TABIA SABA ZA WAANDISHI NA MAFARISAYO

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

SOMO:      TABIA SABA ZA WAANDISHI NA MAFARISAYO

Leo, tunajifunza Biblia kutoka katika MATHAYO 23:1-13.  Katika mistari hii tunajifunza, “TABIA SABA ZA WAANDISHI NA MAFARISAYO”.  Tutaligawa somo letu la leo katika vipengele viwili:-

(1)   WAJIBU WA KUWAONYA WATU KUHUSU MAFUNDISHO POTOFU (MST.1-2);

(2)  TABIA SABA ZA WAANDISHI NA MAFARISAYO (MST. 2-13).

(1)      WAJIBU WA KUWAONYA WATU KUHUSU MAFUNDISHO POTOFU (MST. 1-2)

Awaye yote kati yetu, aliyekabidhiwa kundi la kondoo za Mungu, na kufanywa na Roho Mtakatifu kuwa mwangalizi ndani yake (MATENDO 20:28); inambidi kufahamu waziwazi wajibu wake wa kuwaonya watu walio chini ya uongozi wake, kuhusu mafundisho potofu ya dini mbalimbali na viongozi wa dini mbalimbali.  Hatupaswi kuacha kutekeleza wajibu huu kwa visingizio vya kuacha kusema dini za watu wengine na kuwafanya kondoo tunaowaongoza wararuliwe na kuangamizwa.  Hapa, anawaambia waziwazi makutano na WANAFUNZI WAKE juu ya tabia za Waandishi na Mafarisayo, na kuwaonya wajihadhari na mambo yao; bila kuogopa kusema dini za watu wengine.  Mara kwa mara, Yesu aliwapa tahadhari wanafunzi  WAKE KUHUSU MAFUNDISHO POTOFU YA Waandishi, Mafarisayo na Masadukayo.  Waandishi hawa walikuwa siyo waandishi wa habari, bali watu waliosoma Neno la Mungu katika Torati na kulitafsiri (NEHEMIA 8:1-9).  Kwa nafasi hiyo, walitafsiri kwa kuongoza yasiyokuwamo katika torati na kupunguza yaliyokuwamo katika torati kulingana na matakwa yao.  Mafarisayo, walikuwa baadhi ya Wayahudi waliojikinai kuwa ni wenye haki kuliko wengine, ingawa waliyashika mapokeo yaliyotungwa na wanadamu yaliyokuwa kinyume na Neno la Mungu.  Mafarisayo hawa, waliyashika mapokeo hayo na kuyashindania sana na walitaka kila mtu ayafuate (MATHAYO 15:2; MARKO 7:8-13; LUKA 18:11-12; WAGALATIA 1:14).  Masadukayo, ilikuwa ni dini ambayo hawakuamini juu ya mafundisho ya kiyama ya wafu au ufufuo wa wafu, kuwapo kwa malaika au kuwepo kwa roho na mambo ya rohoni; ambayo yote haya Mafarisayo waliyaamini (MARKO 12:18; MATENDO 4:1-2; 23:8).  Yesu Kristo, alitumia muda mwingi mno katika mafundisho yake, kufundisha juu ya tabia na mafundisho potofu ya Waandishi, Mafarisayo na Masadukayo.  Karibu nusu ya mafundisho yake yanawahusu watu hawa!  Waziwazi, aliwaambia wanafunzi wake kujihadhari na mafundisho yao (MATHAYO 16:5-12).  Ikiwa hatuwafundishi kondoo waziwazi, ni rahisi kuchukuliwa na mafundisho ya mashetani ya nyakati hizi za mwisho.  Viongozi wa Kanisa la Kwanza, waliwaonya kondoo wao juu ya MBWA MWITU (MATENDO 20:29-30), MBWA (WAFILIPI 3:2), na WATUMISHI WA SHETANI WANAOJIGEUZA KUWA WATUMISHI WA KRISTO (2 WAKORINTHO 11:13-15).  Waliwafundisha kujiepusha nao, na kutokuwakaribisha nyumbani mwao (WARUMI 16:17; 2 YOHANA 1:9-11).  Sisi nasi ikiwa ni watumishi wa Kristo, hatupaswi kusita kuwaonya kondoo kuhusu mafundisho ya Mashahidi wa Yehova, Sabato, William Branham, n.k.; au Watumishi wa Shetani wanaojigeuza kuwa ni watumishi wa Kristo, kwa jinsi wanavyowadanganya watu na wakadhani kwamba, nguvu ya Mungu wetu ni kumuangusha kila mtu chini ili apate chochote kutoka kwake, hata iwe ni KAZI!  Na wengine wanaowapa watu mimba za miaka mitatu na kudai ni miujiza ya Mungu, n.k.;  Kwa kufundisha hivi, kinyume cha imani za Masadukayo, inaweza ikatusababishia kuwa na maadui wengi na hata kutupwa gerezani, lakini hatupaswi kuogopa, Malaika wa Bwana, atatumwa kututoa gerezani (MATENDO 5:17-20).

 

(2)      TABIA SABA ZA WAANDISHI NA MAFARISAYO (MST. 2-13)

1.         HUKETI KATIKA KITI CHA MUSA (MST. 2) – Waandishi hawa, walisimama katika kiti cha Musa (mimbari au MADHABAHU ya mti – NEHEMIA 8:4), NA KUFUNDISHA NA KUHUKUMU KAMA Musa ingawa hawakuwa na maisha ya nuruni kama Musa (2 NYAKATI 17:7, 9; 19:5-9).  Hatimaye, alikuja Yesu Kristo, yule aliyenenwa kwamba atakuja kwa mfano wa Musa (KUMBUKUMBU 18:18-19; MATENDO 3:20-23).  Huyu Yesu ndiye wa kusikilizwa na siyo Mafarisayo wanaowafundisha watu kufanya mambo ambayo hayako katika Neno la Mungu, kwa visingizio kwamba vikao vya Ulaya viliyapitisha!

 

2.         HUNENA LAKINI HAWATENDI (MST. 3) – Waandishi na Mafarisayo wana sauti ya Yakobo, lakini mikono yao ni ya Esau (MWANZO 27:22); wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwamwitu wakali (MATHAYO 7:15-16).  Wanahubiri Neno la Mungu, ingawa wao ni wana wa Ibilisi, na tamaa za baba yao ndizo wapendazo kuzitenda (YOHANA 8:44).  Watumishi wa Mungu wanapaswa kunena na kutenda wanayoyafundisha (WARUMI 2:17-24; MATENDO 1:1; WAFILIPI 3:9; 4:9).  Ikiwa mtu anajifanya Kiongozi wa Kanisa, na anahubiri na kufundisha asiyotenda mwenyewe, huyo ni Farisayo na Mwandishi.  Bwana atusaidie, tusiwe miongoni mwa Waandishi na Mafarisayo.  Mtu anayewahubiri watu na kuwafundisha Neno la Mungu ambalo yeye mwenyewe halitendi, anafanana na kengele zinazowaita watu kuja Kanisani, wakati zenyewe hata siku moja hazijaingia Kanisani; na kibao kinachowaelekeza watu njia ya kwenda Dodoma wakati chenyewe kimetiwa zege chini na hakijaenda Dodoma!

 

3.         HUWATWIKA WATU MIZIGO WASIYOWEZA KUIBEBA WENYEWE (MST. 4) – Huwaambia watu wafanye mambo ambayo wao wenyewe hawawezi kuyatenda!  Kiongozi yeyote wa Kanisa, anapaswa yeye mwenyewe kuwa kielelezo, kwa kutoa mfano (1 WAKORINTHO 11:1; WAFILIPI 3:17).  Kiongozi yeyote ambaye anampigia kelele anayemwongoza, kutoa ripoti ya Uinjilisti, wakati yeye mwenyewe hawezi kutoa riporti yake ya Uinjilisti au ya Makanisa ya Nyumbani, au haiandiki kwa ukamilifu, huyu ni Mwandishi na Farisayo.

4.         HUTENDA MATENDO YAO ILI KUTAZAMWA NA WATU (MST. 5) – Hirizi ambazo walizivaa Mafarisayo na Waandishi, hazikuwa za kawaida za kiganga tunazozifahamu leo.  Wao walichukua karatasi iliyotengenezwa kutokana na ngozi ya mnyama halafu wakaandika vizuri vifungu vinne vya maandiko yafuatayo: KUTOKA 13:9-11; 13:11-16; KUMBUKUMBU 6:4-9, 11:13-21.  Baada ya kuandika, karatasi hii iliwekwa katika ngozi ndogo iliyofumwa kama hirizi, na hirizi hizi walizivaa katika mikono yao, na kwenye vipaji vyao vya nyuso kwa mapokeo ya tafsiri ya KUTOKA 13:9.  Hirizi zao zilikuwa kubwa (zilipanuliwa) kuliko za wengine.  Walikuwa na lengo kuonekana kwa watu kwamba ni Watakatifu, huku mioyoni mwao, walikuwa mbali mno na Neno la Mungu.  Neno linataka nje na ndani kuwe sawa, na tuanze kwanza kuandika Neno la Mungu katika vibao vya mioyo yetu!  (MITHALI 7:1-3; MATHAYO 23:25-26).  Vilevile, Mungu alikuwa ameagizo Waisraeli wavae nguo za kuwatambulisha kuwa wao ni tofauti na MATAIFA.  Ndivyo anavyoagiza kwetu pia hata leo (HESABU 15:37-41; WARUMI 12:2).  Sasa basi Mafarisayo, katika kuvaa kwao waliongeza ukubwa wa vishada hivyo au mapindo hayo, au matamvua ili waonekane kwa watu kwamba wao ni watakatifu sana katika mavazi, na wako tofauti na mataifa; huku walikuwa wanatenda dhambi mno sirini!  Huu ni unafiki.  Siku ya mwisho Mungu ataleta matendo yote hukumuni; ya SIRINI kwanza, na yale yanayoonekana kwa watu.  Ndipo itakuwa kilio na kusaga meno (MHUBIRI 12:14; WARUMI 2:16).

  1. 1.     HUPENDA HESHIMA (MST. 6-7, 11-12) – Waandishi hawa na Mafarisayo, kama karamuni hawakuwekewa viti vya mbele, basi ujue hawatashiriki katika karamu hiyo.  Walipenda kuwa wa kwanza (3 YOHANA 1;9).  Viti vya mbele lazima vikaliwe na watu, lakini tukifikia kuona kwamba bila kupewa kipaumbele basi hatuko tayari kuendelea na lolote jingine, Kanisani au kokote, hivyo ni kutengeneza sanamu na kuiabudu wenyewe, ni dhambi.  RABI licha ya kumaanisha BWANA NA MWALIMU (YOHANA 13:13), inamaanisha mtu MKUBWA au MKUU.  Waandishi hawa, waliwafundisha watu kwamba mtu asipowaita “RABI” atamfanya Mungu asionyeshe uwepo wake katika Israeli!  Walipenda ukubwa, na matokeo yake wakadhiliwa.  Ni muhimu kufahamu kwamba heshima, ni kama KIVULI.  Kadri unavyokifuata kivuli na kukikimbiza, ndivyo kinavyozidi kukukimbia.  Kadri unavyokuwa hukitaki kivuli, na kukikimbia, ndivyo kinavyozidi kukufuata.  Ni muhimu kuwa wanyenyekevu kwa kuwa watumishi, ikiwa tunataka tuheshimiwe!  Tukiwa na kiburi, tutapata malipo mabaya (MST.11-12, ZABURI 31:23).
  1. 1.     HUPENDA KUITWA MWALIMU, BABA, KIONGOZI (MST. 8-10) – Kuitwa majina haya siyo tatizo linalozungumzwa.  Mungu ameweka wengine kuwa WAALIMU (WAEFESO 4:11).  Mtume Paulo, anajiita BABA (1 WAKORINTHO 4:14-17; FILEMONI 1:10).  Kanisa pia lina VIONGOZI (WAEBRANIA 13:17).  Linalozungumzwa hapa ni kwamba, asiwepo Mwalimu, Baba au Kiongozi ambaye atakuwa mtunga sheria.  Hiyo ni kazi ya Kristo, ya Mungu Baba peke yake.  Sheria zote ziwe katika Neno la Mungu tu!  Sisi sote ni ndugu, ni wanafunzi, hatupaswi kuchukua nafasi ya Mkuu wa Shule na kutunga sheria!  Baba aliye juu ya yote, na katika yote, na ndani ya yote, ni Mungu na Kristo ndiye Kiongozi Mkuu (WAEFESO 4:6; WAEBRANIA 2:10).  Waandishi, wao walitunga sheria za kwao ambazo haziko katika Neno!  Vivyo hivyo na Mafarisayo (MATENDO 13:1).
  1. 2.     NI WANAFIKI (MST.13) – Unafiki katika lugha ya asili, ni kufanya mchezo wa kuigiza.  Kujifanya Kaburu wakati wewe ni Mtanzania.  Kujifanya mkristo au uliyeokoka kumbe wewe ni mwana wa Ibilisi kama Mafarisayo.  ANGALIA MFANO WA UNAFIKI: ZABURI 28:3; 55:21.

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s