UMUHIMU WA KUWA NA HEKIMA

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Mkuu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA.

SOMO: UMUHIMU WA KUWA NA HEKIMA

                         (MATHAYO 13:53-54)

Baada ya Yesu Kristo kuimaliza mifano yake katika MATHAYO 13:3-52, alitoka akaenda zake, na kuzidi kufundisha katika nchi yake.  Kila aliyemsikia Yesu, alishangaa KWANZA juu ya HEKIMA yake kabla hata ya kuiangalia miujiza yake (MST. 54).  Hekima ya Yesu, ilionekana mapema tangu katika utoto wake na ilizidi kuongezeka katika kukua kwake (LUKA 2:40,52).  Kama Mungu angemwambia kila mtu aliyeokoka, “OMBA UTAKALO NIKUPE“, na Mungu akampa kila mtu nafasi ya kuchagua jambo moja tu; halafu ikachukuliwa takwimu au sensa ili kuonyesha watu wangapi wameomba jambo lipi, inaelekea wengi ungekuta wameomba “KARAMA ZA KUPONYA NA MATENDO YA MIUJIZA“ na “UTAJIRI WA MALI NA FEDHA“.  Sulemani alipata nafasi ya namna hiyo, lakini alimwomba Mungu “HEKIMA“            (2 NYAKATI 1:7-10); hakuomba uwezo wa kutenda miujiza wala mali na fedha.  Sulemani alijua sana juu ya miujiza aliyoifanya Musa na Yoshua.  Lakini hakuweka hayo ya kwanza.  Wachache leo, wangeomba Mungu hekima.  Kuchagua kwanza lolote kabla ya hekima, ni kukosa ufahamu.  Ukipata hekima, yote mengine utayapata kama Sulemani (2 NYAKATI 1:11-12).  Kilichomtofautisha sana Yesu na watu wengine ni hekima yake kabla hata ya miujiza yake.  Yesu anaitwa “HEKIMA ITOKAYO KWA MUNGU“ (1 WAKORINTHO 1:30).  Ili sisi nasi tufahamu umuhimu wa kuwa na hekima, na kutafuta hiyo kwanza, tutaangalia somo letu la leo katika vipengele vinne:-

 

(1)            MAANA YA HEKIMA;

(2)            THAMANI YA HEKIMA YA MUNGU;

(3)            KAZI YA HEKIMA YA MUNGU;

(4)            JINSI YA KUPATA HEKIMA YA MUNGU.

 

Ebu basi tuangalie kipengele kimoja kimoja kama wanafunzi wa Biblia, ili tupate ufahamu.

(1)            MAANA YA HEKIMA

Ziko aina nne za hekima:-

 • HEKIMA YA DUNIA (1 WAKORINTHO 2:6)– Hii ni elimu au ufahamu unaotokana na kusoma kwingi katika elimu mbalimbali za dunia (MATENDO 7:22);
 • HEKIMA YA TABIA YA KIBINADAMU (YAKOBO 3:1-5) – Uwezo wa kisiasa ulio kwa wanadamu fulani ambao unawawezesha kuitawala dunia hii au kukubalika kiuongozi katika jamii (1 WAKORINTHO 2:6).  Hii huwa tu tabia ya mtu, wakati mwingine tangu utotoni;
 • HEKIMA YA SHETANI (YAKOBO 3:15) – Uwezo wa ziada wa kishetani unaomuwezesha mtu kufanya dhambi kwa ubingwa;
 • HEKIMA YA MUNGU AU HEKIMA ISHUKAYO KUTOKA JUU (YAKOBO 3:15;            1 WAKORINTHO 2:6-8).
 1.                      i.      Uwezo wa Ki-Mungu unaokuwa juu ya mtu unaomuwezesha kufahamu njia ya ki-Mungu ya kupata ufumbuzi wa tatizo;
 2.                     ii.      Uwezo wa Ki-Mungu wa kuwaelewesha watu mpaka wanaamua kuyafuata yaliyo ya Mungu kwa furaha na amani.
 3.                    iii.      Ufahamu usio wa kawaida juu ya mambo ya Ufalme wa Mungu, unaokuwa juu ya mtu (2 PETRO 3:15-16).
 4.                    iv.      Ufahamu usio wa kawaida unaokuwa juu ya mtu unaomuwezesha kufahamu machache yatakayotokea siku za mbeleni na kufanya maandalizi mazuri kabla hayajatokea (1 WAKORINTHO 12:8).

Hii ndiyo hekima aliyokuwa nayo Yesu na Sulemani, ambayo kila mtu aliyeokoka anapaswa kuitafuta kwa bidii.

 

(2)            THAMANI YA HEKIMA YA MUNGU

Mtu akiwa na hekima ya Mungu atafanikiwa sana katika kazi ya Mungu (MHUBIRI 10:10).  Mtu mwenye hekima ana nguvu (MITHALI 24:5).  Maneno ya kinywa chake mwenye hekima yana neema, utapenda kumsikiliza tofauti na mpumbavu asiye na hekima (MHUBIRI 10:12-13).  Watu watatoka mbali kuja kumsikiliza (1 WAFALME 4:30-34).  Hekima ni ya thamani kuliko lolote jingine (MITHALI 8:11; MHUBIRI 7:11-12; MHUBIRI 9:18; MITHALI 16:16).  Biblia inasema, “Mpende jirani yako kama nafsi yako”.  Mtu apataye hekima ya Mungu, hujipenda nafsi yake (MITHALI 19:8).  Katika Karama za Roho Mtakatifu, karama ya neno la Hekima, inatajwa ya kwanza (1 WAKORINTHO 12:8-10).

(3)            KAZI YA HEKIMA YA MUNGU

 1. KUJUA JINSI YA KUONDOA MANUNG’UNIKO AU MIZOZO KATIKA JAMII (MATENDO 6:1-3);
 2. KUJUA JINSI YA KUKATA MASHAURI AU KUTOA HUKUMU (1 WAFALME 3:16-28);
 3. KUFAHAMU YANAYOTUPASA KUSEMA KATIKA MAJADILIANO NA MTU WA AINA YOYOTE (MATENDO 6:9-10; LUKA 21:14-15; MATENDO 7:9-10:
 4. KUJUA JINSI YA KUFASIRI MANENO TUNAYOAMBIWA AU TUNAYOYASIKIA (MHUBIRI 8:1);
 5. KUJUA WAKATI WA KUFAA WA KUZUNGUMZA AU KUFANYA JAMBO AU WAKATI WA KUONYA NA JINSI YA KUONYA (MITHALI 25:11-12);
 6. KUJUA JINSI YA KUVISHINDA VITA VYA KIROHO VILIVYO JUU YETU (MHUBIRI 9:14-16);
 7. KUJUA JINSI YA KUJIBU MASWALI YA MAFUMBO NA KUGUNDUA MAFUMBO YA KIJANJA NA KIBINADAMU (2 NYAKATI 9:1-3, 5-7; 2 SAMWELI 14:1-8, 18-19);
 8. KUVUTA ROHO ZA WATU (MITHALI 11:30);
 9. KUJUA JINSI YA KUITULIZA HASIRA YA MTU (MITHALI 16:14);
 10. KUMUWEZESHA MTU KUTAMKA MAARIFA (MITHALI 15:2)

Hekima itakufundisha ni wakati upi wa kunyamaza au kusema (MARKO  14:55-62).  Hekima itakufundisha ni wakati upi wa kukemea (LUKA 13:31-32).  Hekima itakufundisha ni wakati upi wa kufundisha kwa kitendo (MARKO 7:1-8) au ni wakati upi wa kujibu swali kwa swali (MATHAYO 21:23-27).

 

 

(4)            JINSI YA KUPATA HEKIMA YA MUNGU

 1. Kufahamu thamani ya hekima na kutoidharau (MITHALI 14:6);
 2. Kuwa mkamilifu au mtakatifu (1 WAKORINTHO 2:6; YAKOBO 3:16-17);
 3. Kukubali kuwa mpumbavu (1 WAKORINTHO 3:18);
 4. Kuwa mnyenyekevu yaani kuwa mbali na kiburi na majivuno (MITHALI 11:2);
 5. Kuwa mwepesi wa kushaurika na kufundishika (MITHALI 19:20);
 6. Kumcha au kumhofu Mungu (ZABURI 111:10);
 7. Kuenenda pamoja na wenye hekima (MITHALI 13:20);
 8. Kuwa tayari kutoa muda wote na moyo wote kusikia mafundisho ya Neno la Mungu (MITHALI 8:33; 2 TIMOTHEO 3:15).  Neno la Mungu ni hekima ya Mungu (LUKA 11:49);
 9. Kuwa na roho ya utulivu na kuzuia maneno (MITHALI 17:27; MITHALI 10:19);
 10. Kuomba kwa imani na kwa bidii mpaka upokee (YAKOBO 1:5; 2 NYAKATI 1:10).

Maandiko, yanataka kila mmoja wetu awe na hekima (WARUMI 16:19).  Mungu wetu aliazimu tangu milele kutupa hekima wakati huu wa Agano Jipya zaidi sana kuliko wakati wa Agano la Kale (1 WAKORINTHO 2:7).  Hekima ni Karama kuu kuliko zote na Biblia inatufundisha kutaka sana karama zilizo kuu (1 WAKORINTHO 12:31).

MUNGU ANAJUA NIA, SHAUKU NA BIDII ULIYO NAYO KATIKA KUTAKA KUMTUMIKIA MUNGU LAKINI HUWEZI KUFANYA MENGI YA KUMTUKUZA BILA HEKIMA.  Uwe na busara, kuanzia sasa mwombe Mungu hekima, na usimwache mpaka amekubariki.  Je, utakuwa miongoni mwa wenye busara?  Ikiwa ni hivyo, Mungu atakutumia kufanya mambo makubwa.

Unaweza kuingia katika somo “VITU VIPYA NA VYA KALE PAMOJA NA JUYA” kwa kubofya link hii, https://davidcarol719.wordpress.com/vitu-vipya-na-vya-kale-pamoja-na-juya/

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “note” hii, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s