HAKUNA MTU ALIYEMWONA MUNGU

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

MAFUNDISHO YASIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA (S.K.B.) – KITABU CHA YOHANA

Somo la kwanza “NURU HALISI” INGIA HAPA; https://davidcarol719.wordpress.com/nuru-halisi/

SOMO 2:          HAKUNA MTU ALIYEMWONA MUNGU

L

eo, tunaendelea kujifunza Kitabu cha YOHANA na tutaangalia kwa makini YOHANA 1:15-28.  Katika mistari hii, pamoja na mambo mengine, tutajifunza juu ya, “HAKUNA MTU ALIYEMWONA MUNGU”.  Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika mistari hii katika vipengele vitano:-

(1)WAJIBU WA KUMSHUHUDIA YESU (Mst. 15);

(2)YESU NI ZAIDI YA NABII (Mst. 15);

(3)NEEMA NA KWELI (Mst. 16-17);

(4)HAKUNA MTU ALIYEMWONA MUNGU (Mst. 18);

(5)KUJITAMBULISHA KWA YOHANA MBATIZAJI (Mst. 19-28).

 

(1)      WAJIBU WA KUMSHUHUDIA YESU (Mst. 15)

Yohana alimshuhudia Yesu, akapaza sauti yake.  Kila mtu aliyeokoka ni shahidi wa Mungu (ISAYA 43:10).  Mara tu baada ya kuokolewa, kila mmoja wetu anawajibika kumshuhudia Yesu kwa watu wote kwamba ni Mwokozi mwenye uwezo wa kumsamehe mtu dhambi zake na kumpa uwezo wa kuzishinda.  Tunapaswa kushuhudia hivi waziwazi kwa kumkiri Yesu mbele ya watu, tukipaza sauti zetu bila aibu kama Yohana.  Tukiionea haya Injili yaani kumwonea haya Yesu na kuacha kumshuhudia, yeye naye atatuonea haya na kuacha kutukubali kuingia mbinguni (WARUMI 1:15-16; LUKA 9:26; MATHAYO 10:32-33).  Vile vile tunajifunza hapa kwamba katika kushuhudia kwetu tunapaswa kumshuhudia Yesu anayeokoa.  Hatupaswi kushuhudia kwamba dini zetu au madhehebu yetu ndiyo mazuri kuliko mengine.  Tuwashuhudie watu juu ya Yesu Mwokozi, wakiisha kuokolewa, ndipo tuwaeleze kuja kujifunza Neno la Mungu Kanisani ili waukulie Wokovu (1 PETRO 2:12; 1 YOHANA 1:1-2).

(2)      YESU NI ZAIDI YA NABII (Mst. 15)

Yesu alikuja nyuma ya Yohana Mbatizaji, lakini amekuwa mbele yake, kwa maana alikuwa kabla yake!  Maana yake nini maneno haya?  Yesu kama mtu au mwanadamu alizaliwa na tena kuanza huduma yake nyuma ya Yohana Mbatizaji.  Alikuja ulimwenguni nyuma ya Yohana Mbatizaji.  Yohana alimtangulia kuzaliwa na kuanza huduma.  Hata hivyo, Yesu kama Mungu, alikuwako kabla ya Yohana Mbatizaji (YOHANA 8:58; WAKOLOSAI 1:17-18; MIKA 5:2).  Yesu amekuwa mbele yake Yohana maana yake yeye ni mkuu zaidi kuliko Yohana Mbatizaji (YOHANA 1:27; 3:30-31).  Yesu anaitwa mkuu, Mwana wa Aliye juu (LUKA 1:31-32), lakini Yohana Mbatizaji anaitwa Nabii wake aliye juu (LUKA 1:76).  Yesu ni zaidi ya nabii.  Yesu ni Mungu pamoja nasi (MAHAYO 1:23; WAFILIPI 2:5-8).  Kwa misingi hiihii, Bikira Mariamu ni mama yake Yesu kama mwanadamu, lakini siyo mama yake Yesu kama Mungu.  Mungu hana mama (WAEBRANIA 7:3).  Kuna jambo jingine la kujifunza hapa.  Yohana Mbatizaji alimtangulia Yesu kuzaliwa na kuanza huduma ya Utumishi wa Mungu hapa duniani, lakini alipokuja Yesu nyuma yake, huduma yake ilikuwa kuu kuliko ya Yohana.  Hatupaswi kuona ajabu.  Mungu anaweza kufanya huduma ya mtu aliyezaliwa nyuma, kuokoka nyuma na kuanza huduma nyuma ya wazee waliomtangulia, kuwa na huduma iliyo kuu kuliko ya wazee hao.  Mungu anaweza kumbariki mdogo, akamwacha mkubwa kama kwa Yakobo na Esau au kwa Efraimu na Manase (WARUMI 9:10-16; MWANZO 48:8-19).

(3)      NEEMA NA KWELI (Mst. 16-17)

Neno Neema lina maana mbili.  Neema, ni upendeleo wa kuchaguliwa, bila kustahili kutokana na matendo yoyote aliyoyafanya mtu au sifa aliyo nayo mtu.  Neema pia, ni uwezo wa kushinda katika tabia na Utumishi wa Mungu sawasawa na mapenzi yake, tunaopewa na Mungu bila gharama yoyote au nguvu zetu.  Tunaokolewa kwa neema tu kwa njia ya imani (WAEFESO 2:4-5, 8-9).  Baada ya kuokoka pia, ni muhimu kufahamu kwamba tunafanya mapenzi yote ya Mungu kwa Neema ya Mungu.  Tumepokea Neema juu ya Neema.  Torati ilikuja kwa mkono wa Musa.  Yesu aliileta kweli.  Kweli ya Yesu ni ngumu zaidi kuifanya kuliko Torati (MATHAYO 5:27-28; 38-41; 43-48).  Hata hivyo siyo sisi tunaofanya.  Tukijifunza juu ya kweli yoyote na kuona ni ngumu, hatuna haja ya kuikimbia bali tunatakiwa kukikaribia kiti cha neema cha Mungu kwa ujasiri na hapo tunapoomba neema tunapewa neema ya kutuwezesha kuyafanya tuliyojifunza.  Kwa neema hiyo, Yesu ndiye anayefanya ndani yetu lile linalompendeza Mungu (WAEBRANIA 13:20-21).  Torati ya Musa haikuwa na msaada wowote wa kumsaidia mtu kuifanya.  Hakika tumepokea NEEMA JUU YA NEEMA, NEEMA NA KWELI!

 

(4)      HAKUNA MTU ALIYEMWONA MUNGU (Mst. 18)

Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote maana yake nini?  Mbona maandiko mengine yanataja watu waliomwomba Mungu?  (ANGALIA KUTOKA 24:9-11).  Linalosemwa hapa ni kwamba mtu hawezi kumwona Mungu kwa MACHO YA KIMWILI.  Yako macho ya aina nyingi.  Yako macho haya yanayoonekana na tena yako macho tunayoyatumia kuona katika ndoto wakati macho haya ya kawaida tumeyafumba, na tena yako macho ya rohoni.  Mtu hawezi kumwona Mungu ambaye ni Roho kwa MACHO YA KIMWILI, akaishi, kwa macho ya kimwili, mtu anaweza kumwona Mungu kwa sehemu tu ya umbo na siyo uso (HESABU 12:8; KUTOKA 33:17-23; 1 TIMOTHEO 6:16).  Hata hivyo, mtu anaweza kumwona Mungu anapokuwa katika Roho, kwa macho ya rohoni.  Mahali popote mtu alipomwona Mungu, alimwona katika hali hii, macho ya mwili na mwili wote ukiwa hauna sehemu katika jambo hili (UFUNUO 1:9-10; 2 WAKORINTHO 12:1-4; EZEKIELI 1:1, 26-28; DANIELI 7:9; MATENDO 7:56).  Katika roho, mtu ndipo pia anaweza kusema na Mungu uso kwa uso kama rafiki yake (KUTOKA 33:11).  Tunalojifunza hapa ni kwamba, Musa na watu wengine waliomwona Mungu kwa macho ya rohoni, walifanya hivyo kwa muda kidogo tu na wakarudia macho ya mwilini, lakini Yesu ambaye ni Mungu Mwana ndiye pekee aliye karibu na Baba (kifuani pake), hivyo wakati wote amekuwa akimwona.  Huyu ndiye aliyemfunua Mungu kwetu.  Tukiiona tabia ya Yesu alipokuwa duniani, tumeiona tabia ya Mungu.  Ni chapa ya nafsi yake (YOHANA 14:8-9; WAEBRANIA 1:3).  Yesu ni zaidi ya Musa!  Huyu ndiye aliyemfunua Mungu kwetu kuliko Musa maana anamjua zaidi.  Katika nyumba ya Mungu, Musa anaitwa mtumishi, na Yesu anaitwa mwana (WAEBRANIA 3:5-6).  Mtumishi wa nyumbani hawezi kumfahamu Baba mwenye nyumba kama mwana wake mwenyewe! Inatupasa kumsikia Yesu zaidi kuliko Musa (MATHAYO 17:1-5).

(5)      KUJITAMBULISHA KWA YOHANA MBATIZAJI (Mst. 19-28)

Wayahudi walituma kwake makuhani na walawi (wasaidizi wa makuhani) kutoka Yerusalemu na wakamwuliza Yohana Mbatizaji, “WEWE U NANI?” (Mst.19). Makuhani walikuwa watu wasomi wa neno la Mungu, wenye mamlaka katika Uyahudi na watu walioheshimiwa sana.  Hawa kutokana na kusoma kwao, walitarajiwa zaidi kumfahamu Yohana Mbatizaji ni nani kuliko watu wengine, lakini hawakuwa wamefunuliwa.  Mara kwa mara Waheshimiwa, Wasomi na watu wenye mamlaka katika jamii ambao tunatarajia wangekuwa wanaelewa upesi kuhusu wokovu, hawa wamekuwa hawapati mafunuo yoyote kutokana na kiburi na majivuno yao. Kwa kukosa mafunuo, wamekuwa wakiuliza “Wokovu ni nini?  Yesu ni nani?  Kweli ni nini?” n.k. (YOHANA 18:37-38; MATHAYO 11:25).  Kutokea kwa Yohana Mbatizaji kulikuwa kwa kushangaza miongoni mwa Wayahudi.  Baada ya maisha yake ya utoto, hawakumwona kabisa tena.  Maisha yake yalikuwa majangwani akila nzige na asali ya mwitu mpaka alipotokea kwao (LUKA 1:80; MATHAYO 3:4).  Mara tu baada ya kutokea na kuanza kuhubiri, makuhani walishangaa kuona watu wote wanamwendea na kubatizwa na kushangaa kwamba mbona anabatiza?  (MATHAYO 3:1-2, 5-8; YOHANA 1:25).  Mtu hawezi kuwa Mtumishi wa Mungu anayetumiwa na Mungu mpaka awe tayari kuishi mbali na watu muda mwingi wa maisha yake na kutenga muda mrefu akizungumza na Mungu kuliko watu.  Mtu anayependa mazungumzo na watu wakati wote, hawezi kutumiwa na Mungu kuvuta maelfu ya watu kama Yohana Mbatizaji.  Wachungaji wanaopenda mazungumzo na mizaha na kukaa kwenye magenge ya watu wa kawaida, watashangaa sana huduma ya mtu anayeishi majangwani jinsi inavyovuta watu wengi na kuuliza HUYU NI NANI? MBONA HATUMJUI!  Wanaweza wakafikiri anatumia hirizi au uganga kuwabatiza wengi hivyo!  Yohana Mbatizaji hakutumia hirizi au uganga, siri ilikuwa kukaa majangwani.  Alijitambulisha kwamba yeye ni sauti ya mtu aliaye nyikani.

JE, UNATAKA KUOKOKA SASA?

Tunasoma haya katika LUKA 1:77, “Uwajulishe watu wake wokovu, katika kusamehewa dhambi zao”.   Hii ina maana kwamba ukiisha kutubu dhambi zako leo utasamehewa kwa hakika, na hivyo kupata wokovu mara moja.  Je, kweli utasamehewa?  Jibu ni Ndiyo!  Yesu mwenyewe anasema katika YOHANA 6:37, “……….Wala yeyote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe”.  Hivyo kwa dhahiri, leo hii, dakika hii hii, utasamehewa na kupata wokovu.  Je, uko tayari kuokoka sasa na kuhesabiwa miongoni mwa wale watakaoingia mbinguni na kuishi na Mungu milele, hata wakiiaga dunia sasa hivi?  Ukiwa tayari kuifuatisha sala ifuatayo ya toba, mara tu baada ya sala hii, nitakuombea na kwa ghafla utawezeshwa kushinda dhambi.  Je, uko tayari kuifuatisha sala hii sasa?  Najua uko tayari.  Basi sema maneno haya,  “Mungu Baba, natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Naomba unisamehe na kuniosha dhambi zangu kwa damu ya Yesu iliyomwagika msalabani.  Niwezeshe kushinda dhambi kuanzia sasa.  Liandike sasa jina langu katika kitabu cha uzima mbinguni.  Asante kwa kuniokoa, katika Jina la Yesu, Amen”.  Sasa ninaomba kwa ajili yako, “Mungu Baba msamehe kiumbe wako huyu dhambi zake zote, na mpe uwezo wa kushinda dhambi kuanzia sasa na kumuokoa. Mbariki kwa baraka zote katika Jina la Yesu, Amen”.  Tayari umeokoka.  Ili uzidi kuukulia wokovu, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI!!!

                                     . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

                                                          . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .         

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “note” hii, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s