KUOGOPA KUTENGWA NA SINAGOGI

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

 

SOMO:  KUOGOPA KUTENGWA NA SINAGOGI

K

atika mfululizo wa masomo ya Biblia kutoka katika Kitabu cha YOHANA, laeo tunajifunza YOHANA 9:6-34.  Ingawa kichwa cha somo letu la leo ni, “KUOGOPA KUTENGWA NA SINAGOGI“, kuna mengi ya kujifunza katika mistasri hii.  Tutaligawa somo letu la leo, katika vipengele saba:-

(1)  KUMPONYA KIPOFU KWA TOPE NA MATE (MST. 6-7);

(2)  BADILIKO KUBWA BAADA YA KUOKOLEWA (MST. 8-9);

(3)  UMUHIMU WA KUSHUHUDIA JUU YA MIUJIZA TUNAYOIPATA (MST.    

  10-11);

(4)  KUTENDA MEMA BILA KUNGOJEA ASANTE (MST. 12);

(5)  YESU HAKUISHIKA SABATO (MST. 13-17);

(6)  KUOGOPA KUTENGWA NA SINAGOGI (MST. 18-23);

(7)  KUTOKUWA TAYARI KUFUNDISHWA (MST. 24-34).

 

(1) KUMPONYA KIPOFU KWA TOPE NA MATE (MST. 6-7)

Yesu Kristo, katika kumponya kipofu huyu tangu kuzaliwa alitema mate chini, akafanya tope kwa yale mate; kisha akampaka kipofu huyo tope za macho, na kumwambia akanawe katika birika ya Siloamu.  Kwa nini Yesu alifanya hivi?  Alitaka kutufundisha mambo mengi.  Mate na tope ni vitu vinavyodharauliwa na kuonekana ni uchafu.  Kutemewa mate ni ishara ya kufedheheshwa au kudharaulika (ISAYA 50:6).  Nyakati za Biblia, iliposemekana kwamba mtu fulani ametupwa nje au kukanyagwa kama matope ya njiani, ilimaanisha kwamba amedharaulika au ameaibika (MIKA 7:10; ZABURI 18:42).  Yesu Kristo, alidharauliwa na kukataliwa na watu.  Alihesabiwa si kitu na tna alihesabiwa hana uzuri wowote, na hawakumtamani, kama ilivyo kwa tope na mate (ISAYA 53:2-3).  Kwa jinsi hii ya kumponya kipofu, Yesu alitufundisha kwamba uzima na miujiza, vinapatikana kwake Yesu anayedharauliwa na kuonekana si kitu.  Kipofu huyu aliambiwa aende kunawa katika birika la Siloamu.  “Birika“ hapa, maana yake BWAWA.  Maji ya bwawa la Siloamu, pia yaliitwa maji ya Shiloa.  Maji ya bwawa hutembea polepole tofauti na maji ya mto.  Maji ya Shiloa katika unabii, yanafananishwa na Masihi Yesu Kristo.  Kuyakataa maji ya Shiloa yapitayo polepole, na kufurahi kwa ajili ya Resini na mwana wa Remalia (Mfalme wa Shamu na Samaria), katika unabii, ni kumkataa Masihi Yesu Kristo na kuyafurahia mapokeo ya wazee ya Waandishi na Mafarisayo (ISAYA 7:8-9; 8:5-6; MARKO 7:8-9).  Kipofu huyu aliambiwa anawe maji ya Shiloa au maji ya bwawa la Siloamu, aliambiwa amkubali Yesu Kristo aliye Masihi na kuyaacha mapokeo ya wazee.  Alipofanya hivyo, alipata uzima.  Ndivyo ilivyo hata leo.  Uzima uko katika neno la Kristo na siyo maneno yaliyotungwa na wanadamu (YOHANA 6:63).  Hapa alikandika tope machoni mwake kipofu tendo ambalo lingemfanya hata anayeona, asione lolote tena!  Hata hivyo tendo hili, ndilo lililoleta uzima.  Ni muhimu kufahamu hapa kwamba, njia za Mungu za kutupa miujiza yetu, ziko juu sana na tena ziko tofauti na njia za Kibinadamu (ISAYA 55:8-9).  Kuna jambo jingine la kujifunza hapa.  Mwanadamu mwenye dhambi ni kipofu tangu kuzaliwa.  Anapomwamini Yesu Kristo aliyetumwa (Siloamu maana yake “Aliyetumwa“), macho yake yanafumbuliwa na hivyo anaokolewa.  Hakuna wokovu kwa mwingine awaye yote isipokuwa kwa Yesu anayedharauliwa (YOHANA 9:39-41; MATENDO 26:18).

 

(2) BADILIKO KUBWA BAADA YA KUOKOLEWA (MST. 8-9)

Kipofu huyu alipofumbuliwa macho na Yesu , majirani zake walishindwa kumtambua, na kudhani siyo yeye au labda amefanana na yule waliyekuwa wanamfahamu.  Baada ya kuokolewa, ndivyo mtu aakavyokuwa.  Badiliko lake kimaisha liakuwa kubwa kiasi ya kwamba majirani na wale wote waliokuwa wanamfahamu, watashangaa na kudhani siye, labda amefanana na yule waliyekuwa wanamfahamu.  Atakuwa mbali na anasa za dunia na kupenda tu kumwelekea Yesu na neno lake.  Ikiwa tunasema tumeokolewa na hatuna badiliko kubwa linalowafanya majirani na marafiki zetu waone tuko tofauti sana, madai yetu kwamba tumeokoka siyo ya kweli.

 

(3) UMUHIMU WA KUSHUHUDIA JUU YA MIUJIZA TUNAYOIPATA (MST. 10-11)

Mtu huyu kipofu alipofumbuliwa macho yake na kupata muujiza wake, alieleza au kushuhudia kwa ujasiri jinsi alivyopokea muujiza.  Roho Mtakatifu katika maandiko haya anatupa ushuhuda wa mtu huyu akitufundisha umuhimu wa kushuhudia juu ya miujiza tunayoipata.  Yesu Kristo hutiwa moyo sana kufanya miujiza mikubwa kwa mtu yule aliye tayari kushuhudia jinsi alivyotendewa muujiza na kumrudishia mungu utukufu.  Ni muhimu kukumbuka kwamba miujiza, kazi yake ni kuzidhihirisha kazi za Mungu waziwazi hadharani na kumpa utukufu au heshima Yesu Kristo (YOHANA 9:1-3; 11:4).  Mtu yule aliyekuwa na pepo wengi (Legioni), katika MARKO 5, alipopata muujiza wake, alitaka awe pamoja na Yesu kimyakimya tu bila kushuhudia.  Yesu hakupendezwa na jambo hilo na alimuagiza aende kushuhudia kila mahali (MARKO 5:18-20).  Vivyo hivyo, Yesu hapendezwi na yeyote anayepata muujiza na kutaka kuendelea na Yesu kimyakimya tu bila kushuhudia.  Kuna baraka za ziada kwa yule anayezingatia fundisho hili (LUKA 17:7-10).

 

(4) KUTENDA MEMA BILA KUNGOJEA ASANTE (MST. 12)

Yesu Kristo, baada ya kumponya kipofu huyu, aliondoka na hakuonekana tena.  Kipofu aliporudi kumtafuta, hakumwona.  Hakungojea asante yoyote kwake.  Sisi nasi tunapaswa kutenda mema iwe ni kuwaombea wagonjwa na wenye shida na lolote lile jingine, bila kungoja asante au sifa yoyote, kama watumwa tunaofanya yanayotupasa kuyafanya (LUKA 17:7-10).

 

(5) YESU HAKUISHIKA SABATO (MST. 13-17)

Maandiko mengi yanadhihirisha kwamba Yesu hakuishika Sabato (MST. 16; LUKA 13;14; 14:1-6; YOHANA 5:16-18).  Yesu alikuja kuikomesha Sabato, sawasawa na unabii katika maandiko (HOSEA 2:11).  Kushika sabato, ilikuwa ni ishara au kivuli tu cha Yesu Kristo aliye PUMZIKO kwa wote waliolemewa na mizigo (WAKOLOSAI 2:16-17; MATHAYO 11:28).  Leo Wakristo tunamshika Yesu aliye Sabato na wala hatuishiki Sabato tena!  Hapa Yesu alisemekana kwamba hakutoka kwa Mungu, na tena ni mwenye dhambi (MST. 24), kwa sababu ya kutokuishika Sabato.  Washika Sabato wa leo, kama Mafarisayo vivyo hivyo, watatuhesabu na sisi tusioishika Sabato kama Bwana awetu Yesu, kuwa ni wenye dhambi.  Hatupaswi kuona ajabu.  Mtumwa si mkubwa kuliko Bwana wake (YOHANA 15:20; 1 YOHANA 2:6).  Tuzidi kufuata kielelezo cha Yesu.

 

(6) KUOGOPA KUTENGWA NA SINAGOGI (MST. 18-23)

Wazazi wa mtu huyu aliyekuwa kipofu, waliijua kweli kwamba mtoto wao alifumbuliwa macho na Yesu; lakkini hawakuwa radhi kuambatana na hiyo kweli, kwa sababu waliwaogopa Wayahudi kwamba watawatenga na sinagogi lao.  Ndivyo walivyo wengi leo, baada ya kuokolewa na kuijua kweli kuhusu Ubatizo wa Maji tele, kutofungiwa nira na wasioamini, na mafundisho mengine, wanashindwa kuambatana na hiyo kweli kwa kuogopa kutengwa na masinagogi au makanisa yao.  Itatufaidia nini kufanya hivyo?  Ni nani tunayempendeza au tunayemshawishi, ni Mungu au wanadamu?  Tukitafuta kuwapendeza wanadamu badala ya Mungu, tunakuwa upotevuni, na kuwa mbali na mifano ya watakatifu waliotutangulia (WAGALATIA 1:10-11; ZABURI 73:25).  Wengine wanaona uzito kutengwa na makanisa yao sababu ya uzee wa Kanisa au Vyeo vingine kama wakuu wanaotajwa katika YOHANA 12:42-43.  Hii ni hatari.  Kupenda vyeo ni mtego mkubwa wa kututoa katika mapenzi ya Mungu.  Yesu hakukubali cheo kimtoe katika mpango wa Mungu kwake (YOHANA 6:15).  Inatupasa kuiga mfano wake.

 

(7) KUTOKUWA TAYARI KUFUNDISHWA (MST. 24-34)

Waandishi na Mafarisayo, walijiona wanajua, hawakukubali kufundishwa na mtu waliyemwona hajui lolote (MST. 34).  Watu wengi wako kama watu hawa.  Wanajiona wao tu ndiyo wanajua, na hawako tayari kusikia mafundisho kutoka kwa mtu yeyote.  Hiki ni kiburi, na siyo njia ya kupata baraka za Mungu (1 WAKORINTHO 8:2; ZABURI 73:22).  Jambo jingine la kujifunza hapa, ni jinsi ya mtu aliyekutana na Yesu siku moja tu alivyokuwa mhubiri (MST. 27-31).  Baada tu ya kuokoka, ni wajibu wa kila mmoja wetu kuwahubiri wengine na kuwaleta kwa Yesu, bila kungojea kujua sana Biblia.  Tunajifunza pia kwamba dhambi zinatufanya tusisikilizwe na Mungu na kujibiwa.  Hatuna budi kuhakikisha tumekuwa mbali na dhambi kwa kuokolewa, ili tupate baraka tele na kusikilizwa na Mungu (MST. 31: MITHALI 15:29).

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s