UFAHAMU KUHUSU MIUJIZA YA MUNGU NA JINSI YA KUZIFAHAMU ISHARA NA AJABU ZA UONGO ZA SHETANI NA MANABII WAKE WA UONGO

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

 

SOMO 15.

UFAHAMU KUHUSU MIUJIZA YA MUNGU NA JINSI YA KUZIFAHAMU ISHARA NA AJABU ZA UONGO ZA SHETANI

NA MANABII WAKE WA UONGO

 

NENO LA MSINGI:

2 WATHESALONIKE 2:9:

“Yule ambaye kuja kwake ni kwa mfano wa KUTENDA KWAKE SHETANI, KWA UWEZO WOTE, NA ISHARA NA AJABU ZA UONGO.”

<><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><> 

K

atika somo la leo la Kanisa la Nyumbani, tunajifunza somo muhimu linaloambatana na majira tuliyo nayo ya nyakati za mwisho.  Siku hizi, mahali pengi duniani ikiwamo Tanzania, kumezuka watu wa kila namna wakisema ni watumishi wa Mungu na kwamba wamepewa karama ya kutenda miujiza kwa ajili ya kuwasaidia watu.  Kwa sababu hii, watu kila mahali wanamiminika kuwafuata, wakihitaji watoto au uponyaji mbalimbali wa mwili.  Sehemu nyingine watu hao wanaodaiwa kuwa ni watumishi wa Mungu, wanatumia maji ya baraka kuponya; wengine wanatumia sanamu ya Bikira Maria; wengine wanawapeleka watu makaburini; wengine wanakwenda kupewa maji mahali inaposemekana alitokea Bikira Maria; wengine wanapewa madaftari ambamo humo wameandikiwa kwamba “Mungu” amesema watazaa mtoto wa kiume na wameandikiwa jina la kumwita, au mtoto wa kike na jina ambalo “Mungu” amemchagulia, na kupeleka madaftari hayo kila mara kuombewa na kukatazwa kwenda kliniki n.k.  Wengine wamebeba “mimba” zilizotokana na maombezi ya watu hawa kwa miaka miwili bila kujifungua na kupata mateso makali mno.  Wengine wameshuhudia kwamba wamepona kabisa baada ya kuhudumiwa na watu wa jinsi hiyo.  Hapa ndipo penye mtego.  Ili tusinaswe na mitego ya namna hii, Kanisa la Mungu linapaswa kufahamu Biblia inasema nini kuhusu Miujiza, Ishara na Ajabu za Mungu na zile za Shetani.

 

SHETANI ANA UWEZO WA KUFANYA MIUJIZA, ISHARA NA AJABU ZA UONGO

Miujiza kadhaa kwa kipimo kidogo cha uwezo ulio na mpaka.  Wakati wana wa Israeli walipokuwa hawajatoka Misri, waganga na wachawi wa Farao, walifanya miujiza kwa uwezo wa shetani:

(a)       Wachawi hawa walipozibwaga fimbo zao chini, ziligeuka kuwa nyoka kwa mfano wa muujiza alioufanya Mungu kwa kuwatumia Musa na Haruni [SOMA KUTOKA 7:8-12]

 

(b)       Wachawi hawa walifanya muujiza wa kubadilisha maji kuwa damu kwa mfano wa muujiza alioufanya Mungu kwa kuwatumia Musa na Haruni [SOMA KUTOKA 7:19-22].

 

Unaona!  Shetani ana uwezo wa kufanya miujiza na ishara.  Biblia inasema katika:

UFUNUO WA YOHANA 16:14:

Hizo ndizo roho za MASHETANI, zifanyazo ishara, zitokazo na kuwaendea wafalme wa ulimwengu wote, kuwakusanya kwa vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi.”

Wakati wa dhiki Kuu, roho za Mashetani zitafanya ishara kubwa, hata kufanya moto kutoka mbinguni uje juu ya nchi mbele ya wanadamu.  [SOMA UFUNUO 13:11-13].

Lakini pamoja na ufahamu huu ulio nao sasa kwamba Shetani ana uwezo wa kufanya ishara na miujiza, bado inakupasa kufahamu jambo moja.  Shetani ana mpaka katika uwezo wake wa kufanya miujiza.  Hana uwezo wa Mungu wa KUTENDA MAMBO YOTE.  Shetani hawezi kutenda mambo yote.  Wachawi na waganga wa Farao ingawa walifanya miujiza tuliyoiona, hata hivyo walishindwa kufanya muujiza alioufanya Mungu kwa kuwatumia Musa na Haruni; pale walipoyabadilisha mavumbi ya nchi kuwa chawa.  Wachawi hao waliposhindwa walikiri mbele ya Farao kwamba uwezo wa Mungu uko juu mno kuliko uwezo wao.  [SOMA KUTOKA 8:16-19]Wachawi na waganga wa Farao pia walishindwa kuzuia majipu yenye kufura yaliyotumbuka juu ya wanadamu wote wa Misri kutokana na mavumbi aliyoyarusha Musa hewani.  Wachawi hao nao walipigwa majipu hayo [SOMA KUTOKA 9:8-11].  Fimbo ya Haruni ilizimeza fimbo za wachawi kudhihirisha uwezo wa Mungu ulivyo mkubwa mno kuliko wa majeshi yote ya shetani [SOMA KUTOKA 7:11-12].

 

ISHARA, AJABU NA MIUJIZA YA SHETANI WAKATI WOTE INA  LENGO LA KUWAPOTEZA WANADAMU ILI WAANGAMIZWE

MATHAYO 24:24:

“Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu WAPATE KUWAPOTEZA, kama yamkini, hata walio wateule.”

Ishara, ajabu na Miujiza ya Shetani ndiyo maana inaitwa pia “NGUVU YA UPOTEVU” kwa jinsi ambavyo miujiza hiyo ilivyo madanganyo ya udhalimu kwa hao wanaopotea ambao hawataki kuiamini kweli ya Mungu na kuokolewa na hatimaye kuzidi kuipenda kweli katika wokovu.  Nguvu hiyo ya upotevu juu ya wanadamu, hatimaye inawafanya wanadamu hao kuhukumiwa na kwenda Jehanum ya moto.  [SOMA 2 WATHESALONIKE 2:7-12].  Kwa sababu hii, Kanisa la Mungu lazima liwe macho na kufahamu waziwazi jinsi ya kuzifahamu ishara, ajabu na miujiza ya Shetani na kutofautisha na ile itokanayo na Mungu.  Kwa maarifa haya, ni rahisi kuziepuka kazi zote za Shetani na manabii wake; na pia kuwasaidia wengine waliokwisha kunaswa.

 

ALAMA TISA ZINAZOAMBATANA NA ISHARA, AJABU NA MIUJIZA

 INAYOTOKANA NA MUNGU

Kwa kuangalia alama hizi tisa zifuatazo, na kuhakikisha kwamba ZOTE ZINAKUWEPO; ndipo tunapoweza kuzitambua ishara, ajabu na miujiza inayotokana na Mungu na kuifahamu na kukwepa miujiza ya Shetani na manabii wake:

(1)       Mtu anayetumiwa kufanya ishara, ajabu au miujiza na Mungu, inabidi awe ameamini au kuokolewa;  akikiri mwenyewe wokovu ulio katika Kristo Yesu na kuushuhudia.

MARKO 16:17;  “Na ishara hizi zitafuatana na hao WAAMINIO …..”.

Mtu yeyote asiyeokolewa na kukiri wokovu na kuushuhudia, hawezi kufanya miujiza itokanayo na Mungu.  Miujiza hiyo hutokana na Shetani.

(2)       Huduma ya Uponyaji au Ishara yoyote inayotokana na Mungu lazima iambatane na Biblia au Neno la Mungu kwa kuwa Neno la Mungu ndiyo dawa ya Ugonjwa na tena ndilo linalofanya

miujiza.  Huduma yoyote ya uponyaji wa miujiza isiyoambatana na Biblia au Neno la Mungu, inatokana na Shetani.

ZABURI 107:20:      “HULITUMIA NENO LAKE, HUWAPONYA, huwatoa katika                                                   maangamizo yao.”

MITHALI 4:20-22:    “Mwanangu, SIKILIZA MANENO YANGU; ….UZISIKIE KAULI                                              ZANGU …..MAANA NI UHAI kwa wale wazipatao, na AFYA YA                                            MWILI WAO WOTE.”

YOHANA 6:63:         “…..MANENO HAYO NILIYOWAAMBIA niroho tena NI                                                            UZIMA.”

(3)       Huduma yoyote ya Uponyaji wa Miujiza inayotokana na Mungu, LAZIMA iambatane na kuhubiri Injili na kufundisha Neno la Mungu, Angalia maandiko:

(a)       HUDUMA YA YESU:

(i)         Kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao na vipofu kupata kuona tena, KULIAMBATANA na kuwahubiri maskini habari njema [SOMA LUKA 4:18].

(ii)          Yesu alipokuwa akifundisha Neno la Mungu ndipo uweza wa Bwana ulipokuwapo kuponya:

LUKA 4:17:

“Ikawa siku zile mojawapo ALIKUWA AKIFUNDISHA …. NA UWEZA WA BWANA ULIKUWAPO APATE KUPONYA.”

 

(4)       YESU ALIPOWATUMA WANAFUNZI KUFANYA HUDUMA YA UPONYAJI

Wakati wote Yesu Kristo alipowatuma wanafunzi wake na kuwapa uwezo wa kuponya maradhi, au kuwaambia wapoze wagonjwa kwa miujiza; jambo hilo LILIAMBATANA na kutumwa kuhubiri au kuutangaza ufalme wa Mungu.  Mambo haya mawili lazima yaende pamoja.

LUKA 9:1-2: “Akawaita wale Thenashara, akawapa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi.  Akawatuma WAUTANGAZE UFALME WA MUNGU NA KUPOZAWAGONJWA.”

LUKA 10:1-2, 9:  “Basi, baada ya hayo Bwana aliweka na wengine,sabini, akawatuma wawili wawili …. Akawaambia … WAPOZENI WAGONJWA waliomo, WAAMBIENI, UFALME WA MUNGU UMEKARIBIA.”

MATHAYO 10:7-8:  “Na katika kuenenda kwenu, HUBIRINI,mkisema, Ufalme wa Mbinguni umekaribia.  POZENI WAGONJWA, FUFUENI WAFU, TAKASENI WENYE UKOMA, TOENI PEPO; mmepata bure, toeni bure.”

Katika kujifunza juu ya Huduma ya Yesu ya miujiza na uponyaji, na ile ambayo aliwapa wanafunzi wake; umeona kwamba kuponya wagonjwa kwa miujiza na kufanya ishara na ajabu zinazotokana na Mungu, LAZIMA kuambatane na kuhubiri Injili, na kuwaambia watu watubu dhambi zao na kuokolewa maana ufalme wa Mungu umekaribia.  Ukimwona mtu anasema ni mtumishi wa Mungu na kwamba eti amepewa karama na Mungu kuponya wagonjwa, halafu akawa nyumbani kwake tu au ofisini kwake na watu wanamwijia kuponywa bila kuelezwa habari za kutubu na kuokolewa, ufahamu huyo ni nabii wa uongo, na anatumia NGUVU YA UPOTEVU ya Shetani kufanya ishara za uongo.  Uponyaji wa Miujiza wa Mungu hauwi kama hospitali ambapo watu wanaenda kupewa vidonge tu bila kuhubiriwa Injili.  Miujiza lazima iambatane na kuhubiri Injili.  Mtu ukimsikia anasema yeye amepewa karama na Mungu kuponya wagonjwa tu, lakini hakupewa karama ya kuhubiri; hivyo kuhubiri amewaachia wengine, ujue huyo ni nabii wa uongo.  Yeyote aliyepewa kufanya miujiza na Mungu, pia huyohuyo atahubiri Injili.  Yesu, Petro, Paulo, Filipo na yeyote katika Biblia walifanya miujiza PAMOJA NA kuhubiri Injili.

Uponyaji wowote, muujiza wowote, au ishara yoyote inayofanywa kutokana na Mungu LAZIMA IFANYWE KWA JINA LA YESU SOMA:  LUKA 10:17; MATENDO 4:30; MARKO 16:17; MATENDO 3:6;  MATENDO 4:10; MATENDO 3:13, 16; MATENDO 16:18. Jina la Yesu, ndilo linalomtia mtu dhaifu, nguvu.  Imani katika Yesu ndiyo inayoleta uzima [MATENDO 3:16].  Ukimwona mtu anayejiita mtumishi wa Mungu na kwamba anaombea wagonjwa, lakini halitumii Jina la Yesu ila anamtaja “Mungu” tu; ujue mtu huyo ni nabii wa uongo.  Hakuna muujiza wowote wa Mungu pasipo kulitaja jina la Yesu!  “PEPO WANATUTII KWA JINA LAKO”, “KWA JINA LANGU WATATOA PEPO.”  Siyo kwa jina la Mungu au kwa kumtaja Mungu ila kwa jina la Yesu.  LAZIMA Yesu atajwe katika kuufanya muujiza unaotokana na Mungu.

(5)       Mtu anayetumiwa kufanya miujiza, ishara au ajabu na Mungu, hukusanya pamoja na Yesu, na kutumia miujiza kuliongeza Kanisa la Mungu kwa wale waaminio au wanaookolewa.  Lengo la Mungu kutoa uwezo wa kufanya miujiza kwa watumishi wake, ni kuwafanya wasioamini waweze kuamini kwa kuziona nguvu za Mungu.  Huduma yoyote ya miujiza isiyokuwa na lengo la kuwaongeza walioamini kwa Bwana Yesu au katika Kanisa la Mungu siyo huduma ya Mungu.

MATENDO 5:12,14:

“Na kwa mikono ya mitume zikafanyika ishara na maajabu mengi katika watu; ….walioamini wakazidi kwa Bwana, wengi, wanaume na wanawake”.

Miujiza hutumika kukusanya watu na kuwaleta katika Kanisa ambalo kiongozi wake ni Yesu [SOMA PIA LUKA 11:23; MATHAYO 23:37; ZABURI 50:5].

(6)       Mtu anayetumiwa kufanya ishara na Mungu, inabidi awe na Kanisa ambako anaongozwa na kutoa ripoti ya huduma yake inavyokwenda; au ni lazima afanye huduma yake kwa kushirikiana na Makanisa ya Mungu [SOMA MATENDO 14:27; MATENDO 21:17-19].

Tukimwona mtu ambaye inasemekana anafanya miujiza na hashirikiani na makanisa ya Mungu katika huduma yake, au hana Kanisa lolote ambalo anaongozwa na kutoa ripoti ya huduma yake inavyokwenda; basi, ufahamu huyo anatumia “Nguvu ya Upotevu” ya Shetani na ni nabii wa uongo.

(7)       Ishara, ajabu, au miujiza inayotokana na Mungu; hutusogeza katika kumjua, kumwabudu, kumtumikia Yesu Kristo na kushika maagizo yake pamoja na kweli yote ya Neno la Mungu.  Tukiona huduma ya miujiza ambayo inaambatana na maagizo yaliyo kinyume na Neno la Mungu katika nyakati tulizo nazo, kwa mfano kutumia sanamu ya Bikira Maria au sanamu ya Yesu, kufukiza uvumba, kutumia Rozari, kuzuru makaburi, kutumia maji ya baraka, kuwaomba wafu watuombee n.k.; basi tufahamu kwamba huduma hiyo siyo ya Mungu bali ni ya nabii wa uongo. [SOMA KUMBUKUMBU 13:1-4].

(8)       Mtu anayetumiwa na Mungu kufanya ishara, miujiza au uponyaji wowote; hatapokea fedha au zawadi yoyote KABLA ya ishara, muujiza au uponyaji huo au BAADA ya ishara hiyo au uponyaji huo.  Sadaka yoyote itaelekezwa katika kazi ya Mungu iwe Kanisani au namna nyingine na siyo kumpa mtu huyo binafsi kama “asante” ya huduma.  Uponyaji au Muujiza wa Mungu wakati wote ni BURE!  [SOMA:2 WAFALME 5:14-16; DANIELI 5:16-17; 1 WAFALME 13:6-7; MATENDO 8:18-20; MATHAYO 10:8]

(9)       Uponyaji wowote wa Muujiza, au ishara yoyote inayotokana na Mungu; itakuwa ni kwa utukufu wa Mungu, na muujiza huo utampa utukufu au heshima Mwana wa Mungu Yesu Kristo.  Yesu Kristo ni LAZIMA atajwe na kupewa utukufu au heshima yote.  Hatatajwa Mungu tu, ila lazima atajwe Yesu Kristo pia.  Ikiwa mtu anatukuzwa au kupewa heshima kwa miujiza au ishara azifanyazo na kukubali utukufu huo kama Mganga bingwa, na akaendelea kuzifanya ishara hizo, basi ufahamu kwamba huyo ni nabii wa uongo anayetumia “nguvu ya upotevu.”  Mungu KAMWE hampi utukufu wake mwanadamu.

YOHANA 11:4

“Naye Yesu aliposikia, alisema, Ugonjwa huu si wa mauti, bali ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu, ILI MWANA WA MUNGU ATUKUZWE KWA HUO”.  [SOMA PIA ISAYA 42:8; ISAYA 48:11].

Barnaba na Paulo walipotumiwa na Mungu kufanya miujiza na watu wakawapa utukufu kana kwamba ni Miungu, MARA ILE ILE waliukataa utukufu wowote na wakamwinua Mungu aliye hai wakati huohuo.  [SOMA MATENDO 14:8-18].  Wasingefanya hivyo, ingekuwa ni hatari kwao.  Herode alipopokea utukufu kana kwamba ni Mungu, pale pale alipigwa na malaika wa Bwana kwa sababu hakumpa Mungu utukufu na akaliwa na chango na kutokwa na roho  [SOMA MATENDO YA MITUME 12:21-23].

 

H U K U M U

Watu wafanyao ishara na ajabu za uongo za Shetani na kuwapoteza watu, wasipotubu, hukumu yao itakuwa pamoja na manabii wote wa uongo.  Mahali pao ni katika ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti.  KUMBUKUMBU 13:1-5.  Watu wanaowaendea kutafuta ishara, miujiza au uponyaji na kuuamini uongo huo na kuwatetea kwamba ni watumishi wa Mungu kwa sababu walifanya muujiza fulani n.k.; wasipotubu, hao nao WATAHUKUMIWA na kutupwa katika ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti.  [SOMA 2 WATHESALONIKE 2:9-12].  Inakupasa ujilinde, usiwe miongoni mwao.

 

U O N G O   W A   S H E T A N I

Shetani siyo Muumbaji.  Kamwe hana uwezo wa kuumba!  Kwa sababu hii, pamoja na nguvu yake ya upotevu, shetani hawezi kumpa mtu mtoto.  Ampate wapi?  Ilivyo ni kwamba, Shetani ni mjanja, anapowaona watu wakienda kutafuta watoto kwa manabii kama hawa wa uongo, huwasoma watu hao walivyo.  Wengine huwa siyo kwamba wana tatizo lolote.  Ujauzito unaweza ukawa umechelewa tu kutokana na sababu za kawaida tu na hofu ya watu hao ikawafanya waende kwa nabii huyo wa uongo.  Shetani ndiye mleta hofu na tena huweza kumuunganisha mtu na nabii wake wa uongo.  Anapompata mtu mmoja wa namna hii, na baadaye akapata ujauzito katika hali ambayo ingekuwa ni ya kawaida tu, huutumia “muujiza” huo wa uongo kuwapoteza maelfu ya watu.  Ndiyo maana kwa manabii hawa wa uongo, utaona ni wachache sana wanaosemekana wameombewa na kupata mtoto.  Wengi huenda hapo na kusikia hadithi ya mmoja au wawili kwa muda mrefu uliopita.  Ukiwauliza wanasema “Nasikia yuko mmoja alipata mtoto, tena yeye alikuwa mwislamu.”  Zote hizi ni kazi za uongo za Shetani ili kuwapoteza wengi.  Walio wengi wanakwenda huko kwa miaka mingi wakisumbuka na kuteseka na kupata “mimba bandia”.  Utamwona mtu tumbo lake kubwa lakini hajifungui.  Akipimwa kliniki, haonekani mtoto.  Wengine wamekuwa na mimba miaka karibu miwili na mtoto haonekani.  Wengine wanasema ninasikia kitoto kinacheza kwa miaka!  Yote haya ni mapepo.  Baada ya mapepo haya kukemewa kwa Jina la Yesu, yanahama na mtu huyo kuwa huru.  Inatupasa kumwamini Mungu aliye hai.  Yeye aliyempa Zakaria na Elisabeti mtoto wa ajabu, Yohana Mbatizaji katika uzee wao; anaweza kumpa mtoto kila amwaminiye.  Yeye aliyempa Ibrahimu na Sara mtoto wa ahadi Isaka na kumpa Hana mtoto wa ajabu Samweli aliyekuwa nabii mkubwa, ana uwezo wa kumpa mtoto yeyote aaminiye.  Mwamini tu Yesu, utaona mambo ya ajabu!

 

TOFAUTI YA “Mungu” NA “mungu”

Neno “Mungu” na “mungu” katika kutamka, yanatamkwa vilevile.  Ni katika maandishi tu; ndipo unapoweza kuyatofautisha kutokana na herufi kubwa “M” na herufi ndogo “m”.  Ukiamua kuandika herufi zote za majina hayo kuwa kubwa, utaona majina hayo tena yanafanana!  Hapa ndipo penye mtego mkubwa wa Shetani. Waganga wa Kienyeji na manabii hawa wa uongo, hutumia “mungu” yenye herufi ndogo “m” wanapokuwa wanamtaja “mungu” wao Shetani.  Wao ni watumishi wa “mungu” na kamwe wao siyo Watumishi wa Mungu!  Huyo “mungu” wao shetani naye anatoa karama za uponyaji za udanganyifu, anapompa nabii wake ruhusa ya kutumia pepo wa uaguzi [MATENDO 16:16] na pepo wake wa utambuzi

[1 SAMWELI 28:7]  Siyo kusudi la somo letu leo kujifunza jinsi pepo wa uaguzi na pepo wa utambuzi wa shetani wanavyofanya kazi ya udanganyifu, hata hivyo jambo moja tu ni kwamba kuwaendea waganga hawa wanaotumia pepo hawa, ni kumwendea shetani yaani “mungu” wa dunia hii na kutafuta kifo [SOMA 1 NYAKATI 10:13-14].

Manabii hawa wa uongo wanaotumia nguvu ya upotevu, wanapoombea wagonjwa, humwita “mungu” wao shetani.

Angalia tofauti ya “mungu” ikimaanisha shetani na “Mungu” ikimaanisha Mungu aliye hai

[SOMA YONA 1:5-6; 2 WAKORINTHO 4:3-4].

Manabii hawa wa uongo, au waganga wa kienyeji, WANAJUA KABISA kwamba “mungu” wao ni shetani maana huwasiliana naye kama “BOSS” wao na kuwadanganya watu kuwa ni Mungu!  Mara nyingi wanapoandika hupenda kutumia herufi kubwa “MUNGU” ili kuzidi kuwadanganya na kuwapoteza wengi wakidhani ni Mungu aliye hai kumbi ni “mungu”.

 

UFAHAMU ZAIDI KUHUSU MIUJIZA YA MUNGU

Nyakati hizi za mwisho, pamoja na kujifunza yote tuliyojifunza, bado tunahitaji kufahamu zaidi ya haya, kuhusu miujiza; ili tusipeperushwe na “elimu kwa uongo” ya Shetani kuhusu miujiza.  Yafuatayo ni muhimu kuyafahamu kuhusu miujiza ya Mungu.

(1)          MIUJIZA YA MUNGU HAIFANYIKI ILI KUMTHIBITISHA MTU KUWA NI 

MTAKATIFU

Watu wengi waliookoka nyakati hizi, wamevamiwa na elimu potofu kudhani kwamba miujiza inathibitisha kwamba mtu yule aliyehudumu madhabahuni au mkutanoni au katika huduma ya aina yoyote ni mtakatifu sana.  Kutokana na mawazo haya potofu utasikia kundi la watu lililoandaa mkutano likisema “Mungu ameonyesha kwamba hakuna tatizo katika namna yetu ya kuenenda katika wokovu.  Umeona miujiza iliyofanyika?  Ingekuwa tunayoyafanya siyo sawa mbele za Mungu, miujiza yote hii ingefanyika kwetu?”  Utasikia wengine wakisema “Unaona!  Ingekuwa Mchungaji huyu ana hatia mbele za Mungu, je miujiza ingefanyika namna hii katika huduma yake?”  Watu wametumia uwepo wa miujiza kuhalalisha dhambi.  Huku ni kukosa maarifa:

 

(a)       MIUJIZA YA MUNGU HULITHIBITISHA NENO LA MUNGU

Ishara na miujiza hufanyika kulithibitisha NENO na siyo kumthibitisha Mchungaji au kulithibitisha kundi au kulithibitisha Kanisa kwamba linakwenda sawasawa na mapenzi ya Mungu.

MARKO 16:20:

“Wao wale wakatoka, wakahubiri kotekote, Bwana akitenda kazi pamoja nao, NA KULITHIBITISHA LILE NENO KWA ISHARA zilizofuatana nalo.”

(b)       MIUJIZA YA MUNGU HAIFANYIKI KUTOKANA NA UTAKATIFU AU NGUVU ZA MHUDUMU AU NGUVU ZA KUNDI LILILOANDAA MKUTANO

MATENDO 3:12:

“Hata Petro alipoyaona haya akawajibu wale watu, Enyi Waisraeli mbona mnastaajabu haya, au mbona mnatukazia macho sisi, kana kwamba tumemfanya huyu aende KWA NGUVU ZETU SISI, AU KWA UTAUWA (UTAKATIFU) WETU SISI?”

(c)        MIUJIZA YA MUNGU HUFANYWA NA MUNGU KWA AJILI YA NAFSI YAKE MWENYEWE NA SIYO KUTOKANA NA NAFASI YA MTU YEYOTE

Mungu anapofanya miujiza, huifanya kwa ajili ya nafsi yake na kwa ajili ya kujitukuza yeye mwenyewe, na siyo kumtukuza Mchungaji aliyehudumu, au kulitukuza kundi au Kanisa lililoandaa mkutano.

ISAYA 48:11

“Kwa ajili ya nafsi yangu, kwa ajili ya nafsi yangu, nitatenda haya; je! litiwe unajisi jina langu?  WALA SITAMPA MWINGINE UTUKUFU WANGU.”

 

(2)       KUHANI AU MCHUNGAJI ANAYEHUDUMU MKUTANO, ANAWEZA AKAWA KATIKA DHAMBI, NA MIUJIZA BADO IKAWA INATENDEKA

Watu wengine wanafikiri kwamba Kuhani aliyetiwa mafuta, hawezi kufanya dhambi.  Wanafikiri Askofu, Mchungaji, au Mwinjilisti maarufu hawezi kuwa katika dhambi na akawa ameanguka.  Huku ni kukosa ufahamu.  Makuhani waliotiwa mafuta wanaweza kukosa mno na kuwa katika machukizo kama ya mataifa wakimpa nafasi Ibilisi:

MAMBO YA WALAWI 4:3:

“Kama Kuhani aliyetiwa mafuta akifanya dhambi, hata analeta hatia juu ya watu……”.

 

2 MAMBO YA NYAKATI 36:14:

” Na zaidi ya hayo wakuu wote wa makuhani, na watu WAKAKOSA MNO sawasawa na machukizo yote ya mataifa; wakainajisi nyumba ya BWANA aliyoitakasa katika Yerusalemu.”

 

Ndiyo maana Biblia inatupa ushauri wa kufuata kuhusu viongozi wetu wa kiroho.  Inatupasa kuiga imani yao BAADA ya KUUCHUNGUZA SANA MWISHO WA MWENENDO WAO na kuulinganisha na maandiko [SOMA WAEBRANIA 13:7].  Tukiona mwenendo wa Kiongozi fulani wa kiroho hata kama ni wa ngazi ya juu kiasi gani, hauendani na maandiko, kamwe tusiifuate imani yake na kuhalalisha dhambi anayoifanya.

Sasa basi, ukiyajua haya; bado kunakuwa na mtego mkubwa zaidi.  Kuhani aliyetiwa mafuta, akiwa katika hali ya dhambi; anaweza kuhudumia mikutano na miujiza mikubwa ikatendeka.  Katika miaka ya 1940, alikuwepo Mhubiri maarufu sana huko Marekani akijulikana kwa jina la A.A. ALLEN.  Huduma ya mhubiri huyu iliambatana na miujiza mikubwa na ilivuta watu wengi sana.  Jambo la kuhuzunisha ni kwamba alipokufa, madaktari walithibitisha kwamba alikufa kutokana na ulevi wa kiwango cha juu sana; baada ya kufanya uchunguzi wa damu yake na mengineyo katika kuipima maiti yake.

Mhubiri mmoja mwingine huko Nigeria, akiwa ametoka tu kuzini na mwanamke saa za mchana, aligongewa hodi na mgonjwa mmoja aliyetaka maombezi.  Mhubiri huyu alikuwa na sifa kubwa ya miujiza mikubwa kutendeka katika huduma yake.  Mgonjwa huyu akiwa katika hali ya kukaribia kufa alikuja pale akijua kwamba akiombewa anaweza kupona.  Mhubiri yule alipomwona mgonjwa yule na kuiona hali yake, na kuwaza kwamba anataka yeye amwombee wakati ametoka kwenye uzinzi; alipiga magoti na kuanza kuomba kwa machozi kwamba Mungu amsamehe kwa upumbavu alioufanya. Lugha aliyokuwa akiitumia Mhubiri huyu kuomba msamaha kwa Mungu, ilikuwa ni lugha ambayo yule mgonjwa alikuwa haijui.  Kutokana na sababu hii ya kutokuijua lugha, yule mgonjwa alidhani yule Mhubiri anamwombea awe mzima.  Muda mfupi tu, yule mgonjwa akarukaruka na kusema “Bwana asifiwe nimepona.”  Akaondoka kwa furaha sana akirudi nyumbani kwa shangwe baada ya kupokea muujiza huo mkubwa. Yule mhubiri akabaki amechanganyikiwa.  Kwa maneno yake alipokuwa akizungumza na Mchungaji mmoja wa Kanisa moja kubwa huko Lagos anasema “Nimechanganyikiwa.  Njia za Mungu ziko juu sana sizielewi.  Mimi nilikuwa ninatubu dhambi ya uzinzi kwa machozi.  Mgonjwa akafikiri ninamuombea.  Kwa yeye kuamini hivyo akawa mzima mara moja.  Sikuomba lolote juu yake.  Nisingeweza kuomba lolote juu yake katika hali ya kuhukumiwa niliyokuwa nayo.  Ninashangaa hii ni nini!”

Iko mifano mingi ya miujiza iliyotendeka katika huduma iliyo dhahiri katika dhambi. Mhubiri mmoja maarufu Marekani mwenye wake wawili lakini pamoja na hali hiyo, vilema wanatembea, vipofu wanaona na miujiza mikubwa inatendeka katika huduma yake.  Nafasi haitoshi kueleza mifano mingi ya jinsi hii.  Ukisoma Kitabu kinachoitwa “All things are possible”  kilichoandikwa na J. Buckingham, utaona mifano tele!   Sasa swali ni kwamba, kwa jinsi gani miujiza inaweza kufanyika katika hali hii ya dhambi?  Yafuatayo ni majibu:-

 

(a)       IMANI YA MTU BINAFSI ANAYELISIKIA NENO

Yesu Kristo mara nyingi aliwaambia watu “Imani yako imekuponya”

[ANGALIA MATHAYO 9:22; MARKO 10:52]  Yesu pia aliwaambia wengine “Kadri ya Imani yenu mpate” na mara wakafumbuka macho yao [SOMA MATHAYO 9:29-30].  Unaweza kuona hapa kwamba imani ya mgonjwa mwenyewe inaweza ikamfungua mtu yule na muujiza ule usiwe na uhusiano wowote na Mhubiri.  Biblia inasema pia kwamba Imani chanzo chake ni kusikia, na kusikia huja kwa neno la Kristo.  [SOMA WARUMI 10:17].  Mgonjwa anapokuja mkutanoni akiwa hajui lolote kuhusu maisha ya mhubiri, na kusikia Neno la Kristo kwamba Yesu huponya hata leo kwa kuwa yeye habadiliki; mara hupata imani na imani hiyo kumfanya mara moja awe mzima pamoja na Mhubiri yule kuwa katika dhambi.

 

(b)       NENO LA MUNGU KUTHIBITISHWA [MARKO 16:20]

Mahali popote ambapo watu wengi watakusanyika katika mkutano wa Neno la Mungu, lazima neno la Mungu lithibitishwe.  Wahubiri wengi wameifahamu siri hii.  Ukitaka kuona miujiza mikubwa, jambo la kufanya ni kukusanya maelfu au malaki ya watu kuhudhuria kwenye mkutano.  Palipo maelfu ya watu, kuna mengi.  Wengine wanaweza wakawa wametoka mbali sana huenda mamia ya maili kufuata mkutano, huku wakitaka kuona kama kweli Yesu Kristo yuko hai leo.  Wengine wanaweza kuwa waislamu wakiwa wamekuja huku wakibishana na kusema kwamba “Watu hawa ni waongo, haiwezekani kabisa mtu akaponywa eti kwa kuomba kwa jina la Yesu tu.  Huu ni ujanja wao ili kuwafanya watu wengi wawe Wakristo.  Wanachukuana wao kwa wao na kushuhudia uongo.  Ingekuwa ni kweli, basi kwa jina la Mtume Mohammed, tungeona miujiza mikubwa zaidi maana yeye ndiye nabii wa mwisho.”

Mahali pa namna hii, hata kama mhubiri anayehubiri ametoka katika uzinzi au kundi lililoandaa mkutano liko mbali na kweli, ili mradi tu Mhubiri ahubiri Injili ya wokovu na kumtaja Yesu anayeokoa na kuponya, basi miujiza mikubwa itatendeka bila kujali maisha ya mhubiri au hali ya kundi lililoandaa mkutano.  Mungu hayuko tayari kuona malaki ya watu wakiondoka na kulitukana Neno kwamba siyo la kweli kwa sababu ya mhubiri mmoja tu madhabahuni au kundi la watu mia walioandaa mkutano.  Ni lazima alithibitishe Neno lake kwamba ni kweli.  Kwa kufanya hivyo, hamthibitishi mhubiri huyo au kundi hilo kama tulivyotangulia  kuona.

 

(c)       MUNGU ATAFANYA LOLOTE ILI KUZIOKOA ROHO ZINAZOANGAMIA

 

Biblia inasema roho zote za wanadamu ni mali ya Mungu [SOMA EZEKIELI 18:4]  Roho moja ya mwanadamu, ni ya thamani mno mbele za Mungu.  Ni zaidi sana roho za maelfu ya watu.  Mungu hapendi hata MMOJA apotee bali wote wafikilie toba kwa jinsi roho za watu aliowaumba zilivyo za thamani kubwa.  Ni kwa sababu hii ndiyo maana kuja kwa Yesu bado kunakawia [SOMA 2 PETRO 3:9]  Kutokana na ishara ambazo wagonjwa hufanyiwa, watu wengi sana huamua kumfuata Yesu [SOMA YOHANA 6:2]. Kwa sababu hii, wanapokusanyika maelfu ya watu, Mungu anajua kwamba kutokana na ishara kadhaa kwa wagonjwa anaweza kuziokoa roho zake nyingi.  Hataacha kazi yake muhimu ya kuziokoa roho zilizokusanyika kwa ajili ya upumbavu wa roho moja iliyo madhabahuni au roho chache zilizoandaa mkutano.  Roho itendayo dhambi ndiyo itakayokufa.  Ataendelea kufanya ishara ili kuzivuta roho za watu na kuziokoa kutokana na huruma yake.

 

(d)       MUNGU NI LAZIMA AJIPATIE UTUKUFU KATIKA UMATI WA WATU

Miujiza juu ya wagonjwa ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu [YOHANA 11:4]  Mungu anapofanya miujiza, hujipatia utukufu kwa wanadamu kwa jinsi ambavyo kazi zake zinavyodhihirishwa waziwazi [YOHANA 9:3].  Watu wanapomtukuza Yesu kutokana na kazi zake, ndiyo mwanzo wa kuvutwa katika ufalme wa Mungu [SOMA LUKA 7:14-16].  Kwa ajili ya nafsi yake, Mungu atafanya ishara ili ajipatie utukufu na kujionyesha kwamba hakuna mwingine ila yeye.  Hatakubali kulitia unajisi jina lake mbele ya maelfu ya watu kwa ajili ya mtu mmoja aliyesimama madhabahuni.  [ISAYA 48:11].

 

KARAMA ZA MUNGU HAZINA MAJUTO [WARUMI 11:29]

Mungu anapompa karama fulani mtu yeyote kwa Roho Mtakatifu, hajuti wakati wowote na kuziondoa.  Mhubiri fulani anaweza akawa alianza vizuri na mwisho wake ukawa mbaya.  Kwa kuwa karama za Mungu hazina majuto, bado utaona katika huduma ya mtu miujiza pamoja na udhaifu alio nao.

 

MAMBO MATATU YA KUJIFUNZA KUTOKANA NA UFAHAMU HUU

JUU YA MIUJIZA YA MUNGU

(1)       Ni kwa sababu hii Yesu alisema siku ya mwisho watakuwepo watu wengi watakaosema walitenda miujiza kwa jina lake na yeye atawaambia ”  Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu ninyi mtendao maovu” [SOMA MATHAYO 7:22-23].  Tumeona jinsi ambavyo mtu atendaye maovu anavyoweza kutenda miujiza kwa jina la Yesu.  Kufanya miujiza siyo kibali cha kuingia mbinguni bali utakatifu pekee ndiyo tiketi ya kumuona Mungu [WAEBRANIA 12:14].

(2)       Hata kama kwa Mhubiri fulani au katika mkutano fulani ulioandaliwa na kundi fulani au makanisa kadhaa kunatendeka miujiza mikubwa, KAMWE tusizithibitishe dhambi wanazozifanya kutokana na miujiza inayofanyika.  Hatuwezi kusema kuoa wake wawili ni halali kutokana na Mhubiri huyu wa Marekani aliyeoa wake wawili na anatenda miujiza kwa jina la Yesu.  Hatuwezi kusema Ubatizo wa maji tele siyo lazima kutokana na Mhubiri, kundi, au Kanisa linalopinga ubatizo wa Maji tele kuendelea kutenda miujiza.  MIUJIZA SIYO KIPIMO.  Neno la Mungu ndiyo kipimo Yuda alikuwa miongoni mwa wanafunzi ambao walitumwa na Yesu kuhubiri na pepo wakatoka katika huduma yake alipolitumia jina la Yesu.  Hata hivyo, Yuda yuko Jehanum leo.  Miujiza haikumfanya Yuda aingie mbinguni.

Kutokana na kukosa ufahamu huu, wengi wamepotoshwa na Shetani na kuwafuata wengi katika udhalimu wao wakipinga kweli ya Neno la Mungu.  hawa wanaolipinga Neno la Mungu huku wakisema “Hata kwetu mbona miujiza inatendeka” na ukazithibitisha dhambi zao na kuzifanya, utaangamia kama Yuda pamoja nao msipotubu.

(3)       Ikiwa katika huduma yako miujiza inafanyika lakini huendani sawa na Neno la Mungu, inakupasa kuliangalia Neno mara moja na kulifuata baada ya kutubu, au siyo utaangamia kama Yuda.

 

MIUJIZA KATIKA UTAKATIFU

Pamoja na miujiza kuweza kufanywa na watu waliookoka ambao wanatenda dhambi, hata hivyo; kiwango cha miujiza kinachofanyika mahali ulipo Utakatifu, kinakuwa cha juu mno.  Pasipo Utakatifu haiwezekani kufanya miujiza mikubwa kuliko ile aliyoifanya Yesu [SOMA YOHANA 14:12].  Wakati wa Kanisa la Kwanza, miujiza ya ajabu ilifanyika kutokana na kanisa kwenda sawasawa na Neno la Mungu.  Angalia mfano wa miujiza hiyo katika [MATENDO 5:15-16].

 

M A S W A L I

(1)       Je Shetani anaweza kufanya miujiza?  Kama jibu lako ni Ndiyo, toa maandiko ya kuthibitisha jibu hilo.

—————————————————————————————————————-

—————————————————————————————————————-

(2)       Lengo la miujiza ya Shetani ni nini?  Thibitisha jibu kwa andiko.

—————————————————————————————————————-

—————————————————————————————————————

(3)       Taja kwa kifupi alama tisa zinazoambatana na miujiza ya Mungu.

(a)————————————————————————————————————-

(b)————————————————————————————————————-

(c)————————————————————————————————————-

(d)————————————————————————————————————-

(e)————————————————————————————————————-

(f)————————————————————————————————————–

(g)————————————————————————————————————-

(h)————————————————————————————————————-

(i)————————————————————————————————————–

 

(4)       Je miujiza ya Mungu inafanyika ili kumthibitisha Mhubiri, Kundi lililoandaa mkutano au Kanisa?  Kama jibu lako ni siyo, thibitisha jibu lako kwa maandiko.

—————————————————————————————————————-

—————————————————————————————————————-

(5)       Je miujiza ya Mungu inafanywa kutokana na Utakatifu au nguvu za Mhubiri au kundi lililoandaa mkutano?  Kama jibu lako ni siyo, Toa maandiko ya kulithibitisha jibu lako.

—————————————————————————————————————-

(6)       Je Kuhani aliyetiwa mafuta anaweza akafanya dhambi?  Tumia maandiko kujibu.

—————————————————————————————————————-

—————————————————————————————————————-

(7)       Ni kwa sababu zipi tunaweza kuona miujiza mahali ambapo wahudumu wako dhambini?  Taja sababu tano.

(a)————————————————————————————————————-

(b)————————————————————————————————————-

(c)————————————————————————————————————-

(d)————————————————————————————————————-

(e)————————————————————————————————————-

(8)       Je kufanya miujiza ni kipimo cha kuingia mbinguni?  Taja mtu aliyefanya miujiza na kwenda motoni.

—————————————————————————————————————-

—————————————————————————————————————-

<><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><>< 

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “note” hii, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements

One comment on “UFAHAMU KUHUSU MIUJIZA YA MUNGU NA JINSI YA KUZIFAHAMU ISHARA NA AJABU ZA UONGO ZA SHETANI NA MANABII WAKE WA UONGO

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s