nyingine. Tunahitaji mtu mwenye macho mazima anayejua mapenzi yote ya Mungu. Kutushika mkono na kutuongoza, na siyo kipofu mwenzetu. Mtu huyu wa kutuongoza ndiye Neno la Mungu. Tukiongozwa na kitu kingine chochote kile ni sawa na kuongozwa na kipofu. Neni la Mungu ndiyo mkono wa Bwana wa kutuongoza na kutufikisha katika uzima.

( 2 ).  MADHARA YA KUONGOZWA NA KITU KINGINE.

Kama tulivyokwisha kuona, kuongozwa na jambo lolote lile mbali na Neno la Mungu, ni sawa na kusafiri bila dira au ramani, kuongozwa na kipofu, kupuuza alama za barabarani, kutembea gizani  bila mwanga. Ni kuiacha njia. Kwasababu hii hatuna budi kuwa na tahadhari, na kukataa kuongozwa na lolote lile jingine, maana litatuletea madhara. Kwa msingi huo hatupaswi kuogozwa na mapokeo ya wanadamu yaani miongozo ya kidini ambayo haiendani na Neno la Mungu. Kufanya hivyo ni kuwa mbali na Mungu na kumuabudu bure, yaani  bila faida yoyote. Lolote lile tunalolifanya halina budi kulingana na yanenavyo maandiko (1 WAKORINTHO 15:3-4). Hatupaswi kufuata jambo kwasababu tumefundishwa katika dini zetu tangu kuzaliwa. Katika kila jambo tuzingatie kuongozwa na Neno la Mungu, iwe ni namna ya kubatizwa, kazi ya kufanya iliyo mapenzi ya Mungu, namna ya kuishi na mume au mke au lolote lile jingine. Hatupaswi pia kuongozwa na mila na desturi tu, bali katika kila jambo tuongozwe na Neno la Mungu,.kinyume cha hapo hatuwezi kuiona mbingu.

( 3 ).  NENO LA MUNGU, MAMLAKA YA MWISHO KWA MKRISTO.

Katika nchi, kisheria, katiba inaitwa sheria mama, Katika nchi, ni mamlaka ya juu zaidi naya mwisho kwa raia wote wa nchi. Nchi nzima wakati wote sharti iongozwe na katiba. Kwa mfano huu, kwetu wakristo, katika mambo ya ufalme wa Mungu Neno la Mungu ndilo sheria mama. Ni mamlaka ya juu zaidi naya mwisho kwa kila mkristo au yeyote  anayetaka kufanya mapenzi ya Mungu. Neno la Mungu ni mamlaka ya juu zaidi kuliko katiba za makanisa za kibinadamu au maelekezo ya kibinadamu yanayotokana na vikao vya viongozi wa dini walioko Ulaya au waliopo hapa nchini Tanzania. Siku ya mwisho tutahukumiwa sawasawa na Neno la Mungu na siyo maneno yoyote mengine (WARUMI 2;16). Hivyo Neno la Mungu ndiyo sheria mama katika mabo yote ya ufalme wa Mungu. Hukumu yote ya wanadamu wote itatolewa kwa  kuzingatia Neno la Mungu. Linasemaje.

( 4 ).   JINSI YA KUFANYA KIVITENDO ILI TUINGIE MBINGUNI.

  1. 1.             Kuhudhuria kila siku ya ibada, tukiwa na kiu ya  kusikia Neno la Mungu linalotuongoza kufanya nini. Kusoma Biblia zetu na “notes” za  mafundisho tunayoyapata kanisani. Kusikia kaseti au CD za Neno la Mungu. Hatuna budi kulipenda sana Neno la Mungu kuliko riziki yoyote au chakula. (ZABURI 119:11, AYUBU 23:12). Tunapaswa kuhudhuria ibada zote bila kukosa ili tusipitwe na mafundisho ya Neno la Mungu.
  2. 2.             Bila majadiliano, hatuna budi kulifuata Neno la Mungu linasemaje na kulitendea kazi mara moja na kupuuza maneno yoyote mengine iwe ya wazazi, ya kimila na desturi, ya kidini n.k, yaliyokinyume na Neno la Mungu (ZABURI 119:9). Neno la Mungu likisema tuache hili au lile na kufanya hili au lile, basi mra moja tunalitendea kazi mara moja bila kujali gharama (MARKO 9:43-48). Hii ndiyo njia ya kuingia mbinguni. Vinginevyo tutakuwa tunajidanganya, na juhudi zetu nyinginezo ni juhudi za kidini zisizo na maana! Bwana ampe kila mmoja wetu utayari wa kuongozwa na Neno la Mungu katika Jina ja Yesu.

                     NENO LAKO  NDIYO TAA YA MIGUU YANGU

                                NA MWANGA WA NJIA YANGU

                                             ZABURI 119:105

Advertisements

4 comments on “KUONGOZWA NA NENO LA MUNGU

  1. Kweli kama yasemavyo maandiko neno la mungu ni taa.MUNGU AKUONGOZE MTUMISHI,NA AKUPE MAISHA MAREFU YA AMAN NDANI YA KRISTO.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s