NENO LA KUAMINIWA

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

 

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA.

SOMO:         NENO LA KUAMINIWA

L

 eo tena tunaendelea kujifunza Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu.  Leo, tunajifunza YOHANA 3:14-23.  Katika mistari hii, tunajifunza mambo mengi, ingawa somo letu ni“NENO LA KUAMINIWA”.  Tutayagawa mafundisho yote tunayoyapata katika mistari hii, katika vipengele vitano:

(1)NENO LA KUAMINIWA (Mst. 14-17);

(2)HUKUMU KWA KILA MTU ASIYEMWAMINI MWANA WA MUNGU (Mst. 18);

(3)ALAMA KUU YA MTU MWOVU (Mst. 19-21);

(4)KUBATIZA KWA YESU (Mst. 22);

(5)UMUHIMU WA MAJI TELE KATIKA UBATIZO (Mst. 23).

(1)      NENO LA KUAMINIWA (Mst. 14-17)

Katika mistari hii, ndipo tunapojifunza, “Neno la Kuaminiwa, tena linalostahili kukubalika kabisa“, linalotajwa na Mtume Paulo katika 1 TIMOTHEO 1:15.  Mistari hii (Mst. 14-17), ndicho KITOVU cha INJILI.  Kila mtu aliyeokoka, inampasa kuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu mistari hii ili aweze kuishiriki Injili pamoja na wengine.  “KWA MAANA JINSI HII Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe pekee ili kila mtu amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele“ (Mst. 16), ni mstari maarufu na moyo wa Injili.  “KWA MAANA JINSI HII“, inazungumzia JINSI IPI?  Ni jinsi Wana wa Israeli waliokuwa katika kufa, walivyopona, pale walipoamini na kumtazama nyoka wa shaba aliyekuwa ameinuliwa na Musa (Mst. 14-15; HESABU 21:6-9).  Kuna mambo mengi tunayojifunza, tunapolichambua kwa makini NENO LA KUAMINIWA.

1.         Watu wote wenye dhambi ni WAFU, ingawa wanaonekana kuwa ni hai.  Mtu yeyote aliyekufa hawezi kujigeuza, wala kufanya chochote anachopenda.  Maiti hawezi kujizuia kuwekwa katika jeneza au kuzikwa kaburini.  Vivyo hivyo, mtu yeyote mwenye dhambi hawezi kujizuia nafsi yake kunywa pombe, kufanya uasherati, kuvuta sigara, au kufanya dhambi yoyote (WAEFESO 2:1; 1 TIMOTHEO 5:6).  Yesu Kristo, alikuja kwetu ulimwenguni kufanya yafuatayo:

a)     Kama watu tulioko katika kifo kwa jinsi moja na wana wa Israeli waliokuwa wameumwa na nyoka za moto.  Yesu alikuja kutuokoa kwa kutuponya pale tunapomwamini na kumtazama:-

(i)                Mshahara wa dhambi au matokeo ya dhambi ni maumivu ya nyoka mkali mwenye sumu (MITHALI 23:31-32).  Shetani ni Nyoka wa zamani (UFUNUO 12:9), ndiye nyoka aliyemwijia Hawa na kumdanganya.  Majaribu ya Shetani ni mishale ya moto (WAEFESO 6:16).  Hivyo Shetani ni NYOKA WA MOTO.  Nyoka huyu wa moto amemuuma kila mtu mwenye dhambi na yuko katika kufa;

(ii)              Nyoka wa Shaba, ndiye aliyewaponya Waisraeli waliokuwa wameumwa na nyoka za moto.   Biblia inaitaja miguu ya mtu mfano wa Mwanadamu ambaye ni Yesu kuwa kama Shaba iliyosuguliwa  sana (UFUNUO 1:15).  Mtu mfano wa Mwanadamu aliaminiwa kuwa Masihi na Waisraeli kutokkana na DANIELI 7:13-14.  Huyu Yesu ndiye Mwana wa Adamu au Nyoka wa Shaba.  Kwa nini Nyoka wa Shaba?  Nyoka wa Shaba hakuwa na sumu kama nyoka za moto.  Yesu alifanyika dhambi kwa ajili yetu ingawa yeye hakuwa na dhambi.  Nyoka alikuwa melaaniwa (MWANZO 3:14).  Yesu naye alifanyika laana kwa ajili yetu pale alipotundikwa msalabani (WAGALATIA 3:13; TORATI 21:22-23).  Kifo cha Yesu msalabani kinaitwa KUINULIWA JUU YA NCHI (YOHANA 12:32-33).  Yesu alipoinuliwa, ilikusudiwa iwe dawa kwa wanadamu wote walioumwa na nyoka za moto.  Dawa ya sumu ya nyoka za moto, ilitoka kwa Mungu mwenyewe.  Wokovu wetu unatoka kwake tu, siyo kwa matendo yetu ya sheria.

(iii)            Tunaokolewa au kupata uzima kwa kumwamini Yesu.  Wana wa Israeli WALIOAMINI kwamba kumwangalia Nyoka wa Sahab kwa imani tu kutawaponya, waliponywa.  Wale waliopuuza na kusema hawawezi kupona kwa njia rahisi hivyo, walikufa.  Vivyo hivyo Yesu kama Nyoka wa Shaba, anasema NIANGALIENI MIMI MKAOKOLEWE (ISAYA 45:22).  Ni imani tu katika Yeye inayotupa WOKOVU.  Njia nyingine zote, haziwezi kutusaidia, zitatufanya tupate mauti ya milele badala ya uzima wa milele.  Kila mtu amwaminiye hatapotea.

(iv)            Kila mtu aaminiye atapata uzima wa milele.  Wana wa Israeli walipoumwa na nyoka za moto, walikuwa karibu kabisa kuingia Kanaani.  Mtu alipoamini na kumwangalia nyoka wa Shaba, alipona na kuingia Kanaani, kwenye raha iliyoahidiwa.  Vivyo hivyo yeyote anayemwamini Yesu, anapata uzima wa milele na kuingia mbinguni.

b)     Yesu Kristo alikuja kutuokoa kwa kuja kututangazia msamaha wa adhabu ya kifo.  Tulikuwa kifungoni tukiwa tunangoja mauti kama Baraba, akaja kututangazia kufunguliwa (LUKA 4:18).  Hakuja kutuhukumu bali kutupa msamaha.

(i)                Mungu aliupenda ulimwengu, alitupenda sisi upeo kwa kumleta Yesu kutupa msamaha.  Hakufanya hivyo kwa malaika walioasi;

(ii)              Aliupenda ULIMWENGU, siyo Waisraeli peke yao bali ni wote pamoja na Watanzania au Mataifa.

(iii)            Mungu alimtoa Yesu kuuawa msalabani kwa hiari yake na kwa kusudi lake mwenyewe (MATENDO 2:23).  Ndiyo maana Yesu alitabiri na kufundisha KABLA kwamba atakufa kwa kifo cha msalaba na kufufuka.

(iv)            Yesu, hakuja kuuhukumu ulimwengu ingawa tulistahili hukumu na yeye ni Hakimu (YOHANA 5:22).  Ni Hakimu wa Ajabu tofauti na mahakimu wa ulimwengu!  Tukisema “Hatuna hatia“, ndipo tunapopata hukumu, tukikiri tuna hatia na kuhitaji msamaha, tunapata msamaha (YEREMIA 2:35).

2.         Wokovu ni kwa kila mtu amwaminiye hata kama ana dhambi kiasi gani.  Yeyote anayekuja kwake kwa toba hatatupwa nje kamwe (YOHANA 6:37).  Kazi yetu ni kumwamini Yesu kwamba ana uwezo wote wa kutuokoa kama Nyoka wa Shaba.  Ni makosa kusema Yesu nisaidie kuacha hasira, pombe, sigara au dhambi yoyote tukiwa tunawaza kwamba na sisi tuna sehemu yoyote ya kufanya!  Yote yaliyo ya dhambi tunampa yeye, YEYE anatuokoa, kwa kuzichukua dhambi zetu na kuziondoa.

 

(2)      HUKUMU KWA KILA MTU ASIYEMWAMINI MWANA WA MUNGU (Mst. 16) 

Maandiko yananena wazi kwamba yeyote asiyemwamini Mwana wa Mungu, Yesu Kristo, hukumu na ghadhabu ya Mungu inamkalia.  Hawezi kuingia mbinguni (YOHANA 3:18, 36; 1 YOHANA 5:4-5, 11-13; 4:15; 2:23).  Kumwamini Yesu ni lazima kuambatane na kufuata maneno yake Yesu.  Mtu anayesema “Ninamwamini Yesu“ huku hafuati maneno yake, ni mwaongo na hukumu inamkalia (YOHANA 12:48).

(3)      ALAMA KUU YA MTU MWOVU (Mst. 22)

Alama kuu ya mtu mwovu, ni kuchukia nuru.  Nuru ni Neno la Mungu (ZABURI 119:105).  Mtu yeyote ambaye halipendi Neno la Mungu na kulifurahia na kutaka limwongoze, hata kama havuti sigara, hanywi pombe n.k; huyu ni MTU MWOVU mbele za Mungu, na ghadhabu ya Mungu inamkalia.  Hajazaliwa mara ya pili.  Mtoto aliyezaliwa katika hali ya asili, hutamani maziwa ya mama na kuyalilia wakati wote.  Vivyo hivyo, mtu aliyeokoka yaani mtoto wa Mungu, hutamani na kuyalilia maziwa ya Mungu wakati wote (1 PETRO 2:2).

(4)      KUBATIZA KWA YESU (Mst. 22)

Yesu anatajwa kwamba alishinda huko pamoja na wanafunzi wake, AKABATIZA.  Hata  hivyo, inaelezwa tena kwamba Yesu mwenyewe hakubatiza, bali wanafunzi wake (YOHANA 4:2).  Mahali hapa tunajifunza kwamba yale waliyokuwa wanayafanya wanafunzi waliotumwa na Yesu, yalihesabiwa kuwa yamefanywa na Yesu.  Ndivyo ilivyo hata leo.  Lolote analolifanya kwetu Mtumishi wa Mungu, ni Yesu amelifanya.  Maneno ya Mtumishi wa Mungu, ni maneno ya Yesu, hatuwezi kuyatenganisha.  Mtu akiwa mbishi, mkaidi na kuyakataa maneno ya Mtumishi wa Mungu, anakuwa anamkataa Yesu (LUKA 10:16; MATHAYO 10:40;

1 WATHESALONIKE 2:13).  Tukija ibadani, na kulisikia Neno kutoka kwa Mtumishi wa Mungu, tujue ni Mungu anayesema nasi, siyo mwanadamu.  Watu wengine kwa kukosa kujua haya, husema “Mchungaji leo amenisema na kunikemea na kunikaripia mbele ya watu“.  Siyo Mchungaji, ni Yesu mwenyewe.

(5)      UMUHIMU WA MAJI TELE KATIKA UBATIZO (Mst. 23)

Ubatizo wa Ki-Biblia ni lazima uwe wa maji tele.  Yohana hakutafut mto au Yordani bali maji tele.  Maji tele katika ubatizo yanatufanya tuzikwe na kufufuka pamoja na Yesu (WAKOLOSAI 2:12).  Ubatizo wa kunyunyiziwa maji usoni siyo Ubatizo wa Ki-Biblia.  Tunapokata shauri kuacha dhambi na kuokolewa, ndipo tunapokuwa tumenyunyiziwa damu ya Yesu ya kutusafisha dhambi (1 PETRO 1:2)

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

           Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s