HAKIKA ALIKUWA MWANA WA MUNGU

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

SOMO:   HAKIKA ALIKUWA MWANA WA MUNGU

   Leo, tunaendelea kujifunza Sura ya 27 ya Kitabu cha MATHAYO, na tutaangalia MATHAYO 27: 50-66.  Katika mistari hii, tunajifunza juu ya kufa na kuzikwa kwa Yesu.  Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika mistari hii katika vipengele vitano:-

(1)  KUPAZA SAUTI KWA YESU NA KUITOA ROHO YAKE  (MST 50)

(2)  HAKIKA ALIKUWA MWANA WA MUNGU (MST 51-54)

(3)  WANAWAKE KUMTUMIKIA   (MST 55-56)

(4)  KUZIKWA KWA YESU  (MST 57-61)

(5)  KULINDWA KWA KABURI  (MST 62-66)

(1)      KUPAZA SAUTI KWA YESU NA KUITOA ROHO YAKE   (MST 50)

Kulikuwa na giza juu ya nchi yote tangu saa sita hadi saa tisa mchana (MST 45).  Baada ya saa tisa mchana, yaani kati ya saa 9 -10 mchana, ndipo Yesu alipokata roho.  Kulikuwa na maana kamili juu ya kila jambo lililofanyika msalabani.  Saa tisa, ilikuwa ni saa ya kusali ya Wayahudi (MATENDO 3:1).  Saa nyingine za sala ilikuwa saa 3 asubuhi na saa 6 mchana.  Saa ya kusali saa 9, ndipo ulipokuwa wakati wa kutoa DHABIHU YA JIONI (DANIELI 9:21, 1 WAFALME 18:29, 36).  Saa hii ya jioni, ndipo Yesu alipokufa msalabani, na kutolewa kama DHABIHU YA JIONI kwa ajili yetu.  Wakati huu pia, ni ambapo mwanakondoo wa Pasaka alipochinjwa.  Yesu Kristo, alitolewa na kuchinjwa msalabani kama Pasaka wetu, mwanakondoo asiyekuwa na ila wala waa (1 WAKORINTHO 5:7; 1 PETRO 1:19).  Wakati wa kufa kwake Yesu, ALIPAZA SAUTI YAKE kudhihirisha nguvu alizokuwa nazo mpaka wakati wa kufa.  Hakika alijitoa MWENYEWE kufa kwa ajili yetu.  Kwa kawaida, watu wengi wanapokuwa wanakufa hawana nguvu ya kupaza sauti namna hii hasa baada ya mateso makubwa  namna hii.  Lakini, siyo hilo tu, alipaza sauti yake kwa nguvu, kama TARUMBETA zilizokuwa zikipigwa wakati wa kutoa dhabihu (HESABU 10:9-10).  Hakika, Kristo alikuwa dhabihu kwa Mungu, hatuna haja tena ya wanyama (WAEBRANIA 10:1-12; WAEFESO 5:2).

 

(2)      HAKIKA ALIKUWA MWANA WA MUNGU  (MST 51-54)

Baada tu ya Yesu kuitoa roho yake, matukio kadha ya miujiza yalitokea, yaliyowafanya askari waliokuwa wanamlinda kusema “HAKIKA HUYU ALIKUWA MWANA WA MUNGU”.  Sasa, ebu tuyaangalie matukio haya na maana yake:-

  1. PAZIA LA HEKALU LIKAPASUKA VIPANDE VIWILI Ni muhimu kukumbuka kwamba, ulikuwa wakati wa kusali na kutoa dhabihu ya jioni, katika hekalu.  Katika hekalu kulikuwa na Pazia la Hekalu, lenye urefu wa futi 60 kutoka darini hadi sakafuni.  Pazia hili liligawanya kati ya Patakatifu, na Patakatifu pa patakatifu, au mahali patakatifu sana (WAEBRANIA 9:1-3; KUTOKA 26:33).  Ilikuwa hakuna ruhusa ya mtu yeyote wa kawaida kuingia mahali patakatifu hata kuchungulia kwa dakika moja.  Akifanya hivyo, hukumu yake ni kifo (HESABU 4:17-20).  Mahali patakatifu waliingia makuhani peke yao.  Patakatifu pa patakatifu, aliingia Kuhani Mkuu peke yake, tena MARA MOJA KWA MWAKA akiwa na damu aliyoitoa kwa ajili ya nafsi yake na kwa dhambi za watu wengine (WAEBRANIA 9:6-7).  Vilevile kulikuwa na pazia lililowatenganisha Wayahudi na wale wasio Wayahudi (Mataifa) katika hekalu.  Sasa kwenye saa hii ya kusali nguvu ya ajabu isiyoonekana iliyararua mapazia na kuyafanya vipande Kila mmoja akashikwa butwaa pamoja na makuhani.  Pale msalabani, kwa damu yake Yesu, alitupa kila mmoja wetu uwezo wa kuzungumza na Mungu moja kwa moja bila kupitia kwa Kuhani, na pia alitoa pazia lililotutenganisha Mataifa na Wayahudi (WAEBRANIA 10:19-20; WAEFESO 2:14-18).
  2. NCHI IKATETEMEKA  – Tetemeko hili liliwafanya wenye dhambi wote, pamoja na askari waliomlinda kutetemeka kwa hofu.  Dhambi huleta hofu kubwa.  Siyo hilo tu, nchi ilitetemeka kwa hofu na woga wa kufunua kinywa chake kummeza Yesu Kristo ambaye damu yake inanena mema kuliko ya Habili (WAEBRANIA 12:24).  Ikiwa nchi ililaaniwa kwa kumeza damu ya Habili, ni zaidi sana kwa Yesu.  Ilikuwa ni rahisi kufunua kinywa chake na kuwameza Kora, Dathani na Abiramu na watu wa nyumba zao, waliokuwa wamemwasi Mungu (HESABU 16:27-34), kuliko kummeza Yesu asiyekuwa na doa.  Hivyo nchi ilitetemeka.  Vilevile nchi ilitetemeka kwa ajili ya watu wenye dhambi waikaao (AMOSI 8:4-8).
  3. MIAMBA IKAPASUKA  Wanadamu wakimpuuza Mungu na kuacha kumsifu Yesu mawe yatapiga kelele.  Hapa yalifanya hivyo.  Siyo hilo tu, hapa Yesu Kristo aliyaendea majeshi ya Shetani kwa ghadhabu na hasira kuu kwenda kuyavua mamlaka.  Hasira na ghadhabu hiyo ilifanya miamba kupasuka na nchi kutetemeka (NAHUMU 1:6; WAAMUZI 5:4; ZABURI 68:7-8).  Vilevile Yesu Kristo ni mwamba, miamba yote hupasuka mbele zake.  Siyo hilo tu kwa imani katika damu ya Yesu, mioyo yetu iliyo migumu kama jiwe au miamba hupasuliwa na kufanywa mioyo laini kama ya nyama (EZEKIELI 36:26-27).  Ndipo tunapoweza kuziona amri zake ni rahisi mno maana tumetakaswa, tumetahiriwa mioyo yetu.
  4. MAKABURI YAKAFUNUKA  – Makaburi ya Watakatifu waliojulikana Yerusalemu, yalifunuka wakati wa kufa kwa Yesu na kuleta utisho mkuu.  Hata hivyo, walitoka makaburini mwao BAADA YA KUFUFUKA KWAKE YESU kwa kuwa Yesu ndiye mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, limbuko lao waliolala (1 WAKORINTHO 15:20; UFUNUO 1:5).  Baada ya Yesu kufufuka, watakatifu hawa walifufuka nao na kuwatokea wengi Yerusalemu, Tukimwamini Yesu, kama alivyokwenda mbinguni, sisi nasi tutakwenda huko.  Kama alivyofufuka, sisi nasi tutafufuliwa katika Ufufuo wa Uzima (YOHANA 5:28-29).  Akida, yaani mkuu wa kikosi, na maaskari wenzake walipoyaona haya, NDIPO wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu.  Haupaswi kungojea kuyaona haya, ndipo tumkiri Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu, au ni Bwana na Mwokozi wa Ulimwengu.  Hatupaswi kungojea haya ndipo tukubali wokovu.  Tutakuwa tumechelewa.  Wakati wa Kunyakuliwa kwa Kanisa kutakakofanyika wakati wowote kuanzia sasa, Watakatifu watatoka makaburini namna hii na wenye dhambi wataogopa na kutetemeka, na kumkiri Yesu wakati wamechelewa.  Watakaochukuliwa ni wale waliookoka pasipo kuona, bali kwa imani (2 WAKORINTHO 5:7).

(3)      WANAWAKE KUMTUMIKIA MUNGU    (MST 55-56)

Ni uongo wa Shetani kwamba wanawake hawawezi kuwa Watumishi wa Mungu, wakahubiri, wakafundisha, wakatoa pepo au kumtumikia Mungu kwa namna nyinginezo.  Wanawake kumtumikia Mungu, ni jambo la Ki-Biblia hasa.  Nyakati hizi za mwisho, Roho wa Mungu atamwagwa kwa WOTE, binti watatabiri (kuhubiri ni kutabiri pia) na Roho huyu wa Mungu atamwagwa kwa WATUMISHI WA MUNGU WANAUME NA WANAWAKE (MATENDO 2:17-18).  Nyakati za Kanisa la Kwanza, wanaume na wanawake, wote walikuwa watendakazi, wakilihubiri Neno na kulifundisha (MATENDO 8: 1, 4).  Inatupasa kufuata mfumo huu wa ki-Biblia.  Mara kwa mara, katika Biblia, wanawake, wamekuwa na ujasiri wa kumtumikia Mungu na kuwa wanyenyekevu na watii kwa Yesu Kristo na Neno lake, kuliko wanaume.  Hapa tunaona wanawake waliomfuata Yesu kutoka Galilaya, karibu maili 100 kutoka Yerusalemu, wakija kumtumikia Yesu.  Hapa msalabani, hawakuwako wanafunzi wale kumi na moja wa Yesu kasoro Yohana (YOHANA 19: 25-26).  Wengi walikuwa wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea (LUKA 23:27).  Wanawake walikuwepo msalabani mpaka mwisho na tena walikuwapo kwenye mazishi yake (MST 61) na pia wanawake ndiyo waliokuwa wa kwanza kwenda kulitazama kaburi siku ya kufufuka kwa Yesu (MATHAYO 28:1).  Mwanamke ndiye aliyewapelekea habari za kufufuka kwa Yesu, Petro na Yohana, na kuwatia moyo, NDIPO nao wakachangamka!  Hapo mwanzo, walikuwa wamekata tamaa na kwenda kuvua samaki (YOHANA 20:1-3; 21:1-3).  Mwanamke Priska au Prisila alikuwa tayari kukatwa kichwa kwa ajili ya Injili aliyokuwa anaihubiri Paulo na Mwanamke Fibi aliwasaidia wengi mno (WARUMI 16:1-3).  Shime wanawake, tutende kazi ya Bwana! Wanaume pia tupate changamoto kwa watendakazi wanawake ambao wanatenda kazi ya Mungu kwa bidii pamoja na majukumu mengi ya kifamilia waliyo nayo.

(4)      KUZIKWA KWA YESU    (MST 57-61)

  Baada ya kufa, Yesu alizikwa.  Sisi nasi baada ya kufa pamoja naye inatupasa kuzikwa pamoja naye kwa njia ya Ubatizo (WAKOLOSAI 2:12).  Ikiwa tumeifia dhambi kwa kufa pamoja na Kristo kweli, hatuwezi kuwa wabishi kuhusu ubatizo wa maji tele baada ya kuokoka.  MAITI HASEMI, HUZIKWA TU!  Tena kumzika maiti, ni kumfunika kabisa kwa udongo, siyo kumnyunyizia udongo usoni.  Vivyo hivyo, ubatizo ni wa maji tele (YOHANA 3:22-23).  Mwanafunzi wa Yesu aliyekubaliwa kupewa maiti, alikuwa mtu tajiri, mstahiki (Mheshimiwa), mtu wa baraza ya mashauri (MATHAYO 27:57-58; MARKO 15:42-43).  Watu tuliookoka tulio matajiri, wenye vyeo, wenye elimu, inatupasa tuyatumie hayo kwa ajili ya kuishindania Injili.

(5)       KULINDA KWA KABURI   (MST 62-66)

  Wakuu wa Makuhani walimwita Pilato, BWANA, lakini Yesu walimwita MJANJA (MST 62-63).  Ndivyo walivyo viongozi wengi wa dini leo.  Walililinda kaburi na kulitia muhuri au lakiri ambayo siyo rahisi kuifungua, bila kujulikana, wakafikiri ni salama, lakini Yesu akafufuka.  Hata tukiwazuia watu kuifuata kweli kwa kuwazuia kwa lakiri, wataifuata kweli tu.  Neno la Mungu halifungwi (2 TIMOTHEO 2:9).

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

                                                            . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s