UWEZEKANO WA KUMSALITI YESU

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

SOMO:      UWEZEKANO WA KUMSALITI YESU

Leo, tunajifunza Biblia kutoka MATHAYO 26:1-30.  Katika mistari hii, pamoja na mambo mengine, tunajifunza “UWEZEKANO WA KUMSALITI YESU”.  Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika mistari hii katika vipengele tisa:-

(1)  MWISHO WA UTUMISHI WA MTUMISHI WA MUNGU (MST 1-2)

(2)  MAADUI WAKUBWA WA YESU (MST 3-5)

(3)  KUWEKWA TAYARI KWA MAZIKO KWA KKUMWAGIWA MARHAMU (MST 6-13)

(4)  SHINA MOJA LA MABAYA YA KILA NAMNA (MST 14-16)

(5)  SIFA KUBWA YA MWANAFUNZI WA YESU (MST 17-19)

(6)  KUMTUMIKIA MUNGU PAMOJA NA NYUMBA YOTE (MST 20)

(7)  UWEZEKANO WA KUMSALITI YESU (MST 21-25)

(8)  KUANZA KWA MEZA YA BWANA (MST 26-29)

(9)  KUIMBA WAKATI WA HUZUNI (MST 30)

 

(1)       MWISHO WA UTUMISHI WA MTUMISHI WA MUNGU    (MST 1-2)

Mahali hapa, tunajifunza wakati wa kufa kwa Mtumishi wa Mungu.  Mtumishi wa Mungu, hufa baada ya “KUMALIZA MANENO HAYO YOTE” aliyotumwa kuyasema.  Hatuna haja ya kubabaika wala kuogopa.  Yeye anayetutuma, atahakikisha tunakufa tukiwa na “umri mtimilifu” (AYUBU 5:20, 26-27).  Umri mtimilifu wa Mtumishi wa Mungu, ni pale ambapo atakapokuwa amemaliza maneno hayo yote aliyoambiwa na Mungu kuyasema.  Shetani hawezi kutuua kabla ya wakati huo.  Shetani alitafuta kumuua Yesu kabla hajamaliza maneno hayo yote, lakini alishindwa (LUKA 4:29-30; YOHANA 8:58-59; 10:31-39).  Mtume Paulo vivyo hivyo alikufa baada ya kuumaliza mwendo (2 TIMOTHEO 4:6-7).

 

(2)       MAADUI WAKUBWA WA YESU    (MST 3-5)

Tangu mwanzo, mpaka mwisho wa huduma yake, maadui wakubwa wa Yesu, walikuwa viongozi wa dini, wakuu wa makuhani.  Hapa wanafanya shauri “pamoja”, ili wamkamate Yesu kwa hila na kumwua.  Wakuu wa makuhani wanakusanyika pamoja na viongozi wa serikali na waandishi na kupanga mipango ya kumwua Yesu.  Mahali pa kikao chao ni katika “behewa” yaani “Ukumbi wa mikutano” wa Kuhani Mkuu Kayafa.  Wanajua kuwa Yesu ni nabii, na kumwua wakati wa sikukuu, penye watu wengi, itatokea ghasia katika watu, hivyo wanapanga hila ya kumkamata sirini.  Wakuu wa makuhani walifuatilia kuhakikisha eti Yesu hafufuki!  (MATHAYO 27:62-66).  Mtumwa si mkubwa kuliko Bwana wake.  Katika huduma zetu pia maadui wakubwa kwetu watakuwa viongozi wa dini siyo watu wa kawaida.  Ilikuwa hivyo pia kwa mitume (MATENDO 5:17-20).  Bwana atatupigania, tusonge mbele katika huduma zetu.  Yeye atalipa kisasi pia.  Kulingana na waandishi wa historia wa karne ya kwanza, uchungu wa Kayafa aliyemwua Yesu uliendelea kumsumbua na alijiua mwenyewe mwaka wa 35 B.K.

(3)      KUWEKWA TAYARI KWA MAZIKO KWA KUMWAGIWA MARHAMU  (MST 6-13)

Ilikuwa desturi ya Wayahudi katika kuzika, kuuchukua mwili wa mtu aliyekufa na kuufunga katika sanda baada ya kuumwagia manukato ili kupunguza  harufu (YOHANA 19:38-40).  Yesu alimwagiwa marhamu au manukato yenye thamani nyingi na yule mwanamke siyo kwa kumpamba kwa urembo kama wengine wanavyodai, bali kwa kutabiri kifo chake na maziko yake, ili Injili itakapohubiriwa katika ulimwengu wote, ifahamike kwamba kifo cha Yesu hakikuwa kwa ajali, bali kilikuwa kwa makusudi ya kutukomboa, maana kilijulikana kabla.  “Ni wa nini upotevu huu”, ni maneno ya watu wajinga.  Hakuna gharama yoyote kubwa kwa ajili ya Injili.

(4)       SHINA MOJA LA MABAYA YA KILA NAMNA     (MST 14-16)

Shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha (1 TIMOTHEO 6:6-10).  Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu?  Wakampimia vipande au shekel 30 za fedha ambazo zilikuwa sawa tu na thamani ya kumnunua mtumwa mmoja (KUTOKA 21:23).  Wengi wetu ni rahisi kumsaliti Yesu tukipata fedha kidogo tu.  Wengi watampenda Yesu kabla ya kupata kazi, kupata cheo, kupata mume mwenye pesa, kupata gari au mafanikio ya biashara.  Wakiisha kupata hayo, mara humsaliti Yesu.  Itatufaidia nini tukiupata ulimwengu wote na kupata hasara za nafsi zetu?  (MARKO 8:36).  Tumwombe Mungu atupe neema ya kushinda tamaa ya fedha.  Shetani kama mkuu wa ulimwengu, alimwambia Yesu kuwa angempa yote katika milki yake kama angeanguka na kumsujudia, lakini hakumuweza Yesu (MATHAYO 4:8-11).  Wengi wetu tumepewa vitu na shetani baada ya kumuangukia.  Ni heri tuwe maskini kama Lazaro, IKIBIDI, lakini tukae na Yesu milele.  Yuda alifanya dhambi ya kudhamiria.  Alitafuta nafasi ya kumsaliti Yesu.  Hakuruhusu toba tangu mwanzo (MST 16).

(5)       SIFA KUBWA YA MWANAFUNZI WA YESU    (MST 17-19)

Sifa kubwa kuliko zote itakayoonekana kwa Mwanafunzi wa Yesu, ni kufanya kama Yesu anavyomwagiza, na siyo kama dhehebu linavyomwagiza.  “Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza” (MST 19).  Hatuwezi kudai kwamba sisi ni wanafunzi wa Yesu ikiwa hatufanyi yale anayotuagiza katika Neno lake, bali tunaendelea kushika maagizo ya wanadamu na madhehebu kama “Ubatizo wa kunyunyiziwa maji usoni”, ambalo siyo agizo la Yesu bali la wanadamu.  Tukishika maagizo ya wanadamu, tutaaibika siku ya mwisho (ZABURI 119:6, 9).  Hapa pia tunaona akifanya Pasaka au kula mikate isiyotiwa chachu kwa kuwa majira yake ya kufa ni karibu.  Sisi nasi, hatujui tutakufa lini. Huenda wiki hii au mwezi huu, hatujui.  Majira yetu ni karibu.  Yesu pia anarudi hivi karibuni.  Tusikubali kamwe kula chachu ya uovu na ubaya wakati huu, iwe katika kazi zetu au ofisi zetu au popote.  Tujitenge na ubaya wa kila namna (1 WAKORINTHO 5:7-8; 1 WATHESALONIKE 5:22).

(6)       KUMTUMIKIA MUNGU PAMOJA NA NYUMBA YOTE    (MST 20)

Katika chakula cha Pasaka, ilikuwa sheria kumtwaa kondoo mmoja na kumla watu wa nyumba moja (KUTOKA 12:3).  Hapa, Yesu anaila Pasaka pamoja na watu wa nyumba yake, wanafunzi kumi na wawili.  Inatubidi kumtumikia Mungu pamoja na nyumba zetu (YOSHUA 24:15).  Mtu asitenganishwe na mkewe au familia yake katika utumishi wake.  Wito wa mume, ni wito wa familia nzima.  Ikiwa tunamheshimu Mchungaji, tuonyeshe heshima zetu pia kwa mkewe (1 WAKORINTHO 9:5).  Ikiwa tunamjali Mchungaji, tuijali familia yake yote pia.  Mume au mke aliyeokoka peke yake katika familia, asiridhike mpaka familia nzima iokolewe sawa na ahadi ya Mungu (MATENDO 16:31).

(7)       UWEZEKANO WA KUMSALITI YESU    (MST 21-25)

Hatupaswi kujigamba.  Katika kiwango chochote cha kiroho tulichokifikia, bado tunaweza kumsaliti Yesu.  Tunaweza tukafikia ngazi ya kuwa mtume kama Yuda lakini bado uwezekano wa kumsaliti Yesu ukawa unatunyemelea.  Yuda hakumsaliti Yesu kwa kuwa alikuwa hajaokoka kama wengine wanavyodai!  Hakuna Mtume wa Yesu anayechaguliwa kabla ya kuokolewa!  Alikuwa ni mtume halisi, mwenye amri ya kutoa pepo na kupoza wagonjwa na udhaifu wote, ambaye alichaguliwa baada ya Yesu kuomba usiku kucha!  (LUKA 6:12-16; MATHAYO 10:1-4).  Jina lake lilikuwa limeandikwa mbinguni, alihesabiwa pamoja na Petro, Yohana na Yakobo na kupata huduma yao (LUKA 10:20; MATENDO 1:15-17).  Pamoja na kuwa na ngazi hii na kula na Yesu, alimsaliti Yesu!  Hata alipoambiwa “Ole wako”, bado aliendelea kumsaliti bila kutubu.  Pamoja na kutimiza unabii angeweza pia kutubu baada ya kufanya hivyo, kama Petro alivyotubu baada ya kutimiza unabii wa kumkana Yesu mara tatu; lakini hakufanya hivyo.  Tushuke na kumwuliza Yesu, “Ni mimi Bwana nitakayekusaliti?”, na tumwombe neema yake.  Waliorudi nyuma na kuacha wokovu, siyo kwamba tumewazidi kitu chochote (WARUMI 11:17-20; WAFILIPI 2:12; 1 WAKORINTHO 10:12).  Kamwe tusijivune na kusema, “Mimi siwezi kuacha wokovu kwa lolote”.  Bila neema yake Yesu, tunaweza kabisa kumsaliti tukipata sifa, fedha, mafanikio fulani, majaribu fulani n.k.  (MATHAYO 26:33-35, 69-75).

 

(8)       KUANZA KWA MEZA YA BWANA    (MST 26-29)

Hapa tunaona kuanza kwa Meza ya Bwana.  Katika Meza ya Bwana, tunatumia mikate isiyotiwa chachu na uzao wa mizabibu, juisi ya zabibu isiyochachuka.  Chachu ni uovu na ubaya ambao haukuwako kwa Yesu.  Kufanya Meza ya Bwana kabla ya harusi au kabla ya kifo, ni taratibu tu za kibinadamu, hakuna msingi wa Neno la Mungu kufanya hivyo.

 

(9)       KUIMBA WAKATI WA HUZUNI    (MST 30)

Kuimba ni jambo linalompendeza Mungu mno (ZABURI 69:30-31).  Hata hivyo kuimba wakati wa huzuni ni jema zaidi.  Yesu alikikabili kifo katika kuimba tofauti na Waisraeli.  Tumwombe Mungu atupe neema kutokubabaishwa na matukio ya huzuni (MATHAYO 26:38; ZABURI 137:1-4).

…………………………………………………………………………………………………………………………………..

Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!

. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s