MAMBO YA MTU NA MKEWE

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

SOMO:      MAMBO YA MTU NA MKEWE

Leo tunajifunza Biblia kutoka katika MATHAYO 19:1-15.  Ingawa kichwa cha somo letu la leo ni “MAMBO YA MTU NA MKEWE“, kuna mengi ya zaidi tunayofundishwa na Bwana wetu Yesu Kristo katika mistari hii.    Tutagawa mafundisho yetu ya leo katika vipengele vitatu:-

(1)  SIRI YA KUPONYWA NA YESU (Mst. 1-2);

(2)  MAMBO YA MTU NA MKEWE (Mst. 3-12);

(3)  KUBARIKI WATOTO WADOGO (Mst. 13-15).

 

(1)      SIRI YA KUPONYWA NA YESU (Mst. 1-2)

“Makutano mengi (watu wengi) WAKAMFUATA, akawaponya huko”.  Kumfuata Yesu ndiyo siri ya kuponywa na Yesu kwa muujiza.  Tukija kwa Yesu tukiwa na lengo la KUPONYWA tu, lakini hatutaki kuokoka; hatuwezi kuponywa.  Inatubidi tuje kwa Yesu tukiwa na lengo la KUMFUATA, na hiyo ndiyo siri ya kuponywa magonjwa yetu yote.  Kumfuata Yesu maana yake kutii na kulifuata NENO lake (ZABURI 119:9).  Tukiwa bado tunapenda kuendelea kutenda dhambi, ni vigumu kupokea muujiza wa uponyaji, na hata tukipata muujiza huo, ni vigumu muujiza huo kudumu.  Dhambi inaweza kusababisha kupotea kwa muujiza wa uponyaji na kukaribisha yaliyo mabaya zaidi kuliko ya mwanzo.  Ni muhimu kufahamu kwamba magonjwa mengine hayaponyeki kutokana na dhambi (YEREMIA 30:15; YOHANA 5:14; LUKA 11:24-26).  Hatupaswi kamwe kubabaishwa na vitisho vya Shetani vya kutuzuia kumfuata Yesu.  Mambo yote ya uganga, iwe ni hirizi au kinga za aina yoyote na chochote tulichokipata katika ushirikina, ni lazima tuvichome moto (MATENDO 19:18-19).  Tukimfuata Yesu, YEYE ndiye atakayekuwa kinga yetu, maana mkuu wa ulimwengu Shetani, hana kitu kwa Yesu (YOHANA 14:30).

(2)      MAMBO YA MTU NA MKEWE (Mst. 3-12)

Katika mistari hii tunajifunza mambo SABA ya mtu na mkewe:-

  1. MUME MMOJA MKE MMOJA HADI KIFO (Mst. 4) – Tangu mwanzo Mungu alimwumba mume mmoja na mke mmoja, Adamu na Hawa.  Kama mume alihitajika kuwa na mke zaidi ya mmoja, Mungu angewaumba wake wawili, watatu au wanne kwa ajili ya mume mmoja Adamu, lakini haikuwa hivyo.  Yote yanayohusiana na kuoa mke zaidi ya mmoja yaliyofanyika baada ya wakati huo, yalikuwa ni uasi.  Wote wenye mke zaidi ya mmoja waliangamizwa kwa Gharika wakati wa Nuhu.  Walioingia katika Safina, ni waume WANNE na wake WANNE tu; kila mume na mke wake mmoja tu (MWANZO 7:13).  Yesu alikuja kuturudisha katika mpango wa mwanzo wa Mungu.  Kama ilivyokuwa katika siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa wakati wa kuja kwake Yesu; watu wote wenye mke au mume zaidi ya mmoja wataachwa na kubaki katika dhiki kubwa na hatimaye kuangamizwa motoni (MATHAYO 24:37).  Hakuna ruhusa katika Agano Jipya kwa mtu kumwoa mke mwingine, wakati mke wake wa kwanza bado anaishi, vilevile hakuna ruhusa kwa mwanamke kuolewa na mume mwingine, wakati yule wa kwanza bado anaishi.  Ni kifo tu cha mmojawapo kinachoweza kumfanya aliyebaki kuoa au kuolewa tena (WARUMI 7:2-3; 1 WAKORINTHO 7:39).
  2. KUWAACHA WAZAZI NA KUAMBATANA (Mst. 5) – Ndoa inahesabika pale ambapo mtu ambaye hajaoa amepata ruhusa ya wazazi wa msichana ambaye hajaolewa.  Wanapowaacha wazazi na kuambatana, wamekuwa mtu na mkewe (1 WAKORINTHO 7:36).  Vivyo hivyo hapa tunajifunza pia kwamba tunapooana, ni lazima tuwaache wazazi.  Mume hapaswi kumwoa mke na kumleta nyumbani kwa wazazi wake na kuishi naye hapo.  Kabla ya kuwaza kuoa, mume inambidi kutafuta chumba au nyumba mbali na wazazi wake, na kumwandalia makao mkewe, kama vile Bwana Arusi Yesu  alivyokwenda kutuandalia makao sisi bibi arusi wake (YOHANA 14:3).  Kuambatana pia kunatufundisha kwamba mume au mke hapaswi kukubali maneno yoyote ya ndugu zake au wazazi yamtenganishe na mwenzi wake.  Ni lazima kila mmoja aambatane na mwenzake na kuwa upande wake wakati wote na siyo upande wa wazazi au ndugu tena.  Msimamo wao, lazima uwe mmoja.  Kuambatana ni kama kutiwa gundi kwa vitu viwili na vikashikana wakati wote.  Mume hana budi kushikamana na mke katika shida, furaha, magonjwa, kufanikiwa, kutofanikiwa n.k.

 

  1. HATA WAMEKUWA SI WAWILI TENA (Mst. 6) – Mume na mke ni mwili mmoja.  Siyo wawili tena.  Haiwapasi kabisa kufichana masuala ya fedha, madeni n.k.  Vyote vya mume ni vya mke.  Mapato ya mume yanapaswa kufahamika kwa mke na wote kupanga kwa pamoja.  Baada ya kuoana hakuna tena mmoja kusema “HILI NI GARI LANGU’, “HII NI NYUMBA YANGU” n.k., kila kitu ni cha WOTE.  Mume mlevi ni lazima atambue haki ya mkewe kuchukua fedha anayoiita “ya kwake” na kuilisha familia badala ya kuangalia mambo yake mwenyewe tu.  Hata hivyo katika masuala ya imani, kila mmoja anapaswa kujua kwamba kila mtu atalichukua furushi lake na kutoa hesabu yake mwenyewe (WAGALATIA 6:5; WARUMI 14:12).
  2. TALAKA KATIKA UKRISTO (Mst. 6-8) – Hakuna talaka katika ukristo.  Mwanadamu YEYOTE iwe ni Mchungaji, Askofu, Jaji wa Mahakama Kuu ya Rufaa au yoyote hana ruhusa kumtenganisha mtu na mkewe, na cheti chochote cha talaka ni batili, hakitambuliwi na Mungu.  Mungu alichukuliana na watu wa Agano la Kale kwa ugumu wa mioyo yao, lakini hachukuliani na yeyote katika Agano Jipya kwa suala la talaka.  Hata kama mke ameachwa kwa talaka potea, hana ruhusa kuolewa na mwingine (1 WAKORINTHO 7:10-11).
  3. KUMWACHA MKE KWA SABABU YA UASHERATI (Mst. 9) – Hiki ni kisingizio cha watu wengi wasio na maarifa kuwaacha wake zao.  Nyakati za Biblia mtu alipotoa posa kwa mchumba wake, hata kabla hawajaoana, waliitwa mtu na mkewe (KUMBUKUMBU  22:23-24; MATHAYO 1:18-20).  Katika uchumba, kama mke huyo alithibitishwa kuwa amefanya uasherati kwa kuwa na mimba au vinginevyo ilikuwa ni halali kumwacha maana ni dhahiri kwamba siyo mwaminifu.  Ni kwa sababu hiyo Yusufu alitaka kumwacha Mariamu kwa kudhani alifanya uasherati.  Vivyo hivyo, katika Kanisa, watu ambao bado ni wachumba, hata kama posa imekwisha kutolewa; mmojawapo anapothibitika kuwa amefanya uasherati, huyo mwenzake ana ruhusa ya kumwacha kwa sababu inadhihirisha kwamba hajaokoka.  Lakini mtu na mkewe wakiisha kuoana, uzinzi siyo sababu ya kuwaruhusu kuachana.  Mume anapaswa kumsamehe mkewe mara saba mara sabini makosa YOTE kama Mungu katika Kristo alivyotusamehe sisi.  Je, tulisamehewa dhambi zote kasoro uzinzi?  Jibu ni la!  Basi uzinzi siyo kisingizio cha kumwacha mke (WAEFESO 4:32).
  4. UMUHIMU WA KUOA NA KUOLEWA (Mst. 10-11) – Wanafunzi wa Yesu waliposikia mafundisho haya ya Yesu kuhusu ndoa, wakayaona “MAGUMU“ ukiyalinganisha na yale ya Agano la Kale.  Wakasema, “Mambo ya mtu na mkewe yakiwa hivyo, HAIFAI KUOA“.  Yesu akasema ni kwa wale waliojaliwa wanaoweza kukaa bila kuoa au kuolewa.  Maandiko yanasema, AFADHALI WAWILI KULIKO MMOJA (MHUBIRI 4:9-12), tena ni heri kuoa au kuolewa kuliko kuwaka tamaa (1 WAKORINTHO 7:8-9).  Bila kujaliwa na Mungu, ni rahisi kurudi nyuma na kumwacha Yesu kwa sababu ya uasherati.  Kwa sababu hiyo, Biblia inatoa ufumbuzi, “Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe“ (1 WAKORINTHO 7:2).

 

  1. WATU MAALUM WASIOOA AU KUOLEWA (Mst. 11-12) – Wako wanaume ambao tangu kuzaliwa hawana nguvu za kiume, ni matowashi.  Katika hali hiyo, siyo vema kuoa maana wanawake wengi watashindwa kukaa hivyo bila tendo la ndoa.  Hata hivyo kama yuko towashi wa namna hii anayetaka mke wa kumsaidia maisha ya kila siku na yuko mwanamke aliye radhi kukaa naye baada ya KUAMBIWA na kufahamu, hawa wanaweza kuoana!  Wako pia matowashi waliofanywa na watu kuwa matowashi, ili wapate kufanya utumishi wa Malkia n.k.  Hawa nao, wanafuata misingi ya hao waliozaliwa matowashi.  Wako matowashi wengine ambao ni matowashi kutokana na kupewa karama hiyo na Mungu yaani kujaliwa hivyo na Mungu mwenyewe.  Hawa wawe matowashi hivyohivyo kwa ajili ya ufalme wa mbinguni.  Karama ya utowashi inamfanya mtu bila kufanyiwa operesheni yoyote katika viungo vya siri, kuondolewa KABISA tamaa ya mke au mume.  Mtu wa namna hii, katika maisha yake yote, hakuna hata wazo lolote linalokuja kichwani mwake kumtamani mke au mume.  Hii ni karama anayopewa mtu na Mungu, siyo jambo la mtu kuweka nadhiri kwa nguvu zake mwenyewe kwamba maisha yake yote hataoa au kuolewa ili amtumikie Mungu.  Huko ni kujisifia karama kwa uongo (MITHALI 25:14).  Towashi wa namna hii kama alivyokuwa Mtume Paulo, huweza kumhudumia Bwana pasipo kuvutwa na mambo mengine (1 WAKORINTHYO 7:26, 32-35).  Yeye mwenye kupenda karama hii na kutaka kuipokea anaweza kuiomba (1 WAKORINTHO 12:31), na matokeo yake ataona sifa hizo zikiwa kwake.  Wajane wengi humwomba Mungu wakae hivyo na kupewa karama hiyo.  Hata hivyo wako wanaume au wanawake wengine ambao huwa hawana hamu yoyote ya tendo la ndoa kutokana na jinsi ambavyo wanafanya tendo hilo ndotoni na mapepo ya uasherati au mapepo mahaba.  Hiyo siyo karama ya utowashi.  Pepo hawa wanapaswa kukemewa na kuondolewa.  Yafaa nini kuacha uzinzi au uasherati na wanadamu na kufanya hivyo na mapepo?

(3)      KUBARIKI WATOTO WADOGO (Mst. 13-15; MARKO 10:13-16)

Watoto wadogo wanabarikiwa, hawabatizwi.  Yesu katika utoto wake alibarikiwa, hakubatizwa (LUKA 2:27-34).  Kubatizwa ni kwa mtu mwenye akili aliyeisikia Injili binafsi, kuiamini na kisha kutubu dhambi zake (MATENDO 2:38; 8:12; WARUMI 10:13-14).  Watoto wadogo, ufalme wa mbinguni ni wao maana hawahesabiwi dhambi maana hawana akili ya kuifahamu sheria na kupambanua mema na mabaya (WARUMI 4:15; 5:13).

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s