JEHANAMU YA MOTO NI WAPI NA KUKOJE?

ZACHARY KAKOBE

Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

Somo:  Jehanum ya Moto ni wapi na Kukoje?

Miaka ipatayo thelathini iliyopita nilikuwa nimezama sana katika dhambi.  Nikiwa katika lindi hilo la dhambi, sikutaka kusikia chochote kwa mtu yeyote aliyenieleza kwamba niache dhambi, na eti niokoke.  Niliwaona watu wanaohubiri mambo ya kuokoka, wameshindwa maisha (frustrated), wamechanganyikiwa na tena hawajasoma.  Nakumbuka siku moja, mhubiri mmoja alinihubiria na kuniambia, ”Acha dhambi, au sivyo utatupwa katika Jehanum moto”. Unajua nilimjibuje!  Nilimwambia, ”Wewe usinibabaishe na hiyo Jehanum ya moto.  Potelea mbali nikienda motoni, pilipili usizozila zakuwashiani?  Usinifuate katika maisha yangu, chukua “time” yako!”

Baada ya miaka kadha kupita,nilipokuja kusikia mafundisho kuhusu jinsi kulivyo huko Jehanum ya moto, nilikuja kufahamu kwamba yule mhubiri nilimjibu potelea mbali nikienda motoni, kwa sababu tu sikuwa ninaelewa lolote kuhusu jinsi Jehanum kulivyo; kwa kuwa sikuwahi kufundishwa mafundisho hayo na kiongozi wangu wa dini.  Tangu niliposikia mafundisho hayo, maisha yangu yalibadilika kabisa. Mpendwa msomaji, huenda hata wewe hujasikia mafundisho halisi kuhusu jinsi kulivyo Jehanum ya moto, kama mimi nilivyokuwa; ndiyo maana nimeona leo nikushirikishe mafundisho haya kupitia katika “note” hii.  Mungu akubariki kwa kuendelea kusoma “note” hii.  . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .   

           Potelea mbali nikienda motoni, pilipili Usizozila zakuwashiani

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .   

               Biblia inaeleza waziwazi kwamba mtu anapokufa, sekunde ileile ya kufa kwake anakabiliwa na hukumu.  Tunasoma katika WAEBRANIA 9:27, Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu.  Watu wanapofundisha kinyume na kweli ya Neno la Mungu, hufundisha kwamba mtu anapokufa analala tu, na hakuna lolote la hukumu mara moja wakitumia maandiko yafuatayo na kuyatafsiri visivyo – MATHAYO 27:52;  1 WAKORINTHO 15:20;  YOHANA 11:11-14 n.k; na pia wanasema wafu hawajui lolote kwa kutumia maandiko kama MHUBIRI 9:5.  Ilivyo ni kwamba, kinachobaki kaburini ni mwili tu.  Roho ya mtu huondoka na kuingia katika mwili mwingine, unaoitwa mwili wa roho.  Miili tuliyo nayo wanadamu kabla ya kufa inaitwa miili ya asili.  Tunasoma katika 1 WAKORINTHO 15:40, 44, Tena kuna miili ya mbinguni, na miili ya duniani,……Ikiwa uko mwili wa asili, na wa roho pia uko.

Mwili wa asili, ndiyo unabaki kaburini, lakini roho ya mtu huondoka kama tunavyosoma katika MHUBIRI 12:7, “Nayo mavumbi ya nchi kuirudia nchi kama yalivyokuwa, nayo roho kumrudia Mungu aliyeitoa”.  Mwili wa asili, ndiyo unaobaki kaburini, na huo ndiyo unaotajwa kwamba umelala, haujui lolote, na hauna kumbukumbu; lakini pasipo mwili huo, mtu atamwona Mungu na kukabiliana na hukumu yake dakika ileile baada ya kufa (AYUBU 19:26).  Ikiwa mtu ameishi katika mapenzi ya Mungu, mara tu baada ya kufa huchukuliwa mbinguni (LUKA 23:43;  LUKA 16:22).  Ikiwa ameishi na kufa katika dhambi, bila kutubu dhambi zake na kuokoka, hukumu yake mtu huyo, huwa ni kutupwa katika Jehanum ya moto, mara tu baada ya kufa, kama Yule tajiri anayetajwa katika Biblia (LUKA 16:19-24).

Mbinguni ni juu (mbingu ya tatu), lakini kuzimu au Jehanum ya moto, ni pande za chini za nchi (2 WAKORINTHO 12:1-4;  MITHALI 15:24;   ZABURI 63:9;  EZEKIELI 31:14).  Mara mtu anapokufa, hufika kwenye njia panda.  Kila mmoja hupenda kwenda mbinguni kuzuri, hata hivyo ikiwa jina lake haliko katika kitabu cha uzima cha mbinguni, hulazimika kwenda Jehanum ya moto.  Mtu anayetakiwa kwenda motoni, huchachamaa na kukataa kwenda kwenye njia mbaya inayotisha ya motoni.  Hali hii wakati mwingine inaweza kuonekana katika mwili wa asili kwa kumwangalia mtu anavyotapatapa na kuhangaika sana katika kufa kwake.  Kutokana na mtu asivyopenda kwenda motoni na kutaka kwenda mbinguni asikotakiwa, mtu hulazimika kukamatwa kwa nguvu na malaika wa kutisha, na kutupwa katika Jehanum ya moto; inayojulikana pia kwa jina jingine, giza la nje; kama tutakavyoona baadaye kidogo (UFUNUO 19:20;  UFUNUO 20:10;  MATHAYO 25:30).

Huko motoni Jehanum kukoje?  Mwanangu, kunatisha, nashindwa hata nikueleze vipi unielewe. Moto  wa milele, hatukuwekewa wanadamu bali shetani na malaika zake (MATHAYO 25:41).  Kama utakwenda huko baada ya kusoma “note” hii, itakuwa ni kwa sababu ya kiburi chako tu, na kushupaza shingo yako na kukataa kulitendea kazi Neno hili (MITHALI 29:1).  Moto wa Jehanum siyo mahali pa mchezo kama walimu wa uongo wanavyofundisha.  Walimu hawa huwafariji watu na kusema eti mtu ataunguzwa na moto na kutoweshwa na kupotea na kuangamizwa kabisa  na ndiyo mwisho wake. Wanatumia maandiko kama  MATHAYO 10:28 (kuangamizwa) na YOHANA 3:16 (Kupotea).  Kuangamia katika maandiko hakumaanishi kumalizika kabisa, bali kukabiliwa na mauti (ESTA 4:16).  Mauti ya watu walioko motoni, ni mauti ya milele, kama tutakavyoona hivi punde.  Kondoo akipotea, haimaanishi hayupo kabisa ila ametengwa na mchungaji (ISAYA 57:1-3).

Vilevile, neno “kuharibu” linapotumika kuhusiana na adhabu ya milele, halina maana ya kufanya kitu kisiwepo, bali ni kuadhibu vikali (1 WAKORINTHO 3:16-17).  Walimu hawa wa uongo, pia hufundisha  kwamba, eti watu watatoweshwa kama moshi baada ya kuunguzwa kwa kutumia andiko la ZABURI 37:20.  Kutoweshwa hapa ni kutenganishwa na Mungu, kama Adamu na Hawa walivyotoweshwa na kutolewa katika bustani ya Edeni, na hivyo kutengwa na Mungu.  Kwa ujumla, mafundisho yote haya yanatokana na shetani, yanalenga kuwafanya watu waendelee kutenda dhambi, huku wakipuuza ukweli juu ya Jehanum, kwa kuwaza kwamba watateseka dakika chache na kupotea kabisa na ndiyo mwisho. Huu siyo ukweli.  Ukweli kuhusu Jehanum ya moto ni upi basi?  Sikiliza nikuambie!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .                           

                         Ukweli kuhusu Jehanum ya moto, ni upi basi? 

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

               Jehanum ya moto, au kuzimu, ni shimo kubwa na refu sana lililojaa moto.  Wengi tunafahamu jinsi wanawake wanavyouchochea moto wa kuni au mkaa, kwa kuupulizia hewa kwa mdomo, au kipepeo. Sasa basi, moto wa Jehanum nao huchochewa mfululizo, ili usizimike; lakini huchochewa na pumzi ya Bwana, yaani pumzi maalum ya Mungu mwenyewe (ISAYA 14:15;  ISAYA 30;33).  Moto wa Jehanum ni mkali sana kuliko moto wowote tunaoufahamu duniani.  Moto wa gesi wa kuunganishia vyuma, unaotokana na kuwashwa mchanganyiko wa gesi ya “Oxygen”, na “Acetylene”, unaonekana kwa hapa duniani kwamba ni mkali.  Moto huu, siyo chochote, ukilinganishwa na moto wa Jehanum.  Katika karakana au viwanda vya vifaa vya vyuma, chuma huyeyushwa na kuwa uji katika matanuru ya moto mkali unaofikia nyuzi joto 2,000 hadi 3,000 na zaidi.  Moto huu unaoyeyusha vyuma na ukali wake, huo si chochote! (Kumbuka kwamba maji yaliyochemka sana hufikia nyuzi joto 100 tu!)  Moto ulio katikati ya jua linalotuangaza, unafikia nyuzi joto milioni kumi (10,000,000°C).  Moto wa jua nao, si chochote ukilinganishwa na moto wa Jehanum!  Ukali wa moto wa Jehanum, unatisha (WAEBRANIA 10:26-27).  Siyo hilo tu, moto wa duniani una rangi mbalimbali, njano,bluu,mwekundu n.k.  Moto wa Jehanum ni tofauti kabisa; Ni moto wa rangi nyeusi, unaosababisha giza na kumfanya mtu aliye motoni, awaone wenzake wachache tu wa karibu naye, hivyo hamna faraja ya kusema “tuko wengi!”  Moto huu mweusi, ndiyo maana unaitwa “giza la nje” (MATHAYO 8:11-12,  MATHAYO 22:13;  MATHAYO 25:30;  YUDA 1:6).  Siyo hilo tu.  Moto huu wa Jehanum, una meno!  Hivyo una uwezo wa kuwala na kuwatafuna walioko motoni (KUMBUKUMBU 32: 22;  WAEBRANIA 10: 26-27).  Hata hivyo, pamoja na moto huu kumtafuna mtu, bado una sifa ya kumhifadhi mtu huyo na kumfanya asimalizike, kama jinsi chumvi ilivyo na uwezo wa kuizua nyama kuharibika.  Hivyo moto unamtafuna mtu wakati wote, lakini haishi na wala moto wenyewe hauzimiki.  Ndiyo maana unaitwa moto wa milele (MARKO 9: 43-49;  MATHAYO 25:41).

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

                            Moto wa Jehanum, ni moto wa rangi nyeusi 

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

               Moto huu wa Jehanum, huambatana na madini yanayoitwa kiberiti au kwa lugha ya kitaaluma, “sulphur.”  Kwa wale wanaofahamu kidogo somo la shule la “kemia” au “chemistry,” wanafahamu kwamba madini ya “sulphur”, yakiwashwa moto, huwa kama mpira, na hutoa harufu mbaya kama ya mayai yaliyooza.  Harufu ya namna hii inafunika kuzimu yote, na watu walioko huko wanahangaika kushika pua zao, lakini hakuna jinsi!.  Hebu jaribu kuwaza maisha haya, ndiyo yawe ya milele, mpendwa msomaji! Siyo hilo tu! Katika moto huu, wamo funza maalum ambao huwatafuna watu na kufanya matundu mengi makubwa katika miili yao, wakiingia na kutoka, kutoka ubavu hadi ubavu mwingine kutoka kwenye tumbo hadi mgongoni n.k.  Hii hufanya sura za wale walioko motoni, kuwa mbaya mno kama madude tu! (ISAYA 14: 11;  MARKO 9:43-49;  ISAYA 66:24).  Hata kama mtu alikuwa mweupe duniani, huko motoni, huwa ni mweusi tii!

Moto wa milele, huitwa pia mauti ya pili (UFUNUO 21:8).  Kwa nini huitwa mauti ya pili? Uchungu wa mauti unaomfanya mtu kugugumia kwa mateso makali, akishindwa kupumua vizuri na kubaki kusema “Mmh! Mmh! Mmh!”, mpaka watu wanasema heri afe apumzike, uchungu wa jinsi hiyo humkabili mtu aliye motoni, milele na milele.  Kwa lugha rahisi, ni kusema kwamba watu walioko motoni, wakati wote wako katika hali ya kufa, lakini hawafi!  Niseme nini mwanangu ili unielewe!  Watu walioko motoni, hujawa wakati wote na vilio, na tena husaga meno yao kama mtu anayeona baridi kali (MATHAYO 8: 12).  Walioko motoni wanajifahamu, na kuwakumbuka wenzao waliowaacha duniani, na tena wakati mwingi hutoa ndini zao nje, kama mbwa, wakitamani maji kidogo kupoza ulimi kutokana na joto kali linalosababisha kiu kubwa, lakini hawapati maji hata tone!  Juu ya yote hayo katika vilio vyao, humwomba Mungu awahurumie na kuwasamehe lakini Yeye amekwishasema, “Nami jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma” (EZEKIELI 9: 10;  EZEKIELI 8:18).

Watu walioko motoni, hutamani mtu mmoja kati yao atoke motoni aje duniani, awashuhudie ndugu zao, ili waache dhambi, na kukwepa mateso yao, lakini huambiwa kwamba ndugu zao wanapaswa kuyasikia maneno ya manabii walioko duniani, maana hata akitumwa mtu kutoka motoni na kueleza mateso ya huko, watasema ni mwongo, hajaenda motoni.  Tunasoma haya katika LUKA 16:27-31, ”Akasema, Basi, baba, nakuomba, umtume nyumbani kwa baba yangu, kwa kuwa ninao ndugu watano, ili awashuhudie,wasije wao pia wakafika mahali hapa pa mateso. Ibrahimu akasema, wanao Musa na manabii, wawasikilize wao. Akasema, La, baba Ibrahimu, lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu, watatubu. Akamwambia, Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa (hawatashawishika) hata mtu akifufuka katika wafu”.

             Mpendwa msomaji, ikiwa mama yako mzazi alifariki akiwa hajaokoka, ujue yuko motoni, na anakuambia, “Usinifuate huku mwanangu”.  Ikiwa baba yako mzazi alifariki akiwa dhambini, anateseka motoni, na hataki umfuate huko aliko!  Ndugu, marafiki na jamaa zako walioko huko wanakukumbuka sana, na hawapendi ujiunge nao huko, bali wanataka utubu na kuokoka mateso hayo ya moto.  Walioko huko motoni, wakimwona yeyote mwingine kutoka duniani, ambaye alikuwa na nafasi ya kusikia habari kama hizi na akazipuuza, kisha akawafuata huko motoni, humwambia, Je wewe nawe umekuwa dhaifu kama sisi! Wewe nawe umekuwa kama sisi! (ISAYA 14: 10).

Mpendwa msomaji, baada ya kusikia yote haya kutoka kwa nabii aliyetumwa kukuletea ujumbe huu, usifanye moyo wako kuwa mgumu.  Hii ni nafasi ya kipekee ya kuokoka.  Je, unajuaje kama utaamka kitandani baada ya kulala usiku wa leo?  Wakati uliokubalika wa wokovu ni sasa (2 WAKORINTHO 6:2).  Labda utaniuliza, ili uokoke, ufanyeje?  Jibu ni rahisi, kwa imani ukitubu dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha, na kumwambia Yesu Kristo akusamehe, utasamehewa sasa hivi, na msamaha wa dhambi, huambatana na wokovu (LUKA 1:77).  Je, uko tayari kuokoka sasa hivi?  Najua uko tayari. Basi fuatisha sala hii kwa dhati toka moyoni, Mungu baba asante kwa kuniletea ujumbe huu.Natubu dhambi zangu zote, kwa kumaanisha kuziacha. Yesu Kristo nakuomba unisamehe dhambi zangu na kunipa uwezo wa kushinda dhambi na kuniokoa kutoka katika mateso ya moto wa milele. Asante, kwa kuniokoa katika Jina la Yesu.  Amen.  Tayari sasa umeokoka, na kwa hakika unakwenda mbinguni sasa, hata ukifa leo.  Ili uzidi kuukulia wokovu, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “note” hii, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.

                                                         UBARIKIWE NA BWANA YESU!!!

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s