MAPENZI YA MUNGU

Neno la Uzima kutoka kwa Askofu Zachary Kakobe

Tovuti : http://www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : http://www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube : http://www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA
SOMO: MAPENZI YA MUNGU (MATHAYO 15:29-39)
Ni watu wachache sana walio na mashaka kwamba Mungu hana nguvu au uwezo wa kufanya mambo makubwa, lakini ajabu ni kwamba watu wengi sana wana mashaka juu ya mapenzi ya Mungu katika kuwaponya na kuwapa mahitaji yao mengine. Wengi utawasikia wakisema “Ni mapenzi ya Mungu niugue na ataniponya kama akipenda”. Mawazo ya jinsi hii ni kizuizi kikubwa sana cha kupokea lolote kutoka kwa Mungu. Ni makusudi ya somo letu la leo, kujifunza Biblia ili tuifahamu kweli na kuyajua hasa mapenzi ya Mungu kwetu. Tutaligawa somo letu la leo katika vipengele vitatu:-

(1) HURUMA YA MUNGU NA KUHUSIKA KWAKE KATIKA MATATIZO YETU;
(2) MAPENZI YA MUNGU KWETU;
(3) WAJIBU WETU KATIKA KUPOKEA MAPENZI YA MUNGU KWETU.

(1) HURUMA YA MUNGU NA KUHUSIKA KWAKE KATIKA MATATIZO YETU

a) HURUMA YA MUNGU
Katika MATHAYO 15:32, tunaona Yesu akiwahurumia watu kwa sababu HAWANA KITU CHA KULA na mara moja baada ya huruma hiyo akachukua hatua. Huruma mara kwa mara huambatana na kuchukua hatua pale ambapo mtu ana uwezo. Yesu mwenye uwezo wote anatajwa mara kwa mara katika Biblia kuwaonea huruma wale wote wenye mahitaji mbalimbali. Angalia mistari ifuatayo:- MATHAYO 9:36; 14:14; 15:32; 20:33-34; MARKO 1:40-41; 6:34; LUKA 7:11-15. Huruma ya BWANA kwa wamchao inafananishwa na huruma ya baba kwa watoto wake (ZABURI 103:13).
b) KUHUSIKA KWA MUNGU KATIKA MATATIZO YETU
Mungu anasema tumtwike YEYE fadhaa na mizigo yetu yote kwa maana yeye HUJISHUGHULISHA SANA kwa mambo yetu (1 PETRO 5:7; ZABURI 55:22).
(2) MAPENZI YA MUNGU KWETU
Ni muhimu kufahamu kwa hakika kwamba Mungu hapendi kutuona na njaa, magonjwa au matatizo yoyote tuliyo nayo, na pia hapendi yeyote kati yetu apotee na kwenda motoni.
 Kuwaaga wakifunga SIPENDI, wasije wakazimia njiani (MATHAYO 15:32);
 Ukitaka, waweza kunitakasa…….NATAKA, takasika (MARKO 1:40-41);
 Maana HAPENDI mtu yeyote apotee, bali WOTE wafikilie toba (2 PETRO 3:9).
Yesu alipoambiwa “Ukitaka waweza kunitakasa“ alijibu NATAKA kuonyesha mapenzi ya Yesu kwa wagonjwa na wote wenye mahitaji. Ni muhimu hapa kufahamu kwamba Yesu katika kusema “NATAKA“ na kumponya huyo mwenye ukoma alikuwa anaonyesha “MAPENZI YA MUNGU KWETU“ kwa sababu zifuatazo:-
1. Yesu hakuyatafuta mapenzi yake bali ya Baba (YOHANA 5:30; 6:38);
2. Yesu hakufanya neno kwa nafsi yake (YOHANA 8:28);
3. Siku zote Yesu aliyafanya yale yampendezayo Mungu Baba (YOHANA 8:29);
4. Mafunzo ya Yesu kwetu ndiyo mafunzo ya Mungu kwetu (YOHANA 7:16).
Mungu anapenda KUWAPONYA WOTE siyo fulani tu. Maandiko yanaonyesha wazi mapenzi ya Mungu ya kuwaponya WOTE na kumponya KILA MMOJA:- MATHAYO 8:16; 9:35; 12:15; 14:35-36; MARKO 6:56; LUKA 4:40; 17:11-17; MATENDO 10:38.
Kwa misingi hiihii Mungu anapenda kila mmoja wetu apate chakula na nguo (1 TIMOTHEO 6:8) na kufanikiwa katika mambo yote (3 YOHANA 1:2) na tena kila mmoja wetu AOKOKE maana moto wa milele amewekewa Ibilisi tu na malaika zake (MATHAYO 25:41).
(3) WAJIBU WETU KATIKA KUPOKEA MAPENZI YA MUNGU KWETU
1. Kamwe hatupaswi kuomba “Ikiwa ni mapenzi yako” tunapoomba wokovu, utakaso, Nguvu ya Roho Mtakatifu, uponyaji, chakula, mavazi na yote ambayo mapenzi ya Mungu kwetu tumekwisha kuyafahamu. Tukiomba hivyo tunajizuia wenyewe kupokea;
2. Kwa sababu ni mapenzi ya Mungu kutuponya WOTE, kila mmoja wetu wakati wowote ule anapougua anapaswa kuomba uponyaji na kukataa kabisa mawazo yanayomjia yakisema “Ugonjwa huu labda Mungu ametaka autumie kukupeleka mbinguni”. Siyo lazima tufe kwa ugonjwa. Ni lazima kuhakikisha HAJA YETU YA KUPONYWA inabaki palepale mpaka tupokee uzima. Haja yetu ya kuponywa ikiondoka na tukakubali uongo wa Shetani kwa kuangalia hali yetu inavyozidi kuwa mbaya na tukasema “Hakuna matumaini tena”, basi tujue hatutapokea kitu tena (LUKA 9:11);
3. Ni lazima tumpinge Shetani wakati wote tukiwa thabiti katika IMANI tukijua ni mapenzi ya Mungu kwetu kupokea wokovu, utakaso, Nguvu ya Roho Mtakatifu, uponyaji, chakula, mavazi na yote ambayo ni mapenzi ya Mungu kwetu. Tusikubaliane na Shetani kamwe kwamba tutakufa au hatutafanikiwa. Kukubaliana na Shetani ni kujiondoa wenyewe katika kupokea mapenzi ya Mungu. Kinyume chake, tutapokea mapenzi ya Shetani ambayo ni kutuchinja, kutuharibu na kutuibia haki zetu (1 PETRO 5:9; YOHANA 10:10).
………………………………………………………………………………
Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni? Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14). Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27). Kinyonge ni kipi? Ni yule anayetenda dhambi. Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge! Je, wewe ni mtakatifu? Jibu ni la! Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13; YOHANA 14:6). Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii? Najua uko tayari. Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni; “Mungu Baba asante kwa ujumbe huu. Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi. Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha. Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo. Bwana Yesu niwezeshe. Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu. Amen”. Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni. Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu. MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “note” hii, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s