TOBA NA MALIPIZO

ZACHARY KAKOBE

Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SOMO:  TOBA NA MALIPIZO

Somo hili, ni  moja kati ya masomo ya msingi sana katika Ukristo. Tukiwa na ufahamu kuhusu somo hili na kulitendea kazi, ndipo tunapoweza kuonyesha nuru ya maisha yetu ya Ukristo. Tutajifunza somo hili kwa kuligawa katika vipengele sita:-

           ( 1 ).  MAANA YA “TOBA”

           ( 2 ).  MAANA YA “MALIPIZO”

           ( 3 ).  MALIPIZO KATIKA AGANO JIPYA

           ( 4 ).  AINA MBALIMBALI ZA MALIPIZO

           ( 5 ).  FAIDA ZA KUFANYA MALIPIZO

           ( 6 ).  HEKIMA KATIKA KUFANYA MALIPIZO

( 1 ).  MAANA YA “TOBA”

Wokovu unapatikana kwa mtu, mara tu anaposamehewa dhambi zake, baada ya toba ya kweli ( LUKA 1:77 ). Watu wengi hufanya kile kinachodhaniwa kuwa ni toba katika taratibu mbalimbali za kidini, kwa maombi, nyimbo za Liturujia au kwa kutubu mbele ya viongozi wa dini, lakini watu wengi katika hawa, hawapati wokovu, kwa sababu toba zao zimekuwa siyo za kweli. Ili toba iwe toba ya kweli mbele za Mungu, na iweze kuleta msamaha wa dhambi, toba lazima iambatane na haya yafuatayo:-  1. Kuhuzunishwa kipekee moyoni, baada ya mtu kutafakari na kujifahamu kuwa ni mtenda dhambi              ( 2 WAKORINTHO 7:9-10 ).  2.  Kuwa tayari kuacha njia zote za mwanzo zisizompendeza ungu katika mawazo na matendo ( ISAYA 55:7; MITHALI 28:13 ).    3.  Kugeuza uso ili usiyaelekee tena machukizo ya mwanzo ( EZEKIELI 14:6 ).  4. Kuuacha uovu wote na kuutupilia mbali, kugeuka, na kurudi katika njia za Mungu katika moyo mpya na roho mpya, na kuwa tayari kutenda yaliyo ya halali na haki ( EZEKIELI 18;27-28, 30-31; MATHAYOB21:30 ). 5. Kuwa tayari kufanya malipizo yoyote yanayohusika baada ya toba ( KUTOKA 22:2-3 ).

 

( 2 ).  MAANA YA “MALIPIZO

Toba haiwezi kuwa kamili ikiwa haiambatani na malipizo yanayohusika  baada ya toba. Toba bila malipizo yanayohusika, itatufanya tukose amani pamoja na kutubu kwetu, itatukosesha ushindi wa dhambi zinazohusika na hukumu itaendelea kutukalia. Neno malipizo, maana yake ni nini?  Neno malipizo au kwa kiingereza Restitution, tunalolipapata katika KUTOKA 22:2-3; maana yake kuzaa matunda yapasayo toba MATHAYO 3:8, au kutenda matendo yanayopatana na kutubu kwetu MATENDO 26:20. Malipizo, ni kufanya masahihisho ya makosa tuliyoyafanya kwa wanaohusika, ili tuwe na dhamiri isiyo na hatia siyo mbele za Mungu tu, pia na mbele za wanadamu wote wanaotuzunguka, ili wasije wakatulaumu kwa habari ya karama ya wokovu tulioupokea (MATENDO 24:16; 2WAKORINTHO 8:20-21). Ni muhimu kufahamu kwamba, tunapowakosea watu, kwa mfano tunapowadanganya katika mapatano, tunakuwa tumemkosea Mungu vilevile, na hivyo tunasamehewa na Mungu pale tunapofanya marekebisho ya makosa hayo kwa watu hao, baada ya kutubu mbele za Mungu                        ( WALAWI 6:2-5, 7 ). Masahihisho ya makosa ni pamoja na kurudisha kwa wenyewe vitu vilivyoibiwa, kulipa pale tulipodhurumu, kuomba msamaha kwa watu tuliowakosea n.k.

( 3 ).   MALIPIZO KATIKA AGANO JIPYA

Kwa kutofahamu, wako watu wengine ambao wanadai kwamba mafundisho ya malipizo, ni mafundisho ya agano la kale tu,. au ni maagizo ya sheria ya Musa au Torati, na hayahusiki kwetu katika Agano Jipya.. Madai haya, siyo ya kweli. Mafundisho ya malipizo, ni mafundisho ya msingi kwa mtu yeyote anayetaka kumpendeza  Mungu katika nyakati  zote za Biblia. Uwiano wa maandiko yafuatayo, unaonyesha waziwazi kwamba mafundisho ya malipizo ni ya nyakati zote za Biblia, hata wakati huu tulionao wa Agano Jipya.

  1. Malipizo kabla ya sheria ya Musa ( MWANZO 20:1-7;14; 42:1-3; 25-28, 35; 43:1-2 ).
  2. Malipizo wakati wa sheria ya Musa

( a ).  Nykati za Musa ( KUTOKA 22:1,7,14; WALAWI 6:2-5).

(  b ). Baada ya Musa, Nyakati za Wafalme na Manabii ( 1 SAMWELI 12:1-5;                                                                                                      

             2 SAMWELI 16:5-11; 19:16-20 ; EZRA 10:1-4,10-12,19;  EZEKIELI                                                                                                                                                                                   

  33:14-16 ).

      

3.   Malipizo wakati wa Agani Jipya ( MATHAYO 5:23-24; LUKA 17:3-5; 19:8-9;                                                    

             FILEMONI 1:10-19; MATENDO 24:16).

( 4 ).  AINA MBALIMBALI ZA MALIPIZO.

Sasa, tutaangalia kivitendo, yale tunayotakiwa kuyafanya katika kufanya malipizo ya namna mbalimbali:-

1.Malipizo ya kuachana na wanawake au wanaume.

Baada tu ya kuokoka, inatupasa kuangalia kwa makini ikiwa mume au muke tuliyenaye ni wa halali mbele za Mungu. Tunaweza tukawa na mke au mume asiye wetu kihalali ( YOHANA 4:18 ). Mume au mke wetu kihalali ni yule mke au mume wa kwanza katika ujana wetu ambaye tulipata ruhusa ya wazazi wa binti katika kuishi kwetu, ikiwa pande zote mbili tulikuwa hatuna wake au waume wa namna hii ( MATHAYO 19:4-6 ). Tukiwa tunaishi na mke au mume wa mtu, baada ya kuokoka, sharti tufanye malipizo ya toba ya uzinzi na kuachana naye hata kama tumezaa naye watoto ( EZRA  10:1-4, 10-12, 18-19; MWANZO 20:1-7, 14 ). Ikiwa tulikuwa tunaishi na msichana au mvulana kabla ya kuokoka bila kupatikana na ruhusa ya wazazi wa binti, huo ni uasherati. Baada ya kuokoka inatupasa kufanya malipizo ya toba ya uasherati kwa kuachana kabisa na siyo kutafuta kuhalalisha kukaa kwetu wakati bado tupo pamoja. Huko siyo kuacha uovu na kugeuza nyuso zetu zisiyaelekee machukizo. Baaba ya kuokoka, ikiwa tulikuwa na uchumba na mtu ambaye hajaokoka, uchumba huo unavunjwa mara moja, maana haitupasi kuolewa au kumwoa  yeye asiyeamini ( YOSHUA 23;11-13; 2 WAKORINTHO 6:14-15 ; AMOSI 3:3 ). Katika malipizo ya toba ya uasherati au uzinzi tunapaswa kurudisha  vitu vyote tulivyopewa kutokana na uasherati au uzinzi  huo kuonyesha toba ya kweli kadri inavyowezekana.

2.  Malipizo ya toba ya uongo, wizi, uonevu, na kurudisha kisicho chetu kwa halali ( WALAWI 6:2-5 ).

Ikiwa  tumepata pasipoti kwa uongo, wakati sisi siyo raia hatuna budi kurudisha pasipoti hizo na kuwa tayari kwa lolote. Ikiwa tunasoa au kufanya kazi kutokana na vyeti vya shule vya uongo, hatuna budi kufanya malipizo ya uongo na kuwa tayari kwa lolote iwe ni kuachishwa kazi, masomo au adhabu yoyote. Ikiwa tulikuwa tunahubiri uongo kwamba hakuna kuokoka, au ubatizo wa maji tele siyo lazima, n.k…,tunapoijua kweli, hatuna budi kuwaeleza watu kwamba tulikuwa wakosaji katika kuwahubiri hivyo. Hatuna budi kurudisha vyote tulivyo navyo vya wizi, iwe ni vitabu vya shule, maktaba au chochote tulichokiiba kwa mtu au kumnyang’anya au kukipata kwa uonevu ( EZEKIELI 33:14-16 ).Hatuna budi kusalimisha  polisi bunduki, bastola n.k, tulizokuwa tunazitumia katika unyang’anyi na kuwaeleza kuwa tumeokoka. Hatuna budi kurudisha fedha zisizokuwa zetu au kitu chochote kisicho chetu ambacho kimeachwa kwetu kwa makosa ( MWANZO 42:1-3, 25-28, 35, 43;12, 17-18, 20-23 ). Tukipewa chenji iliyozidi au tukipewa vitu zaidi ya tulivyonunua kwa halali, sharti turudishe. Mshahara uliokuja kwetu kimakosa, sharti tuurudishe. Chochote kisicho chetu alichokisahau mtu sharti tukirudishe.

3.  Malipizo ya kuomba msamaha  kwa yule tuliyemkosea kosa lolote.

Katika kosa lolote tunalomkosea mtu, haitoshi tu kutubu mbele za Mungu, sharti turudi kwake yule tuliyemkosea kwa majuto kabisa na kuomba atusamehe, tukikiri na kutaja kwa wazi na huzuni juu ya yale tuliyomkosea. Shimei aliomba msamaha kwa lugha chafu ya kulaani aliyoitumia kwa Daudi ( 2SAMWELI  16:5-7; 19:16-20 ).

       4. Malipizo ya kulipa kitu tulichokipoteza au kukiharibu tulipokabidhiwa.

          ( KUTOKA 22:14; FILEMONI 1:17-19)-Sikuzote hatuna budi kuwa tayari              kulipa kitu tulichokipoteza au kukiharibu tulipokabidhiwa.

       5.  Malipizo ya toba ya kazi au biashara zinazohusiana na dhambi                  ( HABAKUKI 2:15-16 ).-Tunapookolewa, kama inavyotubidi kuacha kufanya kazi ya uasherati iliyokuwa inatupa mapato, hatuna budi kuacha kazi zinazofanana, zinazohusiana na dhambi kwa mfano, kazi ya kuuza pombe au mhudumu wa baa, kuuza sigara, kufanya kazi kiwanda cha sigara, pombe, kuchezesha bahati na sibu, kulima tumbaku, n.k. Nyumba zetu hatuwezi kuzitumia kukodisha baa,  au Disco, n.k. Magari yetu hatuwezi kuyatumia kubeba bia, bangi, n.k.

        6.   Malipizo ya toba ya wizi wa mali ya Mungu

            Tunapaswa kutoa fungu la kumi la mapato  yetu yote kwa wakati uleule tunapopata mapato hayo kinyume chake ni kumwibia Mungu ( MALAKI 3:8-10 ). Tunapotoa zaka au fungu la kumi la mapato yaliyopita baada ya kutumia zaka, hatuna budi kuongeza faini  ya sehemu ya tano juu ya zaka ambayo tungelipa. Vivyo hivyo hatuna budi kuziondoa nadhiri  tunazoziweka                  ( MHUBIRI 5:1-5; HESABU 30:2; ZABURI 50:4; 76:11; 66:13-14 ). Tukichelewa kulipa zaka au kutoa nathiri kwa wakati wake, malipizo ya toba ni kuongeza sehemu ya tano1/5 juu yake. Badala ya 1/10 tunalipa 3/5 n.k.               ( HESABU 5:5-7; WALAWI 6:2-5;  27:30-31 ).

5.FAIDA ZA KUFANYA  MALIPIZO.

Mara tu baada ya kuokoka na wakati wote wa maisha yetu katika wokovu, hatuna budi kuangalia ni wapi ambapo tunapaswa kufanya malipizo ya toba zetu. Kuna faida nyingi za kufanya malipizo haya:-

  • Uchungu wa malipizo, unatufanya tuwe na chuki kubwa ya dhambi  tulizozifanya na matokeo yake tunatiwa mafuta ya shangwe yanayotupa ushindi mkubwa wa dhambi ( WARUMI 12:9; WAEBRANIA 1:9 )
  • Malipizo hutuondolea kuhukumiwa moyoni mwetu na kumfanya mshitaki Ibilisi ashindwe kutushitaki, na hivyo nguvu yetu ya maombi huongezeka ( UFUNUO 12:9-10; 1YOHANA 3:21-22 ).
  • Malipizo huwafanya mataifa kujua maana halisi ya wokovu na kumtukuza Mungu wetu ( 1 PETRO 2:12 ).
  • Malipizo yanaleta uamsho mkubwa kwa mtu binafsi na kufungua milango kwa uamsho katika Kanisa na ulimwengu mzima ( YONA 3:10 ).
  • Malipizo hutuletea amani na watu wote ( WAEBRANIA 12;14 ).
  • 6.  Malipizo yanawarudishia watu haki zao na kuufanya ulimwengu kuwa na haki     ( WARUMI 13:17 ).

( 6 ).  HEKIMA KATIKA KUFANYA MALIPIZO.

Malipizo hayana budi kufanywa kwa hekima, ili yasilete madhara  kwa wengine bali yalete lolote kwetu tu. Kwa mfano siyo hekima kumwambia mume wetu kwamba tulifanya uzinzi na  fulani, kwa kuwataja majina. Hilo litaondoa amani moja kwa moja. Hapo tutamwambia Mungu tu. Ikiwa tulimdanganya mume kuwa mtoto ni wake kumbe tulimpata nje ya ndoa na akajua ni mtoto wake kama wengine katika ndoa, na mtoto akajua huyo ni baba yake, si busara baada ya kuokoka kumwambia mume kwamba  fulani siyo mtoto wako, bali tunatubu kwa Mungu tu. Mungu ni wa amani siyo wa machafuko ( 1 WAKORINTHO 14:33 )

                                                          . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .         

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook, Twitter n.k,  kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “note” hii, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.

                                                         UBARIKIWE NA BWANA YESU!!!

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s