MPANGO WA MUNGU WA WOKOVU

ZACHARY KAKOBE

Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SOMO:  MPANGO WA MUNGU WA WOKOVU

NENO LA MSINGI:

MATENDO YA MITUME 16:30, 32;-

“Kisha akawaleta nje akisema, Bwana zangu yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia neno la Bwana, yeye na watu wote waliomo nyumbani mwake”

Watu waliookoka katika kanisa la kwanza lililokuwa linaongozwa na mitume, walijua sana jinsi ya kumwelezea mtu maana ya wokovu hata yeye naye akaokolewa. Katika neno hili la msingi, tunaona mtu mmoja akiuliza afanye nini apate kuokoka, na hapohapo anaambiwa neno la Bwana na kuelewa analopaswa  kufanya. Watu wote tuliookoka, ni wajibu wetu kuihubiri injili ya Wokovu kwa kila kiumbe. Ni wajibu wetu kuwaambia  watu wote neno la Bwana linalohusu wokovu ili yamkini watu wote wapate kuokolewa. Jambo la huzuni ni kwamba watu wengi waliookoka, hawawezi kumweleza mtu mwingine neno la BWANA hata akaelewa, na yeye akaokolewa. Kanisa la Mungu halipaswi kuwa hivi na kuwaacha wengi wakiangamia! Basi, ni makusudi ya somo hili, kujifunza hatua kwa hatua yanayotupasa kufahamu katika kumwambia  mtu neno la BWANA hata na yeye aokolewe. Ikiwa wewe unayelisoma somo hili hujaokolewa, basi ni siku yako pia kuokolewa baada ya kufahamu yote yanayokupasa kufahamu na kuyafanya.

A: NINI MAANA YA NENO “KUOKOKA” AU “KUOKOLEWA”?

Kuokoka au kuokolewa, ni kunusurishwa, kuopolewa, kusalimishwa au kuponywa kutoka katika maafa makubwa yaliyo dhahiri kabisa kukupata. Inaweza ikawa kuponywa  kutoka katika hatari ya kifo, adhabu kali au madhara yoyote makubwa yaliyo dhahiri. Katika hali ya kukosa matumaini ya kukwepe maafa hayo yaliyo dhahiri, inapotokea ghafla njia ya kusalimika, hapo inasemekana umeokoka.

        ANGALIA MIFANO KATIKA BIBLIA

( a ).Baada ya Yusufu kuuzwa na ndugu zake na kupelekwa kuwa mtumwa huko Misri, ilitokea njaa kubwa sana katika ulimwengu wote wa wakati huo. Watu wengi mno walikufa kwa kukosa chakula, na kulikuwa hakuna matumaini. Ndugu zake Yusufu nao walikuwa katika hatari ya kifo. Kabla ya njaa hiyo, huko Misri Yusufu kwa uwezo wa ajabu wa Mungu, aliaminiwa na kuwa waziri mkuu katika nchi ya Misri, na akatumiwa na Mungu kuhifadhi chakula kingi ambacho hatimaye, kilitumika kuwaokoa ndugu zake katika maafa ya kufa kwa njaa (MWANZO 45:5-7), “Basi sasa msihuzunike, wala msiudhike nafsi, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu. Maana miaka miwili njaa imekuwa katika nchi, iko tena miaka mitano isiyo na kulima wala kuvuna. Mungu alinipeleka mbele yenu kuwahifadhia mazao katika nchi na kuwaokoa ninyi kwa wokovu mkuu”.

       ( b ) Daudi akiwa katika hali ya hatari anaeleza juu ya mtu anayehitajika kuokolewa=Mtu ambaye yuko katika hatari ya kufa baada ya kuzama katika matope mengi na maji yakiwa yamefika nafsini mwake. (ZABURI 69::1-2)”Ee Mungu uniokoe, maana maji yamefika mpaka nafsini mwangu. Ninazama katika matope mengi pasipowezekana kusimama. Ninafika penye maji ya vilindi, mkondo wa maji unanigharikisha”.

       ( c ). Wakati  wa Nuhu, Mungu akiwa amechukizwa na dhambi za watu wa wakati ule, aliwaonya juu ya maafa yatakayokuja, kuwaangamiza wote wasiomtii Mungu. Watu wote wakapuuza ujumbe huo, isipokuwa Nuhu aliyetii na kuunda safina iliyotumika kumuokoa yeye na watu wa nyumba yake kutoka katika maafa ya kufa kwa gharika. Watu wote walikufa kutokana na gharika hiyo isipokuwa Nuhu na wenzake saba waliookolewa katika maafa hayo (WAEBRANIA 11:7)”Kwa imani Nuhu akiisha kuonywa na Mungu katika habari za mambo yasiyoonekana bado, kwa jinsi alivyomcha Mungu aliunda safina, apate kuokoa nyumba yake”.

         B.  MAISHA YA BAADAYE YA MTU MWENYE DHAMBI

               Mtu mwenye dhambi ni lazima atapata adhabu ya milele. Adhabu yake inaitwa mauti ya pili au mauti ya milele ambayo ni kutupwa motoni na kuteswa milele. Hakuna mwenye dhambi atakayekwepe adhabu. Kila mmoja atapata mshahara huo wa dhambi, mauti ya milele au kutupwa Jehenamu ya moto..

MITHALI 11:19-21:-“………….Afuataye maovu hufuata mauti yake mwenyewe……….hakika, mtu mwovu hatakosa adhabu………”

EZEKIELI 18:4, 20 “…………Roho itendayo dhambi itakufa……..”

WARUMI 6:23, “Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti………”

UFUNUO 21:8,”Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na    wazinzi na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waoga wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili”.

Hakuna mtu yeyote mwenye dhambi yaani asiyekuwa na haki mbele za Mungu atakayeokoka katika maangamizo hayo. Kwa sasa mtu mwenye dhambi anaona yuko salama na kwamba amani iko kwake, lakini ghafla uhalibifu wake utamwijia

              1.WATHESALONIKE 5;3,”Wakati wasemapo, kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafla, kama vile uchungu umjiavyo mwenye mamba wala hakika hawataokolewa”.

ZABURI 119:155,’Wokovu u mbali na wasiohaki kwa maana hawajifunzi amri zako ( na kuzitenda )”.

  1. C.     NI  NANI  MWENYE  DHAMBI?

Jibu ni kwamba kila mwanadamu aliyezaliwa na mwanmke, kutokana na asili ya Adamu, yuko miongoni mwa wenye dhambi. Wote wamefanya dhambi. Kwa mtu mmoja Adamu, dhambi iliingia ulimwenguni; na watu wote wakahasabiwa kuwa wenye dhambi. Kutokana na kila mtu kuzaliwa akiwa na asili ya dhambi, kila mtu anatenda dhambi pia. Hivyo watu wote pamoja na wewe, wanazaliwa katika dhambi na pia wote wanatenda dhambi.

MHUBIRI 7:20.”Bila shaka hakuna mwanadamu mwenye haki hapa duniani, ambaye afanya mema, asifanye dhambi”.

ZABURI 53:3.Kila mtu amepotoka, wameoza wote pamoja, hakuna atendaye mema, la! Hata mmoja”.

ISAYA 53:6.Sisi sote kama Kondoo tumepotea, kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe………..”.

WARUMI 3:23, “Kwa sabau wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa utukufu wa Mungu”.

WARUMI 5:12. Kwa hiyo, kama kwa mtu mmoja (Adamu) dhambi iliingia ulimwenguni na kuwa dhambi hiyo mauti, na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi”.

1 YOHANA 1:8, 10. “Tukisema kuwa hatuna dhambi twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo ndani mwetu. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi twamfanya yeye kuwa muongo wala Neno lake halimo mwetu”.

            Unaona basi! Kila mtu anakuwa mwenye dhambi kutokana na uzao wa Adamu.          Kila mtu anazaliwa akiwa na asili ya dhambi. Kama Adamu alivyofanya dhambi, wote tunazaliwa na dhambi ya asili.

AYUBU 15:14. “Je, mwanadamu ni kitu gani, hata akawa safi? Huyo    aliyezaliwa na mwanamke hata awe na haki?

AYUBU 25:4,Basi mtu awezaje kuwa na haki mbele za Mungu? Au awezaje kuwa safi aliyezaliwa na mwanamke?

ZABURI 51:5.Tazama mimi naliubwa katika hali ya uovu; mama yangu alinichukua mamba hatiani”.

AYUBU 14:4. “Ni nani awezaye kutoa kitu kilichosafi kitoke katika kitu kichafu (Adamu) ?”.

MAOMBOLEZO 5:7. “Baba zetu walitenda dhambi hata hawapo, na sisi tumeyachukua maovu yao”.

ZABURI 58:3. “Wasiohaki wamejitenga tangu kuzaliwa kwao, tangu tumboni wamepotea, wakisema uongo”.

Mpendwa msomaji, baada ya kusikia yote haya kutoka kwa nabii aliyetumwa kukuletea ujumbe huu, usifanye moyo wako kuwa mgumu.  Hii ni nafasi ya kipekee ya kuokoka.  Je, unajuaje kama utaamka kitandani baada ya kulala usiku wa leo?  Wakati uliokubalika wa wokovu ni sasa (2 WAKORINTHO 6:2).  Labda utaniuliza, ili uokoke, ufanyeje?  Jibu ni rahisi, kwa imani ukitubu dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha, na kumwambia Yesu Kristo akusamehe, utasamehewa sasa hivi, na msamaha wa dhambi, huambatana na wokovu (LUKA 1:77).  Je, uko tayari kuokoka sasa hivi?  Najua uko tayari. Basi fuatisha sala hii kwa dhati toka moyoni, Mungu baba asante kwa kuniletea ujumbe huu.Natubu dhambi zangu zote, kwa kumaanisha kuziacha. Yesu Kristo nakuomba unisamehe dhambi zangu na kunipa uwezo wa kushinda dhambi na kuniokoa kutoka katika mateso ya moto wa milele. Asante, kwa kuniokoa katika Jina la Yesu.  Amen.  Tayari sasa umeokoka, na kwa hakika unakwenda mbinguni sasa, hata ukifa leo.  Ili uzidi kuukulia wokovu, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

       . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook, Twitter n.k  kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “note” hii, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.

UBARIKIWE SANA KWA KAZI YAKO NJEMA

               

Advertisements

One comment on “MPANGO WA MUNGU WA WOKOVU

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s