MIMI NIMEKUTUKUZA DUNIANI

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

SOMO:            MIMI NIMEKUTUKUZA DUNIANI

L

eo, katika siku hii ya Kuichambua biblia, tunaendelea kujifunza Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu.  Leo, tunatafakari kwa makini YOHANA 17:4-10.  Ingawa kichwa cha somo letu la leo, ni, “MIMI NIMEKUTUKUZA DUNIANI“, hata hivyo, kuna mengi zaidi ya kujifunza.  Tutayagawa mafundisho yote tunayoyapata katika mistari hii, katika vipengele kumi na viwili:-

(1)          MIMI NIMEKUTUKUZA DUNIANI (MST. 4);

(2)          KUIMALIZA KAZI TULIYOPEWA (MST. 4);

(3)          KUOMBA MANENO YALEYALE (MST. 5);

(4)          KUUSTAHIMILI MSALABA NA KUIDHARAU AIBU (MST. 5);

(5)          YESU ALIKUWAKO KABLA YA ULIMWENGU KUWAKO (MST. 5);

(6)          KUTOA HABARI AU RIPOTI YA JINSI TULIVYOUTUMIA MUDA WETU

            (MST.5-6);

(7)          KUPEWA WATOTO NA MUNGU (MST. 6);

(8)          KUHAKIKISHA TUMEPEWA MANENO NA MUNGU (MST. 8);

(9)          KUWA NA HAKIKA YA MAMBO YASIYOONEKANA (MST. 8);

(10)     NAWAOMBEA HAO SIUOMBEI ULIMWENGU (MST. 9);

(11)    KWA KUWA HAO NI WAKO (MST. 9-10);

(12)    YESU KUTUKUZWA NDANI YA WANADAMU (MST.10).

 

(1)            MIMI NIMEKUTUKUZA DUNIANI (MST. 4)

Agizo la Mungu kwetu katika maisha yetu yote, tunapokuwa duniani, ni kufanya yote kwa utukufu wa Mungu, tutendapo neno lolote (1 WAKORINTHO 10:31).  Hatuna budi kuwa na mwenendo mzuri kati ya Mataifa au watu ambao hawajaokoka ili wao wamtukuze Mungu kwamba kweli wako watu waliookoka, hata kama wao wameshindwa kuifuata njia ya wokovu (1 PETRO 2:12; MATHAYO 5:14-16).  Kumtukuza Mungu, ni kufanya matendo ambayo yatawafanya watu wengine kumpa sifa Mungu aliyetuokoa na kuona kwamba neno lake ni kweli na tena ana watu wanaomcha na kuzifuata njia zake.  Yesu Kristo alimtukuza Mungu duniani katika mambo yote aliyoyafanya.  Hatuna budi kujiuliza je, tunampa sifa au kumtukuza Mungu kutokana na mavazi yetu?  Je, tunampa sifa Mungu kutokana na usemi wetu, au maneno yetu yote tunayoyatamka kila siku?  Je, tunampa sifa Mungu kutokana na kazi zetu tunazozifanya?  Je, tunampa sifa Mungu kutokana na tabia zetu kwa ujumla?  Hatuna budi kufahamu kwamba ikiwa tunawapiga wake zetu, hatumtukuzi Mungu.  Ikiwa tumejaa uongo, mizaha na bado tuna matusi vinywani mwetu, hatumtukuzi Mungu.  Ikiwa tunafanya kazi kiwanda cha bia au sigara,k au tunawauzia wengine pombe, n.k, na kuwa kama mataifa tu, katika mienendo yetu, kufanya hivyo, hakumtukuzi Mungu.  Wale watakaomwona Mungu ni wale tu ambao mapak mwisho wao duniani, watathibitika kwamba walimtukuza Mungu duniani kama Yesu.  Bwana atupe neema kumtukuza Yeye duniani.

 

(2)            KUIMALIZA KAZI TULIYOPEWA (MST. 4)

Kiu na shauku ya Yesu Kristo wakati wote, ilikuwa ni kuimaliza kazi aliyopewa (YOHANA 4:34).  Mwishoni mwa kuwepo kwake duniani, alikuwa ameimaliza kazi aliyopewa.  Kazi tuliyopewa sisi, ni kuhubiri Injili kwa kila kiumbe, na kuwafanya mataifa kuwa wanafunzi wa Yesu na kuwafundisha kuyashika YOTE aliyotuamuru Yesu (MARKO 16:15; MATHAYO 28:19-20).  Je, tumekwisha kuimaliza kazi hii tuliyopewa?  Kama sivyo, tunaupata wapi muda wa kuangalia mechi za mpira wa ligi, kucheza draft, bao au karata, kuogelea, kufanya masengenyo, kusoma hadithi za kidunia, au kuangalia vipindi visivyo na maana katika Televisheni?

 

(3)            KUOMBA MANENO YALEYALE (MST. 5)

Hapa Yesu anarudia tena kuomba kwamba Baba amtukuze, kama alivyoomba katika MST. 1.  Ilikuwa kawaida ya Yesu kuomba maneno yaleyale, akiyarudia kwa msisitizo, katika maombi yake MATHAYO 26:44.  Hatupaswi kuogopa kuyarudia maneno yaleyale tunapokuwa tunaomba, na kujaribu kutafuta maneno mapya tu.  Hatuna budi kutokuacha kumwomba Mungu mpaka tupokee.  Mtu hubisha malango mapaka amefunguliwa, na sisi katika maombi yetu hatuna budi kuomba kwa kubisha hodi na kurudiarudia maneno yaleyale, “Hodi, Hodi, Hodi hapa“, mapaka tumefunguliwa (LUKA 11:5-9; 18:1-8).

 

(4)            KUUSTAHIMILI MSALABA NA KUIDHARAU AIBU (MST. 5)

Yesu Kristo katika maombi yake hapa anazidi kuomba utukufu katika ulimwengu ujao pamoja na Baba yake.  Katika maombi yote katika Sura hii ya 17, hagusi lolote kuhusu aibu na mateso ya msalaba yatakayokuja kwake muda mfupi ujao, ingawa anajua kwamba saa imewisha kufika.  Kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake, aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, itakayompata, na matokeo yake akatukuzwa.  Sisi nasi, hatauna budi kuacha kuangalia mateso na aibu tunayoipata kwa ajili ya wokovu wetu, bali tuangalie furaha iliyo mbele yetu (WAEBRANIA 12:1-2)

 

(5)            YESU ALIKUWAKO KABLA YA ULIMWENGU KUWAKO (MST. 5)

Uwiano wa maandiko, unaonyesha jinsi Yesu alivyokuwako kabla ya ulimwengu kuwako.  Aliumba ulimwengu.  Hakuanzia tumboni mwa Mariamu kama watu wengine tu (MIKA 5:2; MITHALI 8:22-30; YOHANA 8:56-58).

 

(6)            KUTOA HABARI AU RIPOTI YA JINSI TULIVYOUTUMIA MUDA WETU (MST.

            6-8)

Katika mistari hii Yesu anatoa habari zake mwenyewe au ripoti ya jinsi alivyotumia muda wake duniani.  Anaeleza jinsi alivyoifanya kazi aliyopewa ya kuwahubiri na kuwafundisha aliopewa.  Kila mtu miongoni mwetu, siku yake ya mwisho duniani atatoa habari yake au ripoti yake, akieleza jinsi alivyoutumia muda wake aliopewa duniani (WARUMI 14:12).  Je, utaeleza habari gani ya jinsi ulivyoutumia muda uliopewa na kuishi miaka 70 au 80?  Zoezi la kutoa ripoti ya kila wiki ya uinjilisti, katika Kanisa hili, tukieleza tumetumia muda gani kuomba, kusoma neno, kusikiliza Kaseti za Mafundisho ya Neno, kushuhudia na kufuatilia watoto wachanga kiroho, ni zoezi la manufaa sana kwetu, hatupaswi kulikwepa.  Zoezi hili linatuandaa kutoa habari zetu siku ya mwisho.

 

(7)            KUPEWA WATOTO NA MUNGU (MST. 6)

“Watu wale ulionipa ………neno lako wamelishika“.  Hatuna budi kukumbuka kwamba, watu wale tunaokabidhiwa kuwafuatilia, baada ya wao kuokolewa, tunakuwa tumepewa na Mungu (WAEBRANIA 2:13).  Inatupasa kutumia muda wetu wote, fedha, zetu zote, na chochote kile tulicho nacho, kuhakikisha watoto hawa tuliopewa, wamelishika Neno la Mungu.  Wakipotea na kuacha wokovu, kutokana na uzembe wetu, roho zetu zitakuwa mahali pa roho zao (1 WAFALME 2);39-40; MATHAYO 18:14).

 

(8)            KUHAKIKISHA TUMEPEWA MANENO NA MUNGU (MST. 8)

Kwa kuwa meneno uliyonipa nimewapa wao“, ni mfano wa Yesu kwa wahubiri na waalimu wa neno la Mungu.  Hatupaswi kutumia akili tu na uzoefu tunapokwenda kuhubiri au kufundisha neno la Mungu.  Hatuna budi kuwa na muda wa kutosha mbele za Mungu na kupokea maeno kutoka kwake, ya kuwapa wote tunaowaendela kuwahubiri.  Hata kama tuliwahi kulifundisha somo hilo, hatuna budi kulichukua upya mbele za Bwana na kupokea meneno ya siku hiyo mpya.  Neno la Mungu ndilo lenye uwezo wa kumbadili mtu, siyo maneno yetu.  Tukitaka kuwa Wahubiri au Waalimu wenye mafanikio kama Yesu, hatuna budi kuzingatia siri hii ya mafanikio.

 

(9)            KUWA NA HAKIKA YA MAMBO YASIYOONEKANA (MST. 8)

“Wakajua HAKIKA ya kuwa nalitoka kwako“.  Walijuaje?  Walijua kwa IMANI!  Hawakungojea kuona kwa macho.  Imani ni kuwa na HAKIKA ya mambo yatarajiwayo au kuwa na bayana au uthibitisho wa mambo yasiyoonekana kwa macho (WAEBRANIA 11:1; 2 WAKORINTHO 5:7).  Tusingoje kupimwa ili tuamini tumepona, vilevile tusingoje kwanza kuona kwa macho uvimbe au ugonjwa wetu wowote kwamba umetoweka.  Tuwe na hakika kwamba ni hivyo, kabla ya kuona kwa macho.. Hiyo ndiyo Imani.

 

(10)       NAWAOMBEA HAO SIUOMBEI ULIMWENGU (MST. 9)

Ulimwengu kama unavyotajwa hapa, ni watu ambao wamelisikia neno la Mungu na wakaacha kumwamini Yesu na kuokolewa, bali wakadumu kutenda dhambi mpaka mwisho wao.  Yesu hana huruma juu ya watu wa jinsi hii.  HAWAOMBEI LOLOTE!  Adhau ya Mungu itakapokuja juu ya watu hawa, Mungu hatataka kusikia maombi ya mtu! (YEREMIA 7:16-20).  Kwa msingi huu, tusipoteze muda wetu kuwaombea wafu ambao hawakuokoka duniani!  Maombi haya hayasikilizwi!  Tuwaombee kabla hawajafa!

 

(11)       KWA KUWA HAO NI WAKO (MST.9-10)

Ni muhimu kufahamu kwamba sisi tuliookolewa ni watu wake Mungu, NI WA MUNGU.  Kuwa wa Mungu maana yake ni nini?  Watu wake mtu, ni wale wa nyumbani mwake hasa wanaoitwa kwa jina lake.  Mke anapoolewa huitwa kwa jina la mume sawa na watoto wake.  Hivyo mke na watoto, ni watu wake baba wa familia.  Baba asiyewatunza wa kwake, ni mbaya kuliko asiyeamini! (1 TIMOTHEO 5:8).  Kwa msingi huu, sisi ni wa Mungu Baba wa Mbinguni, ni watu wa nyumbani mwake Mungu.  Tunapoomba, kuna kitu cha ziada sana katika maombi yetu, tukimkubusha Mungu kwamba sisi ni wake, hivyo tunaomba atupatie chakula, mavazi n.ki.  Hata tukiwaombea wengine walio wake tunataja kama Yesu.  “KWA KUWA HAO NI WAKO“.  (Angalia KUTOKA 32:11).

 

(12)       YESU KUTUKUZWA NDANI YA WANADAMU (MST. 10)

“Nami nimetukuzwa ndani yao“  Yesu hutukuzwa ndani ya wanadamu.  Wanadamu hutumiwa na Mungu kumtukuza Yesu kwa kufanya ishara na maajabu kwa Jina la Yesu n.k.  Mwandamu anatambulika kuwa na sehemu katika lolote linalomtukuza Mungu.  Wamsikieje PASIPO MHUBIRI? (WARUMI 10:13-15) kwa kuwa mwanadamu ana sehemu anayoitambua Mungu, haiwezi kukwepeka watu kumheshimu Mtumishi wa Mungu anayetumiwa kumtukuza Mungu (MATENDO 28:7-9; 5:12-16; YOSHUA 4:14).  Roho Mtakatifu anasema katika MATENDO 5:15“…….. Ili Petro (SIYO YESU) akija, ingawa kivuli CHAKE kimwangukie mmojawapo wao“.  Kusema, “Mhubiri maarufu Mchungaji Kakobe ameingia hapa mjini.  Matokeo yake vilema watatembea kwa Jina la Yesu“, huku siyo kuchukua utukufu wa Mungu.  Mungu mwenyewe huhusika kuwatukuza mno wanadamu! (2 NYAKATI 1:1).  Yesu hutukuzwa ndani ya wanadamu.

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s