SISI HATUJUI

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

SOMO:   SISI HATUJUI

B

ado kuna mengi ya kujifunza katika Kitabu cha YOHANA, katika Biblia zetu.  Leo, tunajifunza YOHANA 14:4-12.  Kichwa cha somo letu la leo, ni “SISI HATUJUI“.  Hata hivyo kuna mengi zaidi ya kujifunza, katika mistari hii.  Tutayagawa mafundisho yote tunayoyapata katika mistari hii katika vipengele tisa:-

 

(1)      SISI HATUJUI (MST. 4-5);

(2)      YESU NI NJIA NA KWELI NA UZIMA (MST. 6);

(3)      MTU HAJI KWA BABA ILA KWA NJIA YA MIMI (MST. 6);

(4)      UTUONYESHE BABA (MST. 7-8);

(5)      SIKU HIZI ZOTE, WEWE USINJIJUE (MST. 9);

(6)      ALIYENIONA MIMI AMEMWONA BABA (MST. 9);

(7)      HAYO MANENO SIYASEMI KWA SHAURI LANGU (MST. 10);

(8)      SADIKINI KWA SABABU YA KAZI ZENYEWE (MST. 11);

(9)      UWEZO MKUBWA KWAKE YEYE AMWAMINIYE YESU (MST. 12).

 

(1)   SISI HATUJUI (MST. 4-5)

Tomaso pamoja na Mitume wenzake, walikuwa wamekaa pamoja na Yesu kwa miaka zaidi ya mitatu wakijifunza ktoka kwake.  Mpaka hatua hii, walikuwa wamejifunza mambo mengi sana.  Walikuwa ni Wahubiri wa Injili, na tena walikuwa wamepewa amri juu ya pepo wachafu, kuwatoa, na kupoza au kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina, pamoja na kufufua wafu (MATHAYO 10:1, 7-8).  Pamoja na hawa kuwa mitume, na kujua mengi, hapa Tomaso kwa niaba yao, anasema “SISI HATUJUI“.  Hili ni fundisho kwetu.  Wengi katikati yetu, wakiisha kuwa na ufhamu kidogo sana, tayari wanajiona wanajua na hawaoni tena umuhimu wa kujifunza.  Wengine wakiisha kuwa Wachungaji, Mama Wachungaji, Wainjilisti au Waalimu, tayari wanaona wanajua na hawaoni tena umuhimu wa kujifunza.  Wengine wakiisha kumaliza Shule ya Uinjilisti au Shule ya Uongozi wanajiona wanajua, na hawaoni tena umuhimu wa kukhudhuria katika madarasa ya Biblia ya Jumapili au Makanisa ya Nyumbani au kusikiliza kaseti za mafundisho.  Wengine wakitoa pepo kwa watu kadha wachache tu au wakionyeshwa maono fulani au kutoa jumbe za unabii au wakiwa na karama za kuponya au karama nyinginezo tayari wanajiona wanajua na hawataki tena kuongozwa au kufundishwa!  Je, tungekuwa Mitume na tukakaa pamoja na Yesu ana kwa ana, na kupewa mamlaka waliyopewa; tungeweza kusema, “SISI HATUJUI?“.  Wengine katikati yetu ni wazito kukubali kwamba wamekosa, wakati wote wanajiona wanajua.  Wengine ni wazito kutubu hadharani katika maombi!  Mitume wa Yesu hawakuwa hivi.  Inatupasa kuiga mfano wao.  Tukijiona tunajua, na tumekwisha kufika, Mungu hawezi kututumia kwa viwango vya juu.  Wote waliotumiwa sana na Mungu, walikuwa ni wale waliokiri kutokujua, hata kama walikuwa na viwango vipi vya kiroho (ZABURI 73:22,24; 1 WAKORINTHO 8:2; WAFILIPI 3:12-15).  Bwana atusaidie kuwa na maisha yaliyojaa kutokujua.

 

(2)  YESU NI NJIA KWELI NA UZIMA (MST. 6)

Yesu hapa anajitaja kwamba ni Njia na Kweli na Uzima:

1)     YESU NI NJIA:  Yesu, NDIYE Njia Kuu ya Utakatifu, aliyetajwa katika ISAYA 35:8.  Kwa damu yake, Yesu alituanzia NJIA MPYA iliyo hai, ya kutuwezesha kupaingia mahali patakatifu (WAEBRANIA 10:19-20).  Wanafunzi wake walicha vyote na kumfuata.  Kwa kumfuata Yesu, waliifuata NJIA!  Ndiyo maana watu waliomfuata Yesu nyakati za Kanisa la Kwanza, waliitwa watu wa Njia hii au Njia ile (MATENDO 22:4; 24:22).  Yesu ametuonyesha Njia ya Ubatizo, usemi, kusamehe na kuwapenda maadui, na katika kila jambo ametuonyesha njia kwa mafundisho yake.  Tukiyafuata mafundisho yake na kuyatendea kazi, tujue tunaifuata Njia.  Tusipoyatendea kazi mafundisho yake, tujue tumekengeuka na kwenda kushoto au kulia, na kuiacha Njia.  Mtume au Nabii yeyote siyo Njia ya kutufikisha mbinguni.  Yesu ndiye Njia.

2)     YESU NI KWELI:  Kweli ni zaidi ya mfano!  Mambo yote ya Agano la Kale, yalikuwa mifano tu au kivuli cha Yesu aliye Kweli.  Sabato ilikuwa mfano au kivuli cha Yesu aliye Pumziko la Kweli (WAKOLOSAI 2:16; MATHAYO 11:28).  Mana iliyoshuka kutoka mbinguni, ilikuwa mfano tu wa Yesu aliye chakula cha Kweli kutoka mbinguni (YOHANA 6:49-51).  Yesu pekee ndieye Kweli, wengine wote ni Uongo, ni wevi na wanyang’anyi, hawawezi kutufikisha mahali pa salama (YOHANA 10:8).  NENO LAKE Yesu ndiyo Kweli, kamwe tusiridhike na maneno yaliyotunga na wanadamu au mapokeo ya wanadamu, kama ubatizo wa watoto wadogo, n.k huo ni uongo (YOHANA 17:17).

3)     YESU NI UZIMA: Watu wote, ni wenye dhambi, ni WAFU (WAEFESO 2:1).  Tunakuwa hai au kupata uzima kwa Mungu, katika Kristo Yesu aliye Uzima (YOHANA 11:25).  Mtu asipokuwa na Yesu moyoni mwake, hana huo uzima, amekufa, ni mfu (1 YOHANA 5:12).

 

(3)  MTU HAJI KWA BABA ILA KWA NJIA YA MIMI (MST. 6)

Maneno haya yako wazi mno.  Bila kumfuata Yesu na neno lake, hakuna jinsi yoyote ya kumwona Mungu.  Wengine husema, “Njia tu ndiyo tofauti, lakini wote tunakwenda kwa Mungu, kama jinsi ambavyo kuna njia nyingi za kufika Mwanza au Arusha“.  Hii, siyo kweli.  Njia ya kufika mbinguni ni moja tu Yesu Kristo (YOHANA 3:18, 36; ISAYA 30:20-21).

 

(4)  UTUONYESHE BABA (MST. 7-8)

Maneno ya Filipo, “Utuonyeshe Baba yatutosha“, yanawakilisha mawazo ya watu wengi.  Wako watu wengi wanaowaza kwamba kama wangemwona Mungu uso kwa uso, ingewatosha kuwafanya wamwabudu na kulifuata neo lake.  Uzoefu, unaonyesha kwamba madai haya siyo ya Kweli.  Adamu na Hawa walikuwa na nafasi ya jinsi hiyo katika Bustani ya Edeni, lakini walimwasi Mungu kuyaasi maneno yake, na kumfuata shetani.  Wazee wa Israeli, walipata nafasi ya kumwona mungu kwa kuuona utukufu wake (KUTOKA 24:9-11).  Hata hivyo, muda usio mrefu kutokea hapo, Haruni aliwaongoza wazee hao na Wana wa Israeli wote, katika kufanyiza sanamu ya ndama, na wakasema huyo ndiye mungu aliyewatoa Misri!  (KUTOKA 32:1-6).  Bila kuwa visingizio, tunapaswa kuonyesha uaminifu wetu kwa Mungu, pasipo kumwona kwa macho, sawasawa na mpango wake.

 

(5)  SIKU HIZI ZOTE, WEWE USINIJUE (MST. 9)

Pamoja na uzuri wa tabia ya kukiri kutokujua, hata hivyo, Mungu anatarajia kuona tunakua kiroho, na kuwa waaliju wa wengine baada ya kujifunza Neno lake kwa siku kadha.  Yesu, hapa, alikuwa amekwisha kukaa na wanafunzi wake kwa zaidi ya miaka mitatu akiwafundisha; na hivyo alitarajia kwamba Filipo angekuwa anamjua Yesu kwa kaisi kikubwa.  Hata leo, wako watu wengine katikati yetu ambao hawakui kiroho kama filipo.  Wana miezi kadha au miaka kadha katika Kanisa hili na wanakuwepo katika ibada karibu zote; lakini wanakuja tu kama picha.  Hawajui mambo mengi na ni kama watoto wachanga tu mpaka sasa.  Hawawezi kushindana na kuwakemea pepo wanapokuwa wamewavamia, hawajui lolote kuhusu mavazi ya Mkristo au malipizo ya Ndoa.  Bado hawajui yawapasayo kuzingatia katika uhusiano wa Wanawake na Wanaume katika wokovu, na wengine hawawezi hata kushuhudia au kufundisha masomo ya mwanzo ya wokovu na kujibu maswali madogomadogo.  Hatupaswi kuwa hivi (WAEBRANIA 5:11-14).  Furaha ya mzazi ni kuona mtoto wake anakua.  Mtoto ambaye hakui, ni kero!  Ndivyo ilivyo kwa Yesu pia.  Tumwombe Bwana ili tukue kasi kiroho na kuwa waalimu.

 

(6)  ALIYENIONA MIMI AMEMWONA BABA (MST. 9)

Watu wanaofuata mafundisho ya William Branham, wanatumia msitari huu kudai kwamba Yesu ndiye Baba.  Haya ni mafundisho potofu.  Yesu na Baba, ni nafsi tofauti.  Kawa mifano iliyo wazi.  Yesu anatufundisha hivyo.  Yesu anajitaja kuwa ni MZABIBU WA KWELI, na Baba yake ndiye MKULIMA, ni vitu tofauti kabisa (YOHANA 15:1).  Hata alipopaa mbinguni, bado yuko mkono wa kuume wa Baba kuonyesha utofauti (MATENDO 7:55-56; UFUNUO 3:21).  Yesu anaposema hapa, “Aliyeniona mimi amemwona Baba“, anamaanisha kwamba tukiiona tabia yake Yesu, tumeiona tabia yake Baba maana Yesu ni CHAPA ya nafsi yake na sura yake Mungu katika tabia (WAEBRANIA 1:1-3; 2 WAKORINTHO 4:4).

 

(7)  HAYO MANENO SIYASEMI KWA SHAURI LANGU (MST. 10)

Wanafunzi wa Yesu hapa, walianza kuzoea maneno ya Mwalimu wao Yesu na kuona kwamba ananena maneno mengine kwa shauri lake tu na siyo maneno ya Mungu.  Ilibidi Yesu awasahihishe na kuwaambia kwamba ni Baba anenaye ndani yake.  Hata leo wako wengine wanaozoea maneno ya Mchungaji na kuyaona ni ya kwake mwenyewe.  Haitupasi kuwa hivi (1 WATHESALONIKE 2:13).

 

(8)  SADIKINI KWA SABABU YA KAZI ZENYEWE (MST. 11)

Ishara na maajabu au miujiza ni kazi za kutufanya tuone huduma fulani imetoka kwa Mungu (YOHANA 2;11; 2 WAKORINTHO 12:12).  Hata hivyo hapa pana mtego mkubwa.  Tunaweza kuona ishara na maajabu katika huduma fulani lakini ikawa haitokani na Mungu kama ishara za waganga wa Misri (KUTOKA 7:11-12, 20-22; 8:6-7).  Ishara kuu kuliko zote ya kuangalia, jinsi maisha ya watu katika huduma yanavyobadilishwa kwa neno la Mungu, na kuwafanya watu waliokuwa na dhambi kuwa safi, watakatifu.  Huduma ya Yesu ilikuwa na ishara hii (YOHANA 15:3).  Hii ni kazi kutufanya tusadiki.

 

(9)  UWEZO MKUBWA KWAKE YEYE AMWAMINIYE YESU (MST. 12)

Tukimwamini Yesu, tuna nafasi ya kufanya kazi kubwa kuliko alizozifanya maana Yeye hayuko duniani kwa sura halisi baada ya kupaa.  Pamoja na Yeye kutokuwako, kazi yake haina budi kuendelea kuliko wakati aliokuwako kwa sisi kutumiwa na Yeye.  Petro aliamini, watu wakapona walipogusa kivuli chake na siyo tu upindo wa vazi lake kama kwa Yesu (MATENDO 5:15-16).

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s