UHUSIANO WA MAGONJWA NA DHAMBI

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

 

SOMO:          UHUSIANO WA MAGONJWA NA DHAMBI

L

eo tena tunaendelea kujifunza Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu.  Leo, tunajifunza YOHANA 4:46-54, na YOHANA 5:1-19.  Ingawa kichwa cha somo letu ni, “UHUSIANO WA MAGONJWA NA DHAMBI”, kuna mambo mengi ya kujifunza katika mistari hii.  Tutayagwa mafundisho yote tunayoyapata katika mistari hii, katika vipengele sita:-

(1)NGUVU VYA ISHARA NA MAAJABU (4:46-48);

(2)KULISADIKI NENO LA MTUMISHI WA MUNGU (4:49-54);

(3)WATAKA KUWA MZIMA? (5:1-9);

(4)UHUSIANO WA MAGONJWA NA DHAMBI (5:10-14);

(5)KUUDHIWA KWA KUTOKUISHIKA SABATO (5:15-18);

(6)MSINGI MKUU WA KUFAHAMU YALE YALIYO DHAMBI (5:19).

 

(1)      NGUVU YA ISHARA NA MAAJABU (4:46-48)

Tunaona hapa Yesu akimwambia diwani mwenye mtoto mgonjwa, “Msipoona ishara na maajabu hamtaamini kabisa?”  Ishara, maana yake tendo lolote linalodhihirisha kwa dhahiri UWEZO WA MUNGU.  Maajabu, ni mambo yanayofanywa na Mungu, yanayomfanya mwanadamu kupigwa na mshangao, kwa kuwa ni tofauti na desturi au taratibu za kibinadamu.  Ishara na maajabu, yana nguvu ya ajabu katika kuihubiri Injili kwa utimilifu.  Wako watu wengi leo katika ulimwengu huu ambao, kama diwani huyu, hawawezi kumwamini Yesu, wasipoona ishara na maajabu.  Diwani huyu, alimwamini Yesu, yeye na wote wa nyumbani mwake, kutokana na ishara na maajabu aliyoyaona 4:52-53.  Huyu, ni mmoja kati ya watu wengi walioamini baada ya kuona ishara na maajabu YOHANA 2:11, 23; 7:31; MATENDO 13:12.  Watu wengi ambao hawajaokoka, watajengewa utayari wa kutusikiliza ikiwa wataona ishara na maajabu MATENDO 8:6.  Siyo hilo tu, ni rahisi kwa watu wengi kuthibitishiwa kwamba huduma zetu zimetoka kwa Mungu, ikiwa wataona ishara na maajabu YOHANA 3:2.  Ni muhimu kwa Kanisa kufahamu kwamba Neno la Mungu bila ishara na maajabu, linaweza kuleta mafanikio ya Injili kwa sehemu tu.  Wengi wasioweza kuamini kwa neno tu, ni rahisi kuamini kwa tendo, kwa ishara na maajabu WARUMI 15:18-19.  Kanisa la Kwanza lilifahamu sana siri hii, na lilidumu kuomba sana kwa ajili ya Viongozi wao, ili Mungu awatumie kufanya ishara na maajabu; nah ii ilikuwa siri ya mafanikio yao makubwa MATENDO 4:29-30, 33; 5:12-14.  Ni wajibu wa kila mmoja wetu basi kutokukridhika na ishara zozote tulizoziona bali kila siku inatubidi kumwomba Mungu kwa ajili ya Mchungaji wetu, ili azidi kutumiwa kufanya ishara na maajabu.  Mchungaji wetu akitumiwa na Mungu kufanya ishara kubwa, ni faida kubwa kwa Kanisa lote ambalo ndilo shamba letu la mizabibu.

 

(2)      KULISADIKI NENO LA MTUMISHI WA MUNGU – 4:49-54

Miujiza mikubwa inapatikana siyo kwa kumwamini Mungu tu, bali pia kwa kuyaamini maneno ya Watumishi wake 2 NYAKATI 20:20.  Ni muhimu kujizoeza kuchukua kwa uzito mkubwa kila neno la Mtumishi wa Mungu.  Akisema, “Enenda mwanao yu hai“, hilo ni neno la Mungu kwetu, tuliamini.  Tatizo, watu wengi wako kama Naamani.  Wao wanataka wawekewe mikono baada ya kueleza matatizo yao yote mojamoja kwa Mtumishi wa Mungu.  Bila hivyo, hawaamini 2 WAFALME 5:10-14.  Hapa tunaona mtoto wa diwani akipona bila kuwekewa mikono, tena akiwa mbali kabisa.  Tutafanya vema tukifuata mfano wa diwani.

 

(3)      WATAKA KUWA MZIMA?  – 5:1-9

Birika inayoitwa hapa BETHZATHA, kwa Kiebrania, ilikuwa ni BWAWA ambalo Mungu alilitumia nyakati za Biblia kama Hospitali ya Rufaa.  Malaika, pasipo kuonekana kwa macho aliyatibua maji.  Yalipokuwa kama maji yanayochemka, mtu wa kwanza kuingia majini, magonjwa yote sugu aliyokuwa nayo yalimwondokea.  Hapa kulikuwa hakuna mahubiri ya Neno, au suala la Imani.  Ulikuwa mpango wa Mungu wa wakati huo wa kuwatibu viumbe wake, kama anavyotumia madaktari leo.  Kwenda hospitali, kunywa dawa, au kukchomwa sindano, siyo dhambi.  Hospitali ni vyombo vya Mungu.  Luka, mwanafunzi wa Yesu alikuwa tabibu au daktari na pia Timotheo alishauriwa na Mtumishi wa Mungu Paulo kunywa daawa ya tumbo, na magonjwa mengine WAKOLOSAI 4:14; 1 TIMOTHEO 5:23.  Hata hivyo Yesu anatuuliza “Wataka kuwa mzima?“, maana yake, tunaamini kwamba anaweza kutuponya bila dawa au daktari, kwa muujiza?  Sawasawa na imani yetu, tunapokea kutoka kwake.  Mtu huyu hapa aliamini, akajitwika godoro lake na kwenda.  Sisi nasi tukiamini, yote yaliyoshindikana mahospitalini, yawezekana kwa Yesu.

 

(4)      UHUSIANO WA MAGONJWA NA DHAMBI – 5:10-14

“Angalia, umekuwa mzima, usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi”, ni mafundisho ya msingi anayotufundisha Yesu, kutuonyesha uhusianao wa magonjwa na dhambi.  Tukitokwa na mapepo au kuponywa magonjwa yetu kwa muujiza, halafu tukaendelea kufanya uasherati, kunywa pombe, kuvuta sigara, kucheza dansi, au kutenda dhambi nyinginezo, ni rahisi kurudiwa na mateso yaleyale MARA SABA ZAIDI – LUKA 11:24-26.  Magonjwa yalikuja kwa mwanadamu, baada ya dhambi kuingia ulimwenguni.  Magonjwa, ni laana inayoambatana na mtu asiyeshika au kulitenda Neno la Mungu KUMBUKUMBU LA TORATI 28:15, 58-61.  Daudi, alifahamu kwamba magonjwa yaliyompata yalitokana na dhambi alizozifanya ZABURI 38:3-7.  Tunapokuja kwa Yesu, kwa kutubu dhambi zetu na kumaanisha kuziacha, ndipo tunapopokea uzima tele; ikiwa tunataka kuombewa tu lakini hatutaki wokovu, Mungu humwachia Ibilisi azidi kututesa YEREMIA 14:19-20; HOSEA 5:15; MITHALI 1:24-28; ZABURI 103:3; MARKO 2:3-12.  HATA HIVYO, BAADA YA KUOKOLEWA NA KUISHI KATIKA Utakatifu, ikiwa tunaona udhaifu fulani na magonjwa bado yapo, hatupaswi kudanganywa na Ibilisi kwamba tumefanya dhambi tusizozijua.  Kudanganyika huko, hupunguza nguvu ya maombi yetu 1 YOHANA 3:21-22.  Elisabeti na Zakaria, walikuwa watakatifu, lakini walikuwa tasa LUKA 1:5-7.  Tunapoona hayo, magonjwa yetu huwa kwa Utukufu wa Mungu.  Tusisite kwa kutokuamini, na siku moja tutaona kwa dhahiri, Mungu akitukuzwa na wengi wakimwamini Yesu, kutokana na kuponywa magonjwa au udhaifu wetu YOHANA 9:1-3; 11:1-4.  Vivyo hivyo, ni muhimu kukumbuka kwamba tunakuwa na ushindi mkubwa juu ya Shetani, tukiwa mbali na udunia, au kufanya mambo kama mataifa katika kuvaa au kusema YAKOBO 4:4; WARUMI 12:2.

(5)      KUUDHIWA KWA KUTOKUISHIKA SABATO (5:15-18)

Yesu Kristo, aliivunja Sabato, hakuishika YOHANA 5:18; 9:16.  Kwa sababu hakuishika sabato, walimwudhi kwa maana kwamba walimwona hafai na kumnenea mabaya 5:16.  Sisi nasi, baada ya kuokoka, inatubidi kumfuata Yesu kwa KUTOKUISHIKA SABATO, maana ametupa kielelezo tumfuate YOHANA 13:15; 1 PETRO 2:21; WAKOLOSAI 2:16-17.  Tukifanya hivyo, tutaudhiwa na washika sabato.  Hatupaswi kuona ajabu YOHANA 15:20; WAGALATIA 4:29.

 

 (6)     MSINGI MKUU WA KUFAHAMU YALE YALIYO DHAMBI (5:19)

Kwa kuokolewa, tumefanyika wana au watoto wa Mungu WARUMI 8:14-16, YOHANA 1:12.  Mwana, hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile analoweza kulitenda Baba yake wa mbinguni.  Tena, tunamfahamu Baba kwa kuyaona aliyoyatenda Yesu YOHANA 14:7-9.  Kabla ya kufanya lolote, ni muhimu kujiuliza “Je jambo hili anaweza kulifanya Yesu?”.  Kama jibu ni HAPANA, tujue ni dhambi kulifanha hilo.  Mambo yote ambayo ni dhambi hayakuandikwa MOJAMOJA.  Biblia ingekuwa kitabu kikubwa sana kwa kufanya hivyo Mungu ametufundisha MISINGI ya kufuata.  Kwa msingi huu, ni muhimu kujiuliza “Je, Yesu anaweza kuwa shabiki wa Yanga au Simba?  Anaweza kufurahia kipindi cha Michezo mbili kosorobo, au Jangala?  Anaweza kufurahia muziki wa dansi?  Anaweza kwenda kutazama au kwenda kuogelea baharini au kutazama mchezo wa ngumi?  Jibu la haya yote, ni hapana, HAWEZI!  Kwa jinsi hiyohiyo sisi nasi baada ya kuokoka, hatupaswi kufanya hayo yote, ni DHAMBI!  Kwa msingi huu ni rahisi kufahamu mengi mengine yaliyo dhambi ambayo hayakuandikwa moja kwa moja katika Biblia.

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s