UTAKASO 2

ZACHARY KAKOBE

Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SOMO: UTAKASO 2

Yesu alipotuokoa, alitutenga na mataifa kabisa. Hata mavazi yetu, lazima yawe na alama dhahiri ya kututofautisha  na mataifa au watu ambao hawajaokoka. Desturi zozote za mataifa katika mavazi na mapambo yote, Mungu anazichukia kabisakabisa. Mavazi yetu lazima yawe tofauti na mavazi ya mataifa, ili wakati wowote tukiyaangalia mavazi yetu; tukumbuke kwamba tuko chini ya utawala wa Bwana mwingine, tofauti na pale tulipokuwa hatujaokoka ( KUTOKA 11:7 ; MAMBO YA WALAWI 20:23-26 ; HESABU 15:37-41 ; ISAYA 3:16-26 ; ISAYA 4:3-4 ; 1TIMOTHEO 2:9-10 ).

Biblia inatuonya tusifuate njia ya mataifa katika kupamba nywele au kujipamba kokote kwa rangi midomoni, kukali nywele au kusuka rasta n.k.Kuvaa heleni, bangili, mikufu au pete. Zote hizi ni njia za kidunia katika mavazi. Haziongezi lolote katika utakatifu wa mkristo ( KUMBUKUMBU 18:9; YEREMIA 10:2; 2WAFALME 17:14-15; WARUMI 12:2 ). Haiwezekani kwa namna yoyote Wakristo kuangaza na kuwa nuru ya mataifa, ikiwa tunavaa kama wao! Leo watu kadhaa katika kanisa la Mungu, wanatetea kujipamba, na kufundisha kwamba mtu aliyeokoka ndiye anapaswa kujipamba kuliko mataifa. Huu ni udunia. Sio Ukristo. Huwezi kuwa rafiki wa dunia na ukafikiri kwamba wakati huohuo unaweza ukawa rafiki wa Mungu. Biblia inasema wazi kwamba kuwa rafiki wa dunia kwa namna yoyote, ni kujifanya adui wa Mungu na kufanya uzinzi ( YAKOBO 4:4-5 ).

Kanisa la Mungu linapaswa kukumbuka kwamba, watu ambao hawajaokoka au mataifa ingawa hawaijui Biblia, sheria ya Mungu imeandikwa mioyoni mwao ( WARUMI 2:14-15 ). Ndiyo maana wakimuona mtu anaiba, wanamhukumu kwa kumpiga hata mawe. Waulize kwamba kosa la wizi limeandikwa wapi katika again jipya, hawawezi kukuonyesha. Watu wa mataifa wanajua mambo ya dunia ni yapi. Wanayaita starehe. Wanajua kuwa mziki wa dansi, sinema, mpira wa ligi n.k ni vitu vyao. Wanajua kuwa kujipamba ni mambo yao! Hata masista wa madhehebu yasiyoamini wokovu, ili waonekane ni watakatifu, wanavaa mavazi tofauti na waumini wenzao. Sasa, leo kanisa la Mungu linawezaje likawashuhudia masista kuhusu wokovu, ikiwa lina watu wanaokali nywele na kujipamba?

Ndiyo maana injili imekuwa ngumu kukubarika Mataifa. Wanasema kuhubiri wokovu, ni biashara! Huwezi kamwe kuwashawishi mataifa kwamba kukali nywele, kusuka rasta, kutia rangi midomoni n.k, ndiyo wokovu! Watakuangalia tu na kukuona umechanganyikiwa. Wanaweza wasikujibu kitu, na ukadanganyika kwamba wamekuelewa! Biblia inasema wazi kwamba haki yetu isipozidi haki ya mafarisayo au watu wa dini, hatuwezi kamwe kuingia katika ufalme wa mbinguni (MATHAYO 5:20 ).

Sasa, jambo la kufahamu hapa ni kwamba udunia katika mavazi, ni jambo linalotoka moyoni na siyo nje tu! Mtoto mdogo sana akivalishwa nguo ya namna Fulani, utaona anatembea kwa malingo huku akijitazama. Jaribu sasa kumbadilidha nguo hiyo. Anaweza akalia na kuzila kula! Mtu ambaye hajatakaswa ni lazima udunia katika mavazi utakuwa kwake moyoni! Inawezekana jambo hili lisidhihirike kwa nje, hata hivyo Mungu akiangalia ndani lipo!

Sasa basi, jithibitishe mwenyewe  kwamba umetakaswa:

Je, unapovaa mavazi yenye viwango vya Kibiblia, moyoni mwako, huyaonei haya mavazi hayo, na kutamani kuvaa kama mataifa? Ofisini mwako wanapokuangalia  unavyovaa na kukuita “mzee” au mtu ambaye siyo wa “Ki-leo”, unajisikiaje moyoni? Unatamani moyoni kuanza kuvaa kama mataifa? Wana wa Israeli walichoka kuongozwa na Mungu na wakatamani wawe na mfalme kama watu wengine. Huu ni udunia. Je, unapoambiwa na watu kwamba kutokana na kuvaa kwako itakuchukua muda kuolewa maana huwavutii wanaume, unajisikiaje moyoni? Je, unapojifunza kwamba arusi za watu waliookoka zinapaswa kuwa za kiasi, na zaidi sana hatupaswi kuvaa shela na mitindo ya mavazi ya arusi za mataifa, unajionaje moyoni? Mawazoni kwako huoni kwamba itakuwa ni aibu na utaonekana wa rahisi sana na asiye na thamani? Mawazoni mwako, huwazi kwamba utaonekana siyo msichana, na watu watafikiri ulianza kukaa na mwanamume huyo kwanza? Ikiwa uko hivi, ujue hujatakaswa.

Je, unapowaona watu njiani  wamevaa heleni za dhahabu, na wewe masikio yako yanaonyesha matundu baada ya kuziondoa  heleni zako, unajisikiaje moyoni? Hakuna tama moyoni ya kuvaa heleni?  Je, unapowaona watu wengine waliookoka wamevaa kama mataifa  na makanisani mwao “wanaruhusiwa” kufanya hivyo ingawa Biblia inakataza, moyoni mwako hutamani kuwa “huru” kama wao? Biblia inawaagiza wanawake kufunika vichwa vyao kwa vitambaa wanapokuwa wakiomba au kusali na kuhutubu, kama dalili ya kuonyesha kumilikiwa kwao na wanaume. Malaika wanafurahia kuona hivi. Je, wewe unafurahia jambo hili kutoka moyoni au kwako ni aibu na mzigo? ( 1WAKORINTHO 11:5-10, 12 ). Ikiwa uko hivyo, hujatakaswa.

Je, wewe mwanamume, unapoona wanawake waliovaa mavazi yenye viwango vya Ki-biblia, moyoni mwako huoni kwamba hawapendezi? Mwanamume, unapowaona barabarani wanawake wamevaa mavazi ya mataifa, mitindo yao ya mavazi haikuvutii moyoni, kiasi cha kufanya uone kwamba mke wako angevaa hivyo ungefurahi sana kutembea naye barabarani? Mwanamume, unapojifunza mafundisho kuhusu mavazi ya wanawake katika kanisa la Mungu, moyoni mwako, huoni kwamba wameonewa na kukandamizwa au kunyimwa uhuru wa kufanya mambo yao? Huwazi moyoni kwamba ungekuwa wewe ni mchungaji, ungewaruhusu kuvaa wanavyotaka?

Je, wewe unayesoma somo hili, moyoni mwako na mawazoni mwako, huwazi kwamba hizi ni “sheria zilizozidi au ni msisitizo mkubwa juu ya mambo madogomadogo katika wokovu?” Ikiwa uko hivi ujue moyoni mwako umejaa udunia. Wewe ni mtu mwenye tabia ya mwili. Hujatakaswa. Biblia inasema kwamba “:Bweha wadogo ndio wanaoiharibu mizabibu yetu inayochanua na kuifanya isitoe matunda. Tunapaswa kuwakamata na kuwaua (WIMBO ULIOBORA 2:15 ).

Mtu aliyetakaswa, kwake, mavazi ya kidunia yatakuwa ni sawa na mavi kabisa. Hayamtamanishi moyoni au mawazoni. Anayachukia na kuyaona yananuka kama mavi ( WAFILIPI 3:8 ). Kwake ulimwengu umesulibishwa, nay eye kwa ulimwengu ( WAGALATIA 6:14 ). Tulipokuwa hatujaokoka, tulikuwa huru mbali na haki, lakini baada ya kuchoka, tunapaswa kuwa huru mbali na dhambi. Tukikubali kuwa huru mbali na dhambi na kuwa watumwa wa Mungu au neon la Mungu, faida yetu ndiyo kutakaswa yaani kuwezeshwa kuupata utakatifu ambao pasipo huo haiwezekani kumuona Mungu. Uhuru wowote wa mtu anayejiita ameokoka, ulio mbali na haki au neon la Mungu, ni uhuru wa mataifa au watu ambao hawajaokoka walio watumwa wa dhambi ( WARUMI 6:20-22 ).

MIFANO YA KIBIBLIA YA WATU WALIOKUWA WAMEOKOLEWA LAKINI HAWAJATAKASWA

  1. WANAFUNZI WA YESU

Wanafunzi kumi na wawili wa Yesu, walikuwa wameokolewa tayari. Mambo yafuatayo, yanathibitisha kwamba walikuwa wameokoka.

( a ). Waliacha vyote na kumfuata Yesu- MATHAYO 4:18-22.

( b ). Petro alimkiri Yesu kuwa ni Kristo na Mwana wa Mungu aliyehai, MATHAYO 16:15-17.

( c ). Yesu alithibitisha kuwa wameacha vyote na kumfuata na akasema wataurithi uzima wa milele katika ulimwengu mpya-MATHAYO 19:27-29.

( d ). Wao pamoja na wengine, jumla yao ilifikia sabini, walikuwa wamefunuliwa neon la Kristo na wakalikubali, majina yao yalikuwa yameandikwa mbinguni na walikuwa wanakemea pepo kwa jina la Yesu na pepo wanatii-LUKA 10:17-24.

            ( e ). Baada ya kulipokea neon, Yesu anasema, ulimwengu uliwachukia kwa kuwa hawakuwa wa ulimwengu kama Yesu asivyokuwa wa ulimwengu-YPHANA 17:14.

            PAMOJA NA JINSI WALIVYOKUWA WAMEOKOKA, BADO WALIKUWA NA TABIA ZIFUATAZO

             ( a ). Petro hakuwa na mawazo yaliyo ya Mungu bali ya wanadamu, na aliweza kumsahihisha Yesu Kristo na kujaribu kumfundisha na kumwelekeza. Hakuwa tayari kuongozwa na neon la Kristo mia kwa mia-MATHAYO 16:21-23.

             ( b ). Katikati yao, kulikuwa na mgawanyiko, walikuwa wangombana wao kwa wao wakigombania ukubwa; na walimjibu Yesu kwa namna isiyo ya unyenyekevu-LUKA 22:24-26; MATHAYO 20:20-22, 25-28; MARKO 9:30-37.

             ( c ). Walikuwa na hasira, wakikasirikiana wao kwa wao-MATHAYO 20:24.

             ( d ). Walikuwa na wivu, walijiona kuwa wao ni wao tu. Yeyote aliyeokoka ambaye hakufuatana nao, walimhesabu kuwa si kitu. Hakukuwa na upendo kati ya wanafunzi wote wa Yesu-MARKO 9:38-39; LUKA 9:49-50.

             ( e ). Walikuwa na roho ya chuki, hasira, kisasi na kutovumilia maudhi. Kutokana na roho hii, walitamani kuomba moto ushuke kutoka mbinguni uwaangamize wasamaria ambao walikataa kumkaribisha Yesu-LUKA 9:51-56.

             ( f ). Walikuwa na tama na kujipenda, wakitaka vizuri vyote view vyao, na walichukia kuona vizuri viko kwa wengine “umimi” ulikuwa bado unawatawala-MATHAYO 26:6-13.

             ( g ). Ilikuwa mzigo kwao kumsamehe aliyewakosea-MATHAYO 18:21-35.

  1. 2.      KANISA LA KORINTHO

Watu katika kanisa la Mungu lililokuwa Korintho, walikuwa wameokoka. Roho wa Mungu alikuwa anakaa ndani yao, na kila mmoja alikuwa hekalu la Mungu ( 1WAKORINTHO 3:16-17 ).

PAMOJA NA JINSI WAKORINTHO WALIVYOKUWA WAMEOKOKA, BADO WALIKUWA NA TABIA ZIFUATAZO:-

( a ). Walikuwa na faraka yaani matengano na magawanyiko, yaliyoleta makundi kadhaa katika kanisa hilo moja. Hawakuwa na nia moja wala shauri moja na tena walikuwa na fitina kati yao-1WAKORINTHO 110-11.

( b ). Wengine walikuwa wanasema niwa Paelo, wengine wa Apolo, wengine wa Kefa au Petro, wengine wa Kristo, na kulikuwa na chuki kati ya kundi moja na lingine- 1WAKORINTHO 1:12-13.

( c ), Walijawa na husuda au wivu na fitina na hata kulikuwa na ugomvi kati ya wale waliojiita wa Paulo na Apolo- 1WAKORINTHO 3:3-5.

( d ). Walikuwa wanashitakiana mahakamani wao kwa wao mbele ya watu wasiookolewa. Hawakuwa tayari kudhurumiwa, na hivyo walitumia nguvu kuvipata vile walivyodhurumiwa hata ikibidi kupelekana polisi kama tunavyoijua leo-1WAKORINTHO 6:1-8.

( e ). Wanawake walikuwa wakorofi, wabishi na hawakuwa wakiwatii na kuwanyenyekea waume zao- 1WAKORINTHO 14:34-35.

( f ). Walikuwa hawataki kuwasikia viongozi wao na kuwatii- linganisha  1WAKORINTHO 9:1-2 na 1WAKORINTHO 4:18-21.

( g ). Wanawake walikuwa wanavaa mavazi ya kidunia, yasiyo ya unyenyekevu, wakishindana wakijionyesha kwa dhahabu na lulu, wakipamba nywele kama mataifa na wakikosa adabu, linganisha 1WAKORINTHO 4:17 na 1TIMOTHEO 2:9-12.

                                    

                                                        YATOKANAYO

Mpaka hapa  umeona jinsi ambavyo inawezekana kabisa mtu kuwa ameokoka, lakini akawa bado anafanya mambo mengi, ambayo hayamwonyeshi kuwa ni tofauti na mataifa. Siyo kwamba hajaokoka, la hasha, ameokoka,  ila hajatakaswa.  Mtu wa namna hii anaweza akawa hapendi kuwa na hasira,lakini akakuta anashindwa bkuizuia hasira. Anatubu, lakini anajikuta anaendelea kuwa na hasira kali baada ya kuudhiwa kwa mambo madogo madogo tu.

WARUMI 7:19

“Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndili nilitendalo”.

 

Katika hali ya namna hii, mtu aliyeokoka ambaye hajapata mafundisho ya utakaso, au aliyepotoshwa kwa kufundishwa kwamba alipookolewa alitakaswa pia wakati uleule; atakuwa anajishangaa na kuona hajui alifanyalo kama kweli ameokoka. Jumla ya namna hii ndiyo anayoieleza Mtume Paulo katika:-

WARUMI 7:15:-

“Maana sijui nifanyalo, kwa sababu lile  nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda”.

Basi sasa, ni makusudi ya somo hili kujifunza juu ya tatizo linalokuwepo juu ya mtu aliyeokoka ambaye hajatakaswa na njia ya kuliondoa. Ni maombi yangu  kuwa utajifunza yote yanayofuata  kwa nia ya kuifahamu kweli, na ukiwa na nia hiyo, kweli hii itakuweka huru ( YOHANA 8:32 ). Huenda somo hili ni “Elimu mpya” kwako, na hujawahi kusikia habari zake. Hii isikufanye utoke katika nia ya kuifahamu kweli hata kama ni mpya kwako, bali uwe na shauku zaidi ya kujifunza maana ya elimu hii mpya; kama walivyokuwa Waepikureo na Wastoiko nyakati za Mtume Paulo ( MATENDO 17:17-20 ). Elimu mpya ikiwa katika  kweli ya Neno la Mungu, inaweza ikatushangaza kama wakati wa Yesu, kutokana na sisi kuwa gizani juu ya kweli yote; lakini tukifungua mioyo yetu na kuipokea , inaweza ikawa chanzo kikubwa  cha baraka kwetu ( MARKO 1:27-28 ). Hivyo basi twende pamoja kujifunza, na kwa kuwa wewe ni  motto wa Mungu; mafuta ya Roho wa Mungu yaliyo ndani yako yatakufundisha juu ya kweli ya somo hili, na kukuthibitishia  kuwa siyo mafundisho ya upotevu ( 1 YOHANA 2:26-27 ).

 

                                                                 KIINI CHA TATIZO   

Tuendelee sasa na somo letu . Kwa nini basi mtu ambaye ameokoka awe bado na tabia mbalimbali, kama zile za wanafunzi wa Yesu, na wanafunzi waliokuwa katika kanisa la Korintho? Jibu ni kwamba “Dhambi ikaayo ndani ya mtu”, haiwi imeharibiwa  kabisa mtu anapokuwa ameokoka, kabla ya kutakaswa. Dhambi hii ikaayo ndani ya mtu, ndiyo kiini cha tatizo.

WARUMI 7:16-17:-

“Lakini kama nikilitenda lile nisilolipenda, nakiri ile sheria ya kuwa ni njema, Basi  sasa ni mimi nafsi  yangu ninayetenda hilo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu”.

Mtu yeyote , anazaliwa akiwa na asili ya dhambi ikaayo ndani yake tangu tumboni mwa mamaye. Kutokana na dhambi ya Adamu, kila aliye wa uzao wa Adamu, anazaliwa akiwa na asili ya dhambi ( ZABURI 51:5; AYUBU 25:4; AYUBU 14:4;  AYUBU 15:14; ZABURI 58:3; MAOMBOLEZO 5:7; MATHAYO 3:7; WARUMI 5:12 ).

 

ASILI HII YA DHAMBI ITOKANAYO NA DHAMBI YA ADAMU, INAPEWA MAJINA 11 KATIKA BIBLIA:-

1.Dhambi ikaayo ndani ya mtu ( WARUMI 7:17,20 ).

2.Utu wa kale au utu wa zamani ( WARUMI 6:6; WAEFESO 4:22-23; WAKOLOSAI 3:9-10 ).

3.Mwili wa dhambi ( WARUMI 6:6 ).

4.Mwili wa nyama  ( WAKOLOSAI 2:11 ).

5.Mwiliwa mauti  ( WARUMI 7:24 ).

6.Nia ya mwili  ( WARUMI 8:6 ).

7.Mwili   ( WARUMI 8:8-9, 12-13; WAGALATIA 5:17 ).

         Kuna majina mawili tofauti katika lugha ya kiyunani yanayotafsiri Kiswahili “mwili”:-

( a ). “SOMA”-mwiliwa mtu uoonekana, jingo ambalo linatunza Roho.

                 ( b ). “SARX”-asili ya mwili wa Adamu ambayo ni ya kufanya dhambi, siyo ya utakatifu

8.Uchafu  ( 2WAKORINTHO 7:1 )

9.Uadui juu ya Mungu ulio ndani ya mtu  ( WARUMI 8:7 ).

  1. 10.  Sheria ya dhambi na mauti   ( WARUMI 8:2 ).
  2. 11.  Upinzani wa Roho ulioko ndani ya mtu   ( WAGALATIA 5:17 )

Wakati wa kuokoka, asili hii ya dhambi inayoitwa utu wa kale au mwili wa dhambi, inasulibishwa tu, lakini wakati wa kutakaswa inabatilishwa au kuharibiwa kabisa ili tusiitumikie dhambi tena ( WARUMI 6:6 ).  Kumbuka kwamba mtu anaweza kusulubishwa , lakini akawa bado kufa mpaka avunjwe miguu kwanza ( YOHANA 19:31-32 ). Hapa unaona tofauti ya kusulubishwa na kuharibiwa.

Pamoja na asili ya dhambi, mtu pia huwa na dhambi za kutenda, kwa mfano kuvuta sigara, kunywa pombe, wizi, ibada ya sanmu, uchawi, uasherati na uzinzi, kuuua n.k Dhambi hizi za kutenda ndizo zinaharibiwa kabisa wakati wa kuokoka, na mtu akawa huru  kutokankatika kuzitenda. Dhambi nyingine kama hasira, wivu, chuki,  kujipenda wewe kuliko unavyowapenda wengine, mawazo machafun.k; zinatoka ndani sana ya mtu mwenye mzizi wa dhambi.

Tungeweza kusema, wakati wa kuokolewa; shina, matawi na majani ya mti  wa dhambi; yanakatwa kabisa na kuharibiwa,  lakini mzizi wa mti huo unakuwa haujang’olewa. Mzizi wa dhambi, unasulibishwa tu wakati wa kuokolewa. Wakati wa kutakaswa, ndipo mzizi huu wa dhambi, unapoharibiwa kabisa.

Mtu aliyeokoka ambaye hajatakaswa, Roho yake inapenda kumpendeza Mungu katika mambo yote , lakini mzizi huu wa dhambi unaoitwa uadui juu ya Mungu ulioko ndani ya mtu, au upinzani wa Roho ulioko ndani ya mtu; unamzuia kuyafanya yale anayotaka kuyafanya. Ni kama jinsi ambavyo jiwe  linaporishwa juu, linavyozuiwa kwenda juu zaidi, na hatimaye kurudishwa chini na nguvu ya uvutano. Mtu wa namna hii, hata kama ameokoka mika 70 iliyopita , anaitwa mtu mwenye tabia ya mwilini, mwanadamu anayeenenda kwa jinsi ya kibinadamu, motto mchanga katika Kristo ( 1WAKORINTHO 3:1-4 ).

Wakati wote anavutwa kutenda matendo yanayoonyesha tabia ya mwili wa dhambi na siyo matendo yanayoonyesha tabia ya rohoni. Hawezi kumpenda Mungu kwa moyo wake wote na roho yake yote.

 

   OPERESHENI YA KUHARIBU DHAMBI IKAAYO NDANI YA MTU

Safari yote ya kiroho ni safari ya imani. Mwanadamu anayeshindwa, kwa imani anamwendea Mungu akiamini kazi iliyofanywa na Yesu msalabani na Mungu mwenyewe anampa uwezo wa kushinda. Sasa basi mtu aliyeshindwa na dhambi na kuishi nje ya mpango wa Mungu, safari ya kwanza, anamwendea Mungu na kumuomba msamaha wa dhambi; na Mungu mwenyewe anampa Wokovu ulioletwa kwetu na Mwokozi Yesu alipomwaga damu yake msalabani kwa ajili yetu. Mtu huyu baada ya kuokoka anatakiwa amwendee Mungu safari ya pili na kumwomba amtakase au ampe utakaso

         Mungu anapomtakasa, mtu anamfanyia operesheni ya kuiharibu kabisa dhambi ikaayo ndani mwake. Operesheni hii tunayofanyiwa kwa imani inapewa majina matatu katika Biblia:-

  1. 1.      Kutahiriwa moyo ( KUMBUKUMBU 30:6; WARUMI 2:29; WAKOLOSAI 2:11 )
  2. 2.      Kutakaswa     ( YOHANA 17:17-19; 1WATHESALONIKE 4:3; 1WATHESALONIKE 5:23 ).
  3. 3.      Kukamilishwa au kufanywa timilifu  ( 1YOHANA 4:17-18; 2WAKORINTHO 13:9 ).

Baada ya operesheni hii, ndipo mtu anapokuwa na moyo safi au moyo mweupe ( MATHAYO 5:8; ZABURI 24:3-4) na kuwezeshwa kuishi maisha matakatifu kama Baba alivyo mtakatifu na pia katika ukamilifu kama Baba alivyo mkamilifu ( MATHAYO 5:48; 1PETRO 1:15-16 ). somo hili ni refu sana , hivyo nitaendelea kurusha kwa neema ya Mungu.Ingia katiak somo LA ” UTAKASO 1″ kwa ajili ya utangulizi.

          JE, UNATAKA KUOKOKA SASA?

Tunasoma haya katika LUKA 1:77, “Uwajulishe watu wake wokovu, katika kusamehewa dhambi zao”.   Hii ina maana kwamba ukiisha kutubu dhambi zako leo utasamehewa kwa hakika, na hivyo kupata wokovu mara moja.  Je, kweli utasamehewa?  Jibu ni Ndiyo!  Yesu mwenyewe anasema katika YOHANA 6:37, “……….Wala yeyote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe”.  Hivyo kwa dhahiri, leo hii, dakika hii hii, utasamehewa na kupata wokovu.  Je, uko tayari kuokoka sasa na kuhesabiwa miongoni mwa wale watakaoingia mbinguni na kuishi na Mungu milele, hata wakiiaga dunia sasa hivi?  Ukiwa tayari kuifuatisha sala ifuatayo ya toba, mara tu baada ya sala hii, nitakuombea na kwa ghafla utawezeshwa kushinda dhambi.  Je, uko tayari kuifuatisha sala hii sasa?  Najua uko tayari.  Basi sema maneno haya,  “Mungu Baba, natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Naomba unisamehe na kuniosha dhambi zangu kwa damu ya Yesu iliyomwagika msalabani.  Niwezeshe kushinda dhambi kuanzia sasa.  Liandike sasa jina langu katika kitabu cha uzima mbinguni.  Asante kwa kuniokoa, katika Jina la Yesu, Amen”.  Sasa ninaomba kwa ajili yako, “Mungu Baba msamehe kiumbe wako huyu dhambi zake zote, na mpe uwezo wa kushinda dhambi kuanzia sasa na kumuokoa. Mbariki kwa baraka zote katika Jina la Yesu, Amen”.  Tayari umeokoka.  Ili uzidi kuukulia wokovu, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI!!!

                                     . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

                                                          . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .         

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “note” hii, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s