MAJI YALIYO HAI

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

 

SOMO:    MAJI YALIYO HAI

 

B

ado tunaendelea kujifunza Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu.  Leo, tunajifunza YOHANA 4:1-26.  Katika mistari hii, ingawa kichwa cha somo letu ni “MAJI YALIYO HAI“.  Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika mistari hii, katika vipengele vinane:-

(1)KUFANYA WANAFUNZI WENGI KULIKO YOHANA (Mst. 1-3);

(2)HATUNA BUDI KUPITA KATIKATI YA SAMARIA (Mst. 4-5);

(3)MWANADAMU KRISTO YETU (Mst. 6);

(4)JINSI YA KUSHUHUDIA (Mst. 7-10);

(5)MAJI YALIYO HAI (Mst. 10-15);

(6)ULIYE NAYE SASA SIYE MUME WAKO (Mst. 16-19);

(7)KUMWABUDU MUNGU KATIKA ROHO NA KWELI (Mst. 20-24);

(8)NINAYESEMA NAWE NDIYE (Mst. 25-26).

 

(1)      KUFANYA WANAFUNZI WENGI KULIKO YOHANA (Mst. 1-3)

Ni muhimu kufuata mfano wa Bwana wetu Yesu Kristo maali hapa.  Tumeagizwa kuwafanya mataifa kuwa WANAFUNZI wa Yesu, siyo kuwaanya wakate shauri tu kuokolewa halafu tukawaacha warudi tena dhambini (MATHAYO 28:19-20).  Baada ya mtu kukata shauri kuokolewa, ni wajibu wetu kuhakikisha anakuwa mwanafunzi wa Yesu, na pia anabatizwa katika maji tele.  Mwanafunzi wa Yesu, ni tofauti sana na mtu aliyekata shauri tu kuokoka.  Mwanafunzi wa Yesu ni mtu aliyekata shauri kuokoka, ambaye tabia ya Yesu na utumishi wake, unaanza kudhihirika waziwazi ndani yake kwa namna mbalimbali (LUKA 14:26, 27, 33; YOHANA 8:31; 15:8).  Mtu aliyekata shauri kuokoka, hawezi kuwa mwanafunzi wa Yesu ila kudumu katika mafundisho ya mitume baada ya kuokoka, hawezi kuwa mwanafunzi wa Yesu bila kudumu katika mafundisho ya mitume baada ya kuokoka (MATENDO 2:41-42).  Kama mtoto mchanga aliyezaliwa anayokuwa katika hatari ya kufa asipopewa maziwa, vivyo hivyo, mtu aliyekata shauri kuokoka, hawezi kuukulia awokovu bila kulishwa neno la Mungu (1 PETRO 2:2).  Kwa misingi hii, haimpendezi Mungu kufanya CRUSADE au mikutano ya Injili, bila kuwa na mzigo wa kuktosha wa kuhakikisha wanaokata shauri wanafuatiliwa na kuletwa katika Kanisa linalofundisha kweli ili waukulie wokovu.  Kuwaambia wabaki katika madhehebu yao yaliyokufa yanayowafundisha watu kuabudu sanamu, ni sawa na kumpa mama aliyekufa, mtoto wa kunyonyesha.  Mtoto huyo naye atakufa.  Tukifanya wanafunzi wengi kuliko watu waliotutangulia, ni muhimu kufahamu kwamba Mafarisayo watatuchukia na kutupiga vita kama walivyofanya kwa Yesu (YOHANA 15:18-20).  HII SIYO AJABU!

 

(2)      HATUNA BUDI KUPITA KATIKATI YA SAMARIA (Mst. 4-5)

Samaria, ilikuwa ni taifa lililokuwa limejaa maasi (MATENDO 8:9-11).  Yesu Kristo ALILAZIMIKA kupita katikati ya nchi hii yenye uasi mwingi alipokuwa anakwenda Galilaya.  Baada ya kuokoka, tutalazimika wakti mwingine kupita katika ya SAMARIA kama Yesu maana hakuja kututoa ulimwenguni (YOHANA 17:15-16).  Jirani aliye mataifa anaweza akawa anafungulia redio yake kwa sauti na redio hiyo ikawa inapiga muziki wa dansi na masikio yetu yakalazimika kusikia muziki huo.  Hatuna budi kupita katikati ya Samaria na hali hiyo ilimpata Yesu, siyo dhambi, maana haikutokana na sisi.  Kwa misingi hiyohiyo, tunaweza tukapanda basi la abiria lenye kaseti za muziki wa dansi au video za dunia, tukawa tumelazimika kupita katika ya Samaria.  Ni wajibu wetu kufanya lile linalowezekana kwetu.  Kama ni video, macho yetu muda mwingi tutayatoa kwenye video hiyo.

(3)      MWANADAMU KRISTO YETU (Mst. 6)

Yesu Kristo ni MUNGU (TITO 2:13, 1 YOHANA 5:20).  Hata hivyo alipokuwa duniani, alikuwa mwanadamu pia (1 TIMOTHEO 2:5).  Alikuwa Imanueli.  Yaani Mungu pamoja nasi wanadamu.  Katika hali ya ubinadamu, ndipo alipochoka baada ya safari (Mst. 6), alipolala usingizi (LUKA 8:22-23), alipoona njaa (LUKA 4:2), alipokula chakula cha mwanadamu (LUKA 24:41-43), alipozaliwa na mwanamke (LUKA 2:6-7), alipoongezeka kimo na kuwa mtoto, kijana na mtu mzima (LUKA 2:40, 42, 52).

(4)      JINSI YA KUSHUHUDIA (Mst. 7-10)

Hapa tunajifunza Uinjilisti kwa Yesu.  Lolote analolizungumzia yule tunayetaka kumshuhudia, tunaanzia na hilohilo.  Maneno “Imekuwaje kutaka maji kwangu“ yalichokoza Injili.  Vivyo hivyo karibu kila neno lafaa kwa kuanzia kushuhudia.  Mtu akisema “Jua kali sna“, tunaanza kusema “Moto wa Jehanum ni mkali zaidi, n.k.“.  Vivyo hivyo Wayahudi walikuwa hawachangamani na Wasamaria kama jinsi Waislamu wanavyoita Wakristo “makafiri“.  Hapa tunajifunza  jinsi ya kuwashuhudia Waislamu na watu dini nyingine zilizo tofauti na Ukristo.  Yesu alipoulizwa swali, “Imekuwaje wewe Myahudi kutaka maji kwangu, nami ni mwanamke Msamaria?“.  Swali hili hakulijibu, alijifanya kama hakulisikia.  Sisi nasi inatupasa kukwepa maswali yoyote yatakayoleta ubishi (TITO 3:9; 2 TIMOTHEO 2:23), kama yanayohusu Utatu wa Mungu n.k; na kusisitiza mtu ampokee kwanza Yesu na kupata ushindi juu ya dhambi na hayo mengine atayafahamu baadaye.  Mtoto wa Shule huanza na darasa la kwanza, siyo la saba!

(5)      MAJI YALIYO HAI (Mst. 10-15)

Maji ya kawaida ya dunia hii hayamalizi kiu.  Ukinywa sasa, baadaye tena kiu inaendelea kuwapo.  Njia zozote za kidunia, haziwezi kutufanya tuishiwe hamu ya kuvuta sigara, kunywa pombe, kuvuta bangi na kula madawa ya kulevya, kufanya uasherati na uzinzi n.k.  Kiu ya dhambi inaondolewa kwa kunywa MAJI YALIYO HAI aliyo nayo Yesu.  Yeyote ambaye hapendi kabisa dhambi na anataka kuziacha kabisa na kuishi maisha yanayompendeza Mungu akimwomba Yesu kwa IMANI ampe maji hayo yaliyo hai; kiu ya dhambi itahama kabisa na atapata uzima wa milele.

(6)      ULIYE NAYE SASA SIYE MUME WAKO (Mst. 16-19)

Baada ya kuokoka, ni muhimu kila mmoja kucheki vizuri kama mume au mke aliye naye ni mwenzi halali mbele za Mungu.  Ukiwa na mume au mke asiye wako, unafanya uzinzi maisha yako yote (LUKA 16:18) na wazinzi hawataurithi ufalme wa mbinguni (1 WAKORINTHO 6:9; UFUNUO 2:8).  Hakuna kuachana na mume wa kwanza au mke wa kwanza kunakoruhusiwa katika Ukristo.  Ni kifo tu cha mwenzi wako wa ujana wako kinachokupa kibali cha kuoa au kuolewa tena.  Kama mmeachana, unapaswa kukaa bila kuolewa au kuoa tena, au kurudiana (MALAKI 2:14-16; WARUMI 7:2-3; 1 WAKORINTHO 7:10-11).  Siyo suala la kufunga ndoa kanisani!  Yule uliyempata wa kwanza katika ujana wako na ruhusa ya wazazi wa msichana ikatolewa, kama hajafa; ndiye mume au mke wako (1 WAKORINTHO 7:36; MATHAYO 19:4-8).

(7)      KUMWABUDU MUNGU KATIKA ROHO NA KWELI (Mst. 20-24)

Watu watakaoingia mbinguni, ni wale wanaomwabudu katika ROHO na KWELI.  Kumwabudu Mungu kwa kutumia sanamu au rozari au kufukiza uvumba au udi au lolote la jinsi hii siyo kumwabudu katika Roho.  Ni kumwabudu katika MWILI.  Ibada ya sanamu, ni tendo la mwili (WAGALATIA 5:19-21; ISAYA 31:7; 1 WAKORINTHO 10:14).  Kumwabudu Mungu katika KWELI ni kuhakikisha mahali tunapoabudu, mafundisho yake yanaendana na NENO LA MUNGU.  Neno la Mungu ndiyo kweli (YOHANA 17:17).  Tukikaa na kuabudu mahali tunapoongozwa na maneno ya wanadamu yaliyotungwa, na kushika tu mapokeo ya wazee wetu, IBADA HIZO NI BURE!!, hazitatufikisha mbinguni (MARKO 7:7-9; 2 PETRO 2:1-3).

(8)      NINAYESEMA NAWE NDIYE (Mst. 25-26)

Mwanamke Msamaria alisema “atakapokuja Kristo ATATUFUNULIA MAMBO YOTE”.  Wako watu wengine katika Kanisa walio kama mwanamke huyu.  Watasikia neno la Mungu linawafundisha, lakini wao watasema wanangoja KUFUNULIWA kwa maono, ndoto au kupata mafunuo mengine.  Hakuna mafunuo mengine ya kungojea.  Unaposikia Neno la Mungu, anayesema nawe katika Neno ndiye Kristo.  Lifuate neno lake ili uisafishe njia yako ya kwenda mbinguni (ZABURI 119:9).

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s