MITHALI YA ZIZI LA KONDOO

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

 

SOMO:  MITHALI YA ZIZI LA KONDOO

L

eo, tena, tunaendelea kujifunza Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu.  Leo tunatafakari YOHANA 9:34-41, na YOHANA 10:1-10.  Katika mistari hii, pamoja na mambo mengine tutatafakari juu ya MITHALI YA ZIZI LA KONDOO.  Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika mistari hii katika vipengele saba:-

(1)         KUTENGWA KWA ALIYEKUWA KIPOFU (9:34-35);

(2)         YESU, MWANA WA MUNGU (9:35-37);

(3)         KUSUJUDIWA KWA YESU (9:37-38);

(4)         FAIDA YA KUKUBALI KUWA KIPOFU (9:36-41);

(5)         MITHALI YA ZIZI LA KONDOO (10:1-6);

(6)         TAFSIRI YA MITHALI YA ZIZI LA KONDOO (10:1-9);

(7)         MAKUSUDI YA KUJA KWA YESU (10:10)

 

(1)                KUTENGWA KWA ALIYEKUWA KIPOFU (9:34-35)

“Wakamtoa nje“, maana yake wakamtenga na sinagogi (9:22).  Nyakati hizi za Biblia Wayahudi walikuwa wana madaraja matatu ya kumtenga mtu na sinagogi.  Kutengwa kwa daraja la tatu, kuliitwa, “NIDDIN“.  Katika kutengwa huku, uongozi wa sinagozi ulimtenga mkosaji kwa siku 30.  Katika siku hizo, mkosaji huyo hakuruhusiwa kuabudu pamoja na wengine.  Vilevile mkosaji huyo hakuruhusiwa kunyoa nywele au ndevu, na pia alitakiwa kuvaa mavazi ya maombolezo, yaliyotumika wakati wa misiba.  Ikiwa baada ya kipindi hiki, mkosaji huyo aliendelea katika UASI, alitengwa kwa daraja la pili, lililoitwa, “CHEREM“.  Katika kutengwa huku, mkosaji huyo ALILAANIWA rasmi, na hakuruhusiwa kuzungumza au kula na mtu yeyote, au kuwa na ushirika wa aina yoyote na watu wengine katika sinagogi hilo.  Vilevile hakukruhusiwa hata kukanyaga nadani ya sinagogi.  Ikiwa mkosaji huyu bado aliendelea katika uasi baada ya hatua hii na kukosa toba ya kweli ndani yake, alitengwa kwa daraja la kwanza lililoitwa “SHAMMATHA“.  Katika kutengwa huku, uongozi wa sinagogi au hekalu, ulimtenga mtu huyu na kumfanya asiwe na ushirika wowote na jamii nzima ya Wayahudi.  Kwa maana nyingi alihesabika kuwa “mataifa“, yaani mtu asiye Myahudi.  Siyo hilo tu, katika daraja hili la kutengwa, uongozi wa sinagogi, ulimtangaza muasi huyo hadharani kwamba amepotea milele, na makao yake ya milele, yatakuwa Jehanum au moto wa milele.  Hata leo katika Kanisa, wakati wa Agano Jipya, kuna kutengwa.  Mtu ambaye ni muasi, anaweza kutengwa na Kanisa katika ngazi mbalimbali (1 WATHESALONIKE 3:14-15; TITO 3:10-11; 2 YOHANA 1:9-11; 1 WAKORINTHO 5:11-13; MATHAYO 18:15-18).  Hatupaswi kuruhusu uasi wa namna yoyote ambao hatimaye unaweza ukatusababisha kutengwa na Kanisa. Mchungaji wa Kanisa kwa sababu mbalimbali, anaweza kumkemea vikali au kumpa adhabu mtu yeyote Kanisani, au kumweka katika kipindi cha nidhamu kwa jinsi moja au nyingine.  Hatupaswi kuzihesabu adhabu hizi kuwa ni kitu kigeni, na tena tunapaswa kufahamu kwamba adhabu hizi, ni kwa faida yetu wenyewe, ili tuushiriki Utakatifu wa Mungu.  Hatupaswi kamwe kuchukia kukemewa na kukatufanya tuache kabisa njia ya kweli ya wokovu (WAEBRANIA 12:5-13; TITO 1:13; MITHALI 15:10).  Mara moja tunapokemewa na Kiongozi wa Kanisa au kupewa adhabu yoyote, hatuna budi kushuka mara moja na kunyenyekea, na kutafuta msamaha kwake, kwa kung’ang’ania sana mpaka tumesamehewa.  Tukiendeleza kiburi, hali hiyo inaweza ikatufanya kupotea milele na kwenda Jehanum.  Tusidhani kamwe kwamba tunaweza tukamuasi Kiongozi wa Kanisa anayefundisha kweli halafu Mungu akawa upande wetu! (LUKA 10:15-16).  Tunapokemewa na Kiongozi wa Kanisa na kuwekwa chini ya nidhamu, kamwe tusimnenee mabaya Mtumishi wa Mungu, ni kuongeza kosa juu ya kosa (MATENDO 23:4-5).  Hata hivyo, tusiogope au kuhofu kutengwa na viongozi wa kanisa walio kinyume na kweli ya Neno la Mungu.  Wakitutenga kwa sababu ya kuisimamia kweli ya Neno la Mungu, Yesu mwenyewe hutupokea.  Hapa, aliyekuwa kipofu, alitengwa kwa kuisimamia kweli, matokeo yake, alipokelewa na Yesu kwa mikono mwili.

(2)            YESU, MWANA WA MUNGU (9:35-37)

Yesu Kristo, tena na tena alijitambulisha waziwazi kwamba Yeye ni Mwana wa Mungu.  Hapa, waziwazi anasema Yeye ndiye Mwana wa Mungu.  Alisema hivyo tena na tena (10:36).  Ni muhimu kufahamu tafsiri halisi ya Yesu, Mwana wa Mungu.  Wayahudi waliifahamu sana tafsiri hiyo ndiyo maana walikuja juu sana wakati awote.  Yesu, Mwana wa Mungu, maana yake YESU NI MUNGU (YOHANA 10:33,36) na tena maana yake YESU NI SAWA NA MUNGU (YOHANA 5:17-18).  Hata sasa, Shetani na wafuasi wake, hawapendi itamkwe wazi kwamba YESU NI MWANA WA MUNGU, maana kutamka hivyo ni kukiri kwamba YESU NI MUNGU!  Hata hivyo ukweli unabaki palepale kwa ushahidi wa maandiko mengi kwamba YESU NI MUNGU (1 YOHANA 5:20; TITO 2:13).  Shetani ni mwongo, Baba wa uongo, yeye anajua waziwazi kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu (MARKO 5:7-8).  Kazi yake shetani ni kuwazuia watu wengi wasiamini kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu, ili wasipate uzima wa milele (1 YOHANA 5:11-12).

(3)             KUSUJUDIWA KWA YESU (MST. 37-38)

Hapa tunaona Yesu akisujudiwa, na yeye mwenyewe akiwa radhi.  Huu ni ushahidi mwingine tena kwamba yesu ni Mungu.  Yesu mwenyewe alisema kwamba, wakusujudiwa ni Mungu peke yake (MATHAYO 4:8-10).  Malaika pia wanakataa kusujudiwa, na wanaeleza kwamba wa kusujudiwa ni Mungu peke yake (UFUNUO 22:8-9).  Kwa msingi huu, Yesu ni Mungu.  Akiwa duniani, alisujudiwa tena na tena (MATHAYO 2:11; 14:33: 28:8-9), na tena aliabudiwa na Wanafunzi wake (LUKA 24:50-52).  Sisi nasi, inatupasa kumsujudia Yesu na kumwabudu.  Ni Mungu wetu!

(4)            FAIDA YA KUKUBALI KUWA KIPOFU (9:39-41)

Kma mtu huyu aliyezaliwa akiwa kipofu (9:1), wanadamu wote, ni wenye dhambi kwa kuzaliwa kutokana na dhambi ya mtu mmoja Adamu (ZABURI 51:5; WARUMI 5:12; 3:23).  Mtu akikubali kwamba yeye ni mwenye dhambi, Yesu Kristo, hamhukumu, bali anamsamehe na kumhesabia haki ya kuingia mbinguni.  Kuna faida kubwa kwa mtu anayekubali kwamba yeye ni kipofu, ni mwenye dhambi.  Anayejiona anaona, au anayjiona ana haki, au anayejiona hana dhambi, Yesu humhukumu kuwa na hatia (YEREMIA 2:35; LUKA 18:9-14).  Mafarisayo hawa hawakukubali kuwa vipofu, na hivyo wakakosa baraka ya kusamehewa.

(5)            MITHALI YA ZIZI LA KONDOO (10:1-6)

Kunena kwa mithali, ni kunena kwa kutumia mifano inayoeleweka katika maisha ya kila siku.  Hapa Yesu anatumia mithali ya zizi la kondoo, ili kuwapa ufahamu Mafarisayo na Waandishi.  Nyakati za Biblia, zizi la kondoo lilitengenezwa kwa uzio wa mawe na miiba iliyowekwa juu ya ukuta huo wa mawe kwa ajili ya usalama wa kondoo.  Zizi liliwekwa mbele ya nyumba ya mwenye kondoo na vyote kwa pamoja vilizungushiwa uzio uliokuwa na mlango.  Kwenye malango huo ndipo alipokaa bawabu au mlinzi.  Mchungaji wa kondoo hawa, alipita mlangoni hapa, kwa ruhusa ya bawabu huyu, na kwenda kuwatoa kondoo nje ya zizi, kwa kuwaita majina, kama vile mbwa wanavyoitwa kwa majina siku hizi za leo.  Mchungaji wa kondoo, aliwatangulia kondoo hawa katika kuwapeleka malishoni na walimfuata.  Mgeni yeyote ambaye siye mchungaji wa kondoo, kondoo hao hawakukubali kumfuata.  Wezi na wanyang’anyi, walipokuwa wanataka kuiba kondoo, hawakupita mlangoni kwa bawabu, bali walikwea penginepo mafichoni katika uzio au ukuta ule.

(6)            TAFSIRI YA MITHALI YA ZIZI LA KONDOO (10:1-9)

Wanadamu wanaofuata maagizo ya Mungu wanaitwa kondoo (ZABURI 100:3; EZEKIELI 34:31).  Katika Agano la Kale, Yesu alitabiriwa kuwa mchungaji wa Kondoo (ISAYA 40:3, 10-11; ZEKARIA 13:7), na katika Agano Jipya, vivyo hivyo anatajwa kuwa ni mchungaji Mkuu wa Kondoo (WAEBRANIA 13;20; 1 PETRO 5:4).  Nyakati hizi za mithali hii ya zizi la kondoo, Mafarisayo, walijiona kwamba wao ndiyo waliokuwa wachungaji halai wa kanisa na kwamba Yesu Kristo alikuwa amejiingiza tu katika uchungaji na hakuwa mchungaji halali, na hivyo hakupaswa kusikilizwa na Myahudi yeyote.  Akijibu hoja hii ndipo Yesu alipowapa mithali hii ya zizi la kondoo ili wajue nani ni Mchungaji halali na nani siyo halali, lakini hawakuelewa.  Yesu hapa anaeleza kwamba Maarisayo kwa kuwa walimkataa Yesu kuwa ni Masihi au Kristo, kwa kufanya hivyo, wameukataa mlango wa kondoo, maana Yesu ndiye mlango wa kondoo (MST. 7).  Kama wameukataa mlango wa kondoo na bado wanataka kuwaonoza kondoo, ina maana wanakwea penginepo, hivyo Mafarisayo ndiyo wevi na wanyang’anyi.  Mafarisayo ni wageni, hivyo kondoo halisi hawawezi kuwafuata, ndiyo maana wanafunzi wengi akiwemo huyu kipofu tangu kuzaliwa, walimfuata Yesu na kuyaacha mapokeo ya Mafarisayo.  Mafarisayo kwa kuwa walikuwa ni wezi na wanyang’anyi, kazi yao ilikuwa ni kuiba roho za kondoo ambazo ni mali yake na kuzipeleka Jehanum.  Hakika Yesu ndiye mlango wetu, tunapokea kwa Mungu lolote kwa Jina lake.  Kwa Jina lake tunaingia mbinguni maana Yeye ndiye Njia (YOHANA 14:6), na vilevile Yeye ni malango unaowazuia mbwamwitu kuturarua.  Wiki ijayo somo:  “MCHUNGAJI NA KONDOO“ tutajifunza mengi zaidi.

(7)            MAKUSUDI YA KUJA KWA YESU (10:10)

Yesu alikuja ili tuwe na uzima tena tuwe nao tele.  Kazi yake kama mlango, ni kumzuia shetani ambaye ni mwizi kuja kutuchinja na kutuharibu.  Yesu kama Mchungaji Mkuu wa kondoo, hututangulia  na sisi kumfuata, hivyo hatuna haja ya kuwa na woga.  Shetani akija, atapambana na Mchungaji wetu Yesu!

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s