MTUME SI MKUU

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

SOMO:  MTUME SI MKUU

L

eo, tena, tunaendelea kujifunza KITABU CHA YOHANA katika Biblia zetu.  Siku ya leo ya Kuichambua Biblia, tutatafakari YOHANA 13:13-20.  Ingawa kichwa cha somo letu la leo ni, “MTUME SI MKUU“, kuna mengi zaidi ya kujifunza katika mistari hii.  Tutayagawa mafundisho yote tunayoyapata katika mistari hii, katika vipengele sita:-

 

(1) YESU MWALIMU NA BWANA (MST. 13);

(2) YESU AMETUPA KIELELEZO (MST. 14-15);

(3) MTUME SI MKUU (MST. 16);

(4) MKIYAJUA HAYO HERI NINYI MKIYATENDA (MST. 17);

(5) MCHANGANYIKO WA WEMA NA WABAYA KATIKA KANISA (MST. 18-19);

(6) MCHUNGAJI MJUMBE WA MUNGU (MST. 20).

 

 

(1)             YESU, MWALIMU NA BWANA (MST. 13)

Wanafunzi wa Yesu, walimwia na umtabua Yesu kama Mwalimu na Bwana wao.  Sisi nasi, ikiwa kweli ni wanafunzi wa Yesu; tunapaswa kumwita na kumtambua Yesu kama Mwalimu na Bwana wetu.  Yesu Kristo anasema hapa kwamba, tukimwita na kumtabua kuwa ni Mwalimu na Bwana wetu, twanena vema, maana ndivyo alivyo.  Nyakati hizi tulizo nazo, watu wengi wanaojiita wameokoka, wanamwita Yesu, Mwalimu na Bwana wao.  Hata hivyo, ni watu wachache sana wanaotambua maana hasa ya Yesu kuwa Mwalimu na Bwana wetu.  Hatupaswi kumwita Yesu, Mwalimu na Bwana wetu, bila kujua maana inayomabatana na majina haya.  Tuangalie sasa maana ya jina moja moja:-

  1. YESU KAMA MWALIMU – Neno la Kiyunani linalotafsiriwa hapa Mwalimu, ni “DIDASKALOS“, lenye maana ya “Mwalimu anayetufundisha na kutufunulia mapenzi ya Mungu ambayo inatubidi kuyafanya, bila mjadala wowote“.  Katika shule za dunia hii, Mwalimu wa Hisabati au Hesabu, akitufundisha kwamba 2 + 2 = 4, tunakubaliana naye bila mjadala wowote na kulichukua jambo hilo kama lilivyo, na kulitendea kazi.  Hatusemi kwa nini 2 + 2, isiwe 3?  Vivyo hivyo, sisi kama wanafunzi wa Yesu, Yesu akitufundisha lolote katika Neno la Mungu, hatuna budi kufahamu kwamba amekwisha kutufunulia mapenzi ya Mungu ambayo inatubidi kuyafanya bila mjadala wowote.  Haitupasi kungojea mafunuo mengine yoyote wala kusema KWA NINI tufanye hili au lile kwa njia hii au ile.  Inatupasa kulichukua lolote analotufundisha kama lilivyo, na kulitendea kazi mara moja; au siyo madai yetu kwamba tumeokoka na eti sisi ni wanafunzi wa yesu, madai hayo yanakuwa si ya kweli.
  2. YESU KAMA BWANA – Neno la Kiyunani linalotafsiriwa hapa Bwana, ni “KYRIOS“, lenye maana “MTAWALA WETU, na tena SISI TU MALI YAKE“.  Kila mtu atakayemkiri Yesu kuwa ni Mtawala wake, ataokoka (WARUMI 10:9).  Yeyote asiyekuwa tayari kutawaliwa na Yesu ni ADUI yake, na hivyo badala ya kuokoka atachinjwa mbele zake! (LUKA 19:27).  Ikiwa tunasema tumeokoka, sharti tukubali Yesu atutawale, na sisi tuwe watumwa wake tu.  Mtawaliwa, hafanyi lolote analolipenda, na tena mtumwa hayuko huru kufanya lolote alipendalo!  Mtawaliwa na mtumwa, hawana budi kufanya yale ayapendayo Mtawala au Bwana.  Baada ya kuokoka, hatuna uhuru wowote wa kufanya lolote tulipendalo, tunafanya yale tu yaliyo sawa na Neno la Mungu.  Uhuru wetu watu tuliookolewa, ni uhuru mbali na dhambi (WARUMI 6:17-18, 20-22).  Kabla ya kuokolewa, tunakuwa huru mbali na haki, tunafanya lolote tunalolipenda hata kama liko kinyume na Neno la Mungu.  Baada ya kuokolewa hatuna uhuru wa namna hii.  Tunatwaliwa na Yesu.  Siyo hilo tu, tunakuwa mali yake Yesu.  Tumenunuliwa kwa thamani kubwa.  Yesu ametununua kwa kumwaga damu yake (1 WAKORINTHO 6:19-20).  Yesu anapotuambia tunatakiwa kuja Kanisani, kutenda kazi yake, kufanya maombi kila siku, kusoma Neno lake n.k., hatupaswi kusema hatuna muda wa kufanya hivyo n.k.  Sisi, siyo mali yetu wenyewe.  Vilevile miili yetu imenunuliwa, ni hekalu la Roho Mtakatifu.  Hatupaswi kuitoa miili yetu na kuwapa makahaba!

(2)     YESU AMETUPA KIELELEZO (MST. 14-15)

Yesu kama Mwalimu, ni Kiongozi au Kamanda anayetupa kielelezo.  Anatufundisha kwa kutoa mfano yeye mwenyewe, na kutuambia tufuate mfano wake katika matendo yetu.  Mwalimu au Kiongozi yeyote wa Kanisa, asiyekuwa Kielelezo, hatuati mfano wa Yesu anavunja miiko ya uongozi.  Viongozi wanaompendeza Mungu na Walimu wa kweli, ni wale wanaowatangulia watu na kuwapa mfano au kielelezo cha yale wanayotaka wayatende wanafunzi wao au wale wanaoongozwa.  Gideoni na Abimeleki, ni mfano wa Viongozi hawa (WAAMUZI 7:17-18; 9:48).  Ikiwa Gideoni na Abimeleki waliweza kuwa Walimu walio vielelezo, nyakati za Agano la Kale, ni zaidi sana sisi tulio katika kipindi cha neema.  Hatuna budi kuwa kama Mwalimu Paulo (WAFILIPI 4:9).  Vile vile, sisi kama wanafunzi wa Yesu, tunapaswa kufanya yote kama alivyofanya Yesu.  Ametupa kielelezo cha KUBARIKIWA katika UTOTO wake na siyo kubatizwa utotoni (LUKA 2:27-34) na pia KUBATIZWA katika MAJI TELE UKUBWANI, tunapokuwa tumejua mema na mabaya (LUKA 3:21-23; MATHAYO 3:13-17).  Tunapaswa kufuata nyayo zake Yesu katika kila jambo alilotuachia kielelezo wakati wote tukiwa duniani.  Kama yeye alivyokuwa ulimwenguni na sisi tuwe hivyo katika mwenendo au tabia (1 PETRO 2:21; 1 YOHANA 2:6; 4:17).

(3)   MTUME SI MKUU (MST. 16)

Yesu hapa, anatufundisha WAZIWAZI kwamba Mtume, si mkuu, kuliko yeye aliyempeleka yaani Yesu mwenyewe.  Yesu, ndiye anayewapeleka mitume kuitenda kazi yake (YOHANA 20:21).  Wakati wote katika mafundisho yetu, hatuna budi kuzingatia kwamba hatupaswi kufuata Agizo lolote la yeyote anayejiita mtume, ikiwa agizo hilo haliendani na Agizo la Yesu aliyempeleka.  Kwa msingi huuhuu, katika Matendo ya Mitume au popote, tunapoona kwamba utendaji wa mitume ulikuwa tofauti na Agizo la Yesu, tujue kwamba tumekosea sisi katika tafsiri ya maandiko hayo.  Kwa usalama wetu na ili tubaki katika imani ya kweli, inatubidi katika hali hiyo kufuata AGIZO LA YESU siyo Agizo la Mitume, maana tunawafuata Mitume kama wao wanavyomfuata Yesu (1 WAKORINTHO 11:1).  Kwa kutokuzingatia msingi huu, na kufuata mafundisho ya WILLIAM BRANHAM, watu wachache wameiacha imani na kubatizwa tena kwa Jina la Bwana Yesu tu na kuukana Ubatizxo unaofanywa kwa Jina la Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu, kwa kudai kwamba Mitume walibatiwa kwa Jina la Bwana Yesu wakati wote (MATENDO 2:38; 8:16; 10:48; 19:5).  Hii siyo sahihi.  Tukiona utata katika jambo hili, ni muhimu kukumbuka kwamba Mtume si mkuu kuliko yeye aliyempeleka yaani Yesu.  Agizo alilotupa Yesu aliye Mkuu kuliko Mtume yeyote, katika Ubatizo, ni kubatizwa kwa Jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu (MATHAYO 28:19).  Mtume yeyote akibadilisha agizo hili, hatupaswi kumfuata, maana mtume si mkuu kuliko yeye Yesu aliyempeleka au kumtuma.  Je, katika maandiko haya, mitume walikosea?  Jibu ni hapana!  Katika maandiko, maneno, “KWA JINA LA“, yanamaanisha pia “KUTOKANA NA AGIZO LA“ (MATENDO 4:7; 9:27-29; MATHAYO 18:5; 18:20; YOHANA 5:43; EZRA 5:1).  Maana hii ya maneno haya, ilifahamika sana kueleweka kwa mtu yeyote Nyakati za Biblia, na hivyo hakukuwa na utata kwa watu nyakati hizo.  Hivyo maana ya “wakabatizwa kwa Jina la Bwana Yesu“, maana yake, “WAKABATIZWA KUTOKANA NA AGIZO LA BWANA YESU“, lilelile la MATHAYO 28:19, la kubatiza kwa Jina la Baba, na Mwana na Roho Mtakatifu.  Hivyo hatupaswi kubabaishwa na mafundisho ya WILLIAM BRANHAM, na kuiacha imani.  Vivyo hivyo, tutumie msingi huu kulipima agizo lolote la mtume yeyote

(4)   MKIYAJUA HAYO HERI NINYI MKIYATENDA (MST. 17)

Kujua bila kuyatenda tuliyoyajua katika neno la Mungu, ni kutafuta mapigo zaidi kuliko yale yatakayompata yule asiyejua (LUKA 12:47-48).  Inakuwa heri ni baraka kwetu, tukiyatenda yale tunayoyajua.  Kuja katika mafundisho kila siku na kutamani tu kuongeza maarifa bila kuyatenda tunayojifunza, ni kuongeza dhambi juu ya dhambi na kutafuta mapigo zaidi ya yule asiyejua.  Ikiwa tumekwisha jifunza na kujua mengi, hatuwezi kujirudisha nyuma na kusema hatujui, ili tusipate mapigo zaidi.  Lakufanya, ni kuyatenda kuomba neema zaidi kuyatenda, ili iwe heri kwetu.  Fadhili za Bwana zina wale wanaoyafanya maagizo yake waliyojifunza.  Hawa ndiyo watu wenye akili (ZABURI 103:17-18; MATHAYO 7:24-27; YAKOBO 1:22-25).

(5)   MCHANGANYIKO WA WEMA NA WABAYA KATIKA KANISA (MST. 18-19)

“Aliyekula chakula changu, ameniinulia kisigino chake“, ni maneno yanayotoa mfano wa mnyama farasi. Farasi anaweza kumpiga teke yeye anayempa chakula.  Ndivyo alivyofanya Yuda Iskariote.  Hata leo, kwa msingi huohuo, ingawa katika Kanisa, wote tunakula chakula kilekile cha kiroho pamoja na Yesu, wako wabaya wasiolitenda Neno, watakaoangamizwa kama Yuda (1 WAKORINTHO 10:1-5).  Yesu anatufundisha sisi Wachungaji na Viongozi wa Kanisa kwamba tukihubiri na kufundisha kama Yesu, kutakuwa na Yuda Iskariote mmoja (1) katika 12 au Iskariote wanane (8) katika 100, au 80 katika 1,000 au 800 katika 10,000!  Wote hawawezi kuwa ngano katika Kanisa.  Magugu hayana budi kuwapo mpaka siku ya mwisho (MATHAYO 13:29-30).  Kazi yetu Wachungaji na Walimu, ni kuyapunguza magugu haya kadri iwezekanavyo kwa mafundisho.

(6)   MCHUNGAJI MJUMBE WA MUNGU (MST. 20)

Mchungaji, ni mtu aliyepelekwa kwetu na Yesu (YOHANA 20:21).  Kuyapokea maneno ya Mchungaji, ni kuyapokea maneno ya Yesu, na hivyo kuyapokea maneno ya Mungu.  Tunaweza tukajipima jinsi tunavyompokea Yesu au Mungu tusiyemwona kwa macho, kwa jinsi tunavyompokea Mchungaji wetu.  Tusipomsikiliza na kumtii Mchungaji, tunamuasi Mungu moja kwa moja.  Hatupaswi kufanya hivyo (LUKA 10:16; 1 WATHESALONIKE 2:13; WAGALATIA 4:13-14; FILEMONI 1:21; 2 WAKORINTHO 6:1-15). …………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s