KUJISHUHUDIA MWENYEWE

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

SOMO:          KUJISHUHUDIA MWENYEWE

T

unaendelea tena, kujifunza Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu.  Leo, tunajifunza YOHANA 5:31-47.  Ingawa kichwa cha somo letu leo, ni “KUJISHUHUDIA MWENYEWE“, kuna mengi zaidi ya kujifunza katika mistari hii.  Tutayagawa mafundisho yote tunayoyapata katika mistari hii, katika vipengele kumi:-

(1)          KUJISHUHUDIA MWENYEWE (MST. 31-33);

(2)          KWELI NI NINI? (MST. 33);

(3)          MTU KUOKOKA AKIWA DUNIANI (MST. 34);

(4)           WAJIBU WA KUWA TAA IWAKAYO NA KUNG’AA (MST. 35);

(5)          USHAHIDI WA KUTUMWA NA MUNGU (MST. 36-37);

(6)          UMUHIMU WA KUYACHUNGUZA MAANDIKO (MST. 38-39);

(7)          HATARI YA KUKATAA KUJA KWA YESU (MST. 40);

(8)          JINSI YA KUWA NA UPENDO WA MUNGU NDANI YETU (MST.

           42-43);

(9)          UMUHIMU WA KUTAFUTA UTUKUFU KWA MUNGU (MST.

           41,44);

(10)       ANAYEWASHTAKI, NDIYE MUSA (MST. 45-47).

 

(1)      KUJISHUHUDIA MWENYEWE (MST. 31-33)

Baada tu ya kuokoka, ni wajibu wa kila mtu kukiri wokovu alioupokea mbele ya watu wote.  Siyo jambo linalomfurahisha Mungu, pale tunapookoka na kukaa kimya bila kuwapa taarifa waume au wake zetu, ndugu, jamaa na marafiki.  Hatuna budi kufuata mfano wa wanafunzi wa yesu waliotutangulia (MATHAYO 10:32; YOHANA 1:41).  Hata hivyo, kujishuhudia wenyewe kwambatumeokoka hakutoshi.  Vicyo hivyo, kujishuhudia wenyewe kwamba tumetakaswa au kujaa nguvu ya Roho Mtakatifu au kujishuhudia wenyewe kwamba tuina karama fulani au ni waalimu, waombaji, n.k; hiyo haitoshi.  Hatuna budi kuwa na mashahidi wawili au watatu wanaothibitisha madai yetu.  Shahidi wa kwanza anapaswa kuwa Mungu (MST. 32; YOHANA 8:17-18).  Shahidi wa pili ni wanadamu wanaotuzunguka, hasa wale wa nyumbani mwetu au katika nyumba tunayoipanga au tulio nao Kanisa moja n.k.  Mume au mke wetu au watu wanaokiri kwamba maisha yetu yamebadilika, au tuna hiki au kile, ni ushahidi wa muhimu katika kuyathibitisha madai yetu.  Yohana alimshuhudia Yesu aliye kweli (MST. 33).

 

(2)      KWELI NI NINI? (MST. 33)

Pilato aliuliza “Kweli ni nini?“ (YOHANA 18:38).  Sisi nasi, haitoshi tu kuwa na dini, ni lazima tuitafute Kweli kwa gharama yoyote.  Kweli ni Yesu Kristo mwenyewe.  Yohana alimshuhudia Yesu aliye Kweli.  Yesu Kristo ndiye Kweli (YOHANA 14:6).  Ikiwa Yesu hayuko mioyoni mwetu, hatuna hiyo Kweli.  Hata hivyo, kuna mengine ya kujifunza zaidi kuhusu Kweli.  Kweli pia, ni Neno la Mungu.  Aliye wa hiyo Kweli, huisikia sauti ya Yesu na kuifuata mara moja.  Maisha yake yote, huongozwa na Neno la Mungu, siyo maneno ya wanadamu (YOHANA 17:17; 18:37; ZABURI 119:9).  Mahali palipo na mafundisho ya Kweli ni mahali anapohubiriwa Yesu Kristo anayeokoa, na panapofundishwa kila jambo kwa kutumia tafsiri sahihi ya Neno la Mungu.  “Kama yanenavyo maandiko”, itakuwa ndiyo mwongozo wa mahali palipo na Kweli, na siyo Katiba! (1 WAKORINTHO 15:3-4)

 

(3)      MTU KUOKOKA AKIWA DUNIANI (MST.34)

Katika msitari huu tunaona Yesu mwenyewe akihubiri wokovu kwa watu waliokuwako duniani, kudhihirisha kwamba mtu anaokoka akiwa duniani.  Maandiko mengi yanadhihirisha pia kwamba wokovu ni hapahapa duniani palipo na dhambi na ushindani, na siyo mbinguni (ZABURI 16:3; LUKA 19:9; TITO 2:11-12; 3:3-6).

 

(4)      WAJIBU WA KUWA TAA IWAKAYO NA KUNG’AA (MST.35)

Yohana Mbatizaji, alikuwa taa iwakayo na kung’aa na watu walipenda kuishangilia nuru yake.  Huu ni wajibu wa kila mtu asemaye ameokoka, kuwa taa iwakayo na kung’aa, au NURU ya Ulimwengu (MATHAYO 5:14).  Nuru, au taa iwakayo na kung’aa, huonekana kwa mbali, haifichiki.  Ikiwa kweli tumeokoka, watu ambao hawajaokoka, watatuona kwa mbali na kuwa mashahidi wa wokovu wetu tunaouzungumza.  Siyo hilo tu, giza haliwezi kuikaribia nuru wala giza haliwezi kushindana na nuru.  Sisi nasi, ikiwa tumeokoka, dhambi ambayo ndiyo giza, haiwezi kutukaribia.  Wakatiwote tutaifukuza na kuishinda dhambi.  Kama Mungu alivyo Nuru, sisi nasi ni nuru, wala hatuwezi kwenda gizani au dhambini kamwe (1 YOHANA 1:5-7; YOHANA 8:12).

 

(5)      USHAHIDI WA KUTUMWA NA MUNGU (MST. 36-37)

Ni rahisi kumfahamu mtu aliyetumwa na Mungu.  Kazi anazozitenda yeye aliyetumwa na Mungu, zitamshuhudia.  Kazi hizo, ni pamoja na kuyanena maneno ya Mungu (YOHANA 3:34), kuishi maisha ya Utakatifu katika kusema, kuwaza na kutenda (1 PETRO 1:15-16, 23; YAKOBO 3:2, 10-12) na pia kuzitenda  kazi zitakazodhihirisha waziwazi uwezo wa Mungu ulio pamoja naye na jinsi Mungu anayotenda kazi pamoja naye (MARKO 16:20).

 

(6)      UMUHIMU WA KUYACHUNGUZA MAANDIKO (MST. 38-39)

Watu hawa waliyachunguza maandiko.  Walitumia muda mrefu sana kusoma maandiko, kwa sababu walijua kwamba uzima wa milele, umo katika maandiko.  Sisi nasi, inatupasa kufanya hivyo, kama jinsi ile ile walivyofanya pia watu wa Beroya (MATENDO 17:10-11).  Hatuna budi pia kujua kwamba uzima wa milele uko katika MAANDIKO.  Tusikubali kamwe kudanganywa na waalimu wa uongo wanaotufundisha kwamba kufanya hili na lile katika maandiko, siyo lazima, na eti leo hatupaswi kuongozwa kwa sheria.  Ni kweli kwamba hatuko chini ya sheria ya Musa, hata hivyo, tuko chini ya sheria ya Kristo, ambayo ndiyo Kweli yenyewe (WAGALATIA 6:2).  Lakini kuna jambo jingine la kutafakari.  Haitoshi tu kuchunguza maandiko wenyewe, lazima pia tukubali kuongozwa na waalimu au siyo hatutafidiaka kama walivyokuwa watu hawa (MATENDO 8:30-31; ISAYA 30:21).

 

(7)      HATARI YA KUKATAA KUJA KWA YESU (MST. 40)

Tusipokuja kwa Yesu kwa kutubu dhambi zetu kwa kumaanisha kuziacha na kutafuta rehema, tutakosa kabisa uzima wa milele bali ghadhabu ya Mungu itatukalia.  Ni muhimu kufahamu kwamba wema wa Mungu kwetu, unatuvuta tu kutubu (WARUMI 2:4-6).  Kwa nini tusije kwake Yesu alitufia msalabani?

 

(8)      JINSI YA KUWA NA UPENDO WA MUNGU NDANI YETU (MST. 42-43)

Hakuna namna yoyote ya kuwa na upendo wa Mungu ndani yetu isipokuwa kwa kumpokea Yesu aliye Pendo, mioyoni mwetu; na kukubali atutawale.  Akitutawala katika kila sehemu ya miasha yetu, kwa neno lake, ilivyo ni kwamba, Pendo mwenyewe atakuwa ndiye anayetutawala na upendo wa MUngu utakuwa ndani yetu, na matokeo yake, tutawapenda watu waliookoka kuliko ndugu zetu wa kimwili (1 YOHANA 3:14-16; 4:7).

(9)      UMUHIMU WA KUTAFUTA UTUKUFU KWA MUNGU (MST. 41-44)

Wako watu wengi ambao wanajisumbua kutafuta kwa nguvu zote, heshima au utukufu kwa wanadamu.  Haitupasi kufanya hivyo.  Tutafute heshima kwa Mungu kwanza, kwa kutoa maisha yetu kumtumikia na kumfuata katika kila Neno, na Baba wa Mbinguni akituheshimu, wanadamu nao lazima watatuheshimu (YOHANA 12:26).  Hii ndiyo siri ya kuheshimiwa na wanadamu.

(10)    ANAYEWASHTAKI, NDIYE MUSA (MST. 45-47)

Watu wengi leo bado wanashika sheria ya Musa katika kushika Sabato, kutokula nguruwe, kutawadha kwingineko kwa ajili ya ibada, kutoa sadaka za wanyama, na kuishika torati ya jino kwa jino na mengineyo.  Hawa wanashitakiwa na Musa mwenyewe, maana Musa aliandika habari za Yesu (KUMBUKUMBU 18:18-19; YOHANA 1:45; MATENDO 3:20-22).  Musa alikuwa anatuongoza kutuleta kwa Yesu aliye PUMZIKO, au SABATO, tuje kwake naye atatupumzisha (MATHAYO 11:28).  Tukitaka Musa asitushtaki basi tumfuate Yesu katika maneno yake yote.

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s