HATARI YA KUPENDA NAFSI

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

SOMO:   HATARI YA KUIPENDA NAFSI

T

unaendelea tena leo, kujifunza Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu.  Leo, tunatafakari kwa makini YOHANA 12:12-28.  Katika mistari hii, tutajifunza “HATARI YA KUIPENDA NAFSI“, pamoja na mengine mengi.   Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika mistari hii, katika vipengele tisa:-

 

(1) KUINGIA KWA YESU YERUSALEMU (MST. 12-15);

(2) UWEZEKANO WA WANAFUNZI WA YESU KUSHINDWA KUYAFAHAMU   

 MAMBO FULANI MWANZONI (MST. 16);

(3) SABABU YA MKUTANO MKUBWA KUMLAKI YESU (MST. 17-18);

(4) KUSHINDWA KWA SHETANI KUZUIA MAFANIKIO YA INJILI (MST. 19);

(5) UTARATIBU WA KUMWONA YESU (MST. 20-23);

(6) JINSI YA KUTOA MAZAO MENGI (MST. 24);

(7) HATARI YA KUIPENDA NAFSI (MST. 25);

(8) MASHARTI NA FAIDA ZA KUMTUMIKIA MUNGU (MST. 26);

(9) JINSI YA KULIONA JINA LA BWANA LIKITUKUZWA KWETU (MST. 27-28).

 

(1)            KUINGIA KWA YESU YERUSALEMU (MST. 12-15)

Wakati huu, ilikuwa siku nne kabla ya Sikukuu ya Pasaka.  Watu wengi walitoka mbali sana na kuja kwenye Sikukuu alizoziamuru Bwana, ili kuja kumwabudu.  Nyakati za Biblia, Mungu hakupendezwa hata kidogo kumwona mtu yeyote anabaki nyumbani wakati anapotakiwa kwenda katika ibada.  Mungu aliweka adhabu kali kwa yeyote aliyepuuza kuhudhuria ibada.  Adhabu hii, iliambatana na kukosekana kwa mvua na kupigwa kwa auni; na ilienea katika jamii yote, au taifa lote ikiwa walipuuza kuhudhuria ibada (ZEKARIA 14:17-19).  Ili kukwepa adhabu hii, watu walitoka mbali sana kwa wingi wao, na kuja kuhudhuria Ibada.  Hata leo, ni vivyo hivyo.  Mungu hapendezwi na yeyote anayepuuza kuhudhuria ibada zote.  Tunajikosesha baraka tele na kujiletea maafa, ikiwa hatuhudhurii ibada zote.  Watu hawa waliposikia Yesu anakuja Yerusalemu walitoka nje kwenda kumlaki.  Habari za kuja kwa yesu kulinyakua Kanisa, tayari zimekwisha kutufikia (UFUNUO 22:7; 3:11; WAEBRANIA 10:37).  Ni muhimu kwa kila mmoja wetu kujiuliza kama tumejiweka tayari kumlaki Yesu na kuonana naye ili tusije tukawa kama wanawali waano wapumbavu ambao hawakujiweka tayari (AMOSI 4:12; MATHAYO 25:1-13).  Watu hawa walimlaki kwa kutwa matawi ya mitende.  Matawi ya mitende, ilikuwa ishara ya ushindi mkubwa.  Wakapiga kelele wakisema HOSANA!  Hosana, ni neno la lugha ya KIARAMU, lenye maana, “BWANA OKOA“.  Wakapiga kelele, wakimkiri yesu hadharani kwamba ni Mfalme wa Israeli na Masihi aliyetabiriwa kwamba atakuja akiwa amepanda punda, naam mwana punda (ZEKARIA 9:9).  Watu hawa waliotoka nje ya Yerusalemu waliwazidi wakaao Yerusalemu na kumpokea Yesu kipekee.  Wa kwanza, atakuwa wa mwisho, tusipoangalia kwa makini!  Sisi tunaojiona kwamba tumekuja Kanisani muda mrefu na ni wenyeji, tuna hatari ya kupitwa na wale wapya wanaokuja ikiwa tumekwisha kulizoea Neno kama watu wa Yerusalemu.  Tunajifunza pia hapa kwamba, huduma zetu huanzia chini, kwenye hori ya kulia ng’ombe, kama Yesu, lakini tukiwa waaminifu na kuitenda kazi ya Mungu bila kujali upinzani tutakaoupata, hatimaye Bwana atatupandisha juu sana, na watu watazishangilia huduma zetu.

 

(2)            UWEZEKANO WA WANAFUNZI WA YESU KUSHINDWA KUYAFAHAMU MAMBO FULANI MWANZONI (MST. 16)

“Mambo hayo, wanafunzi wake hawakuyafahamu HAPO KWANZA“.  Inahitaji kufunuliwa na kutiwa nuru macho ya miyo yetu, ili tuyaelewe mambo ya Mungu, yanapokuwa katika hatua za mwanzoni (WAEFESO 1:17-18).  Huduma ya Paulo Mtume, ingawa ilitoka kwa Mungu mwenyewe, haikukubalika Yerusalemu, walipokuwapo Mitume wenye karama mbalimbali (MATENDO 9:15,26; WARUMI 15:30-31).  Hatupaswi kuona ajabu, wanafunzi wa Yesu wanapokuwa hawafahamu kwamba huduma zetu zimetoka kwa Mungu.  Ni kawaida katika hatua za mwanzo kwa wanafunzi kutokuelewa mambo fulani fulani, lakini tukidumu kutenda kazi, hatimaye yale yaliyofichika huwa wazi.  Tunaweza pia kujifunza somo fulani mwanzoni, tukawa hatulielewi; baadaye ndipo ufahamu ukatujia.  Ndiyo maana ni muhimu sana kuomba kwamba Mungu atupe roho ya hekima na ya ufunuo katika kulijua Neno lake na pia atutie nuru macho ya mioyo yetu ili tuyafahamu maneno yake pale tu tunapoyasikia.

 

(3)            SABABU YA MKUTANO MKUBWA KUMLAKI YESU (MST. 17-18)

Mkutano mkubwa walikwenda kumlaki Yesu, kwa kuwa walisikia kwamba alikuwa amefanya ishara ya kumfufua Lazaro kutoka kaburini.  ISHARA, ni tendo lolote linalodhihirisha waziwazi uwezo wa Mungu unaoweza kuyafanya yale yale yasiyowezekana kwa wanadamu.  Yesu Kristo alikuwa ametoa mahubiri mazuri sana katika hekalu na masinagogi mengi Yerusalemu.  Hata hivyo, hakuwahi kupata kuona mkutano mkubwa hivi ukimlaki mpaka pale walipoona ishara hii kubwa.  Hii inatufundisha umuhimu wa miujiza katika injili ikiwa tunataka kuwavuta wengi kwa Yesu.  Neno peke yake, halitoshi, lisipoambatana na ishara (WARUMI 15:18-19).  Hatuna budi kuomba ishara kubwa zifanyike kati yetu kulithibitisha Neno, ili mkutano mkubwa uvutwe (MATENDO 4:29-30; MARKO 16:19-20).

 

(4)            KUSHINDWA KWA SHETANI KUZUIA MAFANIKIO YA INJILI (MST. 19)

Pamoja na mabaraza ya Mafarisayo na maamuzi yao kinyume na Yesu, bado umati mkubwa unamfuata hapa kiasi ya kwamba wanajiona hawafai neno lolote maana ulimwengu wote unakwenda nyuma yake.  Hatupaswi kubabaishwa na vita vya Shetani katika huduma zetu.  Kadri anavyounguruma, ndivyo tunavyozidi kushinda na zaidi ya kushinda (WARUMI 8:35-37).

 

(5)            UTARATIBU WA KUMWONA YESU (MST. 20-23)

Mahali hapa kulikuwa kuna umati mkubwa waliotaka kumwona Yesu, baada ya kusikia juu ya ishara aliyoifanya ya kumfufua Lazaro.  Hata hivyo, kila mmoja hakuweza kumwona Yesu tu kama alivyotaka.  Kulikuwa na utaratibu wa kufuata.  Hapa tunaona wakimwendea filipo na Filipo akaenda akamwambia Andrea kisha ndipo taarifa zikamfikia Yesu na kuwa tayari kuwaona.  Katika Kanisa kubwa kama hili, hatuna budi kufuata utaratibu huu pia.  Kabla ya kumwona Mchungaji, inatubidi tuwaone Viongozi wa makanisa ya Nyumbani, Seksheni, Zoni, Mhudumu Mkuu n.k.  Utaratibu huu ni wa lazima kwenye umati mkubwa wa watu.  Matatizo yote yakimwndea mtu mmoja, siyo mapenzi ya Mungu, maana mengine yaliyo madogo yanaweza kupata ufumbuzi kwa viongozi wengine (KUTOKA 18:13-26), na kumpa Kiongozi wetu nafasi ya kutosha ya kuutafuta uso wa Mungu, na kushughulikia yale yaliyo magumu.

(6)            JINSI YA KUTOA MAZAO MENGI (MST. 24)

Mbegu kabla ya kutoa mazao mengi, hufa kwanza, na kuzikwa ardhini, ndipo huota na kutoa mazao mengi.  Yesu alikufa na kuzikwa, kisha akafufuka na kutuvuta wote kwake (MST. 32).  Hatuwezi kupata mazao mengi, ikiwa hatuko tayari kuona fedha zetu zainakufa pale tunapotoa fungu la kumi la mapato yetu na sadaka.  Hatuwezi kutoa mazao mengi ikiwa tunajiona tunajua.  Hatuna budi kuzika kiburi na majivuno na lolote linalotufanya tujione tunajua; ndipo tunapoweza kutoa mazao mengi.

 

(7)            HATARI YA KUIPENDA NAFSI (MST. 25)

Kuipenda nafsi yetu, ni kutaka kutimiza matakwa yote ya miili yetu.  Ni muhimu kufahamu kwamba mwili, sikuzote hushindana na Roho zetu (WAGALATIA 5:16-17).  Mwili hutaka tufanye yasiyo mapenzi ya Mungu.  Mwili hautaki tufanye maombi, tusome Neno la Mungu, tushuhudie na kufuatilia watoto wachanga kiroho n.ki.  Mwili, hutaka tuupambe kinyume na Neno la Mungu.  Tukizipenda nafsi zetu, hatuwezi kumtolea Mungu, kumtumikia au kufanya lolote linalompeneza Mungu.  Matokeo yake, tutaziangamiza nafsi zetu.  Hatuna budi kuzichukia nafsi zetu na kutiisha miili yetu na kuzifanya roho zetu ziwe na utawala juu ya miili yetu na kukatalia matakwa yake.

 

(8)            MASHARTI NA FAIDA ZA KUMTUMIKIA MUNGU (MST. 26)

Wengi wetu wanapenda kumtumikia Mungu, lakini hawajui masharti ya kumtumikia.  Sharti kubwa ni KUMFUATA kwanza katika tabia (1 PETRO 1:15-16).  Tukijaribu kumtumikia bila kumfuata, tunalitukanisha Jina la Mungu wetu bure (WARUMI 2:21-24).  Tukiwa na tabia ya Kristo, kisha tukamtumikia, pale alipo yesu, ndipo tutakapokuwa.  Mungu Baba hutuheshimu na kutupa kipaumbele katika mengine yote hapa duniani (KUTOKA 23:25-26; ISAYA 65:13-14).  Hatimaye tutapata thawabu kubwa mbinguni kama wafanyakazi bora wanavyopata tuzo katika Serikali na Mashirika.  Tuzo ya Mungu ni ya kipekee mno.

 

(9)            JINSI YA KULIONA JINA LA BWANA LIKITUKUZWA KWETU (MST. 27-28)

Roho yake Yesu ilifadhaika kwa ajili ya dhambi zetu.  Hili lilimfanya Baba alitukuze Jina lake kwek.  Sisi nasi, roho zetu zikifadhaika kwa ajili ya dhambi za watu wengine na kuwaombea kwa kuugua ili waokoke, Jina la Bwana litatukuzwa kwetu na tutaona mambo makubwa kama Habakuki (HABAKUKI 1:2-4).

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements

2 comments on “HATARI YA KUPENDA NAFSI

  1. keep on preaching Bishop, real your lesson is so wonderful then it has left my faith from ascertain level of understanding God, my request to you is to continue teaching the reality and truth of Jesus Christ so that most of believers could gain message from what God has given to you and be able to deliver to us.

    • keep on preaching Bishop, real your lesson is so wonderful then it has left my faith from ascertain level of understanding God, my request to you is to continue teaching the reality and the truth of Jesus Christ so that most of believers could gain message from what God has given to you and be able to deliver to us.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s