MAOMBI YA YESU

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

SOMO:  MAOMBI YA YESU

L

eo, tunaanza kujifunza SURA YA 17 ya Kitabu cha YOHANA, katika Biblia zetu.  Kuna mengi sana ya kujifunza katika sura hii.  Yesu Kristo, alikuwa mwombaji wa kipekee sana.  Wakati mwingine alikesha usiku kucha katika kumwomba Mungu (LUKA 6:12).  Alfajiri na mapema sana, alitoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko (MARKO 1:35).  Muda mrefu, alifanya maombi na dua, pamoja na kulia sana na machozi (WAEBRANIA 5:7).  Hata hivyo, pamoja na maisha yake yote kuwa maisha ya maombi, hakuna mahali pengine katika Biblia, ambapo kuna rekodi ndefu ya maombi yake aliyoyaomba, kama tunavyoiona katika sura hii.  Katika sura hii nzima ya maombi ya Yesu, kuna mengi ya muhimu ya kujifunza, ndiyo maana Roho Mtakatifu aliona vema katika sura hii kuweka rekodi ndefu ya maombi haya maalum.  MATHAYO 14:22-23; LUKA 22:40-46.  Kwa kuanzia, leo tutatafakari kwa makini YOHANA 17:1-3.  Tutajifunza mistari hii, kwa kuigawa katika vipengele saba:-

(1)      MAOMBI YA YESU (MST. 1);

(2)      KUINUA MACHO KUELEKEA MBINGUNI KATIKA MAOMBI (MST.1);

(3)      SAA IMEKWISHA KUFIKA, MTUKUZE MWANAO (MST. 1);

(4)      SABABU YA KUMWOMBA MUNGU ATUTUKUZE (MST. 1);

(5)      CHANZO HALALI CHA MAMLAKA YETU (MST. 2);

(6)      MPANGO WA MUNGU WA KUTUPA WOTE UZIMA WA MILELE

      (MST.2);

(7)      JINSI YA KUPATA UZIMA WA MILELE (MST.3)

 

(1)            MAOMBI YA YESU (MST. 1)

Kwa kuangalia maombi ya Yesu katika sura hii nzima kuanzia mstari wa kwanza tunajifunza yafuatayo kuhusu maombi:-

  1. UMUHIMU WA MAOMBI – Ikiwa Baba hakumtukuza Yesu mpaka Yesu alipofanya maombi na dua, tena kwa kulia sana na machozi (WAEBRANIA 5:7); ni muhimu kuelewa kwamba mpango wa Mungu, hauwezi kutimilika kwetu kwa ukamilifu, ikiwa tutatupilia mbali MAOMBI!  Hatuna kitu kwa kuwa hatuombi! (YAKOBO 4:2).  Kupokea kwetu kunategemeana na jinsi tunavyoomba (LUKA 11:9-10; ZABURI 2:8).  Mafanikio ya Yesu yalitokana na maombi.  Aliishinda dhambi wakati wote, kwa kuwa alikuwa mwombaji; hata akawafundisha wanafunzi wake kuomba ili wasiingie majaribuni (MATHAYO 26:40-41).  Tukiwa tunapenda kulala tu na kufanya mambo mengine tu, hatuwezi kupata mafanikio ya Yesu Kristo.  Mungu hufanya mambo makubwa, anaposikia kwanza maombi yetu.  Huo ndiyo mpango wake.  Hawezi kuupinga mpango wake huu.  Hata tukiwa usingizini, ili Mungu afanye jambo fulani kwa mfano kutuokoa katika ajali au kuibiwa n.k., kwanza hupandikiza roho ya maombi ndani YETU, na tunaweza kushitukia tunakemea bila kujifahamu sana.  Sura nzima hii ya 17, inawekwa maalum kwetu ili kutufundisha umuhimu wa maombi.

 

  1. MAOMBI BAADA YA KUHUBIRI AU KUFUNDISHA – Baada ya Yesu kusema maneno hayo (MST. 1) yaani kufundisha maneno mengi katika sura zilizotangulia, alianza kuomba, akiwaombea wanafunzi wake.  Hapa anatufundisha wahubiri au waalimu wa Biblia, umuhimu wa kuwaombea wanafunzi wetu mara tu baada ya kumaliza mafundisho kwao.  Kupanda na kutia maji, ni kwetu sisi, lakini mwenye kukuza ni Mungu.  Tunapowaombea waliotusikiliza, mara tu baada ya kuwahubiria au kuwafundisha maombi hayo huwafanya wakae katika neno hilo tulilowafundisha.
  2. MAOMBI YA KUIOMBEA FAMILIA – Tunajifunza jambo jingine katika maombi ya Yesu.  Yesu Kristo aliishi na wanafunzi wake kama familia yake.  Alikuwa pamoja nao na kuhusika na maisha yao yote.  Yesu alikuwa ndiye Mkuu wa familia hiyo.  Hao sasa anaomba kwa ajili ya familia yake.  Ni muhimu kwa Baba katika familia kufahamu wajibu wake wa kuiombea au kuibariki familia yake akmtaja mke wake na watoto, licha ya kufahamu pia baraka za kutimiza wajibu wa kuiongoza familia yote katika wokovu (MWANZO 18:19; 2 SAMWELI 6:20).
  3. MAOMBI WAKATI WA KUAGANA – Yesu hapa alikuwa anaagana na wanafunzi wake.  Muda mfupi unaofuata anagesulibishwa msalabalni, na kuachana nao kwa muda.  Wakati huu wa kuagana, Yesu anawaombea wanafunzi wake.  Hatuna budi kuombeana sisi na wale tuwapendao, tunapokuwa tunaagana, iwe wanakwenda safari au popote (MATENDO 20:36-38).
  4. MAOMBI YA KUWAOMBEA KONDOO – Yesu kama Mchungaji mwema wa kondoo (YOHANA 10:11-16), hapa anawaombea kondoo wake; akitufundisha wajibu wa Mchungaji kuwaombea anaowaongoza iwe ni Kiongozi wa Zoni, Seksheni au Kanisa la Nyumbani.  Kutokufanya hivi, ni kuacha kufuata kielelezo cha Yesu.

 

(2)            KUINUA MACHO KUELEKEA MBINGUNI KATIKA MAOMBI (MST. 1)

Yesu aliinua macho kuelekea mbinguni mara kadha alipokuwa akiomba (YOHANA 11:41).  Watu wengine hufundisha kwa upotofu kutumia mistari hii kwamba tunapoomba hatutakiwi kufumba macho, bali tukodoe macho tukiyaelekeza mbinguni eti kama alivyofanya Yesu!  Hii siyo kweli.  Bado kuna uwezekanao mkubwa kwamba Yesu aliinua macho kuelekea mbinguni huku akiwa ameyafumba.  La msingi la kufahamu hapa ni kwamba macho ya nafsi zetu au mioyo yetu, ndiyo tunayopasa kuyainua kuyaelekeza mbinguni kwa Baba na kuweka moyo wetu wote katika maombi (ZABURI 25:1).  Kufumba macho hutusaidia kuomba bila kuifanya akili yetu kuvutwa na mambo mengine.  Hata hivyo siyo sheria tuliyowekewa ya kufuata.  Hatuna budi kuangalia mazingira yanayotukabili na kutumia hekima.  Kwa mfano siyo busara kuomba tukiwa tumefumba macho wakati tunaendesha gari, tunapotaka kuomba juu ya hatari inayotukabili.

 

(3)            SAA IMEKWISHA KUFIKA, MTUKUZE MWANAO (MST. 1)

Yesu Kristo, aliifahamu saa yake ya kufa, tofauti na wanadamu wengi (MHUBIRI 9:12).  Ikiwa sisi hatuifahamu siku yetu ya kufa, hatuna budi kuwa waangalifu zaidi sana kujiweka tayari wakati wote.  Maana ya neno “KUTUKUZWA“, kama linavyotajwa hapa, ni “KUPEWA USHINDI MKUBWA“.  Yoshua anatajwa kwamba alitukuzwa baada ya kuvuka Yordani na watu wake kwa ushindi mkubwa na kuukabili Yeriko, kinyume na matarajio ya maadui ambao alidhani asingeweza kuwafikia kwa sababu ya mto Yordani kufurika (YOSHUA 4:10-14).  Vivyo, hivyo Yesu alipoomba, “Saa imekwisha kufika, mtukuze Mwanao“, alimaanisha, Saa imekwisha kufika, mpe ushindi mkubwa Mwanao apate kumponda kichwa Ibilisi msalabani kama ilivyotabiriwa.  Saa kufika, ilikuwa inaaja mapambano na mamlaka ya giza ya Shetani pale msalabani (LUKA 22:53).

 

(4)            SABABU YA KUMWOMBA MUNGU ATUTUKUZE (MST. 1)

Yesu aliomba kutukuzwa ili amtukuze bba.  Tunapomwomba Mungu atupe ushindi katika mtihani, hatuna budi kuomba hivyo ili mafanikio yetu yawe ni kwa ajili ya kumtumikia Mungu.  Tunapoomba mafanikio kazini, katika biashara n.k., hatuna budi kuomba hivyo tukiwa tuna nia ya kuitenda kazi ya Mungu zaidi kutokana na mafanikio hayo.  Tukimwomba Mungu atuponye, hatuna budi kuwa na nia ya kuutumia uzima wetu katika kumtumikia Mungu.

 

(5)            CHANZO HALALI CHA MAMLAKA YETU (MST. 2)

Kwa unyenyekevu mkubwa, Yesu anajitaja kupewa mamlaka na Baba, sembuse sisi?  Ni muhimu kufahamu kwamba mamlaka yoyote tuliyonayo wanadamu, tumepewa kutoka juu na Baba.  Bila Yeye, sisi hatuna kitu (YOHANA 19:9-11).  Yeye aliyetupa mamlaka pia, ana haki ya kuiondoa kwetu.  Hatupaswi kulalamika hata kidogo tunaposimamishwa uongozi, au tunapofanywa wasaidizi wa Viongozi wengine ingawa mwanzoni tulikuwa Viongozi wa Zoni, Seksheni au Makanisa ya Nyumbani n.k.

 

(6)            MPANGO WA MUNGU WA KUTUPA WOTE UZIMA WA MILELE (MST. 2)

Yesu ana mamlaka juu ya wanadamu wote wenye mwili, na mamlaka yake itamhukumu kila asiyemwamini leo (YOHANA 5:22; 3:18,36).  Hata hivyo, hapendi hata mtu mmoja apotee na kuangamizwa motoni, ila anapenda kila mmoja afikilie toba na kuupata uzima wa milele (2 PETRO 3:9).  Kwa nini tuukose uzima huu wa milele, kwa kudhani labda tumeandikiwa kwenda motoni?

 

(7)            JINSI YA KUPATA UZIMA WA MILELE (MST. 3)

Jinsi ya kuupata uzima wa milele, ni kumjua Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo aliyemtuma.  Hapa maneno, “Mungu wa pekee wa kweli“, hayaonyeshi kwamba Yesu siyo Mungu, kama wengine wanavyodai.  Yesu Kristo anatajwa pia kwamba Yeye ndiye Mungu wa Kweli, na Uzima wa milele (1 YOHANA 5:20).  Hapa maneno, “Mungu wa pekee wa kweli“, ni maneno yanayoelezea jinsi Mungu alivyo tofauti na miungu au sanamu kama Baali na wengine kama Artemi na Waefeso (MATENDO 19:26-28).  Kumjua Mungu au Yesu Kristo kunathibitika kwetu, pale tunapozishika amri zake , na huo ndiyo uzima wa milele (1 YOHANA 2:3-4).

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s