KUFUNGWA KWA YESU

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

SOMO:  KUFUNGWA KWA YESU

L

eo tena, tunaendelea kujifunza Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu.  Leo, tutatafakari kwa makini YOHANA 18:12-27.  Katika mistari hii, pamoja na mambo mengine, tutajifunza juu ya “KUFUNGWA KWA YESU“.  Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika mistari hii katika vipengele saba:-

 

(1)      DHAMBI HUHESABIWA KWA WOTE WANAOISHIRIKI (MST. 12);

(2)      KUFUNGWA KWA YESU (MST. 12-14);

(3)      KUMFUATA YESU KATIKA DHIKI NA MATESO (MST. 15-16);

(4)      KUKOTA MOTO NA WENYE DHAMBI KWA KUOGOPA MATESO

      (MST. 18);

(5)      KUHOJIWA KWA YESU (MST. 19-21);

(6)      KUPIGWA KOFI KWA YESU (MST. 22-23);

(7)      UWEZEKANO WA KUMKANA YESU (MST. 17, 25-27).

 

(1)    DHAMBI HUHESABIWA KWA WOTE WANAOISHIRIKI (MST. 12)

Kikosi cha askari na watumishi wa Wayahudi walikuwa zaidi sana ya 600 kama tulivyoona katika somo lililopita.  Kikosi cha askari peke yake kilikuwa na askari wapatao 600 licha ya watumishi wa Wayahudi ( Wakuu wa Makuhani na Mafarisayo) ambao walikuwa wengi pia.  Jemadari anayetajwa hapa, Kiyunani anaitwa, “CHILIARCHOS“, ambaye alikuwa Komanda wa kijeshi wa askari 1,000.  Sasa basi, mamia ya watu hawa wote wanatajwa hapa kwamba “WALIMKAMATA YESU, WAKAMFUNGA“ (MST. 12).  Kiutendaji, haingekuwa rahisi kwa mamia wote hawa kumkamata yesu kwa mikono yao maana wengine wangekosa hata pa kumshika Yesu.  Hivyo ni dhahiri kwamba waliotumia hasa mikono yao kumkamata Yesu na kumfunga, walikuwa wachache, lakini hapa Roho Mtakatifu katika maandiko anawahesabia WOTE dhambi ya kumkamata na kumfunga Yesu.  Hapa tunajifunza kwamba dhambi huhesabiwa kwa wote wanaoishiriki kwa njia moja ama nyingine (ZABURI 50:17-18; WARUMI 1:32).  Sauli alihesabiwa kuwa mwuaji, pale aliposimama karibu, akakubali na kuzitunza nguo zao waliomwua Stefano (MATENDO 22:20).  Ndivyo ilivyo kwetu leo pia.  Tukitumia nyumba zetu kutunzia mali ya wizi, sisi nasi tunahesabiwa ni wezi.  Tukinunua mali ya wizi, kwa mfano spea za magari, n.k., wakti tunajua kwamba ni mali ya wizi, tendo hilo linatufanya tuhesabiwe kuwa ni wezi.  Tukikukbali watu wafanye uzinzi na uasherati katika nyumba zetu za kulala wageni, tendo hilo linatufanya tuhesabiwe kuwa na sisi ni waasherati na wazinzi.  Tukinyamaza kimya pale tunapomsikia mwenzetu anamsengenya au kumnenea mabaya Mchungaji wetu na kuacha kutoa taarifa hizo kwa Kiongozi, tendo hilo linatufanya sisi nasi tuhesabiwe dhambi ya kumnenea vibaya Mtumishi wa Mungu au kumgusa Masihi au mpakwa mafuta wa Mungu (HESABU 12:8-10; ZABURI 105:14-15).  Vivyo hivyo, tunapozishiriki dhambi nyinginezo.

 

(2)    KUFUNGWA KWA YESU (MST. 12-14)

Kulingana na historia ya Karne ya Kwanza, askari hawa walimfunga Yesu kwa kamba na pingu za chuma au mikatale.  Walimfunga mikono yote kwa nyuma, na mikono yake ikachuruzika damu nyingi, halafu wakamfunga mnyororo wa chuma shingoni na kumburuta kama aburutwavyo kondoo.  Nyakati hizo, mtu aliyefungwa hivi na kwenda kuuawa, alitajwa kama amekufa afavyo MPUMBAVU kama Abneri! (2 SAMWELI 3:32-34).  Yesu alikufa afavyo mpumbavu kwa ajili yetu sisi wapumbavu!  Kuna jambo jingine la kujifunza hapa.  Ikiwa Yesu alifungwa jinsi hii, sisi nasi tukimfuata si ajabu tukipatwa na vifungo kama Mtupe Paulo (WAKOLOSAI 4:18).    Hata hivyo, kuuuna jambo jingine la kiroho la kujifunza.  Tunapofanyaaa dhambi, Biblia inasema kwamba tunakuwa tumefungwa kwa KAMBA ZA DHAMBI (MITHALI 5:22), au KONGWA la makosa yetu (MAOMBOLEZO 1:14).  Yesu Kristo asiyejua dhambi, alifanywa kuwa dhambi kwa ajili yetu ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye (2 WAKORINTHO 5:21).  Yesu alifungwa kamba na mikatale hii, ili iwakilishe kamba zetu za dhambi ili sisi tufunguliwe kamba hizi kwa kumwamini yeye.  Yesu Kristo, kama Isaka mtoto wa Ibrahimu wa ahadi, hapa alifungwa ili akatolewe kuwa dhabihu (MWANZO 22:9).  Jambo jingine la kujifunza hapa ni kwamba tukifungwa kwa kuonewa kwa ajili ya Bwana, tujue kwamba hiyo ndiyo jinsi yetu ya kukwezwa na Mungu au kupandishwa ngazi.  Yusufu aliuzwa utumwani na kufungwa gerezani kwa pingu na minyororo ya chuma, lakini matokeo yake alipokuwa mwaminifu hata katika hayo alipandishwa ngazi na kuwa Waziri Mkuu wa Misri (ZABURI 105:17-21).  Paulo Mtume alifanywa kuwa Mtume aliyefanya kazi kuliko Mitume wote (1 WAKORINTHO 15:10), kutokana na vifungo vyake.  Njia ya Mungu ya kutukweza, ni kutudhili au kutushusha kwa vifungo mbalimbali.  Uweza wa Mungu hutimilika kwetu tunapokubali kufanywa dhaifu (2 WAKORINTHO 12:7-9).

 

(3)    KUMFUATA YESU KATIKA DHIKI NA MATESO (MST. 15-16)

Baada ya yesu kukamatwa na kufungwa, wanafunzi wote walimwacha na kukimbia (MATHAYO 26:55-56).  Hata hivyo katika mistari hii, tunaelezwa kwamba Petro pamoja na mwanafunzi mwingine walimfuata katika mateso yake.  Maneno “mwanafunzi mwingine“, hutumika mara nyingi kuzungumzia juu ya Yohana mwenyewe (YOHANA 20:2-4).  Hata hivyo, hapa (MST. 15), anatajwa mwanafunzi aliyejulikana kwa Kuhana Mkuu.  Wanafunzi wa Biblia kwa msingi huu, wanasema kwamba hapa hatajwi Yohana, ila anaweza kuwa Yusufu wa Arimathaya au Nikodemo (YOHANA 19:38-39; marko 15:43; YOHANA 3:1).  Petro na mwanafunzi mwingine hapa walimfuata Yesu katika dhiki na mateso.  Tunajifunza jambo kubwa hapa.  Ni rahisi kumfuata Yesu katika shangwe na pambio na miujiza.  Wengi wetu tuna utayari wa kumfuata Yesu katika hali hii tu (LUKA 19:33-38; YOHANA 6:26); tunapopatwa na dhiki au mateso, hatuna utayari tena wa kumfuata Yesu.  Huu siyo Ukristo (MATHAYO 13:20-21).  TUMEPEWA SIYO kumwamini Yesu tu, ila na kuteswa kwa ajili yake (WAFILIPI 1:29-30).  Hata hivyo hapa Petro ingwa alimfuata Yesu alifika mahali fulani akasimama nje mlangoni, hakuingia.  Wengine tutaanza vizuri kukabiliana na mateso kwa mume kwa ajili ya wokovu au kuwa radhi kufukuzwa kazi kwa ajili ya kukataa kufanya uzinzi na Boss n.k., lakini mateso yakizidi, tunaacha kumfuata Yesu, tunasimama nje mlangoni.  Haitupasi kuwa hivi.

 

(4)    KUKOTA MOTO NA WENYE DHAMBI KWA KUOGOPA MATESO (MST. 18)

Kwa kuogopa mateso, Petro alijichanganya na wenye dhambi na kukota moto pamoja nao, na kuwa radhi kusikia jinsi walivyoshangilia kuhusu kukamatwa kwa Yesu.  Ndivyo wengi wetu tulivyo.  Kwa kuogopa dhihaka na mateso, tutakuwa radhi kujichanganya na wenye dhambi walio kinyume na wokovui na kuwa upande wao, na kuko9ta moto pamoja nao.  Kwa nini iwe hivi?  Ni heri tupate mateso na kuachwa na mume, mke au yeyote!  Baba na Mama wakituacha Bwana atatukaribisha kwake (ZABURI 27:10).

 

(5)    KUHOJIWA KWA YESU (MST. 19-21)

Mahojiano ya mwanzo aliyohojiwa Yesu katika kesi yake ilikuwa habari za wanafunzi wake na habari za mafundisho yake.  Hapa tunajifunza jinsi Shetani anavyokasirika kuona wanafunzi wanaojifunza mafundisho ya kweli katika huduma zetu.  Kama ilivyokuwa kwa yesu, Shetani atafanya kila njia kutukamata na kutufunga.

 

(6)    KUPIGWA KOFI KWA YESU (MST. 22-23)

Ikiwa Yesu alipigwa kofi bila kosa lolote sembuse sisi?  Tukipigwa makofi na waume zetu, hatupaswi kuona ajabu.  Mtumwa si mkubwa kuliko Bwana wake (YOHANA 15:18-21).  Mtumishi huyu mwenye dhambi alimpiga kofi Yesu.  Sisi nasi tukiwa wenye dhambi, kwa dhambi zetu za ulevi, uzinzi n.k., tunampiga makofi Yesu.

 

(7)    UWEZEKANO WA KUMKANA YESU (MST. 17, 25-27)

Petro alijigamba pamoja na wanafunzi awote kwamba hawawezi kumkana Yesu hata ikibidi kufa (MATHAYO 26:34-35).  Matokeo yake hapa Petro anamkana Yesu MARA TATU siyo mara moja.  Hatupaswi kujivuna bali kuogopa na kuitumainia neema ya Mungu kila siku ya kutufanya tuendelee na wokovu, bila hivyo tunaweza kumkana Yesu mara tatu au zaidi (WARUMI 11:20; 1 WAKORINTHO 10:12; WAEBRANIA 4:16).

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s