TUFANYEJE ILI TUPATE KUZITENDA KAZI ZA MUNGU?

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

 

SOMO:          TUFANYEJE ILI TUPATE KUZITENDA KAZI ZA MUNGU?

L

eo, tena tunaendelea kuichambua Biblia yetu, kwa kujifunza Kitabu cha YOHANA.  Siku hii ya leo, tunatafakari kwa makini YOHANA 6:26-59.  Kuna mengi mno ya kujifunza katika mistari hii ingawa kichwa cha somo letu ni “TUFANYEJE ILI TUPATE KUZITENDA KAZI ZA MUNGU?”.  Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika mistari hii katika viengele tisa:-

 

(1)  KUMTAFUTA YESU ILI KUPATA MIKATE (MST. 26);

(2)  MSIKITENDEE KAZI CHAKULA CHENYE KUHARIBIKA (MST. 27);

(3)  TUFANYEJE ILI TUPATE KUZITENDA KAZI ZA MUNGU? (MST. 28-29);

(4)  UMUHIMU WA TAFSIRI SAHIHI YA MAANDIKO (MST. 30-32);

(5)  HAKIKA YA WOKOVU (MST. 37);

(6)  KUFANYA MAPENZI YA MUNGU MAISHA YOTE (MST. 38-40);

(7)  NYENZO INAYOTUMIKA KUMFANYA MTU AOKOLEWE (MST. 44);

(8)  MIMI NDIMI CHAKULA CHA UZIMA (MST. 33-35, 47-59);

(9)  UMUHIMU WA KUFUNDISHWA NA MUNGU (MST. 41-43, 45-46).

 

(1)      KUMTAFUTA YESU ILI KUPATA MIKATE (MST. 26)

Yesu Kristo, Bwana wetu, huwa haridhiki tu na kutosheka, anapotuona TUNAFANYA jambo fulani.  Huchunguza NI KWA NIA IPI AU KWA NINI TUNAFANYA jambo hilo.  Wanadamu, hatuwezi kumficha kitu.  Watu hawa walimfuata Yesu.  Jambo hilo, kwa NJE, linaonekana jema, lakini NDANI ya mioyo yao, walikuwa na nia mbaya.  Nikodemo alimfuata Yesu kwa sababu aliona ishara (YOHANA 3:1-2), lakini hawa walimtafuta na kumfuata Yesu siyo kwa sababu waliona ishara, bali kwa sababu walikula mikate wakashiba.  Sisi nasi ni muhimu kujiuliza tuna nia ipi katika kumfuata Yesu kwa kuja Kanisani, kuhubiri au kutoa mali zetu n.k.!  Nia yetu ikiwa siyo njema, Yesu anajua na hapendezwi nasi!  Wengine wanakuja Kanisani kwa kufuata wanaume au wanawake, wengine wanakuja Kanisani ili kudumisha urafiki na watu fulani wanaowapa faida fulani, wengine wanakuja kutafuta uponyaji wa magonjwa yao tu, lakini wokovu hawataki.  Wengine wanahubiri au kutoa mali zao kwa nia ya kutafuta sifa au kuonekana n.k.  Yote haya siyo mema.  Hatuna budi kufanywa upya nia zetu ili tumpendeze Mungu na kuwa wakamilifu (WARUMI 12:2).  Tusiwe kama mataifa wanaofanya kila jambo kwa nia chafu.  Kabla ya kufanya lolote, tujiulize, tuna nia njema katika kulifanya hilo?

 

(2)      MSIKITENDEE KAZI CHAKULA CHENYE KUHARIBIKA (MST. 27)

Siyo kwamba Mungu hataki tufanye kazi kwa lengo la kutafuta chakula.  Hayo ni mapenzi ya Mungu kwetu (2 WATHESALONIKE 3:12).  Kinachozungumzwa hapa, ni kutumia muda wetu wote au mwingi, kutafuta chakula cha mwili tu au utajiri usiodumu, na kuacha kutenga muda wa kutosha kutafuta chakula cha roho zetu, yaani Neno la Mungu.  Kufanya hivyo siyo vema, maana mambo ya chakula na utajiri, ni ya dunia hii tu.  Mtu akifa, haendi na chochote (ZABURI 49:16-20; MITHALI 23:4-5; LUKA 21:34-36).  Watu wengi wanaokitendea kazi chakula chenye kuharibika, wanakuwa katika hatari ya kukaa Kanisani muda mrefu, bila kukua kiroho, maana hawana muda wa kuhudhuria ibada zote kutokana na shughuli za dunia, na hivyo Neno la Mungu kwao, halizai matunda (MATHAYO 13:12).

 

 (3)     TUFANYEJE ILI TUPATE KUZITENDA KAZI ZA MUNGU? (MST. 28-29)

Kuna jambo kubwa la kujifunza haa tunapoangalia jinsi Yesu alivyolijibu swali hili.  Kazi ya Mungu, ni kumwamini Yesu.  Watu hawa kama watu wengi walivyo leo, walitamani kuzitenda kazi za Mungu bila kwanza kutubu na kuacha dhambi zao na kuokolewa.  Jambo hili halina maana yoyote mbele za Mungu.  Jambo la kwanza halina budi kuwa KUOKOKA, KABLA ya kuhubiri Neno la Mungu, kujiunga na kikosi cha maombi, kutoa sadaka kwa ajili ya Injili au kujiunga na kwaya au kufanya kazi yoyote ya Mungu, ili kazi yetu iwe na maana mbele za Mungu na kutupa baraka (ZABURI 50:16; MITHALI 28:9; 15:8; 21:3; AMOSI 5:21-24; 6:5).   Vile vile tunajifunza hapa kwamba kumwamini Yesu, ni kazi ya Mungu, maana yake mtu hawezi kumwamini Yesu mpaka Mungu afanye kazi ndani yake (MATHAYO 16:15-17; 11:25-27; YOHANA 6:44).

 

(4)      UMUHIMU WA TAFSIRI SAHIHI YA MAANDIKO (MST. 30-32)

Mtu akitaka kuitimiza tamaa yake mwenyewe, anaweza kuchukua msitari wowote wa Biblia na kuutafsiri isivyo sahihi na kuufanya umtetee katika kunywa pombe, kuvuta sigara, kuwa na wake wengi, n.k.  Kufanya hivi, ni kujidanganya mwenyewe.  Watu hawa walisema kama vile ilivyoandikwa.  Aliwapa chakula cha mbinguni ili wale, wakitaja (ZABURI 78:24); na kutafsiri kwamba aliyewapa chakula hicho ni Musa.  Yesu akawasahihisha na kusema tafsiri hiyo siyo sahihi.  Aliyewapa chakula hicho ni Mungu.  Tunaonywa kutoitafsiri Biblia kama tunavyopenda na tena tunashauriwa kutumia KWA HALALI neno la kweli au maandiko (2 PETRO 1:20; 2 TIMOTHEO 2:15).

 

(5)      HAKIKA YA WOKOVU (MST. 37)

Tukija kwake Yesu na kukiri kwamba sisi ni wenye dhambi, na kuja kwake kwa toba, huku tukimaanisha kabisa kuacha dhambi, hatuna budi kuamini kwa imani kwamba wakati huohuo tunasamehewa na kuokolewa.  Hatupaswi kuenenda kwa kuona, bali kwa imani.  Kuenenda kwa imani, ni kuongozwa na Neno la Mungu, siyo hisia zetu.  Yesu anasema hapa, YEYOTE AJAYE kwake, kwa misingi hii, hatamtupa KAMWE, hakika atamsamehe na kumuokoa.  Hatuna budi kulichukua neno hili kama lilivyo na kuliamini pamoja na maandiko mengineyo (ISAYA 55:7; 44:22; 1:11; ZABURI 103:12; YOHANA 1:12).  Bila kuwa na hakika hii ya wokovu, Shetani atatudanyanya kila siku na tutajiona bado kuokoka kwa sababu ndogo ndogo tu.  Hata hivyo hakika ya wokovu, inaambatana na mtu aliyepata uwezo wa kushinda dhambi na anasa za ulimwengu.  Mtu asiye na uwezo huu, hajafanyika mtoto wa Mungu, na kwake kuwa na hakika ya wokovu, ni kujidanganya zaidi.

 

(6)      KUFANYA MAPENZI YA MUNGU MAISHA YOTE (MST. 38-40)

Yesu, hakuja duniani kufanya mapenzi yake bali ya Mungu baba.  Hili, halina budi kuwa fundisho kwetu.  Maisha yetu yote duniani, hatupaswi kufanya mapenzi yetu, yaani kufanya lolote tunalotaka kulifanya; bali tufanye kama tunavyojifunza katika neno la Mungu.  Hivi ndivyo alivyofanya Yesu (YOHANA 8:28-29).  Vile vile, mapenzi yake ni kwamba wote anaotupa, yaani wale wote waliokata shauri kumfuata Yesu tunaokabidhiwa kuwafuatilia asipotee hata mmoja (MATHAYO 18:14).  Hivyo hatuna budi kutumia bidii yote kuwatembelea na kuwafundisha na kuwaombea na kuja nao Kanisani ili walishwe zaidi Neno la Mungu.

 

 (7)     NYENZO INAYOTUMIKA KUMFANYA MTU AOKOLEWE (MST. 44)

Mtu haokolewi kutokana na ufundi wetu wa kuhubiri na kumsomea maandiko mengi kutoka katika Biblia yote, na kuchukua siku nzima tukisema naye.  Nyenzo inatumika kumfanya mtu aokolewe, ni Mungu Baba MWENYEWE KUMVUTA MTU HUYO.  Asipovutwa na Baba, kazi yetu yote ni bure.  Hivyo, kuhubiri kwetu hakuna budi kuwa kwa imani, tukimtegemea Roho Mtakatifu anayemhakikikishaia mtu kwamba ni mwenye dhambi na kwamba kweli anastahili hukumu kama asipolifuata neno tunalomhubiria mabalo ndiyo haki (YOHANA 16:7-8).  Injili yetu iwe fupi yenye kumwelezea mtu jinsi ya kushinda dhambi na kumwachia Mungu kazi ya kuokoa.

(8)      MIMI NDIMI CHAKULA CHA UZIMA (MST. 33-36, 47-59)

Yesu, ndiye chakula au mkate ushukao kutoka mbinguni.  Kuna mengi ya kujifunza kuhusu Yesu kama mkate au chakula cha uzima na tena kuna mengi ya kujifunza tunapomfananisha Yesu na MANA iliyoshuka wakati wa Musa.  Yesu Kristo, alizaliwa Bethlehemu.  BETHLEHEMU, maana yake NYUMBA YA MKATE.  Yesu alikuja kwetu kama mkate wa uzima.  Sadaka za Bwana za kuteketezwa, ziliitwa CHAKULA CHA MUNGU  (WALAWI 21:21-22).  Yesu Kristo, ndiye Sadaka kuu ya Bwana iliyompendeza (WAEBRANIA 9:14, 28), na hivyo Yeye ndiye Chakula cha Mungu, halisi.  Mkate au mana inayoshuka kutoka mbinguni wakati wa Musa (KUTOKA 16:11-35), haikuwa na uzima.  Ilipowekwa kwa muda kidogo tu iliingia mabuu au funza na kutoa uvundo (KUTOKA 16:19-20).  Yesu yeye ni hai milele na milele, ni chakula kisichooza.  Kaburi halikumuweza!  Mana pia iliokotwa asubuhi sana na kulipokuwa na jua kali, iliyeyuka (KUTOKA 16:21).  Tunapaswa kumtafuta Yesu atuokoe, mapema!  Tukichelewa atayeyuka, hatutamwona tena!  Mana ililiwa siku zote mpaka walipoifikia Kanaani (KUTOKA 16:35).  Sisi nasi tunapaswa kulila neno la Mungu siku zote mpaka tufike mbinguni.  Uliwekwa ukumbusho wa Mana (KUTOKA 16:31-33), kama Meza ya Bwana ilivyo ukumbusho wa Yesu aliye mkate wa uzima.  Mana ilikuwa tamu (KUTOKA 16:31), kama Neno la Mungu lilivyo tamu, kama Yesu alivyo mtamu au mwema tukimwonja (ZABURI 34:8; 1 PETRO 2:3).  Yesu kama Chakula  kilichoshuka kutoka mbinguni, inadhihirisha pia kwamba hakuanzia kwa Mariamu (MIKA 5:2; YOHANA 8:58).

(9)      UMUHIMU WA KUFUNDISHWA NA MUNGU (MST. 41-43, 45-46)

Watu hawa kama wengi wetu, hawakuelewa lolote kuhusu Yesu alivyofananishwa na Mana.  Yesu akawaelezea umuhimu wa kufundishwa na Mungu.  Haitoshi kusoma Biblia zetu tu nyumbani, sisi nasi hatuna budi kuhudhuria ibadani kila Jumatatu, Jumatano, Jumamosi na Jumapili, ili tufundishwe na Mungu.  Tutawezaje kuelewa bila kuongozwa?  (MATENDO 8:30-31).

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s