NURU HALISI

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

MAFUNDISHO YA

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA (S.K.B.) – KITABU CHA YOHANA

SOMO:  NURU HALISI

L

eo, tunaanza kujifunza Kitabu cha YOHANA.  Kuna mengi mno ya kujifunza katika Kitabu hiki.  Leo tunaanza kukichambua Kitabu cha YOHANA kwa kuangalia YOHANA 1:1-14.  Katika mistari hii, pamoja na mambo mengine, tutajifunza juu ya NURU HALISI.  Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika mistari hii katika vipengele sita:-

(1)NENO ALIKUWA MUNGU (Mst. 1-5);

(2)YOHANA, MTU ALIYETUMWA KUTOKA KWA MUNGU (Mst. 6-8);

(3)NURU HALISI (Mst. 9-10);

(4)UWEZO WA KUFANYIKA WATOTO WA MUNGU (Mst. 11-12);

(5)KUZALIWA MARA YA PILI (Mst. 13);

(6)NENO ALIFANYIKA MWILI (Mst. 14).

 

(1)                        NENO ALIKUWA MUNGU (Mst. 1-5)

“Neno“ linalotajwa hapa, siyo “neno“ la kawaida linalomaanisha usemi.  Hapa Neno ni nafsi aliye hai kwa sababu ya maneno yanayoambatana na Neno –  “KULIKUWAKO“, “ALIKUWAKO, “ALIKUWA“, na “HUYO“.  Kama “Neno“ hapa lingekuwa maana yake ni usemi, yangetumika maneno “LILIKUWAKO“, “LILIKUWA“ na “HILO““NENO“ anayetajwa katika mistari hii ni Yesu Kristo.  Yesu Kristo, anaitwa NENO au NENO LA MUNGU (Angalia 1 YOHANA 5:8; 1 YOHANA 1:1; UFUNUO 19:13).  Yesu Kristo alikuwapo tangu zamani za mwanzo, hakuanzia alipozaliwa na Mariamu (MIKA 5:3; YOHANA 8:58).  Kabla ya kuja duniani na kuzaliwa na Mariamu alikuwako.  Neno huyu au Yesu Kristo ni Mungu.  Vyote vilivyoumbwa, vilifanyika kwa Neno au kwa Yesu.  Mungu aliumba mbingu na nchi kwa Neno la Bwana, Yesu Kristo (ZABURI 33:6; WAKOLOSAI 1:13-18; WAEBRANIA 1:2; 1 WAKORINTHO 8:6).  Siyo kwamba Mungu alimtumia Yesu kama chombo cha kuufanya ulimwengu kama mtu anavyotumia shoka, LA HASHA!  Baba na Neno na Roho Mtakatifu ni umoja (1 YOHANA 5:8).  Neno huyu ni Mwana, YESU KRISTO (MATHAYO 28:19).  Neno alikuwa Mungu.  Yesu Kristo ni Mungu (TITO 2:13).  Yesu aliumba ulimwengu na vyote vilivyomo.  Muumbaji ni Mungu (YEREMIA 10:10-12).  Ndani ya Yesu ndimo ulimokuwa uzima maana yake Yeye niye CHANZO cha uzima wa viumbe (MWANZO 1:20; 2:7).  Ule uzima ulikuwa nuru ya watu (MST. 4) maana yake nini?  Pumzi ya mwanadamu au uzima wetu, ndiyo taa ya BWANA aliyotupa kutuwezesha kupeleleza yote (MITHALI 20:27).  Uzima ndiyo unaotupa akili ya kupambanua mema na mabaya kama kwa kutumia nuru.  Kiumbe kisicho na uzima hata kama kina macho, hakina nuru, yaani hakina akili wala ufahamu wa kupeleleza mambo na kuyajua.  Nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza.  Giza linahusishwa na mabaya, maovu au dhambi; na nuru kuhusishwa na matendo mema  (YOHANA 3:17-21; 1 YOHANA 1:5-7).  Yesu Kristo ni nuru ambayo haikuwezwa na giza yaani dhambi.

(2)                        YOHANA, MTU ALIYETUMWA KUTOKA KWA MUNGU (Mst. 6-8)

Hapa Neno la Mungu linatufundisha tofauti kati ya Yohana Mbatizaji na Yesu Kristo.  Jina, “YOHANA” maana yake, “YEYE AMBAYE BWANA AMEMTOA KWA NEEMA”.  Yohana alitolewa na Bwana kwa neema, na ni tofauti kabisa na Yesu Kristo.  Yesu ni Neno ambaye ni Mungu bali Yohana ni MTU aliyetumwa kutoka kwa Mungu.  Mungu huwatumia watu kuwa wajumbe wake, tunapokea kutoka kwa Mungu (MALAKI 2:7).  Pamoja na kwamba wachunaji ni watu kama Yohana, waliotumwa na Mungu kwetu, tunaposikia maneno kutoka kwao, siyo maneno ya watu bali ya Mungu aliyewatuma.  Yohana Mbatizaji, alikuja kwa ushuhuda  (MST. 7).  Wakati wa Agano la Kale, Mungu alitumia “maskani ya ushuhuda” – KUTOKA 38:21; “mbao mbili za ushuhuda” – KUTOKA 31:18: “sanduku la ushuhuda” – KUTOKA 40:21, n.k.  Sasa, anaamua kumtuma MTU kuwa ushuhuda.  Huyu anakuja tena kuishuhudia ile nuru Yesu Kristo.  Yohana siye nuru bali nuru ni Yesu Kristo.  Yohana alikuwa kama nyota ile ya mashariki iliyowaongoza mamajusi mpaka alipokuwapo Yesu.  Mtumishi yeyote wa Mungu, yeye siye nuru bali ni nyota inayotuongoza kwa yeye aliye nuru Yesu Kristo.

 

(3)                        NURU HALISI (Mst. 9-10)

Nuru halisi ni Yesu Kristo.  Ingawa Yohana Mbatizaji ni nyote inayowapeleka watu kwa Yesu, yeye ni nuru ndogo sana ukimlinganisha na Yesu aliye Nuru halisi.  Kwa jinsi ambavyo Yesu ni Mwumbaji.  Yeye ndiye ambaye anayewatia wau nuru au akili na ufahamu wa mambo yote.  Injili ya Yesu, ni habari njema kwa ulimwengu waote, lakini mahubiri ya Yohana Mbatizaji yalikuwa kwa waliokuwa Yerusalemu, na Uyahudi wote, na nchi zote za kandokando ya Yordani (MATHAYO 3:5).  Ukilinganisha nuru ya Yohana na nuru ya Yesu, nuru ya Yohana ni kama mshumaa unaoangaza katika chumba kimoja, lakini nuru ya Yesu ni kama jua linalomuangazia kila mtu anayefumbua macho yake.  Mafunuo ya Mungu sasa ni kwa watu wake wote waliomo nyumbani, Wayahudi na Mataifa na siyo kwa Wayahudi peke yao (MATHAYO 5:15).  Yesu Kristo anafananishwa na nuru iliyochomoza na kulitenga giza wakti wa kuumbwa ulimwengu (MWANZO 1:1-3).  Yesu Kristo alikuja kama Nuru halisi iliyotupa nje giza la dhambi lililokuwa limeufunika ulimwengu.  Alikuwako ulimwengunbi (MST. 10), pale alipokuja ulimwenguni, hatimaye aliuacha ulimwengu na kwenda kwa Baba (YOHANA 16:28).  Yesu alipokuja katika ulimwengu aliouumba, sisi aliotuuumba hatukumtambua!  Ni huzuni kubwa.  Ng’ombe amjua bwana wake lakini sisi hatukumjua (ISAYA 1:2-3).

(4)                        UWEZO WA KUFANYIKA WATOTO WA MUNGU (Mst. 11-12)

Yesu alikuja kwake (kwa ulimwengu) wala “alio wake“ hawakumpokea.  Walio wake wanaotajwa hapa ni Waisraeli au Wayahudi ambao walihesabiwa kuwa taifa la Mungu lililokuwa tofauti na mataifa yote mengine (KUMBUKUMBU LA TORATI 4:7-8); 2 SAMWELI 7:23), KUTOKA 19:3-5).  Katika hali ya kawaida, ingefikiriwa kwamba Waisraeli ndiyo ambao wangekuwa wa kwanza kumpokea Yesu kama taifa lote, lakini haikuwa hivyo.  Wao walikuwa na Torati iliyomnena mno Yesu, walikuwa wamesikia sana juu ya unabii unaomtaja waziwazi kwamba atatokea Bethlehemu na atazaliwa na bikira, n.k.  Alijitambulisha kwao kwa ishara na maajabu, hata hivyo hawakumpokea.  Isitoshe, wakuu wa makuhani ambao walitoka katika kabila ya LAWI waliitwa kabila la Mungu (KUMBUKUMBU LA TORATI 18:1-5).  Ungewaza kwamba hawa wangemheshimu Mungu wao, na kumpokea Yesu kabla ya yeyote mwingine; lakini haikiwa hivyo.  Wao ndiyo waliokuwa msitari wa mble katika kumkataa, kumpinga na kumsulibisha Yesu.  Ndiyo ilivyo na leo.  Katika hali ya kawaida ni rahisi kufikiri kwamba watu wenye majina yaliyomo katika Biblia na wanaojiita wakristo, kama akina Paulo, Emmanuel, Mary, Elizabeth, Danieli, Daudi au David, Anna, Filipo au Phillip n.k; walikulia katika madhehebu ya kikristo na kushika Biblia tangu utotoni, wangekuwa wepesi kumpokea Yesu na kuokolewa, kuliko Waislamu, Wapagani, Wahindu, Wabudha n.k; lakini ni kinyume.  Wengi wao ndiyo wapinzani wakubwa wa wokovu kama watu wa kabila ya LAWI.  Wanatumia madhabahu kuhubiri kwamba “Hakuna kuokoka duniani!“  Mtu anjiita Mkristo, wakati anakataa kuokoka, yuko miongoni mwa “walio wake ambao hawakumpokea“.  Yesu anabisha mlango wa kila moyo wa mtu, na yeye anayemkaribisha na kumpokea, anampa uwezo wa kufanyika mtoto wa Mungu (UFUNUO 2:20; YOHANA 1:12).   Katika hali ya kawaida, mtoto anatarajiwa kuyasikia maneno ya baba yake na kuyatii mara moja.  Nyakati za Biblia, mtoto ambaye alikuwa mwana mkaidi, mshupavu, asiyetii sauti ya baba yake alipigwa mawe hata akafa (KUMBUKUMBU LA TORATI 21:18-21).  Mtu yeyote hawezi kuwa kweli mtoto wa Mungu anayeyasikia maneno yake na kuyatii mara moja mpaka apewe uwezo wa kufanyika mtoto wa Mungu UWEZO huo ndio unaomuwezesha kuyasikia maneno ya Mungu na kuyatii.  Kwa kuzaliwa kila mtu ni mtoto wa Ibilisi, hawezi kuyafanya yanayompendeza Mungu (ZABURI 51:5; YOHANA 8:44; 1 YOHANA 3:10).  Hatuwezi kuokolewa na kufanya yanayompendeza Mungu kwa kutumia nguvu zetu tu, bali kwa KUWEZESHWA na Yesu pale tunapokuja kwake kwa toba tukiwa tumemaanisha kuacha dhambi kabisa (WAKOLOSAI 1:10-11; MITHALI 28:13).

(5)                        KUZALIWA MARA YA PILI (Mst. 13)

Mtu hawezi kuwa mtoto wa Mungu mpaka amezaliwa mara ya pili.  Siyo kwamba anazaliwa tena kwa mapenzi ya mwili yaani kwa namna ya kawaida bali kwa roho (YOHANA 3:3-6).  Mtu anaposikia neno la Mungu lenye uzima na kuliamini na kutubu dhambi zake kwa kumaanisha kuziacha, palepale kwa IMANI anazaliwa mara ya pili, si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika (1 PETRO 1:23).  Katika tendo hili la imani, mtu hupewa uwezo wa kushinda dhambi na ulimwengu, na kufanyika mtoto wa Mungu ( 1 YOHANA 5:1, 4-5).

(6)                        NENO ALIFANYIKA MWILI (Mst. 14)

Neno, yesu Kristo ambeye ni Mungu alifanyika mwili, aliuvaa mwili wetu na kuwa Mwana wa Adamu (WAEBRANIA 2:14).  Wako watu wanaofundisha kwamba Yesu ni mtu aliyefanyika Mungu kama Musa, kwa kutumia andiko la KUTOKA 7:1.  Hii nidyo roho ya mpinga Kristo (2 YOHANA 1:7).  Aliuvaa mwili dhaifu na kusulibishwa katika huo (MATHAYO 26:41; 2 WAKORINTHO 13:4).  Aliuvaa mwili unaokufa (ZABURI 78:39; 1 PETRO 3:18).  Alikuja katika mfano wa mwili ulioleta dhambi ulipotamani chakula (WARUMI 8:3).  Alikaa kwetu wakaidi (ZABURI 68:18), tukaona utukufu wake (YOHANA 2:11). Somo la 2 ni “HAKUNA ALIYEMWONA MUNGU” ingia hapa; WWW.davidcarol719.wordpress.com/hakuna-mtu-aliyemwona-mungu/

JE, UNATAKA KUOKOKA SASA?

Tunasoma haya katika LUKA 1:77, “Uwajulishe watu wake wokovu, katika kusamehewa dhambi zao”.   Hii ina maana kwamba ukiisha kutubu dhambi zako leo utasamehewa kwa hakika, na hivyo kupata wokovu mara moja.  Je, kweli utasamehewa?  Jibu ni Ndiyo!  Yesu mwenyewe anasema katika YOHANA 6:37, “……….Wala yeyote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe”.  Hivyo kwa dhahiri, leo hii, dakika hii hii, utasamehewa na kupata wokovu.  Je, uko tayari kuokoka sasa na kuhesabiwa miongoni mwa wale watakaoingia mbinguni na kuishi na Mungu milele, hata wakiiaga dunia sasa hivi?  Ukiwa tayari kuifuatisha sala ifuatayo ya toba, mara tu baada ya sala hii, nitakuombea na kwa ghafla utawezeshwa kushinda dhambi.  Je, uko tayari kuifuatisha sala hii sasa?  Najua uko tayari.  Basi sema maneno haya,  “Mungu Baba, natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Naomba unisamehe na kuniosha dhambi zangu kwa damu ya Yesu iliyomwagika msalabani.  Niwezeshe kushinda dhambi kuanzia sasa.  Liandike sasa jina langu katika kitabu cha uzima mbinguni.  Asante kwa kuniokoa, katika Jina la Yesu, Amen”.  Sasa ninaomba kwa ajili yako, “Mungu Baba msamehe kiumbe wako huyu dhambi zake zote, na mpe uwezo wa kushinda dhambi kuanzia sasa na kumuokoa. Mbariki kwa baraka zote katika Jina la Yesu, Amen”.  Tayari umeokoka.  Ili uzidi kuukulia wokovu, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI!!!

                                     . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

                                                          . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .         

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “note” hii, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s