NENO HILI NI GUMU

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

 

SOMO:          NENO HILI NI GUMU

S

iku ya leo ya Kuichambua Biblia, inatupelekea kuzidi kujifunza Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu.  Leo tunajifunza YOHANA 6:60-71, na YOHANA 7:1-16.  Ingawa kichwa scha somo letu la leo ni  “NENO HILI NI GUMU“, kuna mengi zaidi ya kujifunza katika mistari hii, katika vipengele kumi:-

(1)      NENO HILI NI GUMU (6:60-62, 66-69);

(2)      MANENO YA MUNGU NI ROHO, TENA NI UZIMA (6:63-65);

(3)      MMOJA WENU NI SHETANI (6:70-71);

(4)      WAJIBU WA KUKWEPA KUUAWA (7:1);

(5)      MAANA HATA NDUGUZE HAWAKUMWAMINI (7:2-5);

(6)      WAKATI WA YESU TOFAUTI NA WAKTI WETU (7:6);

(7)      KUCHUKIWA KWA MTU ALIYEOKOKA (7:7);

(8)      KWENDA KATIKA SIKUKUU BILA YESU (7:8-10);

(9)      YUKO WAPI YULE (7:11-13);

(10)       KUJUA ELIMU BILA KUSOMA (7:14-16).

 

(1)      NENO HILI NI GUMU (6:60-62, 66-69)

Baada ya Yesu kuwafundisha wanafunzi wake kwamba Yeye ndiye chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni, na kwamba mtu akila mwili wake na kuinywa damu yake ndipo atakapokuwa na uzima wa milele; wanafunzi wengi waliona mafundisho hayo ni magumu.  Wakayanungu’unikia mafundisho hayo na kusema, ni nani awezaye kuyasikia yaani hakuna awezaye kuyafanya au kuyatenda.  Yesu akawaambia, Je, neno hili (mafundisho haya) yanawakwaza?  Kutokana na ugumu waliouona katika mafundisho haya, wanafunzi WENGI, wakarejea nyuma, wasiandamane na Yesu tena.  Wakaamua kumwacha Yesu.  Yesu hakuwabembeleza wala kushusha viwango vya mafundisho yake ili waendelee kumfuata, kinyume chake, aliwageukia na wale mitume Thenashara (12), akawaambia “Je, ninyi nanyi mwataka kuondoka?“  Simoni akamjibu “Twende kwa nani?“  Wewe unayo maneno ya uzima wa milele“.  Maneno ya uzima wa milele ni MAGUMU, na kamwe Yesu hashushi viwango vyake vya kuingia mbinguni.  Chochote kilicho kinyonge kinachoshindwa kuyatenda mafundisho haya, kamwe hakiwezi kuingia mbinguni (UFUNUO 21:27).  Ikiwa sisi ni waalimu au wachungaji tunaomfuata Yesu kama kielelezo chetu, tujifunze hapa kwamba, hatupaswi kushusha viwango vya Neno la Mungu kwa kuhofu kwamba washirika wetu watakimbia na kutuacha!  Wakiondoka na waondoke.  Mtu anayeliacha Kanisa kwa kushindwa kuyatendea kazi maneno magumu huyu siyo mwanafunzi halisi wa Yesu.  Hafai katika ufalme wa mbinguni.  Walitoka kwetu ili wafunuliwe kwamba siyo wote walio wa kwetu yaani siyo wote waliookolewa.  Mtu aliyeokoka, amri za Mungu kwake siyo nzito!  (1 YOHANA 2:19; 5:3-4).  Mtu aliyeokoka, kamwe, hawezi kukwazwa na Neno la Mungu (ZABURI 119:165).  Twende kwa nani?  Tukiliacha Neno kwa kuwa ni gumu na kuwaendea wachungaji wenye kushudha viwango vya Neno la Mungu, tunawaendea WAFARIJI WENYE KUTAABISHA.  Watakufariji leo, halafu kesho tutataabika motoni (AYUBU 16:1-2).  Tukikutana na neno gumu, tukikaribie Kiti cha Neema kwa ujasiri na tumwombe Mungu atupe neema ya kulifanya.  Kwa jinsi hii, Yesu MWENYEWE, atalifanya neno hilo gumu ndani ya mioyo yetu (WAEBRANIA 4:16; 13:20-21; YOHANA 1:16-17; TITO 2:11-12).

 

(2)    NAFASI HII IMEACHWA WAZI KWA  AJILI YA MAANDIKO NA KIPENGELE  HUSIKA.

 (3)     MMOJA WENU NI SHETANI (6:70-71)

Yuda Iskariote, mmoja wa mitume wa Yesu, hapa Yesu anamwita shetani!  Kwa nini?  Wanafiki na wasaliti wa Yesu na Neno lake, hawana ubora wowote kuliko shetani mwenyewe.  Siyo tu kwamba Shetani alimwingia Yuda, bali Yuda anaitwa kuwa naye ni shetani.  Maana mojawapo ya jina Shetani, adui wa Mungu.  Mtu akimwacha Yesu na Neno lake na kuupenda ulimwengu kama Dema (2 TIMOTHEO 4:10), mtu huyo ni rafiki wa dunia na hivyo ni adui wa Mungu (YAKOBO 4:4); kwa jina jingine, ni Shetani!  Mtu aliyekuwa ameokoka halafu akaanguka, ni sawa na shetani aliyekuwa malaika halafu akaanguka.  Bwana ampe neema kila mmoja wetu ili tusiitwe “Shetani“ kwa kuacha Wokovu!  Hapa, Petro alifikiri wote 12 hawawezi kumwacha Yesu pale aliposema “Twende kwa nani?“, kumbe Yesu alijua kwamba siyo wote walio safi.  Mtu kuwa na cheo kikubwa katika Kanisa siyo ushahidi kwamba mtu huyo hawezi kumwacha Yesu!  Anaweza akawa shetani kabisa kama Yuda.

 

(4)      WAJIBU WA KUKWEPA KUUAWA (7:1)

Hatupaswi kujiingiza tu mikononi mwa maadui zetu na kuuawa KABLA ya wakati wetu, kwa visingiziao vya kuwa tayari kufa kwa ajili ya Kristo.  Yesu alipotafutwa kuuawa kabla hajatimiza kazi ya Mungu aliyotumwa kuifanya, alijificha (YOHANA 8:59; 11:53-54).  Hatuna budi kuchukua tahadhari zote ili maadui zetu wasipate nafasi ya kutuua.  Mume asiyeokoka akileta bunduki kutaka kukuua, kimbia na kujificha.  Huu siyo woga!  Hatuna budi kuwa na busara kama nyoka!  Nyoka ni mwepesi sana wa kujificha na kukwepa kuuawa (MATHAYO 10:16).  Tukifukuzwa katika mji mmoja, tukimbilie mji mwingine (MATHAYO 10:23).

 

(5)      MAANA HATA NDUGUZE HAWAKUMWAMINI (7:2-5)

Ishara halisi ya kutomwamini Yesu au kutokuokolewa, ni kumkosoa, kumpa ushauri na kumfundisha Yesu badala ya kutulia na kuongozwa na Neno lake, kama walivyofanya hapa watu hawa.  Tunapoona Neno la Mungu lina makosa na kutaka kulisahihisha, hiyo ni ishara halisi ya kutookolewa.  Nduguze  hawakumwamini Yesu, walikuwa hawajaokoka.  Ukiwa mtoto wa mchungaji, au ndugu yake, hiyo siyo ishara ya kuokolewa.  Kila mtu anasimama peke yake (EZEKIELI 18:20; WAGALATIA 6;5).

 

(6)      WAKATI WA YESU TOFAUTI NA WAKATI WETU (7:6)

“Haujafika bado wakati wangu, ila wakati wenu sikuzote upo“, ni maneno ya Yesu hapa.  Sisi wanadamu, tukitaka kitu au tukimwomba Mungu kitu fulani, huwa tunataka tupewe dakika ileile bila kujua wakti wa Yesu ni fotauti na wakati wetu.  Yeye anajua wakati ulio mzuri wa kutupa kitu fulani.  Tukiwa na subira, hatimaye ndipo tutafahamu ni kwa nini kilichelewa kutufikia.  Ukimpa gari mtoto wa miaka mitano na kumwambia aendeshe, nio kutafuta kumwua.  Utangoja mpaka akue.  Yesu vivyo hivyo anajua wakati unaofaa wa kutupa hiki au kile.  Tunajifunza pia kwamba Yesu hana wakatiwa kupoteza ana ratiba ya shughuli zake na kila wakati ni wa kufanya kazi ya Mungu.  Sisi nasi kama Wakristo, hatupaswi kutumia wakati ovyo na kuupoteza bila kutenda kazi ya Mungu kwa kuomba, kusoma Neno n.k.   Wakati ni mali! (WAEFESO 5:15-16).

 

(7)      KUCHUKIWA KWA MTU ALIYEOKOKA (7:7)

Ikiwa kweli tumeokolewa, na tunazishuhudia kazi za ulimwengu huu ya kuwa ni mbovu; ulimwengu huu yaani watu wa dunia hii (ambao hawajaokolewa), lazima waatuchukia.  Hii ni kawaida ya Ukristo (YOHANA 15:18-19; 17:14; 1 YOHANA 4:5; WAGALATIA 4:28-29).  Tunapaswa kushikilia msimamo wetu wa wokovu kwa gharama yoyote.  Hata tukichukiwa na wazazi, ndugu, mume, mke, marafiki n.k; tusonge mbele! Taji inatusubiri.

 (8)     KWENDA KATIKA SIKUKUU BILA YESU (7:8-10)

Watu hawa (nduguze Yesu), walipenda kufanya kila neno kwa kutafuta kutazamwa na watu na kupenda kujulikana (YOHANA 7:2-4).  Sikukuu ya Vibanda, ilikuwa ni kumbukumbu ya Wana wa Israeli kukaa katika vibanda jangwani na ilikuwa wakati wa kusanyiko kubwa la ibada (WALAWI 23:34).  Watu hawa walikwenda kwenye ibada ili kutafuta kujulikana na kutazamwa.  Hawakuwa na nia ya kujifunza Neno la Mungu.  Yesu aliwaambia waende, lakini hakufuatana nao (YOHANA 7:8-10).  Wako watu wengi wa jinsi hii leo.  Wanakuja Kanisani Jumatatu, Jumatano, Jumapili ili kujionyesha tu.  Hawa wanakuja peke yao bila Yesu!  Yesu hufuatana na wale wanaokwenda katika ibada kufuata Neno la Mungu.

 

(9)      YUKO WAPI YULE (7:11-13)

Watu hawa walishindwa kusema “Yuko wapi Kristo au Yesu“.  Kusema hivyo kungekuwa kukubali kuwa ni Mwokozi na Masihi.  Wengine walimwona Yule ni mtu mwema tu na siyo Mwana wa Mungu, wengine waliona kuwa anawadanganya watu!  Siyo ajabu sisi nasi yakitupata.

 

(10)    KUJUA ELIMU BILA KUSOMA (7:14-16)

Yesu Kristo hakusoma popote duniani, lakini mafunzo yake yalitoka kwa Mungu!  Hatupaswi kujidharau kwa kuwa hatujasoma shule za duniani au vyuo vya Biblia.  Tunaweza tukatumiwa kama Petro na Yohana (MATENDO 4:13).  Ikiwa tumesoma pia tujifunze kumtanguliza KWANZA, Roho Mtakatifu.

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s