KUSULIBISHWA KWA YESU

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

SOMO:   K U S U L I B I S H W A    K W A    Y E S U

Leo, tunaendelea kujifunza Biblia, kwa kuendelea kukichambua Kitabu cha MATHAYO.  Leo, tutajifunza kwa undani, MATHAYO 27:26-50.  Katika mistari hii, tutajifunza juu ya KUSULIBISHWA KWA YESU.  Tutaligawa somo letu la leo katika vipengele viwili:-

(1)  KUPIGWA NA KUDHIHAKIWA KWA YESU    (MST 26-31)

(2)  KUSULIBISHWA KWA YESU   (MST 32-50)

 

(1)       KUPIGWA NA KUDHIHAKIWA KWA YESU   (MST 26-31)

Kabla ya Yesu Kristo kupelekwa kusulibiwa, alipigwa kwanza na kudhihakiwa.  Alipigwa mijeledi.  Mjeledi, ulikuwa ni zana ya Kirumi ya kuuadhibu vibaya mwili.  Mjeledi, ulikuwa ni namna ya mpini au kishikio, kilichoambatanishwa na kamba kama kumi na mbili za ngozi, zenye matawi ya mifupa iliyochongoka au namna ya mabati yaliyochongoka.  Mtu anayepigwa, alifungwa kwa kamba kwenye mti au nguzo kabla ya kupigwa (MATENDO 22:24-25).  Alivuliwa nguo na kupigwa uchi wa mnyama.  Alipigwa matako, mgongo, kiuno na hata tumbo na uso.  Adhabu hii, ilikuwa mbaya sana kiasi kwamba wengi walizimia na kufa.  Mtu alipigwa mijeledi kufikia 40 (KUMBUKUMBU 25:3).  Wayahudi walipunguza na kufanya “mapigo arobaini kasoro moja” (2 WAKORINTHO 11:24).  Warumi walizidisha.  Ni dhahiri Yesu alipigwa mijeledi siyo chini ya arobaini.  Ikiwa mjeledi uliotumika ulikuwa na kamba 12, ina maana jumla ya michirizi ya mapigo hayo ilikuwa 40×12=480.  Mahali ambapo mjeledi ulirudi hapohapo kwenye sehemu moja, ulinyofoa nyama kipekee kwa mabati yale au mifupa iliyochongoka.  Mwili wa Yesu uliharibiwa pasipo mfano, kwa mijeledi hiyo (ISAYA 52:14).  Baada ya kupigwa mijeledi namna hii, bila kupumzika, alichukuliwa na askari wa liwali Pilato kwenye PRAITORIO, nyumba ya Uliwali, kama Ikulu.  Yesu hapo akazungukwa na kikosi kizima (Kiyunani: SPEIRA) cha askari Watesaji wapatao 600!  Huyu Pilato aliyesema kuwa haoni hatia ya Yesu, sasa anairuhusu nyumba yake itumiwe kumdhihaki.  Hii ni dhambi kubwa.  Tukiwa wenye nyumba au vichwa vya nyumba, hatupaswi kumruhusu mtoto wetu au mtu yeyote kumdhihaki Yesu katika nyumba zetu kwa kuleta sinema za video za kidunia, picha chafu, pombe, makahaba, sanamu za watakatifu, mambo ya ushirikina au lolote lililo kinyume na Injili.  Kufanya hivyo ni kukubaliana nao wayatendao  (WARUMI 1:32).  Katika Praitorio, walimfanyia Yesu yafuatayo:-

 1. WALIMVUA NGUO  (MST 28)  – Aibu ya uchi ililetwa kutokana na dhambi ya Adamu (MWANZO 3:9-11).  Ili Yesu atukomboe katika dhambi, alikubali aibu hiyo ili atupe uwezo wa kuvaa mavazi meupe ya kuficha aibu yetu ya uchi wetu.  Kila mwenye dhambi yuko uchi mbele za Mungu.  Kwa kumwamini Yesu, anavikwa mavazi hayo meupe (UFUNUO 3:17-18).
 2. ALIVIKWA VAZI JEKUNDU (MST 28) – Mavazi mekundu yalikuwa ya Wafalme.  Hapa walimvika vazi kuukuu jekundu la kumdhihaki “Mfalme wa Wayahudi”.  Lakini lilitendeka jambo kubwa hapo.  Dhambi zetu zilikuwa nyekundu kama bendera (nguo ya kifalme) – ISAYA 1:18.  Yesu Kristo alipovaa vazi jekundu, alichukua dhambi zetu ili azitundike msalabani na kutuosha kwa damu yake.
 3. ALIWEKEWA TAJI YA MIIBA (MST 29) – Miiba hii, haikuwa pambo, bali ilikuwa inatumika kumfundisha mtu na kumpura nyama ya kichwa kwa kupigiliwa kichwani (WAAMUZI 8:7,16). Yalikuwa ni mateso makuu.  Miiba, ilikuja duniani kutokana na laana iliyosababishwa na dhambi (MWANZO 3:17-18).  Alifanyika laana, ili kutuondolea laana.
 4. WALIMWEKEA MWANZI MKONONI (MST 29) – Wafalme, walishika fimbo mkono wa kuume kama alama ya mamlaka.  Huyu walimwekea mwanzi kwa dhihaka, wakijaribu kuonyesha kwamba ufalme wake ni kama unyasi unaotikiswa na upepo (MATHAYO 11:7).  Walikosea sana, Ufalme wake ni wa milele na fimbo yake ni ya adili (ZABURI 45:6).
 5. WALIMPIGIA MAGOTI KWA KUMDHIHAKI (MST 29) – Kila anayemdhihaki leo Yesu, atake asitake, siku moja atapiga goti mbele zake kikweli (WAFILIPI 2:8-10).
 6. WALIMTEMEA MATE (MST 30) – Baada ya hayo, akatemewa mate tena kama wakuu wa makuhani walivyomfanyia hapo awali, kumwaibisha.  Aliichukua aibu yetu.  Tulimtemea mate Yeye mwenye uso uliobarikiwa unaong’aa kuliko jua!  Lilikuwa jambo la huzuni.
 7. WALIMPIGA KWA MWANZI (MST 30) – Waliutwaa mwanzi na kuzidi kuishindilia miiba kichwani.  Alipigwa kwa sababu ya makosa yetu.  Baada ya hapo, wakamchukua kwenda kumsulibisha.

 

(2)      KUSULIBISHWA KWA YESU    (MST 32-50)

Yesu alisulibishwa nje ya lango la Yerusalemu, ili atutakase kwa damu yake (WAEBRANIA 13:12).  Wayahudi, hawakumstahi Mwana wa Mungu, walimtupa nje ya shamba la mizabibu la Yerusalemu, na wakamwua, kama alivyotabiri (MATHAYO 21:37-39).  Alionekana hafai Yerusalemu kama wenye dhambi wengi wanavyoona hafai kwao.  Alitoka huku akiuchukua msalaba mwenyewe (YOAHANA 19:17).  Hatimaye wakamwona mtu Mkirene, jina lake Simoni, WAKAMSHURUTISHA auchukue msalaba wake.  KIRENE ilikuwa ndiyo mji mkuu wa nchi ya LIBYA (LIBIA), iliyoko Afrika ya Kaskazini (MATENDO 2:10); hivyo Simoni alikuwa Mwafrika.  Hakupenda, bali alishurutishwa.  Yesu alikufa kwa ajili ya Afrika pia.  Waafrika tuamke na tuache kuweka macho yetu kwa Wazungu tu!  Kama Simoni, inatupasa kuuchukua msalaba wa Yesu kila siku yaani aibu, mateso, dhihaka, dharau n.k.  kwa ajili ya wokovu wetu (MST 32, LUKA 9:23).  Walimchukua mpaka mahali panapoitwa GOLGOTHA, katika lugha ya Kiebrania.  Jina hilo katika lugha ya Kiyunani ni CALVARIA.  Kiingereza ni CALVARY (LUKA 23:33 KJV BIBLE).  Kiswahili, Fuvu la Kichwa au KALVARI.  Kulingana na Mwandishi ORIGEN wa Karne ya Kwanza, Kalvari, ni mahali panaposadikiwa kwamba ndipo lilipoonekana Fuvu la Kichwa cha Adamu, mtu wa Kwanza kuishi duniani.  Hapohapo ndipo Adamu wa Pili Yesu Kristo, alipotupatanisha na Mungu.  Hapo yalifanyika yafuatayo:-

 1. ALISULIBISHWA – Mikono ilitanuliwa mpaka mwisho wake na kupigwa misumari kwenye msalaba kila mmoja peke yake.  Miguu kwa pamoja nayo ilipigwa msumari ukaingia msalabani.  Yote yalifanyika msalaba ukiwa chini.  Kisha msalaba ulichukuliwa na kutupwa katika shimo kwa kishindo kama nguzo ya umeme.
 2. ALIPEWA DIVAI ILIYOCHANGANYIKA NA NYONGO (MST 34) – Watu waliokuwa wanasulibishwa, walipewa kinywaji hiki ili kuwapunguzia maumivu yao,  kwa kuharibu fahamu zao, kama dawa ya ganzi.  Yeye hakutaka kuinywa, alitaka maumivu yote (kikombe chote) ayapate kikamilifu kwa ajili yetu.
 3. WALIGAWANA MAVAZI YAKE  (MST 35) – Walitimiza andiko la ZABURI 22:18.  Mavazi, ni alama ya Utukufu.  Yesu aliugawa Utukufu wake kati yetu sisi tuliokuwa tumepungukiwa na utukufu wa Mungu na kuwa uchi.
 4. WALIWEKWA WALINZI KUMLINDA   (MST 36) – Walidhani atatoka msalabani!  Walinzi hawa walikuwa mashahidi wa nguvu za Yesu na wakakiri kuwa alikuwa Mwana wa Mungu (MST 54).
 5. WAKAWEKA MASHTAKA JUU YA KICHWA CHAKE (MST 37) – Kwa kawaida, kila aliyesulibishwa, ilibidi kuandika makosa yake kwenye ubao, na kuuweka juu ya kichwa chake, ili ifahamike amekosa nini mpaka akasulibiwa.  La kushangaza, Pilato aliandika “YESU MNAZARETI, MFALME WA WAYAHUDI”.  Wakiuu wa Makuhani wakamwambia asiandike hivyo, bali ya kwamba Yule aliyesema, Mimi ni Mfalme wa Wayahudi.  Pilato akajibu, NILIYOYAANDIKA, NIMEYAANDIKA (YOHANA 19:19-22).  Mungu wetu ana uwezo wa kumfanya mwanadamu yeyote hata aliye kinyume chetu, kutimiza mapenzi ya Mungu kwetu, kinyume kabisa na mapenzi yake.
 6. ALISULIBISHWA PAMOJA NA WANYANG’ANYI  (MST 38) – Alihesabiwa pamoja na hao wakosao, sawasawa na ISAYA 53:12.  Yeye alikuwa katikati yao kama Mkosaji Mkuu!  Ili sisi tusamehewe dhambi zetu.
 7. ALITUKANWA NA KUSHUTUMIWA   (MST 39-44) – Walitikisa vichwa vyao (MST 39).  Kutikisa kichwa ilikuwa ni dalili ya dharau, mshangao, na kuzomea (ISAYA 37:22; YEREMIA 18:16; MAOMBOLEZO 2:15) kwa kuona “kuanguka” kwake!  Alianguka ili sisi tupandishwe.  Walisema kama ni Mfalme wa Israeli ashuke msalabani, lakini hakushuka ili wamwamini.  Yesu hawezi kutenganishwa na msalaba au aibu na mateso.  Tukitaka kumwamini Yesu wa kutupa raha tu na utukufu, hayupo.  Msalaba ni lazima (2 TIMOTHEO 3:12; WAFILIPI 1:29).
 8. KULIKUWA NA GIZA JUU YA NCHI YOTE   (MST 45-50) – Jua lilipatwa kwa saa tatu nzima kuanzia saa 6-9 mchana.  Kulikuwa giza!  Yesu alipokuwa anazaliwa, nyota ya mashariki yenye mwanga mkali ilitokea (MATHAYO 2:9).  Msalabani, Yesu alikuwa anaondoka nchini.  Mtu pasipo Yesu, yaani mwenye dhambi, moyoni mwake ni GIZA ZITO.  Yesu ni nuru.  Dhambi ni Giza.  Alisema kwa lugha ya Ki-Shamu, “Eloi, Eloi, lama sabakthani”.  DHAMBI ZETU, zilimtenganisha Yesu na Mungu.  Maovu yanatugenganisha na Mungu (ISAYA 59:1-2).  Hawakuielewa lugha wakadhani anamwita Eliya!  Hatuwezi kuielewa lugha ya Yesu, mpaka tuokoke!!!  Walimnywesha siki iliyowekwa kwenye sifongo (sponji) eti atoe kiu kwa kinywaji kichungu!! (ZABURI 69:21)  Ole, kwa mwenye dhambi.

 

 

MWAMINI YESU ALIYESULIBISHWA, UTAOKOKA MARA  (MATENDO 16:31)

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s