KISIPOTEE CHOCHOTE

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

SOMO:          KISIPOTEE CHOCHOTE

S

iku ya leo ya Kuichambua Bibilia, tunaendelea kujifunza Kitabu cha YOHANA.  Leo tunatafakari YOHANA 6:1-25.  Ingwa kichwa cha somo letu leo, ni  “KISIPOTEE CHOCHOTE“, kuna mengi zaidi ya kujifunza katika mistari hii.  Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika mistari hii, katika vipengele kumi:

(1)      SABABU YA MKUTANO MKUU KUMFUATA YESU (MST. 1-2);

(2)      YESU KUKETI PAMOJA NA WANAFUNZI WAKE (MST. 3);

(3)      UMUHIMU WA MKATE WA KIROHO NA KIMWILI (MST. 4-5);

(4)      KUJARIBIWA KWA IMANI YETU (MST. 5-10);

(5)      NGUVU YA SHUKRANI (MST. 11);

(6)      KISIPOTEE CHOCHOTE (MST. 12-13);

(7)      HAKIKA HUYU NI NABII YULE (MST. 14);

(8)      KUJITENGA KWA YESU (MST. 15);

(9)      WANAFUNZI WA YESU BAHARINI (MST. 16-21);

(10)       KUMTAFUTA YESU KWA BIDII (MST. 22-25).

 

(1)      SABABU YA MKUTANO MKUU KUMFUATA YESU (MST. 1-2)

Mkutano mkuu au watu wengi kwa maelfu, walimfuata Yesu, kwa sababu waliziona ishara alizowafanyia wagonjwa.  Kila alipokwenda Yesu, aliponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina (MATHAYO 9:35).  Ni muhimu kufahamu kwamba ni mapenzi ya Mungu kuona tunaponywa magonjwa tuliyo nayo.  Tunapoomba juu ya uponyaji wa magonjwa yetu, ni makosa kuomba, “Ikiwa ni mapenzi yako, niponye”.  Neno la Mungu linaeleza waziwazi kwamba ni mapenzi ya Mungu sisi kuwa wazima (YOHANA 10:10; MARAKO 1:40-41; 1 YOHANA 3:8).  Tukiomba kwa imani, ni hakika tutaponywa.  Kuomba kwa imani ni lazima kuambatane na kuomba bila manung’uniko (1 WAKORINTHO 10:10), na tena kuomba bila wivu (YAKOBO 4:2).  Kuomba kwa kunung’unika ni kusema kwa mfano, “Mungu wangu, umeniokoa kwa nini basi, ikiwa unaniacha ninateseka?  Nimekukosea nini?  Kuliko mateso haya, ni heri nife”.  Kuomba kulikojaa wivu, mfano wake ni kusema, “Mungu mbona fulani na fulani wao umewaponya hali wameokoka juzijuzi tu, mbona mimi huniponyi kama wao?”.  Maombi ya jinsi hii ni maombi yasiyoweza kutupa majibu.  Jambo jingine muhimu la kujifunza ni umuhimu wa ishara wanazofanyiwa wagonjwa.  Hatuna budi kama Kanisa kuzidi kuomba ili ishara hizi zifanyike katikati yetu kwa wingi ili wengi wamfuate Yesu (MATENDO 4:24, 29-30).

(2)      YESU KUKETI PAMOJA NA WANAFUNZI WAKE (MST.3)

Mwanafunzi wa Yesu, ni mtu yule aliyejitia nidhamu kulitii na kulifuata neno lake Yesu kwa gharama yoyote (ZABURI 119:4-9).  Tukiwa wanafunzi wa Yesu, tunakuwa tumeketishwa pamoja na Yesu mlimani, katika ulimwengu wa roho (WAEFESO 2:6).  Ikiwa tumeketi pamoja na Yesu, kwa nini tutishwe na uchawi aus nguvu za Shetani?  Kila uchawi au silaha itakayofanyika juu yetu haiwezi kufanikiwa (HESABU 23:22-23; ISAYA 54:17).

(3)      UMUHIMU WA MKATE WA KIROHO NA KIMWILI (MST. 4-5)

Kabla ya Yesu kutoa mkate wa kimwili kwa watu hawa, aliwapa KWANZA mkate wa kiroho, Neno la Mungu.  Ni muhimu kwa kila mmoja wetu kufahamu kwamba hatuwezi kuishi kwa mkate au chakula cha kimwili tu.  Hatuna budi kutoa kipaumbele kwa chakula cha kiroho (MATHAYO 4:4; YOHANA 6:48-49).  Ikiwa tunailisha miili yetu mara tatu kwa siku na kuzilisha roho zetu mara moja tu, Jumapili, tena kwa dakika chache; matokeo yake ni mauti ya milele ya roho zetu.  Vivyo hivyo, tunajifunza hapa kwamba Mungu anapenda kuona tunapata mikate ya kimwili au chakula cha kimwili.  Ikiwa hapa aliona umuhimu wa watu hawa kula kwa muujiza mkubwa, sisi nasi atahakikisha anatupa chakula cha kimwili hata ikibidi kwa miujiza.  La muhimu ni kuutafuta ufalme wa Mungu kwanza yaani chakula cha kiroho kwanza, na chakula cha kimwili hakika atatupa (MATHAYO 6:33).

 

(4)      KUJARIBIWA KWA IMANI YETU (MST. 5-10)

Kama Yesu alivyomjaribu Filipo hapa na kuona imani yake, sisi nasi atatujaribu imani yetu.  Atatuachia vipindi fulani fulani vigumu ili aone kama tutaendelea kuamini kwamba anaweza kushughulika nasi katika magumu yoyote na kutupatia mema.  Hpa Filipo alibabaika katika mtihani huu wa imani vivyo hivyo Andrea.  Wao waliwaza katika mwili tu kwa kutumia akili na wakaona haiwezekani kuwalisha watu hao maelfu.  Dinari 200 ilikuwa yapata mshahara wa miezi minane wa nyakati hizo au fedha yetu ya sasa TShs. 25,000.= .  Fedha hizi zisingetosha kuwalisha maelfu hao.  Inatupasa kushinda mtihani wa imani kwa kutokukubali kutumia akili na kuwaza kwamba ufumbuzi wa tatizo letu utatokea namna gani.

(5)      NGUVU YA SHUKRANI (MST. 11)

Kwa shukrani tu, mikate michache na samaki wachache waliweza kulisha watu maelfu.  Kuna nguvu kubwa sana katika kushukuru.  Shukrani zilileta nguvu kubwa iliyomfufua Lazaro (YOHANA 11:41-44).  Shukrani, zilimuongezea mmoja kati ya wale wakoma kumi kitu cha ziada.  Shukrani zake, Yesu aliita IMANI! (LUKA 17:11-19).  Tunakosa baraka nyingi kwa kukosa kujua nguvu ya shukrani.  Maandiko yanatupa msisitizo mkubwa wa kushukuru.  Tukiwa wepesi wa kushukuru kwanza kabla ya kuomba, tutajiweka katika nafasi ya kupokea miujiza mikubwa na baraka tele (WAKOLOSAI 3:15; 4:2; 2:6-7;1 WATHESALONIKE 5:17-18).  Vile vile hapa, tunajifunza umuhimu wa kushukuru kabla ya kula.  Shukrani na kuomba kabla ya kula, hukitakasa chakula na kukifanya kiwe baraka kwetu (1 TIMOTHEO 4:4-5).

 

(6)      KISIPOTEE CHOCHOTE (MST. 12-13)

Ubadhirifu au ufujaji mali ya umma ni kosa la jinai.  Vivyo hivyo Mungu wetu anataka tutumie kwa uangalifu mkubwa kila kitu anachotupa iwe ni fedha, nguo, chakula au chochote kile.  Tunapaswa kuangalia vizuri vifaa vya Kanisa au mali yoyote ya Kanisa tunavyokabidhiwa.  Tukipewa pesa yoyote na kutumwa kufanya hiki au kile, lazima tukumbuke agizo la Yesu “Kisipotee chochote“.  Ufujaji wowote wa chochote tunachopewa na Mungu ni dhambi.  Inatubidi kutumia fedha anayotupa Mungu na kuangalia matumizi yaliyo ya lazima.  Tukiwa wafujaji au wabadhirifu wa kile tunachopewa, tunajifungia mlango wa kupata vingine  kutoka kwa Mungu (TITO 3:14).

 

(7)      HAKIKA HUYU NI NABII YULE (MST. 14)

MAPEMA SANA Mungu alisema angeleta nabii ambaye kila mmoja angewajibika kumsikia au siyo angeadhibiwa (KUMBUKUMBU 18:18-19).  Watu walimngoja nabii huyu kwa miaka mamia wasimwone.  Alipotokea Yohana Mbatizaji walimwuliza kama yeye ndiye “Nabii yule“, akajibu “La“ (YOHANA 1:21).  Hatimaye wakatambua kuwa nabii huyu ni Yesu, na maandiko mengine yanathibitishas hivyo (MST. 14; MATHAYO 21:10-11; YOHANA 1:45; 5:46; 7:40; MATENDO 3:20-23).

 

 (8)     KUJITENGA KWA YESU (MST. 15)

Walipotaka kumshika Yesu na kumfanya awe Mfalme wao, Yesu alijitenga, akaenda tena mlimani yeye peke yake.  Hatuna budi kuangalia lolote linalokuja kwa lengo la kutuongezea elimu, maslahi, cheo, sifa n.k; lakini linataka litutoe katika mapenzi ya Mungu.  Kazi yoyote ambayo itatufanya tusihudhurie ibada, ni lazima tujitenge nayo.  Mume anaposema atatupa hiki na kile ikiwa tutaacha kuja Kanisani, tujue huu ni mtego.  Hatuna budi kujitenga na matakwa ya Ibilisi ya kutuangamiza kiroho.  Elimu, cheo au safari yoyote itakayotutoa katika mapenzi ya Mungu, ni lazima tujitenge nayo.  Siyo kila kitu kinachoonekana ni kizuri kinatokana kwa Mungu.  Tukiwa wachanga kiroho halafu watu wakaja kuitushika na kuktutaka tuwe Waalimu wa Faragha zao, au wazee wao wa Kanisa, hatuna budi kujitenga nao na kuwaambia “Bado tunajifunza“.  Hii ndiyo siri ya kushinda.

(9)      WANAFUNZI WA YESU BAHARINI (MST. 16-21)

Katika safari yetu baharini au ulimwenguni, kila mwanafunzi wa Yesu katikati yetu, sharti atakutana na upepo mkuu.  Hata hivyo wakati wowote wa magumu, Yesu huwa pamoja nasi akisema, “Ni mimi usiogope“.  Tukijua hivyo na kuacha kubabaika, mara mlango wa kutokea utaonekana na kwa muujiza mkubwa chombo kitafika salama nchi kavu kufumba na kufumbua (1 WAKORINTHO 10:13).

(10)    KUMTAFUTA YESU KWA BIDII (MST. 22-25)

Ili tumwone Yesu, hatuna budi kumtafuta kwa bidii kama watu hawa (MITHALI 8:17).  Kumtafuta Yesu kwa bidii, ni kulitafuta Neno lake kwa bidii na kulitendea kazi.  Tusiridhike na hatu yoyote tuliyoifikia katika kulijua Neno la Mungu, bali tulitafute Neno zaidi na zaidi (1 WAKORINTHO 10:13).  Tuhakikishe tunahudhuria kila ibada kwa gharama yoyote, na kuwa na moyo wa kujifunza kila siku, na kwa hakika tutamwona Yesu atakavyotubariki kiroho na kimwili.

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s