SAA INAKUJA NA SASA IPO

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

SOMO:  SAA INAKUJA NA SASA IPO

L

eo, tunaendelea tena kujifunza Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu.  Tutatafakari YOHANA 5:20-30, katika mafundisho yetu ya leo.  Ingawa kichwa cha somo letu la leo, ni “SAA INAKUJA NA SASA IPO“, kuna mengi ya kujifunza katika mistari hii.  Tutayagawa mafundisho yote tunayoyapata katika mistari hii, katika vipengele vinane:-

(1)      BABA AMPENDA MWANA (MST.20);

(2)      UWEZEKANO WA KUTENDA KAZI KUBWA ZAIDI (MST.20);

(3)      YESU KRISTO NI SAWA NA MUNGU (MST.21-23, 26);

(4)      HAKIMU YESU KRISTO (MST. 22,27);

(5)      JINSI YA KUKKWEPA HUKUMU (MST. 24);

(6)      SAA INAKUJA NA SASA IPO (MST. 25);

(7)      UFUFUO WA UZIMA NA WA HUKUMU (MST.29);

(8)      HATARI YA KUFANYA NENO MWENYEWE (MST.30).

 

(1)      BABA AMPENDA MWANA (MST.20

Mungu Baba ampenda Mwanawe Yesu Kristo.  Alimpenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu YOHANA 17:24.  Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kwamba watu wote waliompokea Yesu Kristo mioyoni mwao, hawa nao ni watoto wa Mungu YOHANA 1:12.  Kumpokea Yesu moyoni maana yake kumpisha kiti cha udereva katika mioyo yetu.  Kabla mtu hajampokea Yesu, yeye mwenyewe huwa dereva katika moyo wake.  ANAJIENDESHA na kujipelekeka popote anapotaka kwenda, iwe ni katika uasherati au uzinzi, iwe ni kwenye baa ya pombe, iwe ni kwenda kununua sigara na kuzivuta, iwe ni kwenda kufanya wizi, n.k.  Kumpokea Yesu moyoni, ni kutoka katika usukani wa moyo na kumpisha Yesu AKUENDESHE, awe dereva.  Naye akituendesha, hawezi kutupeleka katika uzinzi, uasherati au dhambi  yoyote, atatuendesha sawasawa MAMBO YA WALAWI 26:13.  Tunapomfanya Yesu awe dereva wetu, ndipo tunapokuwa watoto wa Mungu.  Ni muhimu kuelewa pia kwamba, tukiwa watoto wa Mungu.  Mungu anatupenda kama anavyompenda yesu Kristo YOHANA 17:23.  Je, Mungu alimpendaje Yesu?  Je, alimletea magonjwa?  Jibu ni la!  Alifurahia kuona ana uzima wakati wote.  Kwetu pia, ni vivyo hivyo.  Upendo aliouonyesha kwa Yesu ni wetu pia.  Alimpenda kumfanya mshindi juu ya Shetani na dhambi, akamfanya mtendakazi hodari, akampa ulinzi wa malaika n.k; na sisi pia, anapenda tuwe hivyo.  Hatuna budi kuamini.

 

(2)      UWEZEKANO WA KUTENDA KAZI KUBWA ZAIDI (MST.20)

Yesu Kristo, mapema tu katika huduma yake, alikiri kwamba atafanya kazi kubwa kuliko alizokuwa ameanza kuzifanya mpaka watu wastaajabu.  Sisi nasi, hatupaswi kuridhika na lolote tulilokwisha kulifanya katika utendaji wetu wa kazi ya Mungu.  Bado kuna uwezekanao mkubwa wa kutenda kazi kubwa zaidi kwa kila amwaminiye Yesu.  Siyo tu kwamba kuna uwezekanao wa kutenda kazi alizozifanya Yesu, bali kuna uwezekano wa kufanya kazi zilizo kubwa zaidi YOHANA 14:12.  Wanafunzi wa Yesu waliomsikiliza akisema haya, akina Petro na wengineo, waliamini, na Petro akafanya kazi ambazo hakuzitenda Yesu MATENDO 5:15-16.  Watu wengi katika Kanisa la Mungu duniani, wanafikiri kwamba waliyotenda Mitume, sisi hatuwezi kuyafanya.  Huu ni upungufu mkubwa.  Siyo waliyotenda Mitume tu, hata na zaidi ya yale aliyoyatenda Yesu.

(3)      YESU KRISTO, NI SAWA NA MUNGU (MST. 21-23, 26)

Yesu tunapomtaja kwamba ni Mwana wa Mungu, maana yake nyingine ni kwamba Yeye, ni sawa na Mungu (YOHANA 5:18).  Katika mistari hii, Yesu anathibitisha jinsi alivyo sawa na Mungu.  Watu hawa walimdhihaki mtu yeyote aliyesema kwamba mtu akifa anaweza tena kufufuka (MATENDO 17:32).  Waliamini kwamba kufa ndiyo mwisho wa kila kitu.  Hapa Yesu anasema kwamba uhai wa mtu umetoka kwa Mungu, na hivyo akiutoa, anaweza tena kuurudisha.  Hii ni kazi anayoweza kuifanya Mungu peke yake.  Sasa basi, anasema, kama  Baba anavyoweza kuhuisha, yaani kuwapa tena uzima wafu, yeye naye anaweza kufanya vivyo hivyo.  Siyo hilo tu, Mwamuzi au Hakimu mwenye haki ni Mungu tu (ZABURI 7:11, 58:11), na anayetajwa kuwa ni Muhukumu mwenye nguvu ni Bwana MUNGU (UFUNUO 18:8).  Sasa kama jinsi Mungu alivyo Hakimu, Yesu naye ni Hakimu huyu mwenye haki.  Siyo hilo tu, Baba ana uzima nafsini mwake, maana yake uzima uliotokana na Yeye mwenyewe tofauti na wanadamu ambao uzima wetu ulitokana na uzima wa Mungu (MWANZO 2:7).  Yesu hapa, anasema, kama Mungu alivyo UZIMA, yeye naye pia ni Uzima (YOHANA 14:6).  Yote haya yanathibitisha jinsi Yesu alivyo sawasawa na Mungu Baba, na inatupasa kumheshimu kama tunavyomheshimu Mungu Baba.

 

(4)      HAKIMU YESU KRISTO (MST. 22, 27)

Maandiko yanaeleza waziwazi kwamba Yesu ndiye Hakimu atakayeuhukumu ulimwengu wote.  Yeye ndiye anampa hukumu mtu mara tu baada ya kufa (WAEBRANIA 9:27).  Ikiwa amekufa katika dhambi, anatupwa katika moto wa milele, na ikiwa amekufa katika wokovu anakwenda mbinguni.  Mataifa yote yatakusanyika mbele zake Yesu, Mwana wa Adamu kwa hukumu.  Maandiko yafuatayo yanataja waziwazi juu ya Hakimu Yesu Kristo (YOHANA 5:22; MATHAYO 25:31-32; MATENDO 10:42; WARUMI 2:16; 2 TIMOTHEO 4:1).

 

(5)      JINSI YA KUKWEPA HUKUMU (MST. 24)

Kulisikia Neno la Yesu na kulitendea kazi kwa imani, ndiyo jinsi ya kukwepa hukumu.  Hakimu Yesu Kristo, hukumu yake ni tofauti na jinsi Mhakimu wa Duniani wanavyotoa hukumu zao.  Mtu anapoletwa kwa Hakimu wa duniani, anatakiwa kukiri kosa au kukataa kwamba hakufanya kosa, hata kama anasema uongo, ndipo kesi inapoanza kusikilizwa!  Muundo au mfumo huu wa hukumu katika ulimwengu huu, ni tofauti kabisa na mfumo wa hukumu ya Hakimu Yesu Kristo.  Jinsi ya kukwepa hukumu ya Yesu Kristo, ni KUKIRI KOSA na kuziungama dhambi zote kwa kumaanisha kuziacha.  Hapo ndipo tunaposamehewa mara moja na kukwepa hukumu.  Lakini wengine kwa kutokufahamu, wanasema hawana dhambi.  Hawa wanaojikinai kuwa ni wenye haki, hukumu itakuwa juu yao, maana watu wote wametenda dhambi, hakuna atendaye mema, la, hata mmoja (YEREMIA 2:35; ZABURI 51:5; 58:3; WARUMI 3:12, 23; 1 YOHANA 1:8-10; MITHALI 28:13).

 

(6)      SAA INAKUJA NA SASA IPO (MST. 25)

“Saa inakuja, na sasa ipo, wafu watakaposikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai“.  Hapa Yesu anaeleza juu ya mambo matatu tofauti.  Saa inakuja, anazungumzia wakati wa ufufuo wa uzima na Ufufuo wa hukumu ambapo watu waliokufa watafufuliwa na kupata uzima wa milele au hukumu kama tutakavyojifunza katika kipengele kinachofuata.  Wakati wa Ufufuo wa Uzima na Ufufuo wa hukumu, ni WAKATI UJAO, bado haujakuwapo.  Saa sasa ipo, anazungumzia, kwanza jinsi ambavyo atawafufua watu waliokufa kwa sauti tu tofauti na Eliaya na Elisha walivyofanya katika kufufua.  Eliya alijinyosha juu ya mtoto aliyekufa mara tatu na kumwomba Mungu roho ya mtoto imrudie (1 WAFALME 17:21-22).  Elisha pia alipanda juu ya kitanda cha mtoto aliyekuwa na kuwa macho yake juu ya macho ya maiti, mikono yake juu ya mikono ya maiti, kinyuwa chake juu ya kinywa cha maiti, na kujinyosha juu yake, halafu akatembea ndani ya nyumba na kupanda kujinyosha tena juu yake, ndipo mtoto akafufuka (2 WAFALME 4:32-35).  Yesu hakufanya mikikimikiki yote ile katika kufufua watu wakati wa “Saa sasa ipo“.  Alimwambia maiti, “Kijana nakuambia, inuka“ akaisikia sauti yake na kufufuka (LUKA 7:14).  Alisema pia, “Msichana nakuambaia inuka“, mara maiti akasikia sauti yake na kufufuka (MARKO 5:41-42) na tena alisema “Lazaro njoo huku nje“, akasikia sauti yake na kufufuka (YOHANA 11:43-44).  Pili, Yesu katika “Saa sasa ipo“, anazungumzia jinsi watu ambao hawajaokoka wanaoitwa WAFU, watakavyofufuka na kuhuishwa na kupata uzima wa milele watakaposikia sauti ya Yesu au Neno lake (WAEFESO 2:1).  Wengi waliookoka waliposikia Neno lake hata leo wengi wanaokoka wanapolisikia Neno lake.

 (7)     UFUFUO WA UZIMA NA WA HUKUMU (MST. 29)

Mtu aliyeokoka anapokufa moja kwa moja dakika ileile anakwenda mbinguni (LUKA 23:39-43; 16:22; MATHAYO 17:1-3; WAFILIPI 1:21-23; 2 WAKORINTHO 5:6,8).  Mtu huyu anapokufa, roho yake huvaa mwili wa roho au wa mbinguni na kwenda mbinguni (1 WAKORINTHO 15:40, 41, 44, 46).  Hatimaye katika Ufufuo wa Uzima wote waliokwenda mbinguni, watafufuliwa tena yaani watakuja katika miili ya duniani na kuiungana na waliopo duniani, kubadilishwa tena na kupaa kumlaki Yesu wakti wa kunyakuliwa kwa Kanisa.  Huu ndiyo Ufufuo wa Uzima au Ufufuo wa Kwanza au ufufuo ulio bora (1 WATHESALONIKE 4:15-17; 1 WAKORINTHO 15:51-54).  Watu wanapokufa bila kuokolewa, hakika ileile wanawkenda motoni au kuzimu penye mateso makali (LUKA 16:22-24).  Wanaenda motoni bila kuelezwa kwa nini wamepewa hukumu hiyo.  Hawa watafufuliwa tena katika Ufufuo wa Hukumu au Ufufuo wa pili ili kuelezwa kwa nini wanastahili kutupwa katika ziwa la moto milele.  Hapa ndipo watakapojitetea bila kusikilizwa (UFUNUO 20:11-15; MATHAYO 7:22-23;  LUKA 13:25-28).

 

(8)      HATARI YA KUFANYA NENO MWENYEWE (MST.30)

Kufanya neno au jambo lolote tu analopenda mtu hata kama ni kinyume na Neno la Mungu, ni kufanya neno mwenyewe.  Yesu hakufanya hivi maisha yake yote.  Hakuyatafuta mapenzi yake, bali mapenzi yake yeye aliyempeleka yaani Mungu Baba.  Alifanya kila jambo sawasawa na mapenzi ya Mungu au Neno lake.  Sisi nasi kama tunajiita Wakristo, tunapaswa kufuata kielelezo chake Yesu Kristo.

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Munu zitakuwa nawe..

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s