NGAMIA KUPITA KATIKA TUNDU LA SINDANO

 

 

 

 

 

 

 

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

SOMO:     NGAMIA KUPITA KATIKA TUNDU LA SINDANO

Leo, tunajifunza Biblia kutoka katika MATHAYO 19:16-30.  Kwa wakati mmoja pia, tutayalinganisha maandiko haya na yale ya MARKO 10:17-31 na LUKA 18:18-30; ili kupata yote tunayotakiwa kujifunza katika somo letu la leo.  Tutayagawa mafundisho yetu ya leo tunayoyapata katika MATHAYO 19:16-30, katika vipengele sita:-

(1) KUJARIBU KUINGIA MBINGUNI KWA KUFANYA MEMA (MST. 16-21);

(2) JINSI YA KUWA MKAMILIFU (MST. 20-21);

(3) JINSI ILIVYO SHIDA KWA TAJIRI KUINGIA KATIKA UFALME WA MBINGUNI (MST. 22-24);

(4) YOTE YAWEZEKANA KWA MUNGU (MST. 25-26);

(5) THAWABU ZA MTU ANAYEACHA VYOTE NA KUMFUATA YETU (MST. 27-29);

(6) WA KWANZA KUWA WA MWISHO NA WA MWISHO KUWA WA KWANZA (MST. 30).

 

(1)      KUJARIBU KUINGIA MBINGUNI KWA KUFANYA MEMA (Mst. 16-21)

Hapa tunajifunza juu ya mtu mmoja ambaye alifundishwa kutenda mema tangu utoto wake na akafanya yote yaliyoelekezwa kuyatenda kutokana na jitihada zake.  Akawa amezishika amri za Mungu tangu utoto wake (LUKA 18:21), na kuona kwamba hakuna jingine alilopungukiwa ili kuurithi uzima wa milele.  Ni kweli kabisa kwamba alizishika amri, hata Yesu alithibitisha hivyo lakini katika kipimo cha Mungu, akaonekana bado AMEPUNGUKIWA NA NENO MOJA (LUKA 18:22).  Hakuwa na sifa ya kuingia mbinguni kutokana na mema aliyoyatenda.  Mbele za macho ya Mungu, hakuna mwanadamu mwema hata mmoja.  Mwema ni Mungu peke yake.  Hapa Yesu anamwambia kwamba ikiwa anamwita mwema, basi hiyo inathitibisha kwamba Yesu ni Mungu (LUKA 18:18-19).  Matendo yoyote mema ambayo atayafanya mwanadamu kwa jitihada zake binafsi, ni kama nguo iliyotiwa unajisi (ISAYA 64:6), hayafai lolote katika kumpa sifa ya kuingia mbinguni.  Mbele za Mungu, wanadamu WOTE kwa kuzaliwa na kutenda, ni wenye dhambi (ZABURI 51:5; 58:3; AYUBU 25:4; MHUBIRI 7:20; WARUMI 3:10-12, 23).  Mwanadamu yeyote hata akijitahidi namna gani kuzishika amri za Mungu kwa nguvu zake tu, bado atakwenda tu Jehanum.  Ni kutaabika BURE (AYUBU 9:29-31).  Huu ndiyo msingi ulio batili wa taratibu nyingi za kidini za wanadamu – kujaribu kuingia mbinguni kwa kufanya mema fulani.

(2)      JINSI YA KUWA MKAMILIFU (Mst. 20-21)

Mtu akitaka kuwa mkamilifu na kuwa na sifa ya kuingia mbinguni, sharti AUZE VYOTE ALIVYO NAVYO na kuwapa maskini.  Kitu ukikiuza, hakiwi chako tena.  Inampasa mtu auze “VYOTE“, vifuatavyo, na kuwa mbali navyo:-

 1. 1.     Auze namna zote za kujihesabia haki kutokana na matendo yoyote mema ya kidini aliyoyafanya, iwe ni kubatizwa utotoni, kupata kipaimara, kufunga mara mbili kwa juma, kutoa zaka katika mapato yake yote, kutokuiba au kutokufanya uasherati tangu utotoni, kutokulewa au kutokuvuta sigara tangu utotoni n.k., na kukubali kubaki bila kitu kwa kukiri kwamba yeye ni mwenye dhambi (LUKA 18:9-14).
 2. 2.     Auze namna yoyote ya kudhani anaweza kufanya lolote lililo jema kwa Mungu pasipo kuwezeshwa na Mungu mwenyewe.  Auze namna yoyote ya kutumainia akili zake, nguvu zake, uwezo wake, maarifa yake na elimu yake katika kutenda lolote lililo jema kwa Mungu na kukubali kubaki bila kitu kwa kukiri kwamba hawezi lolote bila msaada wa Yesu Kristo (YOHANA 15:5; WAFILIPI 4:13; AYUBU 26:2).  Wako watu wengine wanadai wameokoka, lakini wanajaribu kufanya kila kitu kwa nguvu zao na bila kutumainia msaada wa Yesu Kristo yaani neema ya Mungu.  Wanajaribu kuomba, kushuhudia, kufuatilia watoto wachanga kiroho, kutoa ushauri kwa wengine kutenda kazi ya Mungu kwa nguvu zao tu na maarifa yao!  HUU SIYO WOKOVU!
 3. 3.     Auze namna yoyote ya kuenenda kwa kuona na kukubali kubaki bila kitu kinachoonekana kwa macho.  Atubu dhambi zake zote kwa kumaanisha kuziacha kabisa, na kwa IMANI aamini mara moja kwamba amehesabiwa haki ya kuingia mbinguni kwa kuziamini AHADI za Mungu kwake (2 WAKORINTHO 5:7; WARUMI 3:28; ISAYA 55:7; 1 YOHANA 1:809; MITHALI 28:13; MATENDO 3:19).

(3)      JINSI ILIVYO SHIDA KWA TAJIRI KUINGIA KATIKA UFALME WA MBINGUNI (Mst. 22-24)

Itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni.  Ni rahisi zaidi au ni vyepesi ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu (LUKA 18:25).  Miji ya nyakati za Biblia ilizungushiwa ukuta uliokuwa na lango kubwa lililotumika kuingia mjini (LUKA 7:11-12; YOSHUA 8:29).  Lango hili lilikuwa na KILANGO CHA LANGO (MATENDO 12:13).  Kilango hiki cha lango, ni mlango mdogo uliounganika na lango kubwa.  Aidha unaweza ukafungua lango kubwa pamoja na kilango chake au ukafunga lango kubwa na kufungua kilango chake tu.  Ni kama jinsi ambavyo ilivyo kwetu leo.  Kunakuwako lango kubwa la kupitisha watu tu tena wakati mwingine kwa kuinama.  Kilango hiki cha lango, nyakati za Biblia, ndicho kilichokuwa kinajulikana kwa jina “TUNDU LA SINDANO“.  Lango kubwa la mji lilipofunguliwa, watu waliingia na ngamia wenye mizigo mingi kwa urahisi tu, lakini lango kubwa lilipofungwa na kufunguliwa kilango chake tu, ilikuwa ni shida sana kwa ngamia mwenye mizigo kupita.  Kwa shida sana, ngamia wengine walipiga magoti na kutembea kwa magoti, na mtu akahangaika sana mpaka kufaulu kumpitisha ngamia mmoja mwenye mizigo kwenye kilango cha lango.  Sasa hapa tajiri mwenye mali nyingi anafananishwa na ngamia.  Ngamia hubeba mizigo ambayo siyo mali yake mwenyewe bali ya wengine, hatimaye hutua mizigo na kubaki tupu.  Wenye mali wakaichukua.  Ndivyo alivyo tajiri yeyote.  Anapokufa, hutua mali zote alizokuwa amebeba na kwenda akiwa tupu kabisa (ZABURI 49:16-17).  Kilango cha lango ni njia nyembamba iliyosonga iendayo uzimani, (MATHAYO 7:14).  Ni shida sana kwa tajiri kuingia uzimani, kutokana na dhambi zifuatazo zinazomzinga kwa upesi:-

 1. Kuwadhulumu maskini ili awe tajiri zaidi (YAKOBO 5:1-4; YEREMIA 22:13; 1 TIMOTHEO 6:9-10);
 2. Kutokuona “faida“ ya “kuhangaika“ na mambo ya Mungu (AYUBU 21:14-15);
 3. Kuweka tumaini lake katika fedha na mali, kwamba zinaweza kufanya lolote na kwamba hakuna haja ya kumwomba Mungu (AYUBU 31:24-25, 28; MITHALI 18:11; 1 TIMOTHEO 6:17);
 4. Kujivuna kwa sababu ya utajiri, na kuona wengine wote hawafai (1 TIMOTHEO 6:17);
 5. Kujisifu kwa utajiri wake badala ya kujisifu kwa sababu anamfahamu Mungu awapaye watu nguvu ya kupata mali na utajiri (YEREMIA 9:23-24; TORATI 8:17-18);
 6. Kuvutwa kufanya anasa, uasherati na uzinzi n.k; kutokana na uwezo wake wa kifedha na mali (YEREMIA 5:7-9; YAKOBO 5:1,5);
 7. Tamaa ya kupata fedha na mali zaidi, inayomfanya kukosa hata muda wa kuhudhuria katika ibada, kusoma Neno, kuomba na kutenda kazi ya Mungu (MATHAY6O 13:22);
 8. Kutokuwa na utayari wa kutoa mali zake kwa wingi kama alivyopewa, kwa ajili ya kazi ya Mungu.  Aliyepewa vingi, vitatakwa vingi kwake pia (1 TIMOTHEO 6:18-19; LUKA 12:48).

 

(4)      YOTE YAWEZEKANA KWA MUNGU (Mst. 25-26)

Wanafunzi wa Yesu waliposikia mafundisho yake juu ya tajiri walishangaa na kusema nani basi ataokoka, kwa maana kwamba KILA TAJIRI atakwenda motoni.  Yesu akawakazia macho, akawaambia, kwa wanadamu hilo haliwezekani, bali kwa Mungu yote yawezekana.  Siyo kwamba Mungu hapendi watu tuliookoka tuwe matajiri, anapenda mno, ila tu tuwe matajiri kwa kutenda mema yanayopendeza (1 TIMOTHEO 6:18).  Ibrahimu mtu wa imani, alikuwa tajiri aliyebarikiwa katika vitu vyote (MWANZAO 13:2; 24:1).  Ayubu alikuwa mkamilifu na uelekevu, mmoja aliyemcha Mungu na kuepukana na uovu; na hakuwa na mfano wake katika dunia ya nyakati zake, lakini alikuwa tajiri (AYUBU 1:1, 3, 8).  Yusufu wa Arimathaya, mwanafunzi wa Yesu aliyelitoa kaburi lake jipya ili azikiwe Yesu, alikuwa ni tajiri pia (MATHAYO 27:57-60).  Jambo la muhimu ni kumtumaini Yesu kwamba atatupa neema ya kushinda dhambi zinazomzinga tajiri maana yasiyowezekana kwetu, yawezekana kwa Mungu.  Hakuna haja ya kuzitegemea akili zetu kupata utajiri kwa kujitaabisha kufanya yasiyompendeza Mungu (MITHALI8 23:4).  Jambo la muhimu la kukumbuka, kuliko kuwa tajiri na kwenda Jehanum, ni heri kuwa na maombi ya MITHALI 30:7-9.

 

(5)      THAWABU ZA MTU ANAYEACHA VYOTE NA KUMFUATA YESU (Mst. 27-29)

Mtu yeyote aliyeacha nyumba, ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, watoto au mashamba kwa ajili ya kumfuata Yesu, na kwa ajili ya Injili atapokea MARA MIA sasa wakati huu ndugu wengi waliookoka, na mahitaji yake aliyoyapata kutokana na mashamba, ingawa hayo yataambatana pia na UDHIA mara mia moja katika ulimwengu huu na pia atapokea mara mia katika ulimwengu ujao (MARKO 10:28-30).  Kuna heshima ya pekee kwa kila mtu anayekubali kuifuata kweli na kuwa wa mwanzo kwa mfano katika Kanisa lenye watu wachache lisilokubalika kwa wengi (Mst. 28).

 

(6)      WA KWANZA KUWA WA MWISHO NA WA MWISHO KUWA WA KWANZA (Mst. 30)

Umaliziaji katika wokovu ni wa muhimu zaidi kuliko uanzaji.  Yuda na Dema, wote walianza vizuri wakashindwa kumalizia vizuri.  Kamwe, tusijione tunajua (1 WAKORINTHO 8:1-2), wala tusijione kuwa tumefika (WAFILIPI 3:12-15).

 

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s