MMOJA WENU ATANISALITI

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

SOMO:   MMOJA WENU ATANISALITI

N

i neema ya Mungu tena iliyotufikisha Siku ya leo ya Kuichambua Biblia.  Leo, tunaendelea tena kujifunza Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu.  Katika somo letu la leo, tutatafakari YOHANA 13:21-32.  Kichwa cha somo letu ni, “MMOJA WENU ATANISALITI“, ingawa kuna mengi zaidi ya kujifunza katika mistari hii.  Tutayagawa mafundisho yote tunayoyapata katika mistari hii, katika vipengele vinane:-

(1)   MMOJA WENU ATANISALITI (MST. 21);

(2)   UTARATIBU WA KUMWOMBA MTUMISHI WA MUNGU ATUOMBEE

   (MST. 22-26);

(3)   KUMFAHAMU MSALITI KWA ISHARA (MST. 25-26);

(4)   WAJIBU WA KUMLISHA ADUI (MST. 26);

(5)   KUINGIWA NA SHETANI (MST. 27);

(6)   WAJIBU WA KUWAPA MASKINI KITU (MST. 28-29);

(7)   ALAMA KUU YA MTU ALIYERUDI NYUMA (MST. 30)

(8)   KUTUKUZWA YESU KATIKA KANISA BAADA YA KUTOLEWA KWA    

   MSALITI (MST. 30-32).

 

(1)   MMOJA WENU ATANISALITI (MST. 21)

Neno “MSALITI“, kama linavyotumika katika Biblia, maana yake, “Mtu ambaye anaishi maisha yaliyo kinyume na Neno la Mungu, baada ya kuwa amekwisha kujifunza na kuifahamu Kweli ya Neno la Mungu“.  Yesu Kristo anafahamu yote.  Hapa anasema kwa uhakika kabisa, “Amin, Amin, nawaambieni, Mmoja wenu atanisaliti“, akitaja habari za Yuda Iskariote.  Yuda, alikuwa amekwisha kujifunza Neno la Mungu katika Kweli yote, lakini hapa anatajwa kwamba ataiacha Kweli hiyo, na kufanya yaliyo kinyume na yale aliyojifunza.  Yesu Kristo, anazungumza haya, kwa KUFADHAIKA ROHONI au akiwa amejaa sononeko au huzuni kuu rohoni.  Hakuna jambo linalomtia Yesu fadhaiko au huzuni kuu; kama kumwona mtu mmoja aliyejifunza Kweli ya Neno la Mungu akiasi Kweli na kufanya kinyume na Neno la Mungu analolijua.  Ng’ombe au punda, wanakuwa bora mbele za Mungu kuliko msaliti mmoja (ISAYA 1:2-3).  Ng’ombe au punda, wanajua umuhimu wa kudumu katika vibanda na kuwaheshimu walezi au Bwana zao wanaowalisha!  Inakuwa vigumu kuwafanya upya tena hata wakitubu, wasaliti wa namna hii kwa sababu hufanya kwa makusudi yaliyo kinyume na Neno la Mungu, ingawa wanafahamu yanayowapasa kufanya.  Msaliti yeyote, anamsulibisha Mwana wa Mungu mara ya pili kwa nafsi yake na kumfedhehi au kumpa aibu kwa dhahiri (kwa waziwazi).  Awaye yote katikati yetu, hapaswi kuwa msaliti baada ya kujifunza kweli katika Kanisa hili na kutafuta hukumu yenye kutisha (WAEBRANIA 6:4-8; 10:26-31).  Ussaliti, ni kumfanyia jeuri Roho wa neema na kumkanyaga Yesu Kristo aliye Kweli.  Wasaliti, huifanya kazi ya Mungu kuwa ngumu mno, kwa sababu watu wengi hushindwa kuitafuta Kweli ya wokovu kutokana na wasaliti hawa.  Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa Ufalme wa Mungu.  Tukumbuke mkewe Lutu aliyegeuka kuwa nguzo ya chumvi.  Kwa nini tumsaliti Yesu kwa ajili ya chakula kimoja kama Esau aliyeuuza urithi wake wa mzaliwa wa kwanza? (LUKA 9:62:17:32; MWANZO 19:12-26; WAEBRANIA 12:16-17).  Je, wewe ni msaliti?  Mrudie upesi Mungu mwenye rehema na kuomba msamaha kwake na kuacha usaliti (DANIELI 9:9; 2 PETRO 2:20-22).

(2)   UTARATIBU WA KUMWOMBA MTUMISHI WA MUNGU ATUOMBEE (MST.

   22-26)

Simoni Petro, hapa tunamwona akimpungia mkona Yohana (anayejitaja kwamba ni    mmoja wa wanafunzi wake, kwa unyenyekevu (YOHANA 21:24), na kumwambia amwulize Yesu ili wote wapate jibu.  Kwa nini Petro asiulize mwenyewe na kupata jibu?  Yohana alikuwa mwanafunzi aliyependwa tofauti sana na wenzake kwa maana kwamba, alipewa neema ya ziada.  Yeye pekee ndiye aliyechaguliwa na Yesu kupewa “Ufunuo wa Yohana“, katika Agano Jipya.  Katika Agano la Kale, Danieli aliyepewa pia Ufunuo wa siku za mwisho, anatajwa vivyo hivyo, “aliyependwa sana“(DANIELI 9:22-23).  Wakati wote Yohana anatajwa kuegama kifuani mwa Yesu au kumwelekea Yesu kifua chake, ikimaanisha kwamba yeye ndiye aliyekuwa karibu sana na Yesu kuliko wanafunzi wengine wote; kama Mwana alivyo karibu na Baba (YOHANA 1:18).  Vivyo hivyo leo, ingawa sisi sote ni wanafunzi wa Yesu na kila aombaye hupokea (LUKA 11:10) hata hivyo, wako wanafunzi wengine.  Watumishi wa Mungu, walio karibu sana na Mungu kuliko wengine, na waliopewa neema ya ziada, kama Yohana.  Tunapoomba wenyewe na kukosa majibu hatupaswi kuona kitu cha ajabu au cha aibu kuwaendea hawa ili watuombee (YAKOBO 5:13-14).

 

(3)  KUMFAHAMU MSALITI KWA ISHARA (MST. 25-26)

Yohana hapa alimwuliza Yesu, “Bwana ni nani?“, Yesu angeweza kumwambia moja kwa moja kwamba ni Yuda Iskariote, lakini hakufanya hivyo.  Badala yake alimwonyesha ishara ya kumfanya aweze kumtambua Yuda, “Ndiye mtu yule nitakayemtowelea tonge na kumpa“.  Vivyo hivyo tunajifunza jambo kubwa sisi Watumishi wa Mungu.  Tunaweza kuwafahamu wasaliti kwa ishara anazotuonyesha Yesu.  Kutokana na mazungumzo yao yaliyo mbali na utii na kutokana pia na matendo yao yaliyo kinyume na Neno la Mungu, tunaweza kuwafahamu wasaliti hawa.  Kwa matunda yao wasaliti hutambulikana (MATHAYO 7:16-20).  Hata hivyo Bwana pia hutupa ishasra mbalimbali za kuwatambulisha wasaliti waliofichika.  Ishara mojawapo ni kuwaangalia usoni na kuona utukufu waliokuwa nao mwanzo hauko na ishara nyinginezo ambazo huambatana na ushuhuda wa moyoni unaotoka kwa Roho Mtakatifu unaotuashiria mashaka juu ya wasaliti hawa.  Hatupaswi kuzipuuza ishara hizi.

(4)  WAJIBU WA KUMLSIAH ADUI (MST. 26)

Tunaona hapa Yesu akimpa chakula adui yake Yuda Iskariote ambaye atamtia mikononi mwa wauaji muda mfupi ujao.  Kwa kielelezo, hapa Yesu anatufundisha wajibu wetu wa kumlisha adui yetu anapokuwa na njaa.  Tukimtendea mema adui yetu, matendo hayo humpalia makaa ya moto kichwani pake, na tena hutufanya tupate thawabu kubwa (WARUMI 12:19-21; MITHALI 25:21-22)

 

(5)  KUINGIWA NA SHETANI (MST. 27)

Shetani au mfalme wa uwezo wa anga, hutenda kazi katika wana wa kuasi au wenye dhambi wote.  Hata hivyo mtu mwenye dhambi, akiingiwa na Shetani hufanya dhambi kwa namna isiyo ya kawaida.  Hata wenye dhambi wenyewe, humshangaa mtu wa namna hii na kuona anafanya dhambi kuwazidi.  Watu wengi wenye dhambi ni waasherati au wazinzi, walevi, waongo, wezi, n.k.  Hata hivyo, mtu akiingiwa na Shetani mwenyewe, huwa mwasherati au mzinzi kwa namna ya kutisha.  Huwa mlawiti, na kuwalawiti hata watoto wadogo, au hata yeye kutamani kufanyiwa ulawiti, na anaweza kufanya uasherati hata kwenye basi au treni mahali palipo hadharani mno.  Mtu akiingiwa na Shetani, huwa mlevi kupindukia, mwongo kupindukia, mwizi kupindukia n.k.  Mahali pa namna hii, inatubidi kumkemea Shetani aliye ndani yao kama tunavyokemea pepo waliowaingia watu.  Yuda Iskariote alikuwa akitenda dhambi ya wizi, kabla ya kuingiwa na shetani hapa (YOHANA 12:4-6).  Hata hivyo, alipoingiwa na Shetani, kwa ghafla alitoka haraka na kwenda kuchukua vipande thelathini tu vya fedha na kutaka Yesu auawe, jambo ambalo hakuweza kulifanya kabla.  Mtu mwingine pia anaweza kuingiwa na Shetani na kukwa mpinzani wa Injili na huduma zetu kwa namna isyo ya kawaida kama Sauli.

 

(6)  WAJIBU WA KUWAPA MASKINI KITU (MST. 28-29)

Ilikuwa desturi ya Yesu kuwapa maskini vitu, na wanafunzi wake walijua hivyo.  Hatuna budi kuiga mfano wake.  Hatupaswi kuwa na nguo nyingi ambazo hata hatuzitumii, wakati wenzetu katika Makanisa yetu ya nyumbani, Seksheni au zoni, hawana chochote cha kuvaa.  Wako wengine katikati yetu wana nguo zinazowabana au viatu visivyoenea au nguo za watoto wadogo wakati hawana watoto wadogo tena n.k.  Tunapaswi kuwapa maskini vitu hivi.  Mwenye kazu mbili na ampe asiye na kanga; na mwenye vyakula na afanye vivyo hivyo, kulingana na mafundisho ya Neno la Mungu (LUKA 3:10-11).  Watakatifu katika Kanisa la Kwanza, walizingatia sana kufanya hivi (WAGALATIA 2:9-10; WARUMI 15:25-27).  Tunapaswa kufuata mfano wao.  Asiye na nauli, wenye uwezo tumpe nauli ya kuja Kanisani n.k.  Ni heri au baraka kuu kutoa hivi, kuliko kupokea (MATENDO 20:35).

 

(7)  ALAMA KUU YA MTU ALIYERUDI NYUMA (MST. 30)

Yuda Iskariote, baada ya kurudi nyuma na kuacha wokovu kwa kuinuka ili akamsaliti Yesu, ALITOKA MARA HIYO katika kusanyiko la watu waliookoka.  Hii ndiyo alama kuu ya mtu aliyerudi nyuma na kuacha wokovu.  Atatoka katika Kanisa na kukosa hamu ya kushiriki ibada.  Tukimwona mtu asiyependa tena kuja Kanisani mpaka kwa kukshurutishwa, tujue amerudi nyuma.  Tukimwona mtu asiyetaka kushirikiana nasi katika huduma za Makanisa ya Nyumbani, Seksheni au Zoni, TUJUE AMERUDI NYUMA.  Tukiona mtu hataki tumtembelee nyumbani kwake au kazini kwake, tujue amerudi nyuma.

 

(8)   KUTUKUZWA KWA YESU KATIKA KANISA BAADA YA KUTOLEWA KWA

   WASALITI (MST. 30-32)

Baada ya Yuda Iskariote kutoka, Yesu alisema, Sasa ametukuzwa Mwana wa Adamu, naye Mungu ametukuzwa ndani yake na tena atamtukuza mara yaani muda huo huo.  Tunajifunza jambo kubwa hapa.  Tukiwafuga watu wanaodumu kutenda dhambi katika Kanisa, hatuwezi kumwona Yesu akitukuzwa ndani yetu.  Wakitoka, hatupaswi kuhuzunika!  Ndipo tunapomwona Yesu akitenda kazi kipekee ndani yetu.  Vivyo hivyo kwa kusulibishwa Yesu, alitukuzwa pale alipomshinda Shetani msalabani na kisha kupaa mbinguni katika utukufu. …………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s