DHIKI KUBWA

ZACHARY KAKOBE

Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

Somo:  Dhiki kubwa

Tunajifunza somo hili kwa kuligawa katika vipengele saba.

( i ).   Dhiki tofauti na zote

( ii ).   Muda wa dhiki kubwa

( iii ).  Majina yanayotumika kuzungumzia dhiki kubwa

( iv )  Watakaohusika kuileta dhiki kubwa

( v ).   Makusudi ya dhiki kubwa

( vi )   Hali itakavyokuwa wakati wa dhiki kubwa

( vii ). Jinsi ya kuikwepa dhiki kubwa

( I ). DHIKI TOFAUTI NA ZOTE

Wanadamu hapa duniani, wanapitishwa katika dhiki za namna namna. Wanapitishwa katika mateso ya namna namna. Wengine wanapitishwa katika hali nzito ya njaa nchi nzima hali inakuwa mbaya. Nchi ambazo zimewahi kushuhudia njaa kali kama Ethiopia na Somaria, watu watakondeana na kubaki mbavu kabisa. Njaa itakuwa kali kiasi kwamba hata ukipita mjusi watatamani kuurukia waweze kuula lakini hata nguvu za kuurukia mjusi zinaweza kukosekena . Watu wengine watafukiwa na vifusi sehemu zile za India kutokana na matetemeko. Wengine wataweza kupelekwa mbali kwa kurushwa na vimbunga. Dhiki ulizozipata kwa kuanguka katika maporomoko, kwa kupanda milima mirefu kwa shida, hizo siyo dhiki ukilinganisha na dhiki kubwa itakayouijilia ulimwengiu. Dhiki wanazozipata wanadamu kwa kutupwa magerezani na kuteswa na kuumizwa sana, wengine wakiwekwa katika viti ambavyo watateswa sana na polisi ili waweze kueleza yale waliyoyafanya. Watakazwa sehemu zao za siri, watachomwachomwa kwa vitu vyenye ncha kali, watapigwa mijeredi kwa kuwekewa pilipili kwanza sehemu za siri. Hizo siyo dhiki kabisa ukilinganisha na ukilinganisha na dhiki itakayokuja baada ya kanisa kunyakuliwa.  Watu waliookolewa nao wanaweza kupita katika dhiki za namna namna hapa duniani kama vile kutengwa na wazazi, kupigwa na wazazi, kupigwa na mume  au mke kwasababu ya wokovu. Wengine watafungwa, watapigwa mawe hata kuuliwa, hizo ni dhiki kidogo tu. Yesu Kristo alisema “duniani mnayo dhiki lakini jipeni moyo, mimin nimeushinda ulimwengu”.Sikuja kuleta amani bali upanga watakuwepo watu watakaofarakana pamoja nanyi, amani itavurugika”. Dhiki unazozipata kwa  sababu umeokolewa hizo ni dhiki kidogo  sana. Dhiki hizo zinaitwa dhiki nyepesi katika biblia.  ( 2 WAKORINTHO 4:17 ). Watu wote waliookoka walipita katika dhiki za namna namna kwasababu ya wokovu ili waukane wokovu wao. Wamkane Yesu Kristo aliyewaokoa. Wengine walikatwa vichwa  na wengine kusulibiwa kwa namna nyingi. Hayo mateso na mengine mengi waliyoyapata ni dhiki nyepesi ukilinganisha na dhiki kubwa itakayouijilia ulimwengu. Dhiki itakayouijilia ulimwengu inaitwa dhiki kubwa kwasababu ya mateso makubwa yatakayokuwepo ( MATHAYO 24:21 ). Wahubiri wengine wanaiita dhiki kuu lakini kitu kinachotajwa hapo ni dhiki kubwa lakini ni kitu kilekile. (DANIELI 12:1). Utaweza kuona watu watakaookolewa katika dhiki hii kubwa kuwa ni  Waisraeli tu kutokana na agano ambalo Mungu Alilifanya na baba zao (Ibrahimu, Isaka na Yakobo).

( II ). MUDA WA DHIKI KUBWA

Dhiki kubwa inatajwa kwamba itakuwa kwa muda wa juma moja la Danieli. Itakuwa kwa muda wa juma moja la Danieli, juma la savbini. ( DANIELI 9:24-27 ) “Neno juma moja ( DANIELI 9:27)”. Juma Moja linalozungumziwa hapa ndiyo kipindi cha dhiki kubwa. Katika unabii juma moja linazungumziwa kumaanisha miaka saba. (MWANZO 29:27) “Timiza siku zako saba, inamaanisha timiza miaka yako saba”. Juma moja la Danieli linalozungumziwa ni miaka saba ya dhiki kubwa.

Miaka saba ya dhiki kubwa itakuwa imegawanywa katika sehemu  kuu mbili na kila sehemu itakuwa na kipindi cha miaka mitatu na nusu au muda wa miezi arobaini na mbili (miezi 42)  au siku zipatazo 1260. Kutakuwa na mambo yatakayotokea katika miaka mitatu na nusu ya mwanzo na mambo yatakayotokea katika kipindi cha miaka mitatu na nusu iliyosalia (UFUNUO 11:2-3), Miezi arobaini na mbili (miezi 42) na siku elfu moja na mia mbili na sitini nazo zimetajwa zikimaanisha miaka mitatu na nusu. (UFUNUO 13:5). Katika andiko hili inatajwa tena miezi arobaini na mbili (miezi 42) ambayo ni sawa na miaka mitatu na nusu ya kwanza katika kipindi cha miaka saba ya dhiki kubwa. Baada ya kufahamu vipindi hivi viwili vya dhiki kuwa ni muhimu kufahamu jinsi itakavyokuwa katika vipindi hizi viwili tofauti.

Katika kipindi cha kwanza cha miaka mitatu na nusu (miezi arobaini na mbili) ya mwanzo, mpinga kristo atafanya agano pamoja na wana wa Israeli. Atafanya agano na Taifa la Israeli na watadanganyika kwa kiasi kikubwa. Katika kipindi hicho cha miaka titatu na nusu ya mwanzo, kutakuwa na nafuu kwa wana wa Israeli kutokana na agano hilo la uongo ambalo hatimaye litavunjwa na mpinga kristo mwishoni mwa kipindi hiki.. Katika kipindi cha pili cha dhiki kubwa cha miakamitatu na nusu, dhiki itaongezeka hususani kwa wana wa Israeli. Wakati huo agano la mpinga kristo na wana wa Israeli litakuwa limeshavunjika. Kwa nini dhiki itaongezwa kwa wana wa Israeli na kwa makusudi gain? Tutaona sababu hapo mbele kidogo.

( III ). MAJINA YANAYOTUMIKA KUIZUNGUMZIA DHIKI KUBWA.

Yapo majina  mbalimbali yanayotumika kuizungumzia dhiki kubwa na tunapokutana nayo tunaweza kuyachanganya na kufikiri yanazungumzia kitu mambo mengine kumbe yanazungumzia mambo haya. Majina hayo ni :-

( A ). Ghadhabu itakayokuja.

( 1 WAKORINTHO 1:10 )

Tunaweza tukaokolewa na ghadhabu itakayokuja yaani dhiki kubwa. Kanisa, watu waliookolewa hatutakuwepo wakati huo wa ghadhabu ya Mungu kwa wenye dhambi walioukataa wokovu wa Yesu.

( B ). Saa ya hukumu.

           ( UFUNUO 14:7 ).

Wakati wa dhiki kubwa  utakuwa ni wakati wa hukumu  kama tutakavyoweza kuona hapo mbele kidogo

( C ). Adhabu na ghadhabu.

 ( ISAYA 24:21; ISAYA  26: 21)

Hapa inazungumziwa dhiki kubwa na siyo kitu kingine

( D ). Saa ya kujaribiwa.

           ( UFUNUO 3:10 )

Saa ya kujaribiwa itakayoujilia ulimwengu wote ni kipindi cha dhiki kubwa.

( E ). Tabu yake Yakobo.

( YEREMIA 30:7 ).

Andiko hili linazungumzia tabu watakayo wapata hususani wana wa Israeli. Israeli mwanzo iliitwa Yakobo. Tabu yake Yakobo au Tabu yake Israeli. Tutaweza kuona jinsi wana wa Israeli watakavyookolewa kipekee katika dhiki kubwa.

( F ). Uangamivu.

 ( YOELI 1:15 ).

Utakuwa ni wakati wa kuangamizwa kwa wanadamu.

( G ). Siku ya giza na weusi , siku ya mawingu na giza kuu.

           ( YOELI 2;1-12).

Watu watakaokuwepo duniani kwenye dhiki kubwa watageuka nyuso zao, nyuso zitakuwa nyeupe sana kwa hofu. Jasho jembamba  lililojaa chumvichumvi litakuwa limewafunika na watakuwa kama wamepakazwa chumvi kutokana na hofu na matetemo watakay0kuwa wameyapata.

( IV ). WATU WATAKAOHUSIKA KUILETA DHIKI HIYO KUBWA

Dhiki hii itakuwa kubwa sana kutokana na watatu watakaohusika kwa wanadamu Itakuwa ni ole kwa yule atakayekuwa ameachwa na kukabiliwa na hatari itakayokuwa inaujilia ulimwengu. Watatu hao ni akina nani? Watatu hao ni Mungu, Shetani na Mpinga Kristol.

( i ). Mungu.

Mungu atahusika kikamilifu kuileta ghadhabu na mapigo kwa watu.

(  ISAYA 26:21 )

“Mungu  atakuwa anawaadhibu wanadamu walioukataa wokovu”

            (UFUNUO14;7 ) Ni hukumu ya Mungu.

            (UFUNUO15:7 )  Ghadhabu ya Mungu.

Jaribu kuwaza hapa ni Mungu anashusha ghadhabu yake.

( ii )  Shetani.

Ghadhabu kubwa ya Shetani itashushwa kwa wanadamu. Sasa hivi tunaona jinsi Shetani anavyosababisha magonjwa  ya kila namna , akisababisha ajari, akiwafanya watu  wawe vilema, washindwe kutembea , akiwafanya watu wapooze, kuleta majipu juu ya watu kama kwa Ayubu. Hayo anayafanya sasa lakini ghadhabu yake bado haijaja. Shetani atawashukia watu watakaobaki duniani kwa ghadhabu nyingi akijua  kwamba wakati wake  uliobaki kabla ya kutupwa katika ziwa la moto milele na milele utakuwa unaendelea kuwa finyu au mchache. Kwa hiyo, Shetani atashuka akiwa na ghadhabu nyingi kwa wanadamu wenye dhambi ambao waliukataa wokovu na kuachwa wakati wa unyakuo wa kanisa ( UFUNUO 12:12 ).  Si hao tu wawili, yupo wa tatu.

( iii ).  Mpinga Kristo

      Leo tunawapinga Kristo wengi duniani, watu wanaosema Yesu siyo Mwokozi ni wapinga Kristo, wanaosema hakuna kuokoka duniani ni wapinga Kristo, wanaosema Yesu siyo mwana wa Mungu, wanaosema hakuja katika mwili, ( Mungu ) ni wapinga Kristo. Watu wote waoyapinga maandiko matakatifu ya Mungu katika biblia takatifu woye ni wapinga Kristo hata kama wanajiita kuwa ni wakristo. Wapinga Kristo wa namna hii wapo wengi sana duniani bado wanaendelea kufanya kazi zao lakini yupo mmoja Mpinga Kristo anayekuja ( 1 YOHANA 2:18 ). Angalia neno “Mpinga Kristo yuaja” huyo anayetajwa ni mmoja ajaye.

Pia kuna wapinga kristo wengi ambaowamekwisha kuwapo. Yupo mmoja anayeitwa Mpinga Kristo kwa namna ya tofauti na Wapinga Kristo wengi wa sasa. Yupo mpinga Kristo ajaye, anajulikana kwa majina tofauti katika biblia zetu.

( i ). Mpingamizi

( ii ) Asi

( iii ) Chukizo la uharibifu

( iv ) Mnyama

Kwa nini anaitwa mnyama?

Anaitwa mnyama  kwasababu atakuwa ni mkatiri sana kama wa wanyama wakali  walivyo. Kama jinsi Simba asivyokuwa na huruma, anavyoweza kumchana Paa. Kama Mbwa mwitu asivyovyokuwa na huruma, kama Chui, Dubu wasivyokuwa na huruma ndivyo atakavyokuwa. Ukatiri wa kinyama atakaokuwa nao unamfanya kuitwa Mpinga Kristo kuitwa Mnyama.

                                                  ( 2 WATHESALONIKE 2:1-8 ).

Kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo  hakuji mpaka afunuliwe kwanza mpinga Kristo ( ufunuliwe ukengeufu ). Hapa ndipo watu wanapochanganya mambo. Ndiyo maana tunapaswa kujifunza kweli ili tupate kuifundisha kwa wengine.

Kuna  kuja kwa Yesu mara ya mara mbili tofauti. Kuja kwa Yesu duniani kwa mara ya kwanza kulitimia alipozaliwa duniani kama mwanadamu lakini kuja kwa Yesu mara ya pili kutatokea baada ya miaka saba ya dhiki kubwa. Yesu atakuja duniani kutawala kwa miaka elfu moja na ndiyo maana atashuka kwa utiosho mwingi nautukufu mwingi tofauti na alipokuja mara ya kwanza  ambapo wanadamu waliweza kumpiga, kumburuta na kumtemea mate. Alipokuja mara ya kwanza alikuja katika udhaifu kwa kuzaliwa katika hori ya ng’ombe na kuishi maisha ya kimaskini. Atakuja kama Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana na hapo ndipo kila jicho litamwona na kila ulimi kukiri kuwa Yesu ni Bwana. Yesu atakuja na watakatifu ( kanisa ) aliowatwaa miaka saba iliyopita na watatua katika mlima mzeituni alipoondokea wakati anakwende mbinguni akiwa katikati ya wanafunzi wake . Yesu atakuja akiwa amempanda Farasi mweupe.  Ikimbukwe kuwa miaka saba hiyo mbinguni kulikuwa na harusi ya mwana kondoo ( Yesu ) na watu watapokea taji mbalimbali kutokana na kazi waliyofanya wakiwa hapa duniani. Wakati wa unyakuo wa kanisa siyo wakati wa kuja kwa Yesu mara ya pili duniani maana Yesu hatatua juu ya uso wa dunia. Baada ya parapanda kulia watakatifu watatwaliwa kama kwa sumaku na kumlaki Yesu mawinguni. Yesu atakuwa mawinguni pamoja na mwaliko wa malaika wake. Siku hiyo hakuna aijuaye lakini kuja kwake mara ya pili duniani itakuwa baada ya kipindi cha dhiki kubwa yaani miaka saba. Andiko linalochanganya watu ni ( 2 WATHESALONIKE 2:1-8 ) ambalo lina maana kuwa, kuja kwa Yesu kutawala dunia miaka elfu moja ni mpaka afunuliwe kwanza mpinga Kristo ambaye kutawala kwake ni miaka saba. Lakini huyo mpinga Kristo bado hajafunuliwa kanisa ndilo limezuia kufunuliwa kwake. Kanisa likinyakuliwa ndipo natakapofunuliwa. ( MATHAYO 24:25 ; UFUNUO 13:1-6)

Mnyama anayetajwa hapa ni Mpinga Kristo atakayekuwa na ukali wa kinyama Anatajwa kutoka katika bahari. Je, ni bahari gain? Bahari inayotajwa hapo katika unabii inamaana ya kusanyiko kubwa la watu. Mahali lilipo kusanyiko kubwa la watu linaitwa bahari ( ISAYA 57:20 ) Wabaya wengi kwa pamoja wote wanaitwa bahari.  Sehemu nyingine inayosema “bahari ikawatoa wafu wake” ina maana ya dunia kuwatoa wafu wake. Mnyama au mpinga Kristo anatajwa kutoka katika bahari, maana yake atatoka katikati ya watu walioopo duniani. Huyo mnyama atakuwa ni mtu kabisa na kwasababu tuko ukingoni mwa haya mambo kutokea inamaana huyo mtu yupo sasa anangoja kaniosa linyakuliwe ndipo apate kufunuliwa ( UFUNUO 13:1-6 ).Vichwa, Pembe Vilemba ni alama ya nguvuna utawala. ( UFUNUO 17:3, 9-13 ) Ufalme na mamlaka ya kipekee ndiyo nyanazungumzia vilemba saba. Mnyama ( mpinga Kristo ) anatajwa kufananishwa na Chui, Dubu na Simba ambao ni wanyama wakali sana. Ukatiri wa Chui, Dubu na Simba umo ndani ya mpinga Kristo Mpinga Kristo atakuwa na mamlaka ya Kishetani, mamlaka ya kifalme ambayo itamfanya kushirikiana  na wafalme duniani  ( maraisi ) watakaokuwepo . Kuna wafalme ambao hata falme zao zinazidi kuimarika na hao watampa nguvu sana  ya kiuchumi , nguvu ya kivita na kumfanya awe tishio kwa wanadamu  na watu wote dunia yote watalazimika kumsujudia.                                                                    Watu  wanaofundisha kwamba kanisa litakuwepo wakati wa dhiki kubwa, hawataki  watu wajiandae vizuri ndilo lengo la Shetani kuyaleta mafundisho hayo. Kwamba tutapita kwenye dhiki hivyo hatuna haja ya kujiandaa kwa lolote. Hao walimu wanaofundisha hivyo wanachanganya mafundisho.

Mpinga Kristo atakuwa amepewa  uwezo wa kishetani  kama tulivyosoma ( UFUNUO 13:1-8 ). Kutokana na ishara zake na mateso yake atawafanya watu wengi walioachwa kumwabudu Shetani au siyo kuuawa ( UFUNUO 13:13-17 ).. Kwasababu atakuwa na mamlaka ya kipekee atawafanya watu wengi wamsujudie . Mtu ambaye hatakubali chapa ya mnyama ambayo ni namba 666 Hataweza kununua wala kuuza na akikubali atalazimika kumsujudia huyo Mnyama aliyepewa mamlaka na Shetani. Mwenye akili na afahamu. Yesu alisema, “mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu hamkunipokea lakini atakuja mwingine kwa jina lake mtampokea” ( YOHANA 5:43 ).Watu wengi wanaomkataa Yesu leo watalazimika kumkubali mpinga Kristo kutokana na mamlaka atakayokuwa nayo na unabii kuhusiana na hilo lazima utatimia. Wanadamu wengi watampokea na kumsujudia wakifikiri kuwa yeye ndiyo msaada na mkombozi wao kumbe watakuwa wanazidi kuharibikiwa.

( V ).  MAKUSUDI YA DHIKI KUBWA

( I ).  Kuliandaa Taifa la Israeli kumpokea Yesu Kristo kama masihi wao.

Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu alijifunga katika agano au ahadi na ahadi za Mungu haziwezi kutanguka. Mungu alijifunga katika agano kwamba Israeli wote wataokolewa.. Alipokuja kwa ajili yao ( Israeli ) hawakuweza kumpokea kabisa ( YOHANA 1:11 ). Yesu  alikuja kwa ajili ya wana wa Israeli lakini hawakumpokea ndipo akawageukia mataifa. Mungu alishajifunga katika agano na baba zao kuwa atawaokoa wote. Makusudi ya dhiki kuu ni kuwatesa waisraeli na kwa mateso hayoi watamkiri Yesu Kristo kuwa ni Bwana na mwokozi wao  Dhiki hiyo kubwa itawatesa sana waisraeli  lakini wote  watakaokuwa wamefuata masherti kama alivyosema Bwana wetu Yesu. Wote watakaokimbilia milimani kwa kukimbia kukwepe kumsujudia Mnyama ( Mpinga Kristo ) na kukwepe namba yake 666, hao wote ndio watakaookolewa Yesu atakapokuja mara ya pili duniani kwa ajili ya utawala wa miaka elfu moja pamoja na watakatifu. Hawa ndo watakatifu wanaotoka katika dhiki kubwa. Biblia inaposema siku zitafupishwa kwa ajili ya watakatifu ni hao wanaotoka katika dhiki na si vinginevyo ( MATHAYO 24:21-22 ). Hawa wanaotajwq ni watakatifu wanaotoka katika dhiki kubwa na siyo sisi tuliookolewa leo. Baada ya wana wa Israeli kuokolewa  (watakatifu waliotoka katika dhiki ) wataungana na watakatifu ( kanisa ) ambao watakuja na Yesu ili kutawala pamoja nae. Watakatifu watakaotoka kwenye dhiki wataungana na wale ambao Yesu aliwatwaa duniani wakati wa unyakuo wa kanisa miaka saba iliyopita dhiki kubwa ikiendelea duniani na wote kwa pamoja watatawala na Yesu duniani kwa miaka elfu moja.. AGANO LA MUNGU NA WANA WA ISRAELI (  KUMBUKUMBU LA TORATI 4:30-31 ). Wakishakupatwa na mambo hayo yote wakati wa dhiki kubwa, hatimaye Taifa la Israeli litamrudia Bwana. Mungu alijitambulisha kwao kuwa yeye ni Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Mungu hatasahau agano aliloagana na baba zao Ibrahimu, Isaka na Yakobo ( YEREMIA 30:7). Yakobo ni Israeli. AGANO LA MUNGU NA WANA WA ISRAELI ( EZEKIELI 20:37; YEREMIA 30:7; TORATI 4:30-31) UFAFANUZI WA AGANO LA MUNGU NA WAISRAELI                 ( WARUMI 11:25-27 ).  Paulo mtume aliyepewa wingii wa mafunuo kwake tunajifunza mambo ya siku za mwisho ( WARUMI 11:25-27 ) Utimilifu wa mataifa uwasili inazungumzia kunyakuliwa kwa kanisa. Majira tuliyonayo sasa yanaitwa majira ya mataifa. Kwasababu ni wakati wa majira ya mataifa ndiyo maana sasa wana wa Israeli ni wagumu sana kuukubali wokovu. Kuhubiri injili Israeli ni ngumu sana kuliko sehemu nyingine yoyote duniani ( WARUMI 11:25-27, 27-32 ). Hivyo Israeli wote wataokoka.

Katika miaka mitatu na nusu ya kwanza, wana wa Israeli watakuwa na unafuu kutokana na agano la uongop ambalo watakuwa wamelifanya na mpinga Kristo Lakini miaka mitatu na nusu iliyosalia , chukizo la uharibifu litasisimama kikamilifujuu ya Israeli ( DANIELI 9:27; MATHAYO 24:15-21 ). Baada ya miaka mitatu na nusu ya kwanza, mpinga Kristo atavunja agano lake paoja na wana wa Israeli. na kuwatesa kipekee ili wao nao wakubari kumsujudia Mpinga Kristo kama mataifa mengine wanavyofanya. Maandiko hayo yanawazungumzia wayahudi na siyo sisi watanzania ( mataifa ). Biblia katika ( MATHAYO 24: 16 ) inasema kuwa waliop[o uyahudi wanapaswa kukimbilia milimani ili kukwepa kumsujudia Mnyama. Hapa Yesu anazungumzia watu wa Uyahudi ( Israeli ). Hao watakaoikwepa namba 666 ndio watakatifu wanaotoka  katika dhiki kubwa. Yesu anasema ole ni kwa Wanyonyeshao, wenye mamba  maana hao watashindwa kumkimbia Mpinga Kristo na kukamatwa na majeshi yake. Pia anawaambia Waisraeli waombe siku hiyo isitokee siku ya sabato maana waisraeli ni washika sabato. Katika sabato huwa kuna mwendo wa sabato ( MATENDO 1:12 ). Wakati wa sabato, mtu anatakiwa kutembea mwendo wa sabato chini kidogo ya maili moja.. YUmbali kutoka mlima zeituni hadi Yerusalemu ni mwendo wa sabato. Waisraeli wanatakiwa kuomba siku hiyo isitokee siku ya sabato wasije wakashika sheria ya sabato ya kutembea mwendio chini kidogo ya maili moja na kushindwa kumkimbia mpinga Kristo ( MATHAYO 24;21-22 ).

Siku za dhiki kubwa zimefupishwa kwa ajili ya wateule ambao Mungu amekusudia kuwaokoa kutokana na agano ambalo tuekwisha kuliona. Walimu wengine wanachanganya kwasababu ya neno wateule wanafikiri kuwa neno hilo linazungumzia sisi tuliookolewa leo. Neno mteule linapotumika katika  biblia, linatumika katika namna nne tofauti:-

( I ). Yesu Kristo      (  ISAYA 42:1 )

( ii ). Malaika wateule   ( 1 TIMOTHEO 5:21 )

( iii ) Sisi tuliookoka  ( TITO 1:1; 1 PETRO 1:1-2; WARUMI 8:33; LUKA 18:7 )

( iv ) Wateule vilevile ni Taifa la Israeli  ( ISAYA 65:8-9;  ISAYA 45:4 )..

Tunatakiwa kupambanua vizuri ili tusichanganye mambo  na kujikuta tunafundisha watu uongo bila kujua ( YAKOBO 3:1 ).

( II ).   Kuleta hukumu ya adhabu kwa watu wote ambao hawakuukubali wokovu ( waliokuwa wakisema hakuna kuokoka duniani na kumkataa Mwokozi Yesu anayeokoa)                        

                                ( ISAYA 26:20-21; 2 WATHESALONIKE 2: 7-12 )

Kwasababu hawakutaka kuipenda ile kweli wapate kuokolewa, ghadhabu ya Mungu itashuka kwao.

( 2 WATHESALONIKE 2:10-12 )

Nguvu ya upotevu ni nguvu ya mpinga Kristo na ishara zake. Watu wote walioukataa wokovu , Mungu mwenyewe atawaletea nguvu ya upotevu ili wauamini uongo wa mpinga Kristo  wasije wakaokolewa. Mataifa mengine yote isipokuwa Israeli pekee, watampokea mpinga Kristo, watamwabudu, watamsujudia na wataipokea chapa yake ya 666. Watu ambao siyo  waisraeli hawatakuwa na nafasi ya kutubu na kuokolewa. Majira ya mataifa yatakuwa  yamekwisha kupiita wakati wa unyakuo wa kanisa.. Wakati tulionao ndio wakati ambao ni majira ya mataifa, tunaweza kuokoka sasa kwa kuwa parapanda ya Bwana kwa ajili ya unyakuo wa watakatifu ( kanisa ) bado haijalia. Yesu Kristo alikuja kwa waliowake (Waisraeli ) lakini waliowake wakamkataa ( hawakumpokea ) YOHANA 1:11. Ndipo alipoamua kuwageukia mataifa ( MATHAYO 28:19-20; MATENDO 1:8 ).. Wakati tulionao ni wakati wa neema kwa mataifa ( hatukustahili ) lakini kanisa likinyakuliwa utakuwa ni utimilifu au mwisho wa neema ya wokovu kwa mataifa. Huo unaitwa utimilifu wa mataifa  ( WARUMI 11:25-32 ).. Katika andiko hilo kuna siri kubwa sana na ni siri ambayo shetani hataki watu waijue ili wazidi kudanganyika eti na mataifa wataokoka katika dhiki kubwa kumbe siyo kweli. Mataifa yote isipokuwa Israeli tumepewa nafasi moja tu  ( one chance ) na hakutakuwa na wokovu kwa mataifa.

( VI ).   HALI ITAKAVYOKUWA WAKATI WA DHIKI KUBWA

Itakuwa ni kilio na kusaga meno. Kutakuwa na mateso na dhiki ambayo yatafanya watu wauawe na damu yao kumwagwa kama mavumbi na nyama yao kama mavi. Hatakuwepo mtu wa kumlilia mwenzake wala wa kuzika mwenzake, wote watakuwa katika hali nzito ya mateso na dhiki kuu ambayo haina mfano wake.      ( SEFANIA 1:15, 17-18 ). Dhiki italetwa kwasababu watu wamemtenda Bwana dhambi, huu ni uthibitisho kwamba sisi tuliookolewa leo hatutakuwepo wakati wa dhiki kubwa.. Watu watateswa  mateso makuuu na wengi watakufa na miili yao haitazikwa maana kila mtu atakuwa katika dhiki hiyo na hakutakuwepo na mtu wa kumlilia mwenzake maana kila mmoja atakuwa anajililia mwenyewe. Miili ya watu watakaouawa itakuwa samadi juu ya uso wan chi (YEREMIA 25:33). Watu leo wanatenda dhambi na utadhani Mungu hayoko lakini hasira yake Mungu imewekwa akiba , iefichwa kwa ajili ya wakati ule wa dhiki kubwa                   ( SEFANIA  2:1-3 ) Akiba ya hasira ya Mungu itafunuliwa wakati wa dhiki kubwa. Leo mtu anaweza kusema hakuna kuokoka, hakuna Mungu, Yesu siyo Mungu, Yesu hakuja katika mwili n.k, lakini siku ile utalia sana na kusaga meno kutokana na mateso yatakayokuwepo ambayo hayana mfano wake tangu kuumbwa kwa ulimwengu na hayatakuwako tena.

         MAPIGO YATAKAYOMWAGWA JUU YA WANADAMU WAKATI WA DHIKI KUBWA

Mapigo saba ( vitasa saba vya ghadhabu ) yatamwagwa juu ya wanadamu wakati wa dhiki kubwa. Hali itakuwa nzito kwa mateso makuu yatakayokuwepo wakati huo.     ( UFUNUO 15:1; UFUNUO 16;1-6 )

1. Jipu baya bovu    ( UFUNUO 16:1-2 )

Watu duniani watakuwa na majipu mabaya, yanayotoa usaha na harufu mbaya sana. Wataumizwa sana kwa majipu hayo kuliko wakati wa Ayubu.

 2. Maji yote yatageuzwa kuwa damu  (.UFUNUO 16;3-6 ).

Chemchemi zote zitatoa damu. Bahari, Maziwa na Mito vyote vitageuzwa kuwa damu. Wanadamu watanyweshwa damu kwasababu ya damu ya watakatifu iliyomwagwa .Watu waliwaua manabii na mitume hivyo watanyweshwa damu kwa sababu hiyo. Damu itakuwa nzito kiasi kwamba mtu akiinywa ataweweseka mara moja na kuanguka chini na kuzimia. Itakuwa ni  hali nzito sana kunywa damu wakati ule. Viumbe vyote viishivyo baharini, kwenye maziwa na mito vitakufa kutokana na maji yote kuwa damu. Kutakuwa na harufu ya kutisha kutokana na viumbe vyote kufa.

3.. Jua litashushwa karibu sana na uso wa dunia ( UFUNUO 16:8 )

Jua lina joto kiasi cha sentigredi 1,000,000 unaweza  kuona jinsi mates ohayo ya kuunguzwa na joto hilo yatakavyokuwa makubwa sana. Ndiyo maana watu wengi watakufa wakati wa dhiki kubwa. Watu watamtukana Mungu kwa maunguzo hayo ya jua.

4.  Matatameko , umeme na radi vitaachiliwa na Mungu juu ya  uso wa dunia.  ( UFUNUO 16:18 ).

Matetemeko hayo yanatajwa kuwa hayajawahi kutokea tangu dunia kuwako. Matetemeko yanayoripotiwa katika vyombo vya habari ambayo yanasababisha maafa makubwa katika mataifa mbalimbali ni matetemeko madogo sana ukilinganisha na matetemeko yatakayoletwa na Mungu mwenyewe wakati wa dhiki kubwa. Umeme na radi vitakuwa ni sehemu ya mateso kwa wanadamu walioukataa wokovu na kuachwa duniani wakati wa unyakuo wa kanisa.

5. Mvua ya mawe makubwa

     ( UFUNUO 16:21 )

,Mawe yanatajwa kuwa na uzito wa taranta. Taranta moja ni sawa na kg 53 za uzito. Watu watamtukana sana Mungu kutokana na mates ohayo yam awe.

6. Nzige wenye sumu kali

       ( UFUNUO 9:2-6 )

Nzige wenye sumu kali kama ya kuumwa na nnge watakuwepo wengi duniani kwa muda wote wa dhiki kubwa ili kuwatesa wanadamu walioukataa wokovu wa Yesu. Wakati wote watu watakuwa wakiumwa na Nzige hao.

7.  Kutakuwa na giza kuu juu ya uso wa dunia

          ( UFUNUO  16:10 )

( VII ). JINSI YA KUIKWEPA DHIKI HII KUBWA .

Kila anayetaka kuikwepa dhiki hii kubwa  hana budi kujificha ndani na kufunga milango yote kama vile wakati wa Safina ya Nuhu.            ( ISAYA 26:20 )

Kwa kufanya yafuatayo:-

( i ) . Kuhakikisha tunatubu dhambi zetu zote kwa kumaanisha kuziacha na kuokolewa kwa kumwamini mwana wa Mungu Yesu Kristo. ( MITHALI 28:13 ) “ Afichaye dhambi zake hatafanikiwa, bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema”.  ( YOHANA 3:36 ) “ Amwaminiye mwana wa Mungu hahukumiwi”.

( ii )  Kukaa ndani ya Yesu Kristo na kulifuata neno lake na maagizo yake yote ( ZABURI 119:9; ZABURI 119:6  )

( iii ) Kukaa mahali ambapo kuna mafundisho ya kweli ya neno la Mungu.  Tuwe tayari kufata kila tunaloelezwa ambalo ni la kibiblia. Tukiambiwa kumwacha mke wa pili au mume wa pili tuwe tayari. Dhiki utakayoipata kwa kumwacha huyo mume au mke wa mtu mwingine ni ndogo sana ukilinganisha na dhiki kubwa inayokuja. Tukiambiwa tuache kuvaa mavazi ya kidunia     kikahaba ) tusiwe wabishi. Watu wanapoelezwa kuhusiana na mapambo kwamba hayatakiwi kuvaliwa na mtu aliyeokoka wao wanawasikiliza walimu wao wa uongo ambao siku zote wanachanganya mafundisho kwa kutojua kweli ipasavyo. Mapambo yamekatazwa ( 1 TIMOTHEO 2:9-10; 1 PETRO 3:3-5; MWANZO 35:1-5; KUTOKA 33:4-6; EZEKIELI 23:26-30,40, 42; ISAYA 3:16-24; HOSEA 2:13; YEREMIA 4:30, 2 WAFALME 9:30-37, UFUNUO 2:20).

Wanawake wasivae mavazi yawapasayo wanaume wala wanaume kuvaa mavazi yanayowapasa wanawake, kufanya hivyo ni machukizo kwa Bwana ( KUMBUKUMBU LA TORATI 22:5 ). Suruali ni vazi la wanaume kibiblia. Sehemu zote zinazotaja suruali katika biblia inatajwa ikiwa imevaliwa na wanaume. Walimu wa uongo wanawafariji wanawake wapenda dunia            ( 1 YOHANA 2:15-17, YAKOBO 4;4 ) waendelee kuvaa suruali eti hazina shida. Hao ni watumishi wa Shetani ambao wapo kwa mfano wa watumishi wa haki ( 2 WAKORINTHO 11:14 )

Ukiambiwa kubatizwa katika maji tele usibishe ndivyo inavyotupasa ( YOHANA 3:23; WAKOLOSAI 2:12 ). Lazima uzamishwe katika maji kama kuzikwa kwa Yesu ili tushiriki mauti yake.

( iv ). Kukesha wakati wote na kuyatunza mavazi meupe  ya utakatifu. Doa dogo tu husababisha uchafu ( WIMBO ULIOBORA 2:15 ). Lazima tujihadhari na Mbweha wadogo. Dhambi tunazoziona ndogo zinaweza kutuingiza katika dhiki kubwa. Adamu na Hava walifanya dhambi ambayo tungeweza leo kuiita dhambi ndogo. Walikula matunda katika mti waliokatazwa na Mungu lakini adhabu waliyopewa ni kubwa mno kwa kosa hilo tu. Wachungaji na walimu wengi wa uongo , wanaotumiwa na shetani wanaweza kukwambia siyo shida kufanya hili au lile kwa namna ileile ya nyoka alivyowadanganya Adm   na Hawa ( MWANZO 3:1-19 ).

Mpendwa msomaji, baada ya kusikia yote haya kutoka kwa nabii aliyetumwa kukuletea ujumbe huu, usifanye moyo wako kuwa mgumu.  Hii ni nafasi ya kipekee ya kuokoka.  Je, unajuaje kama utaamka kitandani baada ya kulala usiku wa leo?  Wakati uliokubalika wa wokovu ni sasa (2 WAKORINTHO 6:2).  Labda utaniuliza, ili uokoke, ufanyeje?  Jibu ni rahisi, kwa imani ukitubu dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha, na kumwambia Yesu Kristo akusamehe, utasamehewa sasa hivi, na msamaha wa dhambi, huambatana na wokovu (LUKA 1:77).  Je, uko tayari kuokoka sasa hivi?  Najua uko tayari. Basi fuatisha sala hii kwa dhati toka moyoni, Mungu baba asante kwa kuniletea ujumbe huu.Natubu dhambi zangu zote, kwa kumaanisha kuziacha. Yesu Kristo nakuomba unisamehe dhambi zangu na kunipa uwezo wa kushinda dhambi na kuniokoa kutoka katika mateso ya moto wa milele. Asante, kwa kuniokoa katika Jina la Yesu.  Amen.  Tayari sasa umeokoka, na kwa hakika unakwenda mbinguni sasa, hata ukifa leo.  Ili uzidi kuukulia wokovu, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

                                     . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

                                                          . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .         

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “note” hii, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.

UBARIKIWE SANA KWA KAZI YAKO NJEMA

Advertisements

4 comments on “DHIKI KUBWA

  1. Pingback: KUJA KWA YESU KRISTO MARA YA PILI DUNIANI NA VITA YA HAR-MAGEDONI | O-------------------------------------- BAADA YA KUOKOKA,TAFUTA UTAKATIFU

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s