JITAHIDINI KATIKA MAOBI KWA AJILI YANGU

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe   

SOMO KWA KANISA LA NYUMBANI.

SOMO LA 12 JITAHIDINI KATIKA MAOMBI KWA AJILI YANGU

NENO LA MSINGI:

WARUMI 15:30:

“Ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho, JITAHIDINI pamoja nami KATIKA MAOMBI yenu KWA AJILI YANGU mbele za Mungu”.

<><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><

M

singi wa somo letu leo, ni kujifunza umuhimu wa kumwomba Mungu kwa ajili ya Mchungaji.  Kila mmoja anapaswa kufahamu kwa undani wajibu wake wa kumwombea Mchungaji, kama tunahitaji kuona matokeo yaliyoonekana katika Kanisa la Kwanza.

Watu wengi waliookoka wamekuwa hawaelewi umuhimu wa kuomba sana kwa ajili ya Mchungaji wao, jambo hili limekuwa ni moja ya sababu kubwa ya kushindwa kufikia viwango walivyofikia wenzetu katika Kanisa la Kwanza.

Mchungaji kama Kiongozi wetu, anaweza kabisa kusababisha kundi zima kwenda katika njia iliyo sawa au kulipoteza kundi zima.  Pamoja na kuwepo kwa Mungu mwenyewe, bado Wachungaji wana nafasi kubwa ya kuwapeleka Watu wa Mungu katika njia iliyo sahihi au isiyo sahihi [SOMA YEREMIA 50:6].  Inaweza pia ikawa siyo kulipoteza kundi, lakini ikawa ni kulichelewesha kufikia kiwango fulani anachokitaka Mungu.  Tukihitaji kuongozwa kama Mungu apendavyo, na wakati wote tuweze kukua na kuzaa matunda yote kwa wakati wake, inabidi kila mmoja awe na mzigo wa kumwombea Kiongozi.  Mchungaji anaweza kumfanya kila mmoja katika Kanisa kupata taji za kujivunia siku ya mwisho au kumfanya kila mmoja katika Kanisa apate thawabu hafifu siku ya mwisho.  Ili Yesu Kristo amwambie kila mmoja katika Kanisa “Vema mtumwa mwema, kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi”, inabidi tumwombe Mungu mno kwa ajili ya Mchungaji.

Kwa sababu hii, viongozi wa Kanisa la kwanza, waliwafundisha na kuwaeleza Wakristo kila mahali kuwaombea viongozi hao.  Hata Roho Mtakatifu ametenga msitari mfupi kusisitiza jambo hili la muhimu la kuwaombea viongozi.

1 WATHESALONIKE 5:25:           “Ndugu tuombeeni.”

Maandiko yamejaa msisitizo wa viongozi wa Kanisa la Kwanza, kuhitaji maombi kutoka kwa wale walio katika uongozi wao [SOMA WAEBRANIA 13:17-18; 2 WATHESALONIKE 3:1-2; WARUMI 15:30; WAEFESO 6:18-19].  Pamoja na Petro kuwa pamoja na Yesu kwa miaka mitatu, kujazwa Roho Mtakatifu wakati wa Pentekoste, na kutumiwa kutenda miujiza mikubwa baada ya hapo; hata kivuli chake kilipowagusa wagonjwa walipokea uzima; na kutokewa na malaika wakimwongoza n.k.; bado Petro alihitaji maombi ya Kanisa.  [MATENDO 12:5].  Kanisa lilipoomba kwa juhudi kwa ajili ya Petro, ndipo mlango mkubwa ukafunguliwa kwake.  Pamoja na Paulo kutenda aliyoyatenda, siri ya mafanikio yake ilikuwa Kanisa kuomba kwa juhudi kwa ajili yake.  [MATENDO 15:40].  Kwa sababu hiyo basi, ikiwa Petro na Paulo kufanikiwa kwao kulitokana na Kanisa kuomba kwa juhudi kwa ajili yao, hakuna Mchungaji yeyote yule leo, ambaye atafanikiwa kuitenda kazi ya Mungu inavyompasa kama Kanisa lisipoomba kwa juhudi kwa ajili yake.  Kufanikiwa kwa Paulo, kulikuwa kufanikiwa kwa Kanisa zima.  Waliokuwa waaminifu kuyafuata maongozi yao, siku ya kupewa taji, watakuwepo kuambiwa na Yesu, “Vema mtumwa mwema”.  Vivyo hivyo, Kanisa zima leo inabidi liuige mfano wa Kanisa la Kwanza – kuomba kwa juhudi kwa ajili ya Mchungaji.

 

(1)           MAENEO KUMI MUHIMU YA KUMWOMBEA MCHUNGAJI APEWE

UFUNUO WA RAMANI YA UJENZI WA KANISA NA AWEZESHWE

KULIJENGA KANISA KWA RAMANI ITOKAYO KWA MUNGU.

 

Mjenzi wa Kanisa la Mungu anapaswa kuwa Yesu Kristo mwenyewe [SOMA MATHAYO 16:18].  Yesu Kristo ndiye mwenye ramani ya ujenzi wa Kanisa lake.  Mchungaji inampasa kuifahamu ramani hiyo na kulijenga Kanisa kwa nakala halisi ya ramani iliyotoka kwa Mungu.  Katika Biblia, Mungu kila mahali alipotaka kuwepo jengo lake lolote, ilimbidi yeye mwenyewe kutoa ramani yote ya jengo hilo.  Hakutoa nafasi ya mwanadamu kutumia akili zake na ufahamu wake na kulijenga jengo la Mungu kwa ramani ya Kibinadamu.  ANGALIA MIFANO KATIKA BIBLIA:

(a)       SAFINA WAKATI WA NUHU:

Ingawa Biblia inasema kwamba Nuhu alikuwa mtu wa haki na mkamilifu katika vizazi vyake, hata hivyo Mungu hakumuachia kujenga safina kwa ramani yake mwenyewe au maarifa yake.  Mungu aliitoa ramani yote ya Safina, na kutoa maelekezo hata ya mti wa kutumia kuijenga; na Nuhu aliijenga Safina sawasawa na maelekezo yote ya ramani iliyotoka kwa Mungu [SOMA MWANZO 6:13-16, 22].

(b)       MASKANI WAKATI WA MUSA:

Ingawa Musa alikuwa msomi, akiwa na hekima yote ya Wamisri iliyojumuisha ubingwa au utalaam wa ujenzi [MATENDO 7:22]; Mungu hakumuachia kuijenga maskani au hema ya kukutania kwa ramani yake mwenyewe, au maarifa na akili zake.  Mungu aliitoa ramani ya maskani na kutoa maelekezo ya mambo yote na kusisitiza kwamba Musa inambidi aijenge maskani sawasawa na mfano au ramani ileile aliyopewa.  [SOMA KUTOKA 25:9, 40; KUTOKA 26:30; WAEBRANIA 8:5].

            (c)       HEKALU WAKATI WA SULEMANI:

Pamoja na Sulemani kuwa na hekima kuu kuliko watu wote walioko duniani na fedha na utajiri wote, hata hivyo; Mungu hakumuachia Sulemani kulijenga hekalu kwa ramani yake mwenyewe au maarifa na akili zake.  Mungu mwenyewe aliitoa ramani yote ya hekalu kwa babaye Daudi na kutoa maelekezo ya kila kitu na akataka Sulemani alijenge hekalu kwa kufuata ramani hiyo halisi [SOMA 1 NYAKATI 28:11-12, 19].

Katika majira haya, Kanisa au watu waliookoka; ni jengo la Mungu [1 WAKORINTHO 3:9]; maskani ya Mungu na hekalu takatifu la Mungu [WAEFESO 2:21-22].  Ikiwa Mungu alitoa ramani yote ya ujenzi wa Safina, jengo ambalo liliwahifadhi watu wanane tu na wote wengine walikuwa wanyama tu, ni zaidi sana kwa Kanisa au jengo la Mungu linalohifadhi mamia au maelfu ya watu.

Ikiwa Mungu alitoa ramani yote ya maskani ya muda tu jangwani wakati wa wana wa Israeli walipoongozwa na Musa, ni zaidi sana leo kwa Kanisa au maskani ya Mungu iliyo ya kudumu.  Ikiwa Mungu alitoa ramani ya hekalu lililokuwa la kuvunjwa na kuharibiwa baada ya miaka kadhaa, ni zaidi sana leo kwa Kanisa au hekalu lake takatifu ambalo atahitaji kulichukua mbinguni.  Kwa jinsi hiyo hiyo, Mungu hatapenda mwanadamu atumie ramani yake, maarifa yake, akili zake au ujuzi wake; kulijenga jengo la Mungu, maskani au hekalu takatifu la Mungu yaani Kanisa.

Ni kwa sababu hii, kila mtu aliyeokoka anapaswa kumwomba Mungu kwamba ampe Mchungaji wetu ramani na maelekezo yote ya jinsi ya kulijenga Kanisa.  Inatubidi tumwombe Mungu ili kila siku, kila wiki, kila mwezi na kila mwaka, ujenzi wa Kanisa uendelee kuwa katika ramani na maelekezo ya Mungu kupitia kwa Mchungaji wetu.  Kanisa likijengwa kwa ramani ya Mungu, milango ya kuzimu, haiwezi kulishinda; maana linakuwa limejengwa na Kristo mwenyewe.

(2)        APEWE MAFUNUO DHAHIRI KATIKA NENO LA MUNGU

Biblia ni Ufunuo wa Roho wa Mungu.  Hekima yote ya Mungu, imeandikwa katika kurasa chache tu zinazoifanya Biblia.  Inahitaji mafunuo dhahiri katika Neno la Mungu ili kupata jibu la kila jambo.  Hakuna lolote ambalo halina jibu katika Biblia.  “Kipi tukifanye”. “Kwa nini tukifanye”, “Mbinu za kukifanya, “Mifano ya waliokifanya kwa mbinu hizo wakafanikiwa”, n.k.; yote haya na yote katika yote, yana majibu katika Biblia; lakini bila mafunuo dhahiri katika Neno; tutakuwa tunajifunza theolojia tu.  Biblia ni zaidi ya elimu ya theolojia.  Maneno ya Mungu ni Roho, tena ni uzima [YOHANA 6:63]. Maneno ya Mungu hayafundishwi kwa hekima ya kibinadamu, bali yanafundishwa na Roho; na kwa kuwa ni ya rohoni, yanafasiriwa tu kwa maneno ya rohoni [1 WAKORINTHO 2:13].  Maneno ya Mungu yanahitaji kufunuliwa na Roho ambaye huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu [1 WAKORINTHO 2:10].  Ni kwa sababu hizi, kila mtu aliyeokolewa anapaswa kila siku kumwombea Mchungaji ili apewe mafunuo dhahiri katika Neno la Mungu ili tupokee mana itokayo kwa Mungu.  Kwa sababu ya maombi hafifu ya watu waliookoka, Wachungaji wengi leo hawana mafunuo dhahiri katika Neno la Mungu.  Neno la BWANA lililojaa mafunuo dhahiri, ni adimu sana kwa wachungaji wengi leo kama nyakati za mtoto Samweli [SOMA 1 SAMWELI 3:1].  Ni wajibu wa kila mmoja katika Kanisa kuomba kwa juhudi, ili Mchungaji apewe usemi na Roho, kila anapofunua kinywa chake; na pia anene IMPASAVYO kunena na kuihubiri kwa ujasiri SIRI YA INJILI [SOMA WAEFESO 6:18-20].

(3)       APEWE NGUVU NYINGI ZA KUFANYA ISHARA, MAAJABU NA KUPONYA WAGONJWA KWA KULITUMIA JINA LA YESU, ILI KUWAONGEZA WENGI KATIKA KWELI YA NENO:

Neno la Mungu likiwa katika kweli yote, lina UKALI kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena LINACHOMA hata kuzigawanya nafsi na roho; na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake [SOMA WAEBRANIA 4:12].  Kwa sababu hii, mwanadamu ambaye hajaokolewa, hulikimbia Neno la Mungu, halipendi; maana humchoma na kumkata kwa makali.  Mfano wa jambo hili unapatikana katika uvuvi.  Ikiwa mvuvi atatupa ndoana tupu katika maji, samaki anapoiona ndoana hiyo huikimbia.  Ndoana pekee haivutii, ni kitu kinachochoma na kukata kwa makali.  Ili mvuvi afanikiwe, inambidi atafute chambo na kukiweka kwenye ndoana iwe ni minyoo, nyama au dagaa n.k.; kulingana na aina ya samaki ambao mvuvi anataka wanase kwenye ndoana.  Samaki wanapokuja sasa, hawaioni ndoana, ila wanakiona chambo tu.  Chambo kinavutia na kinawafanya wakisogelee na kukitafuna.  Kwa kukitafuna chambo, kumbe na samaki wananaswa.  Vivyo hivyo, sisi ni WAVUVI WA WATU [MARKO 1:17].  Ili watu wanaswe kwenye kweli ya Neno la Mungu ambayo ni ndoana, inatubidi tuwe na chambo cha kuwavutia.  Chambo hiki ni Uponyaji wa Wagonjwa kwa miujiza, ishara na maajabu.  Nguvu ya Mungu inapodhihirika kwa jinsi hii, huwavuta mataifa wengi na kuongezeka katika Kanisa la Mungu.  Kila mmoja katika Kanisa, inambidi amwombe Mungu kwa bidii ili Mchungaji apewe nguvu nyingi za kufanya Ishara, Maajabu na kuponya wagonjwa kwa miujiza mikubwa.  Haitoshi tu kusema Mungu atampa Mchungaji huyo nguvu hizo, Yeye mwenyewe akipenda.  Watu katika Kanisa la Kwanza, hawakusema hivyo, walimwomba Mungu kwa ajili ya nguvu hiyo kwa viongozi, na Mungu akafanya.

MATENDO 4:29-30, 33:

“Basi sasa Bwana …….. ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako Mtakatifu Yesu.  Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote”.

(4)       APEWE HEKIMA KUTOKA JUU KWA BWANA:

Biblia inasema enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima [MITHALI 13:20].  Kuna hekima itokayo juu ya kufanya kila jambo.  Bila hivyo, hatuwezi kujua jinsi itupasavyo kuingia na kutoka.  Ni kwa sababu hii Sulemani aliomba hekima [1 WAFALME 3:7-12].  Hekima ni ya thamani kuliko chochote kile.  Ikiwa Mchungaji ana hekima, basi wale wote wanaoenenda pamoja naye, watakuwa na hekima.  Ikiwa Mchungaji ni mpumbavu, basi wale wanaoenenda pamoja naye, wataumia.  Ni kwa sababu hii, kila mmoja inampasa kuomba kwa jitihada kwa ajili ya Mchungaji, ili apewe hekima.

(5)       AONGOZWE NA ROHO NA APEWE NEEMA KUBWA YA KUISIKIA MARA MOJA SAUTI YA ROHO MTAKATIFU ANAPOMWONGOZA KATIKA KUFANYA MAMBO YOTE:

Kiongozi anahitajika kuongozwa na Roho katika kila jambo.  Kuna wakati wa mambo yanayotatanisha.  Lazima ifahamike uhakika ni upi [ANGALIA MATENDO 10:19-20].

Kuna wakati wa Mungu kwa kila jambo.  Ni lazima kuufahamu wakati wa Mungu.  Jambo linaweza likawa ni jema, lakini siyo wakati wake.  Inambidi Kiongozi kumsikia Roho anapokataza jambo fulani lisifanyike ingawa ni jema, kutokana na wakati huo kuwa siyo wa Mungu kwa jambo hilo kufanyika [ANGALIA MATENDO 16:6-7].  Yesu Kristo aliongozwa na Roho katika kila jambo ndiyo maana huduma yake ilifanikiwa sana [LUKA 4:1].  Kwa sababu hizi, inambidi kila mmoja katika Kanisa, kuomba kwa jitihada yote; ili Mchungaji aongozwe na Roho katika kila jambo kwa kuisikia mara moja sauti ya Roho anapomwongoza kufanya jambo au kutolifanya.

(6)       APEWE UFUNUO JUU YA MBWA-MWITU WANAOKUJA KULIRARUA KUNDI NA HEKIMA YA KUWALINDA KONDOO KATIKA MADHARA

Mahali ambapo Kanisa linashamiri na kuongezeka katika idadi ya watu, kuongezeka katika imani na upendo; mbwa-mwitu huja kulirarua kundi, na wengine hukaa katika kundi wakiwa na mfano wa Kondoo kumbe ni mbwa-mwitu.  Wengine hutoka katika kundi hilo hilo na kugeuka kuwa mbwa-mwitu.  Mbwa-mwitu hawa, kazi yao siyo tu kulirarua kundi, bali huwavuta watu kutoka katika kweli na kutaka wawafuate wao nje ya kweli, kwa kusema mapotovu [SOMA MATENDO 20:28-30].  Mchungaji inabidi awe na macho ya kiroho ya kuwaona mbwa-mwitu na kuwa na hekima ya kuwalinda kondoo katika madhara.  Kanisa inabidi kumwombea Mchungaji juu ya jambo hili.

(7)       APEWE UFUNUO WAKATI WOTE WA WANAFIKI WALIO NDANI YA KANISA ILI CHACHU NDOGO ISICHACHUE DONGE ZIMA:

Kanisa lililo takatifu ndilo ambalo Mungu huliongeza.  Wale waliotangulia wakiwa katika utakatifu, Mungu hufahamu hata wale watakaoongezwa, watakuwa watakatifu

[WARUMI 11:16].  Inatubidi kumwomba Mungu ili Mchungaji awe na macho ya kiroho ya kuwaona wale wanafiki wanaokuwa katika kundi kama kondoo kumbe ni mataifa kwa hali zote, ili awaonye na hata kuwaondoa. [1 WAKORINTHO 5:11-13].

(8)       APEWE KIBALI KWA BWANA NA KWA WATU PIA:

Mchungaji akiwa na kibali kwa Bwana na kwa WATU PIA anaowaongoza, na wengineo; kunakuwa na siri ya ushindi mkuu [1 SAMWELI 2:26].  Mchungaji mwenye kibali kwa Bwana na kwa watu pia, atasikilizwa, na neno lake litakuwa la Baba asemaye na wana.  Kanisa inabidi limwombe Mungu kwa bidii, ili kiongozi awe na kibali kwa Bwana na kwa watu pia; wakati wote.

(9)       APEWE ULINZI MKALI WA MAJESHI YA BWANA, NA KUTIWA NGUVU:

Mchungaji ndiye Shabaha kubwa ya shetani na majeshi yake.  Shetani anajua kwamba akimpiga Mchungaji, kondoo wote watatawanyika [MATHAYO 26:31].  Kwa sababu hiyo, tukimwacha Mchungaji bila kumuunga mkono katika kumwombea, mpango wa shetani kumshambulia unaweza ukafanikiwa.  Mchungaji akiachiwa peke yake vita, huweza kuchoka na mikono yake kuwa dhaifu; na kuwa rahisi kushambuliwa na majeshi ya adui; na kundi zima kutawanywa.  Angalia mfano katika Biblia, uone jinsi majeshi ya shetani yanavyopanga kumshambulia Kiongozi, wakati akiwa amechoka na kuwa dhaifu:

2 SAMWELI 17:1-3:

“Zaidi ya hayo Ahithofeli akamwambia Absalomu, Niache nichague watu kumi na mbili elfu, nami nitaondoka na kumfuatia Daudi usiku huu; nami nitamshambulia wakati atakaokuwa amechoka, na mikono yake imekuwa dhaifu, nami nitamtia hofu; na watu wote walio pamoja naye watakimbia nami nitampiga mfalme peke yake; na hao watu wote nitawarejeza kwako……..”.

Kiongozi kama kamanda wetu, anasongwa na mambo mengi mno, na hivyo ziko nyakati ambazo huchoka na kuwa dhaifu.  Ni wajibu wa Kanisa kuchukua mzigo wa maombi kwa ajili ya Mchungaji, ili mikono yake mizito itiwe nguvu wakati wote na kuhakikisha Kanisa linashinda wakati wote [ANGALIA MFANO: KUTOKA 17:8-13].  Inambidi kila mmoja katika Kanisa kufahamu kwamba Kiongozi kama Kamanda ni wa muhimu kulindwa kuliko askari wa kawaida elfu kumi [SOMA 2 SAMWELI 18:2-3].

Kanisa likiomba, malaika kutoka mbinguni huweza kutumwa na kumtia nguvu Mchungaji, anapokuwa amechoka na kulemewa na vita [ANGALIA MFANO: LUKA 22:41-43].  Inahitajika nguvu ya kipekee kwa kiongozi wetu kufanya yote yanayompasa kufanya na kuzidi kusonga mbele akiliongoza kundi kumfikia Kristo.  Inahitajika pia ulinzi mkali wa majeshi ya Bwana dhidi ya majeshi ya adui ambayo shabaha yao kubwa ni kumpiga Mchungaji.

(10)     APEWE NEEMA YA KUFUNDISHA YOTE YANAYOMPASA KULIFUNDISHA KANISA,NA KULIWEZESHA KANISA KUYAFANYA MAAGIZO YOTE YA MUNGU BILA KUSAZA; ILI AKWEPE HUKUMU:

Mchungaji atatoa hesabu kwa ajili ya roho zote katika Kanisa.  Biblia inaliagiza Kanisa kumsaidia Mchungaji ili afanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua.  Moja ya mambo ya kumsaidia Mchungaji kwa maombi, ni kumwomba Mungu ampe neema yote ya kuyafundisha yote yanayompasa kulifundisha Kanisa na kuliwezesha Kanisa kuyafanya Maagizo yote ya Mungu bila kusaza.  Ikiwa Kanisa litafanya maagizo yote ya Mungu kasoro AGIZO MOJA kutokana na uongozi au mafundisho mabaya ya Mchungaji, basi Mchungaji huyo atastahili hukumu kwa kulikosesha kundi zima.  [ANGALIA MFANO:  2 WAFALME 15:1-5].  Mungu analitaka kanisa liyaangalie MAAGIZO YOTE na kuyafanya [ZABURI 119:6; YAKOBO 2:10].  Hivyo Kanisa lina wajibu wa kumwombea Mchungaji, ili awaeleze yote yanayowapasa kuyafanya na kuomba pia neema kwa kila mmoja Kanisani, kuyafanya maagizo ya BWANA yanayoletwa katika Kanisa kwa mafundisho wa Mchungaji.

MSITARI WA KUKUMBUKA:

1 WATHESALONIKE 5:25:           “Ndugu tuombeeni.”

M   A   S   W   A   L   I

(1)       Je, ni kweli kwamba pamoja na kuwepo kwa Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, bado Mchungaji ana nafasi kuwapeleka watu katika njia iliyo sahihi au isiyo sahihi?

[YEREMIA 50:6]. JIBU: NI KWELI/SIYO KWELI (Futa lisilo sahihi).

Kama ni kweli, Kanisa, linapaswa kufanya nini ili Yesu Kristo siku ya mwisho amwambie kila mmoja katika kanisa “Vema mtumwa mwema, kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno

lililo dogo uwe na mamlaka juu ya miji kumi?”

—————————————————————————————————————-

—————————————————————————————————————-

(2)       Taja Maeneo Kumi muhimu ya kumwombea Mchungaji:

(a)————————————————————————————————————-

(b)————————————————————————————————————-

(c)————————————————————————————————————-

(d)————————————————————————————————————-

(e)————————————————————————————————————-

(f)————————————————————————————————————–

(g)————————————————————————————————————-

(h)————————————————————————————————————-

(i)————————————————————————————————————–

(j)————————————————————————————————————–

(3)       (a)       Shabaha kubwa ya shetani na majeshi yake ni nani katika Kanisa?

——————————————————————————————————-

(b)       Tukimwacha Mchungaji peke yake bila kumwombea, mpango wa shetani wa kumshambulia unaweza ukafanikiwa? JIBU: NDIYO/SIYO.

(c)        Ikiwa jibu lako la (b) ni NDIYO majeshi ya shetani hupanga kumshambulia

Mchungaji wakati akiwa katika hali ipi?

——————————————————————————————————-

——————————————————————————————————-

(d)       Toa mfano wa ki-Biblia ambao majeshi ya adui yalipanga kumshambulia kiongozi, kwa kujua kwamba watu walio pamoja naye pia watakimbia.

——————————————————————————————————-

——————————————————————————————————-

(e)       Nitampiga Mchungaji na kondoo wote watatawanyika katika MATHAYO 26:31; ina  maana gani kuhusiana na kufanya maombi kwa ajili ya Mchungaji?

——————————————————————————————————-

——————————————————————————————————-

(4)       Ni nini kazi ya Ishara, Maajabu na kuponya wagonjwa katika kuwavuta watu kulisikia Neno la kweli, ukilinganisha na kazi ya uvuvi?

—————————————————————————————————————-

—————————————————————————————————————-

<><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><>< 

 

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements

One comment on “JITAHIDINI KATIKA MAOBI KWA AJILI YANGU

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s