UMUHIMU WA KUJIWEKA TAYARI

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

SOMO:        UMUHIMU WA KUJIWEKA TAYARI

Leo, tunajifunza Biblia zetu katika MATHAYO 24:42-51 na 25:1-13.  Katika mistari yote hii, tunajifunza juu ya kujiweka tayari.  Tutayagawa mafundisho tunayojifunza katika mistari hii, katika vipengele vitatu:-

 

(1)  KUKESHA NA KUJIWEKA TAYARI WAKATI WOTE (24:42-44);

(2)  MTUMWA MWAMINIFU MWENYE AKILI (24:45-51);

(3)    MFANO WA WANAWALI KUMI (25:1-13).

 

(1)      KUKESHA NA KUJIWEKA TAYARI WAKATI WOTE    (24:42-44) – Nyakati za Biblia, wakati wa

usiku, uligawanywa katika ZAMU NNE, au vipindi vine.  (LUKA 12:38; MATHAYO 14:25).  Kila zamu, ilikuwa na muda wa saa tatu kuanzia saa 12 jioni hadi 3 usiku ilikuwa ZAMU YA KWANZA.  Kuanzia saa 3 usiku hadi saa 6 usiku ilikuwa ZAMU YA PILI.  Kuanzia saa 6 usiku mpaka saa 9 usiku, iliitwa ZAMU YA TATU; na saa 9 usiku hadi saa 12 asubuhi, iliitwa ZAMU YA NNE.  Mwenye nyumba kama anagaliijua ni zamu ipi ambayo mwivi angekuja, angalikesha na kuwa macho, wala asingeliiacha nyumba yake kuvunjwa.  Kuna mambo kadhaa ya kujifunza hapa:-

1.         BWANA ANAYEKUJA – Bwana anayekuja, ni Yesu.  Kama alivyochukuliwa kwenda juu mbinguni, atakuja tena jinsi iyo hiyo (MATENDO 1:10).  Yesu, ndiye Mhukumu au Hakimu wa Ulimwengu (YOHANA 5:22; MATENDO 10:40-42).  Kuja kwake kunaambatana na HUKUMU.  Atakuja kwetu bila taarifa yoyote kama mwivi.

2.         NYUMBA ITAKAYOVUNJWA – Nyumba ni mtu mwenyewe (WAEBRANIA 3:1-3; 2 WAKORINTHO 5:1-2).  Ikiwa hatutajiweka tayari, Yesu Kristo atakapokuja kama mwivi, atatuvunja na kutuharibu kwa hukumu yake.  Ikiwa atatukuta tunakesha na kuzilinda nyumba zetu, ndipo nyumba zetu zitakapokuwa salama yaani ndipo tutakaposalimika.

3.         SIKU ATAKAYOKUJA BWANA WETU – Kwetu sisi tulioko duniani, siku atakayokuja kwetu Bwana wetu Yesu, kama mwivi; itakuwa katika sehemu mbili:-

(a)       SIKU YA KUFA – Kwa wengine kati yetu, siku yao ya kufa, ndiyo itakayokuwa siku ambayo Yesu kama Hakimu atawajia kama mwivi.  Baada ya mtu kufa, inafuata hukumu (WAEBRANIA 9:27).  Wakati mtu anapokufa, ndipo Yesu anapomwijia kumhukumu.  Kufa siyo ugonjwa wala uzee.  Watu waliokuwa wazima wamekufa kwa ajali na kuwaacha wagonjwa hospitali hawajafa.  Watoto wengine wamekufa kabla ya wazee wao (MWANZO 11:28).  Hakuna mtu anayeijua siku yake ya kufa (MWANZO 27:2).  Kesho, haiko mikononi mwetu (MITHALI 27:1; YAKOBO 4:13-16).  Watu wengine wanaweza kujua kwamba wakati wa kufariki kwao umefika (2 TIMOTHEO 4:6), hata hivyo ni vigumu kuifahamu siku ya kufa.  Watakatifu wamekufa na kuwaacha waovu wakiishi.  Yohana Mbatizaji na Stefano, waliuawa na waovu na wakawaacha wao wanaishi duniani.  Kwa sababu hatujui siku yetu ya kufa, inatupasa kujiweka tayari kuonana na Mungu wakati wote (AMOSI 4:12).  Tusipojiweka tayari kuzilinda nyumba zetu au nafsi zetu, siku ya kufa, Bwana Yesu atazivunja nyumba zetu pale atakapotutupa kwenye moto wa milele.

(b)       SIKU YA KUNYAKULIWA KWA KANISA  (1 WATHESALONIKE 4:15-17) – Siku hii ambayo pia haijulikaniu kwetu, itakuwa siku ya kuja Bwana Yesu kwa wanadamu wengine wote ambao watakuwa hawajafa.  Siku hiyo inaweza kuwa wakati wowote kuanzia sasa.

4.         TUNACHOTAKIWA KUFANYA – 1. KUKESHA – Katika lugha ya ki-Biblia, watu wanaotenda maovu na kuishi kinyume na Neno la Mungu, wanaitwa WATU WALIOLALA USINGIZI (1 WATHESALONIKE 5:4-8).  Watu ambao wanaishi sawa na neno la Mungu na kuwa mbali na uovu, wanaitwa WANA WA  MCHANA, WANA WA NURU au WANA WA KUKESHA.  Waovu, ni wana wa giza, waliolala.  Mtu aliyelala usingizi, hana akili, hajui yanayomzunguka, anafikiri ni salama tu.  Anapoamka, anaweza akajikuta kwamba alibebwa na kuhamishwa chumba, pasipo kujijua.  Ndivyo walivyo waovu, wanafikiri ni salama, lakini siku moja watajikuta wamehamishwa na kuwa katika moto wa milele.

2. KUJIWEKA TAYARI – Kukesha kwetu, yaani kuishi sawa na Neno la Mungu, ni lazima kuambatane na kujiweka tayari WAKATI WOTE na siyo wakati tunapokuwa katika ibada kanisani au katika vikosi vya maombi.  Wakati wote ni lazima tuwe tayari kuonana na Mungu bila mashaka yoyote.  Tunapaswa kuhakikisha kwamba hatuna dhambi yoyote ambayo hatujaitubu au lolote ambalo hatujalirekebisha kwa Mungu, Watumishi wake, na wanadamu wote (WAKOLOSAI 3:5-10, 12-14; 1 YOHANA 2:1-2; 2 YOHANA 1:8).

 

(2)       MTUMWA MWAMINIFU MWENYE AKILI   (24:45-51)

Mtu yeyote aliyeokolewa, ni wajibu wake kufahamu kwamba tumeitwa na Mungu KUMTUMIKIA.  Lengo la juu la kila mtu aliyeokoka, ni kuhakikisha anawapa wengine CHAKULA au kuwalisha wengine Neno la Mungu.  Mtu yeyote ambaye Yesu atamkuta akiwalisha wengine neno la Mungu, ATAMWEKA JUU YA VITU VYAKE VYOTE.  Ni muhimu basi kuona faida ya kushuhudia, kuwafuatilia na kuwalea watoto wachanga kiroho kwa kuwafundisha Neno la Mungu; na kuitumia vema neema ya kuwa Viongozi wa Makanisa ya Nyumbani, Viongozi wa Zoni au Wachungaji.  Inatupasa kuwalisha kondoo za Mungu kwa sababu tunampenda Yesu aliyetuokoa na siyo kana kwamba ni wajibu wetu tu!  (YOHANA 21:17).  Kiwango cha juu cha udhihirisho wetu wa kumpenda Yesu, ni kuwalisha kondoo zake.  Upendo alio nao mama kwa watoto wake ndiyo unaomfanya aone utumishi wake wa kuwatunza na kuwalisha watoto wake uwe utumishi wa furaha.  Mtendakazi yeyote pia anapaswa kufanya utumishi wa Mungu kutokana na kumpenda Yesu siyo ilimradi atoe ripoti au ampendeze Kiongozi Fulani.  Utumishi unaotokana na kumpenda Yesu, ndiyo utakaozawadiwa.   Mtendakazi yeyote ambaye atadhani Yesu anakawia, na kuanza kuwatesa na kuwaumiza kondoo wa Mungu, kutokana na tabia yake isiyoonyesha picha ya wokovu; na kuwafanya kondoo kutaka kurudi nyuma, huyu atatendwa mabaya na Yesu (MATHAYO 24:48-51; LUKA 12:42-48).  Ni muhimu kukumbuka kuwapa chakula kondoo wakati wake ili kukata njaa na kiu yao.

 

(3)       MFANO WA WANAWALI KUMI   (25:1-13)

Nyakati za Biblia, katika mila na desturi za Wayahudi, wanawali au mabikira 10 walikuwa wanamlaki Bwana Arusi kwa niaba ya Bibi Arusi aliyekuwa rafiki yao.  Jambo hili lilifanyika usiku, giza tu lilipoanza na kuonekana kwa nyota.  Ilikuwa ni zamu ya kwanza.  Katika mfano huu, Bwana Arusi alichelewa kuwasili.  Bwana arusi ni Yesu Kristo (YOHANA 3:28-30).  Watu wanaomfuata Mwana Kondoo Yesu Kristo popote anapokwenda ni Mabikira (UFUNUO 14:4).  Leo, tuna watu wengi wanaomfuata Mwana Kondoo Makanisani, kwa nje wanaonekana kuwa sawasawa lakini kumbe katika 10, watano ni WAPUMBAVU, hawana mafuta ya TAA.  Taa inayotajwa hapa ni Neno la Mungu au KWELI (ZABURI 119:105; YOHANA 17:17).  Mafuta ni NEEMA ya Mungu.  Kweli ya Kristo, ilikuja pamoja na Neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu, ni kujaribu kuokolewa kwa matendo ya sheria; haiwezekani! (TITO 2:11-12, 3:4-8).  Bwana arusi atakuja saa tusiyoidhani na ataangalia tu wale waliookolewa kwa neema, na kuishi katika mapenzi yake kwa neema hiyo.  Hao tu ndiyo watakaokuwa katika harusi au furaha yake mbinguni.  Wengine watafungiwa mlango.  Watajaribu kutubu baada ya Dhiki Kuu kuanza, hawatasikilizwa (WAEBRANIA 12:16-17).  Vilevile tujilinde na kujiweka tayari wakati wote pamoja na neema tuliyo nayo.  Tusije tukalala pamoja na neema hiyo.   Wengine walianza vizuri, lakini wameuacha tayari upendo wao wa kwanza, wamelala!  Hawa wako pia katika hatari, inawabidi kukumbuka upesi walipoanguka  na kutubu (UFUNUO 2:4-5).  Tukeshe, maana hatujui siku wala saa!

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawee.

Advertisements

One comment on “UMUHIMU WA KUJIWEKA TAYARI

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s