JE UNAFAHAMU UZURI WA MBINGUNI?

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

Somo:   Je Unafahamu uzuri wa Mbinguni?

Mpendwa msomaji, pole sana na shughuli nyingi za kila siku.  Ninajua kwamba muda wako ni mchache sana, kutokana na shughuli zako nyingi.  Hata hivyo ninakuomba muda wako mfupi tu, ili tuzungumze juu ya jambo muhimu ambalo nimeona kwamba ni vema nikushirikishe.  Je umekubali ombi langu?  Natumaini umekubali.  Asante sana.  Basi ninakusihi tufuatane pamoja katika mazungumzo haya.

Mpendwa msomaji, huenda utakuwa umewasikia watu wengi wanaofiwa na ndugu, jamaa au marafiki zao wapendwa, wakisema, “Mungu waweke mahali pema peponi“.  Jambo hili linadhihirisha jinsi kila mmoja wetu anavyoamini kwamba kuna mahali pema peponi yaani mbinguni na tena inaonyesha jinsi sisi sote tunavyopenda kwenda huko, sisi na jamaa zetu.  Je wewe una shauku ya kwenda mahali pema peponi au mbinguni, baada ya kuiaga dunia hii?  Najua wewe pia una shauku ya kwenda mbinguni siku moja.  Hata hivyo, shauku yako itaongezeka zaidi utakapokuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu uzuri wa mbinguni.  Peponi au mbinguni, ni wapi na kukoje?  Peponi au mbinguni, kuna uzuri usioweza kufananishwa.  Tukifahamu jinsi mbinguni kulivyo kuzuri, kila mmoja wetu atazidi kuwa na shauku ya kufika huko siku moja.  Mpendwa msomaji, tufuatane basi ili upate ufahamu wa kutosha kuhusu mbinguni au peponi.

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

     Peponi au mbinguni ni wapi na kukoje?

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Mbinguni au peponi, ni juu sana, mbingu ya tatu.  Biblia inasema katika 2 WAKORINTHO 12: 2-4, “Namjua mtu mmoja katika kristo,……Mtu huyo alinyakuliwa juu mpaka mbingu ya tatu.  Nami namjua mtu huyo…….ya kuwa alinyakuliwa mpaka Peponi………”   Mbingu ya tatu ni wapi?  Mbingu ya kwanza, ni hii iliyo na mawingu yanayoleta mvua, na mawingu mengine.  Ni anga hili lililo juu ambalo sehemu yake huonekana kwa macho ya kawaida.  Ndege au eropleni zote zinazobeba abiria, huruka katika mbingu hii ya kwanza.  Mbingu ya pili, ni  mbingu iliyo mbali zaidi yenye sayari na nyota zote. Sayari zilizoko katika mbingu ya pili ni pamoja na Zebaki, Zuhura, Mars, Mshtarii, Zahali, Uranus, Neptune, na Pluto.  Sayari nyingine ziko mbali sana.  Kwa mfano umbali wa dunia yetu kutoka kwenye jua ni maili 93 milioni (kilometa 148,800,000), lakini umbali wa sayari ya pluto kutoka kwenye jua ni maili 3,666 milioni (Karibu kilometa 5,900 milioni).  Nyota ziko nyingi sana, zinakisiwa kufikia 400 bilioni! Nyota ziko mbali sana na dunia yetu.  Nyota iliyo karibu zaidi na dunia, iko karibu maili 26,000 bilioni (karibu kilometa 42,000 bilioni).  Sasa basi, baada ya sayari zote hizi na nyota hizi, ndiyo tunafika mbingu ya tatu.  Mbingu ya tatu, au mbinguni, au Peponi, kwa msingi huu ni kilometa mabilioni kwa mabilioni kutoka hapa duniani.  Yesu kristo alipopokelewa na wingu, na kupaa kwenda juu mbinguni (MATENDO 1:9-11), alikwenda mbali sana kiasi hiki.  Huko ndiko waliko watakatifu waliotutangulia.

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .   Mbinguni au peponi, ni kilometa mabilioni kwa mabilioni kutoka hapa duniani

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

Tupige hatua tena na kuangalia mambo mengine.  Sasa je, mtu anapokufa, anasafirije kwenda mbinguni, mbali kiasi hiki?  Hatupaswi kuogopa kifo, ikiwa tunaishi maisha yaliyo mbali na dhambi.  Biblia inasema katika ZABURI 116:15, Ina thamani machoni pa Bwana, mauti ya wacha Mungu wake.  Kufa kwa watakatifu ni faida (WAFILIPI 1:21).  Ni heri kwa wafu wafao katika Bwana (UFUNUO WA YOHANA 14:13).  Kufa kwa mtu anayeishi maisha yaliyo mbali na dhambi, ni mwanzo tu wa utukufu.  Mtu anayeishi maisha mbali na dhambi, anapokufa, roho yake humiminwa katika mwili mwingine wa roho unaitwa mwili wa mbinguni, kama mafuta yaliyo katika chombo kibovu kinachovuja, yanavyoweza kumiminwa katika chombo kingine kilicho kizuri.  Kufa ni kumiminwa!  Mtume Paulo aliyepata neema ya kuchukuliwa na kupelekwa mpaka mbingu ya tatu wakati wa uhai wake (2 WAKORINTHO 12:2-4), ulipofika wakati wa kufariki kwake, alijua ni wakati mzuri wa kumiminwa.  Kwa maneno yake, katika 2 TIMOTHEO 4:6, alisema, Kwa maana, mimi sasa namiminwa, na wakati wa kufariki kwangu umefika.

Kuhusu miili ya mbinguni, Biblia inasema katika 1 WAKORINTHO 15:40-41, 44, Tena kuna miili ya mbinguni, na miili ya duniani, lakini fahari yake ile ya mbinguni ni mbali, na fahari yake ile ya duniani ni mbali.  Kuna fahari moja ya jua, na fahari nyingine ya mwezi, na fahari nyingine ya nyota……Ikiwa uko mwili wa asili, na wa roho pia uko.  Miili hii tuliyo nayo ni mibaya sana.  Ni kama vyombo vibovu. Fahari yake, yaani uzuri wa ile miili ya mbinguni ni zaidi sana kuliko miili hii tuliyo nayo.  Miili ya mbinguni inang`aa mno na kupendeza sana.  Mtu huwa na mwili mzuri zaidi ya ule wa malaika! Mtakatifu anapokata roho, roho yake mara moja humiminwa katika mwili mzuri wa jinsi hii.   Mtu akiwa katika mwili wa mbinguni, atapenda kujitazama wakati wote.  Mwili huu hauna makovu wala ulema wala hauna makunyanzi ya uzee!  Baada ya mtu kuwa na mwili mzuri wa jinsi hii, huvikwa mavazi mazuri meupe sana yanayometameta sana.  Weupe wa mavazi haya, ni weupe usio na mfano duniani (UFUNUO WA YOHANA 3:4-5;  UFUNUO WA YOHANA 7:9;  MARKO 9:2-3).   Baada ya kuvikwa mavazi haya, mtu hufunguliwa mlango wa gari na malaika, na kuingizwa katika gari zuri sana lisilokuwa na mfano duniani. Yako mabilioni ya magari ya Mungu, yanayowasubiri watakatifu.  Biblia inasema katika ZABURI 68:17, Magari ya Mungu ni ishirini elfu, maelfu maelfu.  Mtu huchukuliwa na malaika katika magari haya yanayoitwa magari ya moto, yanayoambatana na farasi wa moto na kuchukuliwa kwenda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli (LUKA 16:22;  2 WAFALME 2:11).

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

Mtu hufunguliwa mlango wa gari na malaika, na kuingizwa katika gari zuri sana

                                                  lisilokuwa na mfano duniani

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

Magari yanayoitwa magari ya kifahari yanayowabeba Marais na Wafalme duniani kama Mercedes Benz, BMW n.k; si mali kitu yanapolinganishwa na magari haya.  Magari ya Mungu hayatumii dizeli au petroli, bali huendeshwa na upepo wa kisulisuli, na huenda kasi sana.  Kwa muda mfupi sana, mtu hufika mbinguni, na hulakiwa na malaika waliotanda njiani kushoto na kulia wakiimba nyimbo za shangwe, inayopita ile ambayo huwako mbinguni, mtu mmoja anapotubu dhambi zake hapa duniani (LUKA 15:10, 32).  Hakuna mapokezi yoyote ya Rais au Mfalme yeyote duniani, yanayolingana na mapokezi ya mtu anayeingia mbinguni, yanayofanywa na malaika.

Sasa tupige hatua nyingine.  Mbinguni kwenyewe kukoje?  Mbinguni ni nchi iliyo bora kuliko nchi yoyote duniani (WAEBRANIA 11:16).  Waza juu ya nchi yoyote duniani inayowavutia watalii wengi kutokana na uzuri wake.  Nchi hii siyo mali kitu ikilinganishwa na Peponi.  Mbinguni ni kuzuri mno! Hakuna usiku wala mchana.  Hakuna joto wala baridi.  Jua au mwezi havitumiki kutoa mwangaza. Utukufu wa Mungu ndiyo nuru ya mbinguni (UFUNUO WA YOHANA 21:23-25).  Neno “Peponi”, linatokana na neno la kiyunani, “Paradeisos”, linalotafsiriwa pia, “Paradiso”, na kwa tafsiri fasaha, lina maana, “bustani nzuri kubwa iliyojaa matunda mazuri” na tena lina maana “mahali palipojaa furaha na raha kuu isiyo na kifani” (UFUNUO WA YOHANA 2:7;  WAEBRANIA 4:1, 11).  Matunda ya miti iliyomo katika bustani hii isiyokuwa na mfano, ni pamoja na mti wa uzima uzaao matunda aina kumi na mbili. Maisha mbinguni, ni pamoja na kula matunda haya katika bustani ya Mungu, na kupunga upepo wa raha kuu isiyo kifani, Paradiso (UFUNUO WA YOHANA 2:7;  UFUNUO WA YOHANA 22:2).

Kipi cha ziada tena kuhusiana na mbinguni?  Mbinguni ni mji uliobuniwa na kujengwa na Mungu (WAEBRANIA 11:10, 16).  Miji yote ya dunia hii imebuniwa na kujengwa na wanadamu wenye upungufu wa ubunifu wa michoro, fedha, vifaa n.k;  Mbinguni, ni mji uliobuniwa na Mbunifu Mkuu, Mungu mwenyewe mwenye uwezo wote.  Hakuna mji kama huu duniani.  Barabara zake siyo za lami, bali ni za dhahabu iliyo kama kioo kiangavu ambayo hakuna mfano wake duniani.  Mtu anapotembea barabarani, hujiona kama katika kioo (UFUNUO WA YOHANA 21:21).  Katika YOHANA 14:2, Yesu anasema katika mji huu kuna “makao” mengi.  Neno la Kiyunani linalotafsiriwa hapa “makao” ni “mone”, linalotafsiriwa katika kiingereza “Mansion”, katika Biblia ya tafsiri ya King James Version.  “Mansion” ni jumba kubwa la kifahari.  Jumba la Meya wa Jiji la London, Uingereza (Lord Mayor of London), linaitwa “Mansion House”. Vinyo hivyo mbinguni, kuna makao mengi, au majumba mengi ya kifahari.  Kila mtu atakayeingia mbinguni, atapewa “kao” au “jumba mojawapo la kifahari”, la kuishi.  Kao lako linakusubiri! Majumba haya, hayakujengwa kwa tofali za sementi au udongo, bali kuta zake zimejengwa kwa madini ya aina nyingi. Biblia inasema katika UFUNUO WA YOHANA 21:18-20, Na majenzi ya ule ukuta wake yalikuwa ya yaspi, na mji ule ulikuwa wa dhahabu safi mfano wa kioo safi.  Na misingi ya ukuta wa mji ilikuwa imepambwa kwa vito vya thamani vya kila namna.  Msingi wa kwanza ulikuwa yaspi; wa pili yakuti samawi; wa tatu kalkedoni; wa nne zumaridi; wa tano sardoniki; wa sita akiki; wa saba krisolitho; wa nane zabarajadi; wa kenda (tisa) yakuti ya manjano; wa kumi krisopraso, wa kumi na moja hiakintho; wa kumi na mbili amethisto”.

Vito hivi au madini haya, yanafanya majumba ya mbinguni, yapendeze mno.  Yaspi, ni madini yanayong’ara sana yenye rangi ya kijani iliyochanganyika na bluu.  Yakuti samawi, ni mawe ya bluu, mazuri sana yenye ugumu unaofuatia madini ya almasi.  Kalkedoni, ni aina ya madini mazuri sana yenye rangi aina nne mbalimbali – nyekundu iliyochanganyika na njano, hudhurungi (brown) iliyochanganyika na nyeusi, bluu iliyochanganyika na nyeupe, na rangi ya maziwa.  Zumaridi, ni madini yenye rangi ya damu. Krisolitho, ni madini yaliyo kama dhahabu, ila yana rangi ya kijani iliyochanganyika na njano. Zabarajadi, ni madini maangavu (yanayoona ndani), yenye rangi ya bluu iliyochanganyika na kijani. Yakuti maanjano, ni madini mazuri yenye rangi ya njano na mchanganyiko wa kijani.  Krisopraso, ni madini yenye rangi tatu pamoja; njano, kijani na bluu.  Hiakintho, ni madini yenye rangi nyekundu iliyochanganyika na njano.  Amethisto, ni madini yenye rangi ya zambarau, yenye bluu na wekundu ndani yake.

Nini zaidi?  Mwangaza wa mbinguni siyo kama wa duniani usio na rangi.  Mwangaza wa mbinguni ni wa rangi ya yaspi  yaani kijani iliyochanganyika na bluu (UFUNUO 21:11).  Mavazi meupe ya wale walioko mbinguni, hubadilika rangi mara kwa mara kutokana na rangi ya mwangaza na ya majengo hivyo kufanya watu wapendeze mno.  Ndani ya makao ya mbinguni kuna fenicha za kifahari.  Fenicha alizoagizwa Musa kuzitengeneza na kuziweka katika maskani, zilikuwa mfano tu wa fenicha za mbinguni (WAEBRANIA 8:5;  KUTOKA 25:9-40).  Chemichemi za maji na mito ya maji ya uzima inauzunguka mji. Mbinguni kuna kula na kunywa, hakuna mauti wala maumivu au taabu (LUKA 22:14-16, 29-30;    UFUNUO WA YOHANA 2:17;  UFUNUO WA YOHANA 21:4-5;  UFUNUO WA YOHANA 14:13).  Kuna kuimba nyimbo za sifa, na vinanda (UFUNUO WA YOHANA 14:2-3;  UFUNUO WA YOHANA 15:2-4). Ufahamu wetu utaongezeka (1 WAKORINTHO 13:12).  Kuna mengi zaidi yasiyotamkika katika lugha hii ya duniani (2 WAKORINTHO 12:4).  Ni heri twenda wenyewe kujionea.  Tusikubali mume au mke kutuzuia kuingia mbinguni maana mbinguni hakuna kuoa au kuolewa (LUKA 20:34-36;  MATHAYO 22:30).

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “note” hii, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.

                                                         UBARIKIWE NA BWANA YESU!!!

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s