NITAMPIGA MCHUNGAJI

Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

TovZACHARY KAKOBEuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

SOMO:      NITAMPIGA MCHUNGAJI

Leo, tunajifunza Biblia kutoka MATHAYO 26:31-46.  Ingawa kichwa cha somo letu ni, “NITAMPIGA MCHUNGAJI”, kuna mengi zaidi ya kujifunza katika mistari hii.  Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika mistari hii, katika vipengele vitano:

(1)            UMUHIMU WA KUJIANDAA KWA AJILI YA MATUKIO YA GHAFLA (MST. 31);

(2)            NITAMPIGA MCHUNGAJI (MST. 31);

(3)            YEYE ASIYETUACHA TUNAPOMWACHA (MST. 32);

(4)            HATARI YA KUACHA KUITUMAINIA NEEMA YA MUNGU (MST. 33-35);

(5)            MAFUNDISHO TUNAYOPATA KWA YESU NA WANAFUNZI WAKE KATIKA BUSTANI YA GETHSEMANE (MST. 36-46).

 

(1)      UMUHIMU WA KUJIANDAA KWA AJILI YA MAMTUKIO YA GHAFLA (MST. 31)

Hapa tunaona jambo la ajabu likitokea ghafla.  Muda mfupi uliopita, wanafunzi walikuwa wanaila Pasaka pamoja na Yesu na kisha wakamalizia kwa kuimba pamoja kwa furaha (MST. 26-30).  Baada tu ya kuimba, waktoka nje kwenda mlima wa Mizeituni.  Wakati huu, ni wakati wa usiku sasa, kwa sababu waliila Pasaka wakati wa jioni.  Hata hivyo, ni wakati wa mbalamwezi, kwa sababu Pasaka ilikuwa inafanyika wakati wa mwezi mpevu.  Sasa, kwa ghafla, Yesu anawaambia wanafunzi wake, “Ningi nyote MTACHUKIZWA kwa ajili yangu USIKU HUU”.  Neno “KUCHUKIZWA” hapa, lina maana “KUTIWA UCHUNGU”, KUPATA JAMBO BAYA; “KUUMIZWA” au “KUUDHIWA”.  Na kweli, usiku uleule jambo baya la huzuni likawatokea.  Hapa tunajifunza jambo kubwa.  Wanadamu, hatujui mambo yajayo.  Tunaweza tukawa katika furaha kubwa sasa, lakini likatupata jambo baya saa moja tu ijayo.  Tunaweza tukatoka asubuhi nyumbani kwa furaha, kwa lengo la kwenda kazini, lakini tukapata ajali kabla ya kufika kazini na kufa papo hapo.  Tunaweza tukawa wajawazito na tukafurahi, lakini wakati wa kwenda kujifungua, tukafa.  Tunaweza tukalala usiku kwa furaha na usiku huo nyumba zetu zikavunjwa na wezi na tukaibiwa vitu vyote na kukatwa mapanga.  Hatujui yatakayozaliwa katika muda mfupi ujao (MITHALI 27:1; YAKOBO 4:13-16).  Kwa sababu hii, ni muhimu kuihakikisha tumejiandaa, ili tusipatwe na matukio ya ghafla bila maandalizi; kwa kufanya yafuatayo:-

 1. Kamwe tusiahirishe siku ya kupokea wokovu.  Tuhakikishe tunatubu dhambi zetu mara moja na kuokolewa SASA.  Tukisema tutaokoka tukijenga nyumba kama fulani au “tukistarehe” kwanza, tunaweza tukawa tunajidanganya kabisa na tukajikuta tumekufa USIKU HUU!  Wakati uliokubalika wa wokovu ni SASA (2 WAKORINTHO 6:2);
 2. Fedha tunazojiwekea akiba, hutusaidia wakti tunapopatwa na matukio ya ghafla.  Vivyo hivyo, tukiwa watu wa maombi kila siku, maombi hayo huwa akiba kwetu kwa ajili ya kupambana na matukio ya ghafla.  Kuombwa kwa mwenye haki kwafaa sana akiomba kwa bidii (YAKOBO 5:16).

 

(2)      NITAMPIGA MCHUNGAJI (MST. 31)

Hapa tunajifunza mambo mawili yafuatayo:

 1. Mchungaji anayetajwa hapa kwamba atapigwa, ni Yesu Kristo.  Kupigwa kwake, kunatimiliza unabii wa ZEKARIA 13:7.  Katika mstari huu, Mungu Baba anamwita Yesu “MCHUNGAJI WANGU” na tena “MTU ALIYE MWENZANGU”.  Yesu ni zaidi ya Mtume yeyote.  Yesu na Baba ni Umoja.  Yesu ni Mungu (YOHANA 10:30-36).  Yesu ni mwenzake baba.  Kama Yesu alivyomwita Baba, Mungu wangu (MATHAYO 27:45),  Baba naye anamwita “Mchungaji wangu”.  Mwanadamu au malaika yeyote hawezi kuwa Mchungaji wake Mungu baba.  Hivyo ni dhahiri kwamba Yesu ni zaidi ya malaika au mwanadamu yeyot.  Yesu ni Mungu.
 2. Wakati wote Shetani hulenga kumpiga Mchungaji, ili kondoo walio chini ya uongozi wake watawanyike.  Furaha ya Shetani inatimilika anapompiga kiongozi wetu mkuu.  Anajua akipigwa huyo basi, kondoo wote watatawanyika.  Lengo kuu la Shetani, siyo kumpiga mshirika wa kwaida wa Kanisa, wala Kiongozi wa Kanisa la Nyumbani au Kiongozi wa Zoni.  Analenga kumwangamiza Mchungaji wetu, na anamtafuta wakati wote (1 WAFALME 22:31-33).  Mchungaji wetu ana shughuli nyingi, na Shetani atamvizia anapokuwa amechoka na kuwa dhaifu, na kumshambulia, akijua kwamba kwa kufanya hivyo kondoo wote watakata tama na kutawanyika ( 2 SAMWELI 17:1-2).  Ni muhimu kwa kila mmoja katika Kanisa kufahamu kwamba Mchungaji wetu ni wa thamani kuliko “watu elfu kumi katika sisi”, walio washirika wa kawaida.  Taifa la Israeli kama Kanisa, liliifahamu siri hiyo ya ushindi, na kujua kwamba akipigwa Mchungaji wao, TAA YAO ITAKUWA IMEZIMIKA ( 2 SAMWELI 18:1-3; 21:15-17).  Ni muhimu kwa kila mmoja wetu, kushindana, na kuwa kinyume na yeyote anayetaka kumwua Mchungaji wetu kwa kumsema vibaya au kumhabiria sifa.  Ikiwa tutakaa kimya tu au kuunga mkono pale Mchungaji wetu anaponenewa mabaya, tutakuwa tunatafuta hukumu ya  kushindwa KUMLINDA MASIHI WA BWANA (1 SAMWELI 26:13-16).  Vile vile ni lazima tukumbuke wajibu wa kila mmoja wetu KUMWOMBEA MCHUNGAJI KILA SIKU, ili asipigwe, na kondoo wote tukatawanyika.  Pamoja na karama mbalimbali zinazotenda kazi kwake na kuwa msaada kwetu, ni muhimu kukumbuka kwamba, bila maombi yetu, ana nafasi ya kusahmbuliwa na kupigwa.  Kwa sababu hii, Mtume Paulo alihitaji mno maombi ya kondoo wake (WARUMI 15:30-31; 1 WATHESALONIKE 5:25, 2 WATHESALONIKE 3:1-2).  Tukiacha kumwombea Mchungaji wetu, basi tunampa nafasi Shetani kuzima uamsho kati yetu.

 

(3)      YEYE ASIYETUACHA TUNAPOMWACHA (MST.32)

Baada ya Mchungaji Yesu kupigwa, wanafunzi wake wote walimwacha, wakakimbia (MST.56-57).  Lakini, kabla ya haya kutokea, tayari anawaambia ingawa mtaniacha, mimi sitawaacha, nitakutana nanyi Galilaya baada ya kufufuka.  Wanafunzi walimwacha hata wakarudia kuvua samaki, lakini yeye hakuwaacha, aliwatafuta na kuzidi kuwaonyesha upendo (YOHANA 21:2-6).  Sisi nasi, tujifunze kuwaonyesha upendo wote waliotuacha kwa sababu moja au nyingine.  Tena, kwa nini tumwache Yesu asiyeweza kutuacha kwa upendo wake?  Kwa nini tumhuzunishe kwa kuacha wokovu?

 

(4)      HATARI YA KUACHA KUITUMAINIA NEEMA YA MUNGU (MST. 33-35)

Petro aliitumainia nafsi yake na kujiona bora kuliko wengine wote, labda kwa jinsi alivyokuwa karibu na Yesu kuliko wengine.  Akapiga kifua na kusema kwa lolote hata kufa, hawezi kumwacha au kumkana Yesu.  Matokeo yake?  Aliyejifanya wa kwanza ndiye aliyekuwa wa mwisho.  Yeye, alimkana Yesu mara tatu, tofauti na wenzake (MATHAYO 26:69-75).  Ni muhimu kujua kwamba Mungu hapendezwi na yeyote anayejitumainia nafsi yake.  Mtu wa namna hiyo, Mungu humwacha.  Tusiwe weesi kuona makosa ya wenzetu tu na kudhani sisi hatuwezi kuanguka.  Bila neema ya Mungu, sisi hatuwezi kufanya lolote, tutakuwa wabaya kuliko yeyote mwingine (YOHANA 15:5; WAGALATIA 6:1; 1 WAKORINTHO 15:8-10; 2 WAKORINTHO 1:8-9).  Tunaweza kuendelea katika wokovu, au katika utumishi wa Mungu, kwa kuitumainia tu neema ya Mungu wakati wote.  Neno “Neema” lisitoke vinywani mwetu (YOHANA 1:16-17).

 

(5)      MAFUNDISHO TUNAYOYAPATA KWA YESU NA WANAFUNZI WAKE KATIKA BUSTANI YA GETHSEMANE (MST. 36-46)

 • Neno, “GETHSEMANE”, maana yake “MASHINE YA KUKAMLIA MAFUTA”.  Yesu, katika Bustani ya Gethsemane, alikamuliwa mafuta ya kutufaa sisi.  Mafuta hulainisha, huifanya ngozi kupendeza, hunenepesha, hufanya chakula kiwe kizuri n.k. Sisi tuliokuwa wabaya, hatufai, tumefanywa wazuri kwa mafuta ya Yesu yaliyokamuliwa Gethsemane (ZABURI 45:7; EZEKIELI 16:8-9; WAEBRANIA 1:9);
 • Yesu aliwatenga Petro, Yakobo na Yohana mara kwa mara mbali na wanafunzi wengine (MST. 36-37: 17:1).  Makusudi yake ilikuwa kuwatayarisha kuwa nguzo (WAGALATIA 2:9).  Tukitengwa mbali na wengine na Kiongozi wetu, tujue tumepewa neema ya kutayarishwa kwa huduma iliyo kubwa.
 • Yesu alihuzunika kiasi cha kufa.  Ilikuwa ni wakati wa mapambano na mamlaka yote ya giza ya Shetani aliyemwangusha Adamu (LUKA 22:53; YOHANA 14:30-31).  Katika mapambano hayo, Shetani alitupwa nje (YOHANA 12:31).
 • Pamoja na amteso kuwa makali, Yesu aliyaita “kikombe cha mateso“ siyo bahari, mto au ziwa la mateso (MST. 39).  Hatupaswi kamwe kuyainua mateso au kazi za Shetani, bali kuzidharau.  Hiyo ndiyo siri ya ushindi.  Shetani hana kitu kwetu kwa Jina la Yesu (MST. 40-41).
 • Aliomba, ikiwezekana mpango wa wokovu kutimizwa bila huzuni hiyo, iwe hivyo, lakini mara moja alisema mapenzi ya Baba yatimizwe (MST. 42).  Ni muhimu kujitia katika mapenzi yake Mungu.
 • Miili yetu ni dhaifu.  Tusijifanye watu wa kiroho sana na kusahau kwamba tuko katika kmiili dhaifu, Ni lazima tuwe na vipindi vya kulala na kupumzika, na pia kula vizuri ili tushinde mapambano ya Shetani.  Adui hutuonea tunapokuwa dhaifu (MST. 45; MARKO 6:30-32).
 • Kwa kawaida, wengi wetu tunapokuwa na huzuni au mateso na tukaona wale tunaowatazamia kutusaidia au kuwa pamoja nasi hawatujali, tunajaa hasira.  Yesu hakuwa hivi.  Aliteswa mwenyewe na akawaambia wanafunzi wakeshe naye wakawa wanalala tu.  Hakuwafokea bali alizidi kuwapenda, na hatimaye akawatia moyo kulala (MST. 40, 44-45).  Tumwombe Mungu atupe neema hii ya kutokunung’unika kwa sababu watu hawatujali, na tuwe wa kumtumaini Mungu tu katika hali hiyo.

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s