AGIZO LA KUTAWADHANA

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

 

SOMO:  AGIZO LA KUTAWADHANA

L

eo, katika Siku hii ya Kuichambua Biblia, tunaendelea tena kujifunza Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu.  Leo tunajifunza na kutafakari kwa makini YOHANA 12:37-50 na YOHANA 13:1-5.  Katika mistari hii, pamoja na mambo mengine, tutajifunza juu ya “AGIZO LA KUTAWADHANA“.  Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika mistari hii, katika vipengele vinane:-

 

(1) UWEZEKANO WA KUTOKUSADIKI BAADA YA KUONA MIUJIZA (12:37-41);

(2) ALAMA KUU YA KUKISUJUDIA NA KUJIABUDU KIUMBE BADALA YA MUNGU (12:42-43);

(3) MAHUBIRI YA MWISHO KWA WAYAHUDI WASIOAMINI (12:44-50);

(4) UPENDO WA YESU KWA WATU WAKE (13:1);

(5) UWEZEKANO WA SHETANI KUTUTIA MOYO WA KUMSALITI YETU (13:2);

(6) YESU ALITOKA KWA MUNGU (13:3);

(7) NIFANYALO WEWE HUJUI SASA LAKINI UTALIFAHAMU BAADAYE (13:7);

(8) AGIZO LA KUTAWADHANA (13:4-15).

 

(1)                                                                 UWEZEKANO WA KUTOKUSADIKI BAADA YA KUONA MIUJIZA (12:37-41)

Yesu Kristo, alifanya ishara au miujiza mikubwa kwa Wayahudi, lakini hata hivyo, wengi hawakumwamini kwamba yeye ndiye Masihi.  Wayahudi waliwaza toka mioyoni mwao kwamba Neno jema haliwezi kutoka Nazareti (YOHANA 1:46) na tena kutoka Galilaya jimbo alilotokea Yesu, hakuwezi kutokea nabii (YOHANA 7:47-52).  Hawakutaka kabisa kukbadili msimamo wao huo.  Lolote waliloliona au kulisikia kwa Yesu, walilipima kwa msimamo wao huo.  Hata miujiza aliyoifanya Yesu, waliipima kwa mtazamo au msimamo wao huo, na kuona kwamba anafanya miujiza na kutoa pepo kwa Beelzebuli mkuu wa pepo (MATHAYO 12:24).  Kutokana na kuendelea na mtazamo wao huo Mungu hakuwafunulia lolote bali aliwapofusha macho na kuifanya mioyo yao mizito ili wasiongoke au kubadilishwa na kuponywa, na Isaya aliyaona hayo mapema katika utabiri wake.  Hata leo ni vivyo hivyo.  Tukiwa hatuko tayari kubadili msimamo au mtazamo wetu juu ya Kanisa fulani, mafundisho fulani, hata tuone Mhubiri wa Kanisa hilo anatumiwa namna gani, hatuwezi kuamini.  Hatari yake ni kwamba Mungu hawezi kutufunulia lolote kwa sababu hatuko tayari kubadili mtazamo wetu.  Hatuna budi kuwa na utayari wa kubadili mitazamo yetu tunaposhuhudiwa vilivyo na Roho Mtakatifu, hata kama tutadharaulika kwa kufanya hivyo.  Tukifanya hivyo tuna heri.

 

(2)                                                                ALAMA KUU YA KUKISUJUDIA NA KUKIABUDU KIUMBE BADALA YA          

MUUMBA (12:42-43)

Kupenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu, maana yake, kukisujudia na kukiabudu kiumbe badala ya Muumba (WARUMI 1:25).  Tukiwa tumeifahamu Kweli ya Neno la Mungu, halafu tukaibadili kweli hiyo kuwa uongo, kwa kuogopa kutengwa na masinagogi au madhehebu yetu, viongozi wetu wa dini, waume zetu, wazazi na ndugu zetu n.k., kwa kufanya hivyo, tunakuwa tunawasujudia na kuwaabudu viumbe badala ya Muumba.  Wengi wetu tunafanya hivi pasipo kujua.  Tutaifahamu Kweli fulani kwa mfano Ubatizo wa Maji tele baada ya kuokoka n.k., lakini tukiona kuitekeleza kweli hiyo kutatufanya tutengwe na masinagogi au makanisa yetu, waume zetu n.k., tunachagua kuibadili kweli hiyo kuwa uongo, na hivyo kumwabudu kiumbe badala ya Muumba.  Hatupaswi kufanya hivyo.

(3)                                  MAHUBIRI YA MWISHO KWA WAYAHUDI WASIOAMINI (12:44-45)

Katika mistari hii tunaona mahubiri ya mwisho ya Yesu, kwa Wayahudi wasioamini.  Baada ya mahubiri haya, Yesu alihusika katika kuwafundisha na kuzungumza na wanafunzi wake tu.  Katika mahubiri haya, Yesu anazidi kusisitiza kwamba asiyemwamini Yesu anakaa GIZANI maana Yeye ndiye Nuru ya ulimwengu.  Asiyekubali maneno yake Yesu, Neno lake ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho.  Maagizo ya Mungu, ni uzima wa milele kwetu.  Tukipuuza agizo lolote la Mungu na kusema tutakwenda mbinguni tutakuwa tunajidanganya.

 

(4)                                  UPENDO WA YESU KWA WATU WAKE (13:1)

Saa ya Yesu kusalitiwa na kusulibishwa, ilikuwa imefika.  Baada ya mahubiri yake mwisho kwa Wayahudi wasioamini, alibaki tu na wanafunzi wake.  Wanafunzi wake hapa ndiyo wanaoitwa WATU WAKE YESU.  Anatupenda upeo!  Atawaacha wengine kando na kubaki na sisi!  Anajishughulisha sana na mambo yetu kama mama au baba anavyojishughulisha na watoto wake ambao ndiyo watu wake (1 PETRO 5:6-7; ZABURI 103:13).

 

(5)                                  UWEZEKANO WA SHETANI KUTIA  MOYO WA KUMSALITI YESU (13:2)

Shetani wakati wote hutafuta mtu wa kummeza (1 PETRO 5:8).  Haogopi kumjaribu mtu yeyote, awe ni Mtume, Nabii, Mwinjilisti, Mchungaji, Mwalimu, Mama Mchungaji, Kiongozi wa Zoni, Seksheni, Kiongozi wa Kanisa la Nyumbani au mtu yeyote.  Shetani alikuwa na ujasiri wa kumjaribu Yesu nyikani na kumtaka eti amsujudie!  Hapa tunaona akimtia moyo wa kumsaliti Yesu aliyekuwa Mtume Yuda.  Baadaye kidogo Mtume Petro naye aliyesema ijapompasa kufa hawezi kumkana Yesu, yeye naye alimkana mara tatu (MATHAYO 26:31-35, 69-75).  Hatupaswi kujivuna na kujisahau, na kujiona kwamba sisi hatuwezi kuanguka katika uasherati, uzinzi au dhambi yoyote na kuacha wokovu.  Tunaweza!  Tunalotakiwa kufanya, ni KUJILINDA na KUKESHA na KUOMBA tukiitumainia neema ya Mungu wakati wote (1 YOHANA 5:18; MATHAYO 26:41).  Kujilinda ni kuwa mbali na mtego wowote unaotunyemelea wa kutufanya tufanye uasherati au uzinzi au dhambi yoyote.

 

(6)                                  YESU ALITOKA KWA MUNGU (13:3)

Yesu hakuanzia tumboni kwa Bikira Mariamu kama wengine wanavyofikiri.  Alitoka kwa Mungu.  Alikuwa ni Mungu aliyedhihirishwa kwetu katika mwili ( 1 TIMOTHEO 3:16).  Bikira Mariamu alikuwa ni mama yake Yesu katika mwili.  Yesu alitoka kwa Mungu, ni Mungu, kisha akarudi mbinguni.  Hivyo Bikira Mariamu siyo mama yake Mungu.  Yeye mwenyewe anajiita majakazi (mtumwa wa kike) wa Bwana (LUKA 1:38).  Jua linapochomoza, siyo kwamba halikuwako kabla, ila lilikuwa linaonekana kwa wengine katika nchi nyingine.  Yesu, JUA LA HAKI; alipozaliwa na Mariamu, alikuwa NURU (Jua) iliyochomoza vivyo hivyo.

 

(7)                                  NIFANYALO WEWE HUJUI SASA LAKINI UTALIFAHAMU BAADAYE (13:7)

Kiongozi wetu, hupewa mafunuo ya mambo yajayo kala yetu tunaoongozwa, ili aweze kutuongoza katika njia vizuri.  Kwa msingi huu, wakati mwingine Kiongozi wetu wa Kanisa anaweza akatuambia tufanye mambo ambayo hatujayafahamu vizuri matokeo yake, maana yake n.k,   Hatuna budi kufanya mara moja na kutoka, bila kujua tuendako kama Ibrahimu (WAEBRANIA 11:8).  Hatimaye ndipo tutakapofahamu vizuri maana ya yale tuliyoambiwa kuyafanya na Kiongozi wetu aliyepewa mafunuo kabla yetu sisi.

 

(8)                                  AGIZO LA KUTAWADHANA (13:4-15)

Hapa tunaona Yesu akiwatawadha miguu wanafunzi wake na kutupa agizo la kutawadhana miguu sisi kwa sisi (13:14).  Watu wengine kwa kutumia maandiko haya, huleta makarai ya maji makanisani mwao na kutaka watu watawadhane miguu.  Hivi sivyo tunavyoaagizwa kufanya.  Hatuoni popote katika Kanisa la Kwanza wakifanya hivyo katika vitabuv yote vinavyofuata hadi Ufunuo wa Yohana.  Sasa agizo hili maana yake nini?  Nyakati za Biblia watu hawakuwa na viatu vya kuingiza kama vyetu, hivyo walipotembea, walijaa vumbi katika miguu na ilibidi kuosha miguu yao, au kutawadha, kabla ya kuingia ndani ya nyumba (WIMBO ULIO BORA 5:3; MWANZO 24:31-32; 43:24; WAAMUZI 19:17-21; 2 SAMWELI 11:8; 1 TIMOTHEO 5:10).  Ilivyokuwa desturi, ni kwamba, wakati wote mtumwa au aliyekuwa mdogo ndiye aliyemtawadha mkubwa au Bwana wake (MWANZO 18:1-4; 19:2; 1 SAMWELI 25:41).  Sasa hapa Yesu aliye Mkubwa, Bwana na Mwalimu, anawatawadha wadogo (wanafunzi wake), lilikuwa fumbo.  Ndiyo maana Petro alikataa mwanzoni, na Yesu akawauliza hatimaye, “Je! Mmeelewa na haya niliyowatendea?“ (13:12).  Hapo mwanzo aliwafundisha kwa nadharia juu ya unyenyekevu, na mkubwa kuwa mdogo, waliposhindania ukubwa, lakini hawakuelewa (LUKA 22:24-27; MATHAYO 20:20-28).  Sasa hapa kwa KITENDO (Practical) anawafundisha kwa kielelezo.  Yeye aliye mkubwa anachukua nafasi ya mtumwa, mdogo.  Hili ndilo agizo lake kwetu kunyenyekeana sisi kwa sisi, na kufuta kushindania au kutafuta ukubwa.  Petro aliyekuwepo hapa, baada ya hapa hatufundishi kutawadhana miguu kwa maji, bali anatufundisha unyenyekevu (1 PETRO 5:5).  Mtume Paulo naye anasisitiza hilo (MATENDO 20:19; WAFILIPI 2:5-7).  Kwa msingi huu, Petro, alipokemewa na Paulo aliyekuja nyuma yake (mdogo), aliyenyenyekea tu (WAGALATIA 2:7-10).

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s