KUINGIA KWA YESU KATIKA BUSTANI

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

SOMO:  KUINGIA KWA YESU KATIKA BUSTANI

L

eo, katika Siku ya Kuichambua Biblia, tunaanza kujifunza na kutafakari Sura ya 18 ya Kitabu cha Yohana katika Biblia zetu.  Leo tutajifunza YOHANA 18:1-11.  Katika mistari hii, pamoja na mambo mengine, tutatafakari juu ya “KUINGIA KWA YESU KATIKA BUSTANI“.  Tutayagawa mafundisho yote tunayoyapata katika mistari hii, katika vipengele vinane:-

1)    MAOMBI KABLA YA KUPAMBANA NA SHETANI (MST. 1);

2)    KWENDA KWA YESU NG’AMBO YA KIJITO KEDRANI (MST. 1);

3)    KUINGIA KWA YESU KATIKA BUSTANI (MST. 1);

4)    YESU NA WANAFUNZI WAKE MAHALI PA MATESO (MST. 1);

5)    ADUI ZA MTU NI WATU WA NYUMBANI MWAKE (MST. 2);

6)    MAADUI WENGINE WA YESU KRISTO (MST. 3);

7)    ALAMA KUU YA KUMSALITI YETU (MST. 5);

8)    SILAHA ZA KIROHO ZA VITA (MST. 4-11).

 

(1)        MAOMBI KABLA YA KUPAMBANA NA SHETANI (MST. 1)

“Alipokwisha kusema hayo“, ni maneno yanayomaanisha alipokwisha kufanya maombi hayo.  Muda wote kabla ya hapa, Yesu alikuwa anaomba maombi yaliyowekwa kumbukumbu yake katika Sura ya 17 ya YOHANA.  Baada ya maombi hayo, Yesu anatoka akiwa tayari kwenda kupambana na Shetani.  Maadui zake (wakiongozwa na Shetani aliyemwingia Yuda) wanapokabiliana naye katika vita hivyo katika MST. 3-6, tunaona wakianguka chini na kushindwa vibaya.  Siyo hilo tu, Yesu anavikabili vita hivi katika hali ya kujiamini sana, akiwa hana wasiwasi wala woga wowote.  Siri ya kuwa hivi ni kufanya maombi mazito kabla ya mapambano.  Tukiwa tunakabiliwa na vikao au mabaraza yoyote yaliyopangwa kinyume chetu katika ukoo, kikazi, n.k., hatuna budi kuwa na kipindi cha kutosha katika maombi kabla ya mabaraza hayo.  Maombi hunyonya wota na wasiwasi tunapokabiliana na adui.  Tunapokuwa tunataka kwenda katika sehemu zilizojaa uchawi au ushirikina n.k., hatuna budi vivyo hivyo kufanya maombi ya kutosha kabla.  Maombi aliyoyafanya Danieli kwa mfano yalimuondolea woga na wasiwasi, pale alipotupwa katika tundu la simba (DANIELI 6:6-23).

 

(2)        KWENDA KWA YESU NG’AMBO YA KIJITO KEDRONI (MST. 1)

Kijito Kedroni kinatokea Yerusalemu na kuendelea hadi Mlima Mizeituni.  Kuna mengi ya kujifunza katika KILA jambo alilolifanya Yesu na zaidi sana yale aliyoyafanya akiuendea msalaba.  Kijito Kedrano inachotajwa hapa, kina maana halisi katika majira haya ya Yesu Kristo.  Daudi akiwa analia pamoja na watu wake alivuka kijito cha Kedroni na kushika njia ya kuupandia mlima wa Mizeituni (2 SAMWELI 15:23,30).  Huu ulikuwa utabiri unaohusiana na Yesu Kristo mwana wa Daudi, pale ambapo angevuka kijito Kedroni akiyaendea mateso.  Siyo hilo tu.  Machukizo yote mbele za Mungu, yalitupwa katika kijito Kidroni au Kedroni au mazingira ya kijito hiki; wakati wa Wafalme waliofanya mapenzi ya Mungu (2 NYAKATI 15:16; 30:13-14; 2 WAFALME 23:4,6).  Yesu alipokwenda ng’ambo ya kijito hiki cha Kedroni pamoja na wanafunzi wake, ilikuwa ni alama ya kutupeleka mbali na machukizo yote pale tunapomwamini Yesu.  Zaidi tena, Yesu alikwenda kuanza mateso yake Mlima Mizeituni uliokuwa MASHARIKI mwa Yerusalemu, na kumaliza mateso yake kwenye mlima wa Kalvari au Golgotha, uliokuwa MAGHARIBI mwa Yerusalemu.  Kwa kuanza mateso mashariki na kumaliza mateso hayo magharibi mwa Yerusalemu, Yesu aliziweka dhambi zetu mbali nasi kama mashariki ilivyo mbali na magharibi (ZABURI 103:12).

 

(3)        KUINGIA KWA YESU KATIKA BUSTANI (MST. 1)

Baada ya Yesu kwenda ng’ambo ya kijito Kedroni, aliingia katika bustani.  Kwa nini aliingia katika bustani hii?  Katika bustani ya Edeni, ndipo dhambi ilipoanza, na tena ndipo laana ilipotangazwa kwa mwanadamu kutokana na dhambi hiyo.  Siyo hilo tu.  Katika bustani ya Edeni ndipo Mungu aliposema atamleta mkombozi, uzao wa mwanamke ambaye atamponda kichwa nyoka yaani Shetani (MWANZO 3:8-19).  Kwa sababu hii Yesu Kristo ili kutukamilisha wanadamu kwa njia ya mateso yake alianza kutoa dhabihu kwa mateso yake katika BUSTANI!  Hata baada ya kufa kwake, alizikwa pia katika bustani ili tupate kuwa viumbe vipya na apate kufuta kwetu laana iliyoletwa kwetu katika bustani (YOHANA 19:40-42).

 

(4)        YESU NA WANAFUNZI WAKE MAHALI PA MATESO (MST. 1)

“Akaingia yeye na wanafunzi wake“, ni maneno yanayotufundisha kwamba Yesu alikwenda na wanafunzi wake mahali pa mateso katika bustani.  Kila mwanafunzi wa Yesu, hana budi kupitia katika vipindi vya mateso na maudhi ya kila namna kutokana na wokovu wetu.  Hatupaswi kuona mambo haya kuwa ni ajabu (WAFILIPI 1:29-30; 2 TIMOTHEO 3:12; 1 PETRO 4:12-16).  Katika vipindi hivi vya mateso, Yesu huwa anatupeleka bustanini.   Hata hivyo, kama wanafunzi walivyomwona Yesu akaiwashindia vita katika bustani na kusema “Waacheni hawa waende zao“ (MST.8), hatuna budi kufahamu na kuamini kwamba atatushindia sisi nasi na kuhakikisha tunaachwa na maadui na kwenda zetu kilaanapotupeleka bustanini.

 

(5)        ADUI ZA MTU NI WATU WA NYUMBANI MWAKE (MST. 2)

Yuda, mtu aliyemfahamu Yesu vizuri na kupajua akaapo, ndiye anayejitokeza kuwa adui wa Yesu.  Tunapookolewa na kuwa wanafunzi wa Yesu tunaolifuata Neno la Mungu kama lilivyo, tutaona wale wa nyumbani kwetu, wawe ni waume zetu, wake zetu, watoto wetu, wazazi wetu, marafiki wa zamani n.k,, wakiwa maadui, wakipinga wokovu tulioupokea na kutukatisha tamaa, na hata kutuletea maudhi na mateso.  Hatupaswi kuona ajabu (MIKA 7:6).  Inatupasa kuwa waaminifu hata kufa pamoja na uadui wao, tukilishikilia Neno la Mungu kwa gharama yoyote ili tupate taji ya uzima (UFUNUO 2:10).

 

(6)        MAADUI WENGINE WA YESU KRISTO (MST. 3)

Kikosi cha askari (Kiyunani “SPEIRA“) kilikuwa kikosi cha askari wapatao 600.  Askari hawa walikuwa askari wa Kirumi ambao waliwekwa kwenye mnara wa Antonia ili kuulinda mji.  Hivyo hawa hawakuwa Wayahudi ila walikuwa MATAIFA.  Watumishi waliotoka kwa wakuu wa Makuhani na Mafarisayo, walikuwa Wayahudi.  Mataifa na Wayahudi walikuwa na uadui lakini hata hivyo walipatana na kuwa upande mmoja kinyume na Yesu.  Ndivyo ilivyo hata kwetu.    Hata ndugu ambao walikuwa hawapatani, tutashangaa kuona wakipatana na kuwa kinyume na imani yetu ya wokovu.  Hatupaswi kuona ni ajabu.  Kwake Yesu pia hapa, wafalme wa dunia pamoja na wakuu wa makuhani walijipanga kinyume chake.  Hata kwetu ni vivyo hivyo, wakati mwingine viongozi wa dini wanaweza kushikiana na viongozi wa dola na kuwa kinyume na Injili ya Kweli.  Hatupaswi kuona ajabu (ZABURI 2:2).  Tukipelekwa mabarazani, Roho Mtakatifu hutupa ya kusema katika mazingira haya (MATHAYO 10:17-20).  Hapa tunaona Yesu akiwa na maadui wengi walio kinyume chake kuliko wale walio upande wake.  Tukimfuata Yesu katika huduma zetu, itakuwa jinsi hiyo hiyo.  Maadui zetu watakuwa wengi kuliko wale walio upande wetu.  Watakaokuwa upande wetu ni wale tu walio wanafunzi wa kweli wa Yesu na wachache wengine.

 

(7)        ALAMA KUU YA KUMSALITI YETU (MST. 5)

Alama kuu ya kumsaliti Yesu, ni kusimama pamoja na wenye dhambi tuliowaacha tulipookoka na kufanya yaleyale wanayoyafanya wao.  Ikiwa kabla ya kuokoka tulikuwa wapenda muziki wa dansi, walevi, wazinzi, waasherati, wezi, wavuta sigara au wasengenyaji n.k., na sasa tumeanza kufanya hayohayo, ina maana sisi ni wasaliti wa Yesu Kristo.  Kwa nini tumsaliti Yesu tunayefahamu mapenzi yake?

 

(8)        SILAHA ZA KIROHO ZA VITA (MST. 4-11)

Simoni Petro alitumia upanga katika vita hivi na Yesu akawa kinyume na tendo hilo.  Yesu yeye, alitumia silaha za kiroho za vita na zikaleta matokeo ya kushangaza.  Kwa yeye kusema “Ni mimi“, kujitambulisha huko kulilifanya jeshi lote la Shetani kuanguka mweleka.  Nasi tunapoliitia Jina la Yesu katika vita vyovyote tunaposema “Kwa Jina la Yesu“, Shetani na majeshi yake huanguka mweleka.  Kwa kutokuamini, wengi wetu haulidharau jina hili lenye nguvu kuliko ngumi au upanga.  Jina la Yesu ndilo silaha yetu kubwa ya kiroho dhidi ya Shetani na ina uwezo mkubwa wa kuangusha ngome zozote (2 WAKORINTHO 10:3-5).  Hata hivyo ikiwa hatujaokoka ni hatari kulitumia Jina la Yesu dhidi ya Shetani.  Hatuna budi kuokoka kwanza (MATENDO 19:13-16).

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements

One comment on “KUINGIA KWA YESU KATIKA BUSTANI

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s