KUONGOKA NA KUWA KAMA MTOTO

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

SOMO:      KUONGOKA NA KUWA KAMA MTOTO

Leo tunajifunza Biblia kutoka katika MATHAYO 17:24-27, na MATHAYO 18:1-4.  Ingawa kichwa cha somo letu la leo ni “KUONGOKA NA KUWA KAMA MTOTO“, kuna mengi zaidi ya kujifunza katika mistari hii.  Tutaligawa somo letu la leo katika vipengele sita:-

(1) SHEKELI KWA AJILI YA YESU NA PETRO (17:24-27);

(2)  SEHEMU YETU YA KUFANYA KATIKA KUKAMILISHWA KWA MIUJIZA                 MINGINE (17:27);       

(3)  NI NANI ALIYE MKUU (18:1-2);

(4)  MAANA YA KUONGOKA (18:3);

(5)  KUONGOKA NA KUWA KAMA MTOTO (18:3);

(6)  MSINGI WA KUWA MKUU MBELE ZA MUNGU (18:4).

 

(1)      SHEKELI KWA AJILI YA YESU NA PETRO (17:24-27)

Shekeli ilikuwa aina ya fedha ya nyakati za Biblia.  Kila mtu mwenye umri wa miaka 20 au zaidi alitakiwa kutoa Sadaka ya Bwana au Kodi ya Bwana – NUSU SHEKELI kila mwaka.  Kazi ya kodi hii ya Bwana, ilikuwa kuhakikisha kwamba kuna fedha ya kutosha kwa ajili ya utumishi wa hema ya kukutania au hekalu – gharama za vitu mbalimbali vilivyohitajika katika Utumishi wa Mungu hekaluni, n.k.  (KUTOKA 30:14-16; 2 MAMBO YA NYAKATI 24:9).  Hii ilikuwa ni kodi inayopelekwa hekaluni na siyo kwa watawala wa dunia.  Watoto wa Wafalme wa dunia, walikuwa hawatozwi kodi ama ushuru bali wafalme wa dunia walipokea kodi kwa wale wasio watoto wao.  Kuambatana na sababu hii, Yesu hakupaswa kutoa kodi hiyo kwa misingi ifuatayo:-

  1. Hekalu lilikuwa lake (MALAKI 3:1);
  2. Hekalu lilikuwa Nyumba ya Baba yake (LUKA 2:46-49; YOHANA 2:14-16);
  3. Kristo ni mwana juu ya nyumba ya Mungu (WAEBRANIA 3:6);
  4. Yesu ni mkuu kuliko hekalu (MATHAYO 12:6).

Ingawa Yesu alikuwa huru kuacha kutoa kodi hii (WANA NI MAHURU), hata hivyo Yesu alitoa kodi hiyo akitupa sisi kielelezo cha kutoa yanayotupasa kutoa kwa Mungu na hata kwa wafalme (MATHAYO 22:17-21; WARUMI 13:7).  Utumishi wa Mungu unahitaji kodi zetu ili kazi ya Mungu ipate kufanyika, na vilevile utumishi wa Serikali unahitaji kodi zetu ili huduma mbalimbali kwa wananchi zipate kuwapo.

(2)      SEHEMU YETU YA KUFANYA KATIKA KUKAMILISHA MIUJIZA MINGINE (17:27)

Kupata shekeli kutoka katika mdomo wa samaki, ilikuwa muujiza mkubwa.  Hata hivyo, Yesu alimwambia Petro kwenda baharini, kutupa ndoana na kuvua samaki, ili aone muujiza huo ukitimia.  Vivyo hivyo, tunapomwomba Mungu atupe muujiza wa kupata kazi itakayotupa mapato au shekili, ni wajibu wetu kutuma barua za maombi ya kazi na kuzifuatilia kwa bidii yote na siyo tu kukaa tu nyumbani.  Tukiomba muujiza wa “Scholarship“ au nafasi ya masomo nje ya nchi, ni wajibu wetu kutuma barua za maombi na kuzifuatilia kwa bidii yote n.k.

(3)      NI NANI ALIYE MKUU (18:1-2)

Kutokana na sifa alizokuwa nazo kila mwanafunzi wa Yesu, kila mmoja alijiona kuwa anapaswa kuwa MKUU WA WOTE.  Yuda Iskariote alikuwa na mfuko wa fedha (YOHANA 13:29), hivyo aliona kuwa anagepaswa kuwa mkuu wa wote.  Ndivyo watu wengi tuliookoka tulivyo, tunafikiri kwa kuwa sisi ni matajiri, basi tuna haki ya kuwa Viongozi katika Kanisa au  kwa kuwa tunashika fedha ya Kanisa basi ni wakuu kuliko wote.  Petro alikuwa msemaji mkuu wakati wote hivyo aliona yeye ndiye.  Wengi wetu kwa kuwa ni wasemaji sana, washuhudiaji sana, waombaji sana, tunaona kuwa tunapaswa kuwa wakuu.  Yuda aliyeandika kitabu cha Yuda, pamoja na Yakobo aliyeandika kitabu cha Yakobo, walikuwa ndugu zake Yesu (WAGALATIA 1:19; MATHAYO 13:55).  Wengi wetu tunafikiria kuwa tukiwa kabila moja na Mchungaji au shemeji zake au ndugu wa namna nyingineyo, basi tuna haki ya kuwa Viongozi katika Kanisa na kuwa wakuu kuliko wote.  Yohana alipendwa na Yesu na kuwa karibu naye (YOHANA 21:20).  Wengine wetu kwa kuwa tuko karibu na Mchuingaji mara kwa mara na kuitwa kwake kila wakati, tunafikiri tuna haki ya kuwa wakuu kuliko wote.  Mathayo alikuwa msomi wa nyakati zile, mtoza ushuru (MATHAYO 9:9).  Wengine wanafikiri kwa kuwa ni wasomi kuliko wengine wote basi wanapaswa kuwa wakuu kuliko wote katika Kanisa.  HIZI ZOTE SIYO SIFA ZA KUWA MKUU MBELE ZA MUNGU.

(4)      MAANA YA KUONGOKA (18:3)

Neno “KUONGOKA“, Kiebrania ni “SHUB“ ambalo maana yake ni “kugeuka na kuacha njia ya mwanzo na kubadilika kabisa“.  Baada ya kuokolewa, hatuwi tumefika.  Tunapaswa kuwa tayari kuongoka siku kwa siku kwa kugeuka na kuacha njia za mwanzo za maisha yetu, na kubadilika kabisa baada ya kulisikia Neno la Mungu kila siku tunapojifunza.  Mtu aliyeokoka ambaye yuko tayari kuongoka kila wakati anapolisikia Neno la Mungu huyo tu ndiye atakayeurithi uzima wa milele.  Wako watu wengine waliookoka wanaolisikia Neno la Mungu kila siku, lakini  hawageuki na kuacha njia zao na kubadilika.  Hawa hawawezi kuuingia Ufalme wa mbinguni pamoja na kusema wameokoka (EZEKIELI 33:12-13, 18).

(5)      KUONGOKA NA KUWA KAMA MTOTO (18:3)

Kama hatuongoki yaani kama hatubadiliki na kuwa kama watoto wadogo, hatuwezi kamwe kuuingia ufalme wa mbinguni.  Ni muhimu kufahamu sifa za watoto wadogo ili zitupe changamoto ya kumwomba Mungu atupe neema ya kuongoka na kuwa kama wao.  Zifuatazo ni sifa za watoto wadogo:-

1.         Hawana kinyongo, ni wepesi kusamehe na kusahau.  Wakati wazazi wao   wanafokeana, wao huwa tayari wamesameheana na kucheza kwa furaha.  Sisi nasi tunapaswa kuwa hivyo (WAEFESO 4:32).

2.         Hucheza pamoja watoto maskini na watoto wa matajiri kwa upendo bila kubaguana.  Sisi nasi tunapaswa kupendana hivyo (YOHANA 13:34-35);

3.         Hukubali kila wanaloambiwa na wazazi bila kubishana.  Wakiuliza hii ni nini; wajibiwa “mbuzi“, basi hulichukua hivyo hivyo.  Sisi nasi tunapaswa kulitii na kulifuata kila neno la Mungu bila kulifanyia mjadala (ZABURI 119:6);

4.         Hucheza pamoja bila kuuliza hata majina au kabila.  Sisi nasi tunapaswa kuwapenda wote waliookoka bila kujali majina ya madhehebu yao (LUKA  :49-50);

5.         Lolote linalowatatiza, huwafanya wawalilie wazazi.  Sisi nasi tunapaswa kuomba bila kukoma na kulia pamoja na waliao (1 WATHESALONIKE 5:17; WARUMI 12:15);

6.         Hujiona hawajui na hivyo huwa tayari kuongozwa wakati wote bila kiburi moyoni.  Sisi nasi inatupasa kuwa hivyo (1 WAKORINTHO 8:2; WAFILIPI 3:12);

7.         Ni wadogo wa kimo na umbo.  Wakati wote wanajifahamu kwamba wao ni wa kutawaliwa.  Sisi nasi tunapaswa wakati wote kujiona ni wadogo kila mahali pamoja na lolote lile ambalo Mungu analitenda kupitia kwetu.  Tujione hatuna nguvu yoyote, hatuwezi lolote bila Yesu na kutupa kiburi na majivuno yote mbali nasi (WAFILIPI 2:3; 4:13; YOHANA 15:5).  Mtoto mdogo hana ulimi mkubwa!  Kijapo kiburi, ndipo ijapo aibu (MITHALI 11:2).  Tuwe tayari kutawaliwa.

8.         Katika michezo yao, watoto hawaoni kinyongo kuongozwa na mdogo kuliko wao anapowapeleka mahali pa kucheza n.k.  Hatupaswi kujivunia akili na kuona sisi tu ndio tunaofaa kuongoza kukataa kuongozwa (WARUMI 12:16).

9.         Huwa hawaoni taabu yoyote wasipoheshimiwa, wakidharauliwa, wakitukanwa n.k.  Huwa hawategemei kukaa mbele kwenye heshima.  Hukaa chini sakafuni wanapokula!  Hatupaswi kuwa watu wa kupenda na kuitafuta heshima (YEREMIA 45:5).

10.       Wamejaa imani.  Ukimwambia mtoto beba ndoo, huibeba bila kujali kwa kuwa amesikia mzazi akimwambia.  Huamini kuwa wazazi wao wana kila kitu kwa ajili ya mahitaji yao.  Sisi nasi tunapaswa kuwa watu wa imani (WARUMI 14:23).  Tuamini kuwa Mungu ana vyote kwa ajili yetu.

(6)      MSINGI WA KUWA MKUU MBELE ZA MUNGU (18:4)

Msingi wa kuwa mkuu mbele za Mungu ni kushuka chini na kuwa kama mtoto mdogo bila kujali chochote tulicho nacho.  Anayetaka kuwa mkubwa, au wa kwanza mbele za Mungu, awe mtumwa au mdogo wa wote (MATHAYO 20:26-27; LUKA 22:24-26).  Siku zote Mungu huwatafuta wale wanaokuwa tayari kuwa wadogo na kuwa tayari kuongozwa.  Hawa ndio ambao wanaoinuliwa juu na Mungu, na kufanya makubwa katika Jina la Yesu.  Yesu alikuwa Mungu lakini alinyenyekea na alipozaliwa kwa umbo la mwanadamu alilazwa kwenye hori ya kulia ng’ombe na kuchukua namna ya mtumwa.  Hiyo ndiyo siri ya mafanikio makubwa ya huduma aliyokuwa nayo (YAKOBO 4:6).

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s