MADHARA YA KUFANYA MAMBO YA KUKOSESHA

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

SOMO:    MADHARA YA KUFANYA MAMBO YA KUKOSESHA

Leo, tunajifunza Biblia kutoka katika MATHAYO 18:5-14.  Ingawa kichwa cha somo letu la leo ni “MADHARA YA KUFANYA MAMBO YA KUKOSESHA“, kuna mengi zaidi ya kujifunza katika mistari hii.  Tutaligawa somo letu la leo katika vipengele vitano:-

(1)  BARAKA ZA KUMPOKEA MTOTO KWA JINA LA YESU (Mst. 5);

(2)  MADHARA YA KUFANYA MAMBO YA KUKOSESHA (Mst. 6-7);

(3)  KUEPUKA KUKOSESHWA NA VIUNGO VYA MWILI (Mst. 8-9);

(4)  ONYO LA KUTOWADHARAU WATOTO WADOGO KIROHO (Mst. 10);

(5)    JINSI ISIVYOMPENDEZA MUNGU KUONA WATOTO WACHANGA KIROHO    WANAPOTEA (Mst. 11-14).

 

(1)      BARAKA ZA KUMPOKEA MTOTO KWA JINA LA YESU (Mst. 5)

“Mtoto“ anayetajwa katika msitari huu ni “Mtoto wa Mungu“ (YOHANA 1:12).  Mtu akipewa

UWEZO wa kufanyika mtoto wa Mungu, anabadilishwa kabisa maisha yake.  Uwezo huo

anaopewa, unamuwezesha mtu kuyasikia maneno ya Mungu, kuyashika na kuyafuata mara

moja bila shida yoyote.  Amri za Mungu kwake siyo nzito!  Uwezo huo pia unamfanya mtu awe

rahisi kuongozwa.  Anayoambiwa na viongozi wake wanaoihubiri kweli ya Neno la Mungu,

anayasikia na kuyafuata mara moja bila ukaidi.  Vilevile mtoto wa Mungu amepewa uwezo wa

kuvishinda vishawishi na anasa za ulimwengu.  Kama mtu hana sifa hizi, huyo siyo mtoto wa

Mungu (YOHANA 8:47; 1 YOHANA 2:4-5; YOHANA 8:54-55; 1 YOHANA 5:3-4; 1 YOHANA 4:6).

Kuna baraka tele katika kumpokea mtoto wa jinsi hii kwa jina la Yesu.  Kumpokea mtoto wa

Mungu kwa jina la Yesu, maana yake kumfanyia mtu tendo lolote jema kwa sababu tu ni mtoto

wa Mungu, siyo kwa sababu ni ndugu wa kimwili, mtu wa kabila lako, mtu uliyesoma naye n.k.

Tukifanya hivyo, tunakuwa tumemfanyia hayo Yesu mwenyewe.  Tukimpa mtoto wa Mungu nauli

ya kuja kanisani, msaada wowote wa kifedha kwa ajili ya mahitaji yake, tukimtafutia kazi ya

kuajiriwa, tukimpa mavazi, tukimpa chochote cha kumfanya aendelee na wokovu kwa furaha,

kwa kufanya hivyo, tunakuwa tumempokea Yesu.  Tunapaswa kuwa mawakili wema wa neema

yoyote tuliyopewa ya ziada kuliko watoto wengine wa Mungu.  Ikiwa sisi tuna nafasi ya kutoa

ajira, tufanye hivyo kwa watoto wa Mungu kwanza, ili tupate baraka tele (1 PETRO 4:10;

WAGALATIA 6:10).

(2)      MADHARA YA KUFANYA MAMBO YA KUKOSESHA (Mst. 6-7)

Mambo ya kukosesha ni sawa kuonekana kwa watu wa ulimwengu wenye dhambi, ambao hawajui wayatendayo, lakini hayapaswi kuonekana kwa mtoto wa Mungu.  Nyakati za Biblia, katika mataifa ya Ashuru, Misri, na Uyunani, mtu aliyetenda kosa kubwa, alifungiwa shingoni jiwe kubwa la kusagia, lenye upana uliopata 1½ na unene wa inchi 3; na kutoswa katika kilindi cha bahari na kufa bila jinsi ya kusalimika.  Hapa Yesu anatufundisha kwamba ni heri kupata adhabu hiyo na kufa kuliko kutupwa katika ziwa la moto, ambako hakuna kufa bali ni maumivu makali milele.  Kutupwa katika ziwa la moto kutampata yeyote mwenye kufanya mambo ya kukosesha kwa namna mbili zifuatazo:-

1.         KUWAKOSESHA WATOTO WA MUNGU – Tunaweza kuwakosesha watoto wa Mungu kwa kufanya yafuatayo:-

(a)      KUVAA MAVAZI YA KUKOSESHA:   Ni wajibu wa wanawake ambao ni watoto wa  Mungu, kuwalinda wanaume waliookolewa (YEREMIA 31:22). Mavazi yoyote ya mwanamke yatakayomfanya mwanamume aumbiwe mawazo machafu ya kumtamani mwanamke kwa uasherati au uzinzi, ni mavazi ya kumkosesha, siyo mavazi ya kumlinda.   Mavazi yoyote yanayoacha makwapa wazi, kifua, tumbo au mgongo wazi ni mavazi ya kukosesha.  Mavazi yanayoonyesha ndani, mavazi yenye matundu, mavazi yanayobana na kuonyesha umbo la mwili, mavazi mafupi yanayoonyesha mapaja ni mavazi ya kukosesha.  Kuchana gauni nyuma au mbele ili kuonyesha “underskirt“, ni kuvaa mavazi yasiyomlinda mwanamume.  Kuvaa kanga zilizofungiwa kifuani na kuacha kifua na magongo wazi mbele ya watu ni kuvaa mavazi ya kukosesha.  Gauni au sketi za wanawake hazina budi kuwa ndefu kiasi cha kufunika magoti mwanamke anapokuwa ameketi.  Vivyo hivyo, wanaume hawapaswi kuvaa hadharani taulo na kuacha tumbo na mgongo wazi, au kuvaa hadharani bukta na kaptula zinazoacha wazi mapaja ya mwanamume aliye mtu mzima.  Yote haya ni mavazi ya kukosesha.

(b)      KUFANYA TENDO LOLOTE LITAKALOMFANYA MTOTO MCHANGA WA KIROHO KUKATA TAMAA YA KUENDELEA NA WOKOVU:  Watoto wachanga kiroho huwaangalia sana wale waliowakuta katika wokovu.  Mtu yeyote aliye na muda katika wokovu anapofanya tendo lolote la uasi wa maneno ya Mungu mbele ya watoto wachanga kiroho, kufanya hivyo ni kuwakosesha watoto ambao Yesu alikufa kwa ajili yao.  Watoto wachanga husema “Ikiwa huyu amefanya hivi, basi na mimi nikifanya siyo vibaya“ au “Kama huyu naye ameshindwa wokovu, basi mimi pia siwezi“, na hivyo kukoseshwa (1 WAKORINTHO 8:10-12; 1 WATHESALONIKE  1:7).  Kiongozi yeyote katika Kanisa kwa kusema na kutenda kwake anaweza kuwavuta wengi kumfuata na hivyo kuwakosesha (2 WAFALME 17:21).

(2)      KUWAKOSESHA MATAIFA – Jambo lolote lile katika kusema na kutenda litakalofanya mataifa waseme, “Huyu anasema ameokoka mbona anafanya hivi .  Waongo hawa, hakuna wokovu duniani“, jambo hilo ni la kuwakosesha mataifa wasiokolewe.  Kufanya hivyo ni kuwafungia watu ufalme wa mbinguni ambao wewe hutauingia, wala wanaoingia huwaachi waingie (MATHAYO 23:13; LUKA 11:52).

(3)      KUEPUKA KUKOSESHWA NA VIUNGO VYA MWILI (Mst. 8-9)

Miguu, Mikono na Macho ni viungo vya muhimu sana mwilini.  Viungo hivi vizuri, hufanya kazi kwa kusaidiana, huwa viwili viwili.  Mguu, mkono, au jicho likiwa moja huwa na upungufu katika utendaji wa kazi iliyokusudiwa.  Kuna vitu, watu, mambo fulani au kazi njema na nzuri ambavyo vinaonyesha kutusaidia au kutupa furaha fulani lakini hatimaye vitatufanya tutupwe Jehanum.  Hatupaswi kuangalia uzuri wa vitu hivyo au msaada wake kwetu bali kuwa tasyari kuviacha ili visifanye tukatupwa Jehanum.  Baada ya kuokoka, hatuwezi kufanya kazi YOYOTE kiwanda cha Bia, Konyagi, Sigara, Chibuku n.k., au kuuza dukani kwetu sigara, pombe, kanga zenye maandishi ya kihuni, mapambo yoyote – bangili, heleni, mikufu, dawa za kukali nywele n.k., hata kama sisi hatuvai vitu hivyo, au kuvinywa au kuvivuta.  Kufanya hivyo ni kumpa jirani yetu sumu, ni sawa na kuvitumia (HABAKUKI 2:15-16).  Kwa misingi hiyo hiyo, hatuawezi kufanya kazi katika Radio ambayo imejaa muziki wa dansi tangu asubuhi hadi usiku au kulima tumbaku katika mashamba yetu au kulima ndizi zilizo maalum tu kwa kutengeneza pombe.  Vitu hivi au kazi hizi zinaweza kuonekana zinatupa msaada mkubwa lakini ni heri kuving’oa na kuwa chongo au kupungukiwa na kuwa na shida na kuingia uzimani.  Kazi yoyote au biashara inayotuzuia kujifunza Neno la Mungu na kumtumikia Mungu, ni vema kuiangalia kwa makini.  Televisheni au Video inayotuzuia kuomba, kusoma Neno au kutenda kazi ya Mungu ni lazima tuiangalie kwa makini hata kama tunaangalia mambo mema.  Radio kaseti ambayo inatufanya tusikilize kwaya tu na kutuzuia kuomba, kusoma Neno au kutenda kazi ya Mungu ni lazima tuiangalie kwa makini.  Mume ambaye siye wa kwetu (YOHANA 4:18), mke wetu ambaye siye wa kwanza kwetu bali ni wa pili, wa tatu n.k.  wote hawa wanaweza kuonekana wanatupa msaada, lakini ni heri tuwang’oe na kuingia mbinguni tukiwa “tumepungukiwa“ na msaada huo.

(4)      ONYO LA KUTOWADHARAU WATOTO WADOGO KIROHO (Mst. 10)

Watoto wadogo wa kimwili huwa kila mmoja ana malaika anayemwangalia.  Ndiyo maana wanaweza kuanguka chini lakini wasiumie kama unavyokuwa umefikiria n.k.  Vile vile, kila mtu aliyeokolewa huwa anahudumiwa na malaika katika kuletewa majibu ya maombi kama ilivyokuwa kwa Danieli n.k.  Kila mtoto wa Mungu, ni wa thamani sana mbele za Mungu (WAEBRANIA 1:13-14; DANIELI 10:4-6, 11-12).  Haitupasi kamwe kuwadharau watoto wachanga kiroho kwa sababu bado hawajaweza kusoma Biblia kama sisi, kuomba au kufanya kazi ya Mungu kama sisi.  Ni wajibu wetu kuwatia moyo katika yoyote madogo wanayoyafanya.  Tendo lolote au maneno yoyote ya kuwavunja moyo au kuwakatishas tamaa ni kumhuzunisha mno Yesu aliyekufa kwa ajili yao.  Kwa mfano ukiwaambia, „“Umeokoka, vizuri, funga mkanda, wokovu siyo lelemama“.  Kusema hivi siyo kuwatia moyo.  Lolote lile katika kusema kwetu au kutenda kwetu lazima liwe na lengo la kuwatia moyo na kuwajenga watoto wachanga kiroho (WARUMI 14:19; 1 WAKORINTHO 14:3; MATENDO YA MITUME 13:43).

(5)      JINSI ISIVYOMPENDEZA MUNGU KUONA WATOTO WACHANGA KIROHO WANAPOTEA (Mst. 11-14)

Mungu hafurahii kuona watu wanaokoka halafu tunawaacha tu hivyo hivyo mpaka wanarudi nyuma na kupotea.  Kabla ya kufanya mikutano yoyote ya Injili ni muhimu kufahamu na kupanga mikakati ya kuhakikisha matunda yanayopatikana yanakaa au kudumu, tusipofanya hivyo tutasababisha maombi yetu kuwa na uwezo dhaifu (YOHANA 15:16).  Tukipata mtu yeyote aliyekata shauri kuokoka, inatupasa kumfuatilia kwa gharma yoyote na kumlinda asipotee, au sivyo roho yetu itakuwa mahali pa roho yake (1 WAFALME 20:39-40).

MTU AKIWA NA SIKIO NA ASIKIE (UFUNUO 13:9)

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s