LAWEZA NENO JEMA KUTOKA NAZARETI?

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA.

SOMO:    LAWEZA NENO JEMA KUTOKA NAZARETI?

       

 Leo, tunaendelea tena kujifunza Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu.  Siku ya leo, tutajifunza na kutafakari YOHANA 1:43-51.  Ingawa kichwa cha somo letu la leo ni “LAWEZA NENO JEMA KUTOKA NAZARETI?”, kuna mengi ya kujifunza katika mistari hii.  Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika mistari hii, katika vipengele sita:-

(1)NIFUATE (Mst. 43);

(2)CHAGUO LA MUNGU LA WATUMISHI WAKE (Mst. 44);

(3)WAJIBU WETU WA KUSHUHUDIA (Mst. 45);

(4)LAWEZA NENO JEMA KUTOKA NAZARETI? (Mst. 46);

(5)MWISRAELI KWELI KWELI (Mst. 47-49);

(6)UTAONA MAMBO MAKUBWA KULIKO HAYA (Mst. 50-51).

 

(1)      NIFUATE (Mst. 43)

Baada ya kazi nzito jana yake, Yesu Kristo siku ya pili yake, yaani siku inayofuata, aliendelea kufanya kazi na kuwaleta watu kwake.  Yesu Kristo alikuwa mchapakazi, hakupoteza muda wowote kwa ulegevu.  Watendakazi wa Mungu vivyo hivyo hawana budi kuwa wachapakazi.  Mtendakazi wa Mungu hawezi kupata mafanikio makubwa ikiwa atafanya kazi ya Mungu kwa ulegevu.  Inahitajika juhudi na bidii kubwa katika utumishi wa Mungu ili kufanya kazi alizozifanya Kristo (YOHANA 9:4; WARUMI 12:11; MHUBIRI 9:10; YEREMIA 48:10).  Kuna jambo jingine la kujifunza hapa.  Mwanzoni mwa huduma ya Yesu Kristo, Yesu alikuwa anapata mtu mmoja, wawili au watatu kwa siku, waliokuwa wanamwijia.  Hatupaswi kuvunjika moyo katika ushuhudiaji wetu mwanzoni, tunapoona tunaleta watu wachache kwa Yesu.  Hatupaswi kudharau siku ya mambo madogo (ZEKARIA 4:10).  Kwa wakati wake, mwanzo mdogo huleta mwisho mkubwa (AYUBU 8:5-7; ISAYA 60:22).  Jambo jingine la msingi tunalojifunza hapa, ni katika ushuhudiaji wa Yesu, anapotumia neno NIFUATE (Mst. 43; MARKO 2:14).  Yesu Kristo anataka tumfuate katika kila jambo kama tunataka tukae naye mbinguni milele.   Tumfuate katika usemi wake, matendo yake na mawazo yake.  Tufuate nyayo zake (1 PETRO 2:21).  Ni muhimu kujiuliza katika kila jambo kama kwa kulifanya tunamfuata Yesu.  Je, tukiwa tunakali nywele, kusuka rasta na kuvaa mapambo ya kidunia kama heleni, bangili au mikufu na kujichubua ngozi zetu kwa madawa; tunamfuata Yesu kweli?  Jibu ni la!  Mungu wetu ametuumba ili tumtukuze kwa namna ileile aliyotuumba bila nyongeza (ISAYA 43:7).  Je, tunapokuwa tunakwenda kutazama mipira ya ligi au kucheza mpira, karata, boxing, draft na michezo mingine ya kidunia kama disco n.k; tunamfuata Yesu?  Je, tunapokuwa watu tuliojaa mizaha, kusema uongo na masengenyo, wivu, fitina, uzushi, rushwa n.k; tunamfuata Yesu kwa kufanya hayo?  Mtume Paulo alimfuata Yesu (1 WAKORINTHO 11:1), na wote wapendao kwenda mbinguni watamfuata Yesu, na siyo kuwafuata waume, wazazi au ndugu wanaopinga wokovu.

 

(2)      CHAGUO LA MUNGU LA WATUMISHI WAKE (Mst. 44)

BETHSAIDA”, maana yake “NYUMBA YA UVUVI”.  Huu ulikuwa ni mji wa wavuvi.  Hapa ndipo palipokuwa nyumbani kwao Filipo, Andrea na Petro.  Yesu aliwafanya wavuvi hawa ambao hawakusoma kuwa MITUME.  Yakobo wa Zebedayo na Yohana nduguye waliokuwa wavuvi pia, hawa nao walichaguliwa kuwa Mitume (MATHAYO 4:21-22).  Hawa nao walikuwa watu wasiosoma (MATENDO 4:13).  Karibu nusu ya Mitume 12, walikuwa wavuvi!  Daudi, mtu aliyeupendeza moyo wa Mungu hata akachaguliwa kuwaongoza Waisraeli, alikuwa mdogo tu na mchungaji wa kondoo (MATENDO 13:22; 1 SAMWELI 16:11-13).  Nabii Amosi, yeye naye alikuwa mchungaji wa kondoo tu na mtunza mikuyu (AMOSI 7:14).  Machaguo ya Mungu ya watumishi wake, yako tofauti sana na machaguo ya kibinadamu.  Tukiwa waaminfu, hata kama hatukusoma shule za dunia au vyuo vya Biblia; Mungu anaweza kutufanya kuwa watumishi wake wakubwa.  Lengo la kuwachagua watu wa jinsi hii ni kwamba wasije kamwe wakaona kwamba walichaguliwa kwa sababu ya “ukuu” wao, na tena watu watakapowaona wakitumiwa na Mungu wamsifu Mungu na siyo watu wale (1WAKORINTHO 1:26-29; MATENDO 4:13).  Kwa misingi hii, hatupaswi kujidharau kutokana na jinsi ambavyo hatukusoma sana.  Bado tunaweza kuwafuatilia, kuwashauri na kuwaongoza wasomi waliotuzidi.  Si kwa uweza wala nguvu zetu bali kwa Roho wa Bwana wa Majeshi anayetutuma, tunaweza kuwa viongozi wa Makanisa ya Nyumbani au Zoni au Wachungaji, n.k. (ZEKARIA 4:6).

 

(3)      WAJIBU WETU WA KUSHUHUDIA (Mst. 45)

Mara tu baada ya Filipo kumfuata Yesu na kuokolewa, alianza kumshuhudia Nathanaeli.  Mungu anamtarajia kila mtu aliyeokolewa kuanza kuwashuhudia watu wengine habari za wokovu.  MARA TU BAADA YA KUOKOLEWA.  Mwanamke Msamaria, yeye anaye alifanya hivyo (YOHANA 4:28-30).  Kama tulivyopokea katika Neno la Mungu mpaka na sisi tukaokolewa, vivyo hivyo, tunapaswa kutoa neneo hilo kwa wengine.  Ni heri au baraka kutoa kuliko kupokea.  Ikiwa tunapokea Neno tu siku ya Jumanne, Jumatano, Ijumaa, Jumamosi, Jumapili, lakini hatulitoi neno hilo kwa wengine; tunajikoseshas baraka nyingi (MATENDO 20:35).

 

(4)      LAWEZA NENO JEMA KUTOKA NAZARETI? (Mst. 46)

Ingawa Yesu alizaliwa Bethlehemu, hata hivyo, Nazareti ndipo mahali alipolelewa (MATHAYO 2:19-23; LUKA 4:16).  Kwa sababu alikulia Nazareti, aliitwa Mnazareti, na yeye pia alijiita hivyo (LUKA 24:18-19; MATENDO 2:22; 3:6; 4:10; 10:38; 26:9; MARKO 16:6).  Mji wa Nazareti, hautajwi katika Agano la Kale.  Vilevile, kwa ujinga wao Waisraeli waliona nabii hawezi kutoka Nazareti katika jimbo la Galilaya.  Vilevile, watu waliotoka Galilaya walidharauliwa.  Mtu akiambiwa “Wewe ni Mgalilaya au Mnazareti“,, ilikuwa ni Neno la dharau (YOHANA 7:41-42, 52; ISAYA 53:3).  Hata hivyo kama wangetafuta na kuona, wangeona kwamba Manabii Yona, Hosea, Eliya, Elisha na wengineo kadha walitokea jimbo hili; na vivile Yesu alizaliwa Bethlehemu ndipo akaendda kukulia Nazareti.  Siyo hilo tu, mji wa Nazareti ulijaa wingi wa watu ambao hawakumwamini Yesu (MATHAYO 13:54, 58).  Mahali hapa, tunajifunza jambo moja.  Mungu hafungwi na mpaka wowote.  Mahali palipodharauliwa na wanadamu, ndipo Mungu anapojiinulia nabii, wanadamu watake wasitake.  Neno jema linaweza kutoka popote, siyo lazima mahali fulani.  Paulo Mtume, alikuwa mwuaji na mtu mbaya, lakini ndiye aliyechaguliwa na Mungu kufanya kazi kuliko mitume waliokuwa pamoja na Yesu (1 TIMOTHEO 1:12-16; MATENDO 7:59-60; 1 WAKORINTHO 15:10).  Kahaba Rahabu anatajwa pamoja na Nuhu, Ibrahimu, Sara, Musa na mashujaa wengine wa imani katika WAEBRANIA SURA YA 11 (Mst. 31).  Wanafunzi wa Yesu katika Kanisa la Kwanza la Mitume Yerusalemu, hawakusadiki kuitwa na kuokolewa kwa Sauli, bali wote walimwogopa (MATENDO 9:26).  Hata hivyo, bado lilizidi kuwa nidyo chaguo la Mungu.  Hatupaswi kudhani Mtumishi wa Mungu lazima awe na historia nzuri na kutoka mahali pazuri!  Kahaba mkubwa, ndiye anayeweza kuwa chaguo la Mungu.  Vile vile hatupaswi kuwa na kasumba ya ukoloni wa kiroho kwamba kila lililo jema lazima litoke Marekani!  Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship limetokea hapahapa Tanzania.  Limetokea Nazareti, na makusudi ya Mungu kulianzisha, yatazidi kudhihirika siku hadi siku.  Tukiwa waaminifu, Wamarekani watakuja kujifunza Tanzania!

 

 (5)     MWISRAELI KWELI KWELI (Mst. 47-49)

Nathanieli alikuwa Mwisraeli kwelikweli kwa jinsi alivyokuwa anatumia muda wake kumtafuta Mungu chini ya mtini na siyo kama Mafarisayo waliokuwa wanapiga panda njiani (MATHAYO 6:2).  Siyo wote walio wa uzao wa Israeli wanaokuwa Waisraeli kweli kweli (WARUMI 9:6; UFUNUO 3:9).  Siyo wote wanaosema kwa mdomo wameokoka, kweli wameokoka.  Kuwa mshirika wa Kanisa la Full Gospel, hakumfanyi mtu awe ameokoka.  Wokovu wetu lazima ujulikane sirini.  Hata tukiwa mafichoni, chini ya mtini, Yesu anatuona (MHUBIRI 12:14).  Je, ni Wakristo kwelikweli au wakristo wa jina?  Tunajifunza jambo jingine.  Pamoja na utuwema wa Nathanaeli, bado ilimbidi kumkiri Yesu ili aokoke (Mst. 49; ISAYA 64:6; WARUMI 3:20-24, 28).

 

(6)      UTAONA MAMBO MAKUBWA KULIKO HAYA (Mst. 50-51)

Yote tuliyoyaona mpaka sasa, hatujaona lolote bado.  Yesu anahitaji kutuonyesha mambo makubwa zaidi, magumu tusiyoyajua (YEREMIA 33:3).  La kufanya tuwe waaminfiu na tusiridhike na hatua yoyote tuliyoifikia.  Tumeokoka, atatuonyesha Utakaso, tumetakaswa atatuonyesha Uwezo utokao juu, tumepata uwezo atatuonyesha mafunuo makubwa zaidi!  Tuyatendee kazi tu tuliyo nayo!  Nathanieli aliona miujiza mingi mno baada ya hapo, na bado!

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

           Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s