YANIPASA NIFANYE NINI NIPATE KUOKOKA?

ZACHARY KAKOBENeno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org

Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries

Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

SOMO LA MAKANISA YA NYUMBANI

SOMO LA 111  : YANIPASA NIFANYE NINI NIPATE KUOKOKA? 

NENO LA MSINGI:

MATENDO YA MITUME 16:30, 32

“Kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, YANIPASA NIFANYE NINI NIPATE KUOKOKA?  Wakamwambia neno la Bwana, yeye na watu wote waliomo nyumbani mwake”.

<><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><

W

atu waliookoka katika Kanisa la Kwanza lililokuwa linaongozwa na Mitume, walijua sana jinsi ya kumweleza mtu maana ya wokovu hata yeye naye akaokolewa.  Katika Neno hili la msingi, tunaona mtu mmoja akiuliza afanye nini apate kuokoka, na hapohapo anaambiwa neno la Bwana na kuelewa analopaswa kulifanya. Watu wote tuliookoka, ni wajibu wetu kuwaambia watu wote neno la Bwana linalohusu wokovu ili yamkini wote wapate kuokolewa.  Jambo la huzuni ni kwamba watu wengi waliookoka, hawawezi kumweleza mtu mwingine neno la BWANA hata akaelewa, na yeye akaokolewa.  Kanisa la Mungu halipaswi kuwa hivi na kuwaacha wengi wakiangamia!  Basi, ni makusudi ya somo la leo la Kanisa la Nyumbani, kujifunza hatua kwa hatua yanayotupasa kufahamu katika kumwambia mtu neno la BWANA hata na yeye aokolewe.  Ikiwa wewe uliyehudhuria leo katika Kanisa la Nyumbani hujaokolewa basi unapokuwa unajifunza somo hili hujaokolewa basi ni siku yako pia kuokolewa baada ya kufahamu yote yanayokupasa kufahamu na kuyafanya.

A:        NINI MAANA YA NENO “KUOKOKA” AU “KUOKOLEWA?

Kuokoka au kuokolewa, ni kunusurishwa, kuopolewa, kusalimishwa au kuponywa kutoka katika maafa makubwa yaliyo dhahiri kabisa kukupata.  Inaweza ikawa kuponywa kutoka katika hatari ya kifo adhabu kali au madhara yoyote makubwa yaliyo dhahiri.  Katika hali ya kukosa matumaini ya kukwepa maafa hayo yaliyo dhahiri, inapotokea ghafla njia ya kusalimika hapo inasemekana umeokoka.

  ANGALIA MIFANO KATIKA BIBLIA:

Baada ya Yusufu kuuzwa na ndugu zake na kupelekwa kuwa mtumwa huko Misri,

ilitokea njaa kubwa sana katika ulimwengu wote wa wakati huo.  Watu wengi mno walikufa kwa kukosa chakula, na kulikuwa hakuna matumaini.  Ndugu zake Yusufu nao walikuwa katika hatari ya kifo.  Kabla ya njaa, huko Misri Yusufu kwa uwezo wa ajabu wa Mungu, aliaminiwa na kuwa Waziri Mkuu wa nchi ya Misri na akatumiwa na Mungu kuhifadhi chakula kingi ambacho hatimaye, kilitumika kuwaokoa ndugu zake katika maafa ya kufa kwa njaa.

MWANZO 45: 5 – 7:

“Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu.  Maana miaka hii miwili njaa imekuwa katika nchi, na iko tena miaka mitano isiyo na kulima wala kuvuna.  Mungu alinipeleka mbele yenu kuwahifadhia masazo katika nchi, NA KUWAOKOA NINYI KWA WOKOVU MKUU“.

Daudi akiwa katika hali ya hatari anaelezea juu ya hali ya mtu anayehitajika kuokolewa mtu ambaye yuko katika hatari ya kufa baada ya kuzama katika matope mengi na maji yakiwa  yamefika nafsini mwake.

ZABURI 69:1 – 2:

“Ee Mungu, UNIOKOE, maana maji yamefika mpaka nafsini mwangu.  Ninazama katika matope mengi, pasipowezekana kusimama.  Nimefika penye maji ya vilindi, mkondo wa maji unanigharikisha.”

Wakati wa Nuhu, Mungu akiwa amechukizwa na dhambi za watu wa wakati ule, aliwaonya watu juu ya maafa yatakayokuja, kuwaangamiza wote wasiomtii Mungu.  Watu wote wakapuuza ujumbe huo, isipokuwa Nuhu aliyetii na kuunda Safina iliyotumika kumwokoa yeye na watu wa nyumba yake kutoka katika maafa ya kufa kwa gharika kuu.  Watu wote walikufa kutokana na gharika hiyo isipokuwa Nuhu na wenzake saba waliookolewa katika maafa hayo.

WAEBRANIA 11:7:

“Kwa Imani Nuhu akiisha kuonywa na Mungu katika habari za mambo yasiyoonekana bado, kwa jinsi alivyomcha Mungu aliunda safina, APATE KUOKOA NYUMBA YAKE”.

B:        MAISHA YA BAADAYE YA MTU MWENYE DHAMBI:

Mtu yeyote mwenye dhambi lazima atapata adhabu ya milele.  Adhabu yake inaitwa MAUTI YA PILI au MAUTI YA MILELE ambayo ni kutupwa motoni na kuteswa milele.  Hakuna mwenye dhambi atakayekwepa adhabu.  Kila mmoja atapata mshahara huu wa dhambi, mauti ya milele au kutupwa Jehanum ya moto.

MITHALI 11:19 – 21:

“——- Afuataye maovu hufuata mauti yake mwenyewe—— Hakika, mtu mwovu hatakosa adhabu——-“.

EZEKIELI 18:4, 20:

“—-Roho itendayo dhambi itakufa————-“.

WARUMI 6:25:

“Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti.”

UFUNUO 21:8:

“Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao, ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti.  Hii ndiyo MAUTI YA PILI.”

Hakuna mtu yeyote mwenye dhambi yaani asiyekuwa na haki mbele za Mungu atakayeokoka katika maangamizo hayo.  Kwa sasa mtu mwenye dhambi anaona kwamba yuko salama na kwamba amani iko kwake, lakini ghafla uharibifu wake utamwijia.

1 WATHESALONIKE 5:3:

“Wakati wasemapo, kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafla, kama vile uchungu umjiavyo mwenye mimba wala hakika hawataokolewa.”

ZABURI 119:155:

“Wokovu u mbali na wasio haki kwa maana hawajifunzi amri zako (na kuzitenda)”.

C.        NI NANI MWENYE DHAMBI?

Jibu ni kwamba kila mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke, kutokana na asili ya Adamu, yuko miongoni mwa wenye dhambi.  Wote wamefanya dhambi.  Kwa mtu mmoja Adamu, dhambi iliingia ulimwenguni; na WATU WOTE wakahesabiwa kuwa wenye dhambi.  Kutokana na kila mtu kuzaliwa akiwa na asili ya dhambi, kila mtu anatenda dhambi pia.  Hivyo watu wote pamoja, na wewe, wanazaliwa katika dhambi na pia wote wanatenda dhambi.

MHUBIRI 7:20:

“Bila shaka hakuna mwanadamu mwenye haki hapa duniani, ambaye afanya mema, asifanye dhambi.”

ZABURI 53:3:

“Kila mtu amepotoka, wameoza wote pamoja, hakuna atendaye mema, La! hata mmoja.”

ISAYA 53:6:

“Sisi sote kama kondoo tumepotea, kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe———“.

WARUMI 3:23:

“Kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu.”

WARUMI 5:12:

“Kwa hiyo kama kwa mtu mmoja (Adamu) dhambi iliingia ulimwenguni na kwa dhambi hiyo mauti na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi”.

1 YOHANA 1:8, 10:

“Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.  Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.”

Unaona basi!  Kila mtu anakuwa mwenye dhambi kutokana na uzao wa Adamu.  Kila mtu anazaliwa akiwa ana asili ya dhambi.  Kama Adamu alivyofanya dhambi, wote tunazaliwa na dhambi ya asili.

ANGALIA MAANDIKO:

AYUBU 15:14:

“Je mwanadamu ni kitu gani, hata akawa safi?  Huyo aliyezaliwa na mwanamke hata awe na haki?”

AYUBU 25:4:

“Basi mtu awezaje kuwa na haki mbele ya Mungu?  au awezaje kuwa safi aliyezaliwa na mwanamke?

ZABURI 51:5:

“Tazama, MIMI NALIUMBWA KATIKA HALI YA UOVU; MAMA YANGU ALINICHUKUA MIMBA HATIANI.”

AYUBU 14:4

“Ni nani awezaye kutoa kitu kilicho safi kitoke katika kitu kichafu (Adamu)?  Hapana awezaye.”

MAOMBOLEZO 5:7:

“Baba zetu walitenda dhambi hata hawako; na sisi tumeyachukua maovu yao.”

ZABURI 58:3:

“Wasio haki wamejitenga tangu kuzaliwa kwao; TANGU TUMBONI WAMEPOTEA, wakisema uongo.” Unaelewa sasa!  Tatizo la mwanadamu liko tangu akiwa tumboni mwa mamaye!  Ana dhambi!  Ndiyo maana mtoto mdogo utamuona anakuwa na hasira, wivu, chuki, ukaidi na ujeuri.  Mtoto mdogo atampiga kofi mamaye kwa kumchelewesha kumpa titi anyonye.  Mtoto mdogo atagombana na mwenzie.  Mtoto mdogo, mapema sana huweza kusema neno “SITAKI” kabla ya maneno ya utii; kuonyesha asili ya uasi na ukaidi iliyomo ndani ya mwanadamu.  Mtoto mdogo atatumwa kununua mafuta dukani, na kuzitumia fedha hizo kununua maandazi akirudi kwa mama atasema uongo kwamba fedha zimepotea.  Mtoto mdogo anavutwa kutenda dhambi kuliko kufanya haki.

Hali ya asili ya dhambi kwa mwanadamu, inamfanya pia kutenda dhambi.  Maisha ya dhambi ndiyo yanayoonekana kuwa ya kawaida kwa mwanadamu.  Kunywa pombe, kuvuta sigara, kufanya uasherati na uzinzi, wizi, rushwa, uongo, usengenyaji, kiburi na majivuno, chuki, ugomvi, hasira, wivu n.k.; ndiyo sehemu ya maisha ya watu.

Sasa basi, kama tulivyoona, kila mwanadamu ni mwenye dhambi kwa kuzaliwa na kwa kutenda.  Kwa sababu hiyo, kila mwanadamu anastahili hukumu.  Anastahili adhabu.  Anastahili mauti ya milele.  Huu ndiyo mshahara halisi wa kila mwanadamu.  Mungu hawezi kumwacha mwenye dhambi bila kumpa mshahara wake [SOMA AYUBU 10:14].

D:        MWANADAMU AFANYE NINI BASI ILI AKWEPE MAUTI YA MILELE?

Jibu ni kwamba, ili mwanadamu aokolewe kutoka katika hukumu, ni lazima atoke katika hali ya kuwa “hana haki” na kuwa “mwenye haki” mbele za Mungu.

MITHALI 11:21b:

“Bali wazao wa wenye haki wataokoka”.

Sasa hapa ndipo penye mtego mkubwa wa shetani.  Wanadamu katika njia zao, wamefanya matendo fulani kwa kudhani yatawafanya wahesabiwe haki kinyume na mpango wa Mungu wa kuwahesabia haki.  Sasa basi, ebu tuangalie mipango hii miwili tofauti.

(a)       MPANGO WA WANADAMU WA KUHESABIWA HAKI AMBAO SIYO SAHIHI

Wanadamu katika dini zao wamepanga kwamba mtu afanye tendo hili na lile ili ahesabiwe haki.  Wengine wamedhania watahesabiwa haki kwa kufanya sakramenti zote, wengine wamedhania watahesabiwa haki kwa kushika nguzo fulani za dini; kutoa sadaka sana kwa maskini, kufunga, kusali mara tano au saba kwa siku, kushika sabato, kwenda Jumapili Kanisani, kuimba kwaya, kuacha sigara na pombe, kujenga mahali pa kuabudia iwe ni Kanisa au msikiti n.k.  Zote hizi ni njia za mwanadamu – kutenda jambo fulani ili kutafuta kuhesabiwa haki.  Hii siyo njia sahihi inayokubalika mbele za Mungu.

WAGALATIA 2:16:

“——– Wala si kwa matendo ya sheria; maana kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki.”

Maana yoyote ya mwanadamu ya kujiosha na kujisafisha moyo wake kwa matendo yoyote ya sheria, sakramenti au kuacha hili na lile; YOTE HAYA NI KUTAABIKA BURE!  Bado tu mbele za Mungu utahukumiwa kuwa ni mkosa na Mungu atakutupa shimoni yaani kuzimu na Jehanum ya moto.

ANGALIA MAANDIKO:

AYUBU 9:29 – 31:

“Nitahukumiwa kuwa ni mkosa; ya nini basi nitaabike bure?  Ingawaje najiosha kwa maji ya theluji, na kuitakasa mikono yangu kwa sabuni; lakini utanitupa shimoni, nami hata nguo zangu zitanichukia.”

Tatizo la mwanadamu linaanzia mbali kama tulivyoona.  Kufikiria kwamba ujitahidi kuacha dhambi hii na hii ni kazi bure.  Kwanza huwezi, na pili, matendo yako ya haki bado mbele za Mungu yanahesabiwa kama nguo iliyotiwa unajisi, kwa sababu sisi sote ni wachafu kutokana na asili ya Adamu ya dhambi ambayo pekee inatosha kukupeleka Jehanum bila kuongezea lolote.

ISAYA 64:6:

“Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi, sisi sote twanyauka kama jani, na maovu yetu yatuondoa, kama upepo uondoavyo.”

Yesu Kristo akielezea jambo hili, alisema kwamba, kufanya matendo ya haki fulani fulani, ni kusafisha nje ya kikombe na huku ndani kikombe ni kichafu.  Ni kufanana pia na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote. Akatoa ushauri kwamba inatupasa kusafisha ndani kwanza

[SOMA MATHAYO 23:25-28] .  Matendo mema yanakuja baada ya mtu kuokolewa.

[SOMA WAEFESO 2:10].

 

(b)       MPANGO WA MUNGU WA KUHESABIWA HAKI

Tunahesabiwa haki kwa imani tu!  Angalia maandiko:

WARUMI 5:1:

“Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na tuwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.”

WARUMI 3:28:

“Basi twaona ya kuwa mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria.”

Kwa imani, tunazaliwa mara ya pili na kuwa na haki ya kuuona ufalme wa Mungu au kuingia mbinguni.  Bila ya kuzaliwa mara ya pili, mtu hawezi kuingia mbinguni:

YOHANA 3:3:

“Yesu akajibu, akamwambia, Amini, amin, nakuambia, mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.”

E.                                                                                                                

Nikodemo hakuelewa maana ya kuzaliwa mara ya pili kama jinsi ambavyo wengi hawafahamu leo.  Nikodemo aliuliza:

YOHANA 3:4:

“Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee!  Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?”  Jibu ni hapana!  Kuzaliwa mara ya pili siyo kurudi tumboni mwa mama yako.  Kuzaliwa mara ya pili ni hivi:

Yesu Kristo anaitwa Adamu wa pili au mtu wa pili aliyetoka mbinguni.  Adamu wa kwanza alitoka katika udongo na alipojaribiwa na shetani, alifanya dhambi.  Adamu wa pili au Adamu wa mwisho, Yesu Kristo, alipojaribiwa na shetani, hakufanya dhambi kamwe.  Kama atulivyoichukua sura ya Adamu wa kwanza na tukawa watenda dhambi, basi kwa imani katika Kristo, Yesu, tunazaliwa mara ya pili na kuchukua sura ya Adamu wa mwisho, Yesu Kristo; mwenye uwezo wa kushinda dhambi.  [SOMA 1 WAKORINTHO 15: 45, 47-49; WAEBRANIA 4:15].  Tunakuwa tumezaliwa kwa Roho yenye kuhuisha.  Hapo mwanzo tumboni mwa mama zetu tulizaliwa katika mwili, tukachukua sura ya yule wa mwili Adamu, sasa tunazaliwa kwa Roho na kuchukua sura ya yule wa Roho; Yesu Kristo. [YOHANA 3:6].  Kwa sababu hiyo, kama jinsi Yesu Kristo alivyokuwa na uwezo wa kushinda dhambi, sisi nasi tunakuwa na uwezo huo pia.  Matokeo haya yanatufanya tuishinde dhambi na kuhesabiwa haki ya kuingia mbinguni.

HATUA SITA (6) ZA KUFUATA ILI KUZALIWA MARA YA PILI, KUHESABIWA HAKI, NA KUOKOLEWA KUTOKA KATIKA GHADHABU YA MUNGU

1.         UKUBALI KWAMBA WEWE NI MWENYE DHAMBI, UMEMWASI MUNGU, NA

UNASTAHILI HUKUMU

Umekwisha fahamu kwamba wewe ni mwenye dhambi kwa kuzaliwa na kwa kutenda.  Ndivyo ulivyo.  Huwezi kukataa.  Maisha yako yanakushuhudia mwenyewe kwamba uko mbali na mapenzi ya Mungu.  Ukiri wazi jambo hili kama walivyofanya watu hawa katika Biblia:

2 SAMWELI 12:13:

“Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia BWANA dhambi ……….”

1 SAMWELI 15:24:

“Ndipo Sauli akamwambia Samweli, nimefanya dhambi; maana nimeihalifu amri ya BWANA…”

YOSHUA 7:20:

“Akani akamjibu Yoshua akasema kweli nimefanya dhambi juu ya BWANA Mungu wa Israeli nami nimefanya mambo haya na haya.”

ZABURI 32:5:

“Nalikujulisha dhambi yangu, wala sikuuficha upotevu wangu.  Nalisema, Nitayakiri maasi yangu kwa BWANA ………….”

2.         USIKITIKE KABISA KWA DHAMBI ZAKO, UZIUNGAME NA KUWA TAYARI KUZIACHA KUANZIA SASA NA UWE TAYARI KUOMBA MSAMAHA

ZABURI 38:18:

“Kwa maana nitaungama uovu wangu, na kusikitika kwa dhambi zangu.”

MITHALI 28:13:

“Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.”

LUKA 18:13:

“Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.”

1 SAMWELI 15:25:

“Basi sasa, nakuomba, unisamehe dhambi yangu …………….”

2 SAMWELI 24:10:

“Ndipo moyo wake Daudi ukamchoma ……. Naye Daudi akamwambia BWANA, nimekosa sana kwa haya niliyofanya; lakini sasa, Ee BWANA, Nakusihi uuondolee mbali uovu wa mtumishi wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa.”

EZRA 10:1:

“Basi hapo Ezra alipokuwa akiomba kuungama, akilia, na kujiangusha kifudifudi mbele ya nyumba ya Mungu wakamkusanyikia katika Israeli wote kusanyiko kubwa sana la wanaume na wanawake na watoto maana watu hao walikuwa wakilia sana.”

EZEKIELI 18:30 – 31:

“…..Rudini, mkaghairi, na kuyaacha makosa yenu yote …… Tupilieni mbali nanyi makosa yenu yote mliyoyakosa; jifanyieni moyo mpya na roho mpya …….”

  1. 1.            UKIRI KWAMBA HUWEZI KUACHA DHAMBI KWA NGUVU NA UWEZO WAKO NA UOMBE MSAADA WA YESU KRISTO MWENYE NGUVU.

Huwezi kuacha dhambi kwa nguvu zako au uwezo wako!  Dhambi ina nguvu na uwezo juu ya mwanadamu.  Kwa nguvu zako, utajaribu kuacha sigara na kutafuna pipi au peremende lakini siku mbili tatu unajikuta unarudia tena kuvuta sigara.  Kiu ya sigara huwezi kuishinda kwa uwezo wako.  Kwa nguvu zako utajaribu kuacha uasherati na uzinzi kwa kuogopa magonjwa ya hatari kama UKIMWI, kisonono au kaswende; lakini utajikuta baada ya muda mfupi tamaa iko palepale.  Utajitahidi kuacha pombe na kuanza kunywa kahawa lakini muda mfupi unashindwa kabisa kuishi bila kunywa pombe.  Ni lazima ukiri kwamba huwezi.  Dini haiwezi kumfanya mtu aishinde dhambi.  Tangu uwe na dini, hujaweza kushinda dhambi.  Watu wenye dini ndiyo ambao wamejaa magerezani wakiwa ni wahalifu wakubwa.  Unachotakiwa kufanya ni kusalimu amri na kuanguka miguuni pa Yesu Kristo aliyeshinda dhambi, yeye atakupa msaada na uwezo wa kuishinda dhambi.

AYUBU 26:2:

“Jinsi ulivyomsaidia huyo asiye na uwezo!  Jinsi ulivyouokoa mkono usio na nguvu!”

4.         MWAMINI BWANA YESU

MATENDO 16:31:

“….. akamwambia, mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.”

INAKUPASA KUYAAMINI YAFUATAYO

(a)       YAAMINI MANENO YOTE YA BWANA YESU

Kumwamini mtu maana yake ni kuyaamini maneno yake.  Kuyaamini maneno ya mtu, kunathibitishwa pale tu unapochukua hatua ya kuyatenda.  Mtu akikuelekeza kwamba njia hii ndiyo inayokwenda Nairobi, ishara ya kuyaamini maneno yake ni kuanza kuifuata njia hiyo. Kumwamini Bwana Yesu ni kuyaamini maneno yote ya Bwana Yesu yaani Biblia na kuwa tayari kulitii na kulitenda kila neno ambalo anatuagiza tulifanye bila uasi wa namna yoyote. Tunaokolewa kutoka katika uasi.

ZABURI 119:6:

“Ndipo mimi sitaaibika, nikiyaangalia maaagizo yako YOTE”.

(b)       UAMINI KWAMBA YESU ALIKUFA MSALABANI KWA AJILI YA

DHAMBI ZETU  NA KUCHUKUA HUKUMU YETU

Yesu alikufa kwa ajili ya dhambi zetu.  Baraba ambaye alikuwa ahukumiwe kifo, aliachwa huru na Yesu akachukua nafasi yake.  Aliposulibishwa, tulisulibishwa pamoja naye na kuisulibisha asili ya Adamu inayotufanya tutende dhambi.  Tulizikwa pamoja naye na kufufuka naye na kupata upya wa uzima.

WARUMI 5:8:

“………. Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.”

ISAYA 53:5:

“Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu.”

WARUMI 6:5-6:

“Kwa maana kama tulivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika tutaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake; tukijua neno hili, ya kuwa utuwetu wa kale, (utu wa Adamu) ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi  tena.”

(c)       UAMINI KWAMBA DAMU YA YESU ILIYOMWAGIKA MSALABANI INA UWEZO  WA KUSAFISHA DHAMBI ZOTE.  UAMINI KUWA HAKUNA WOKOVU NJE YA  DAMU YA YESU.

Mpango wa Mungu, tangu mwanzo kabisa ni damu.  Mungu anapoiangalia damu, ndipo ukombozi unapotokea.  Habili alihesabiwa haki kwa sababu Mungu aliiangalia damu iliyotokana na dhabihu yake [WAEBRANIA 11:3; MWANZO 4:4] ili mwana wa Israeli aweze kuwa salama wakati wana wa Misri walipokuwa wanapata pigo la kufiwa na kila mzaliwa wa kwanza, sharti lililokuwapo ili kuokoka; ni kwamba BWANA alitaka kuona damu katika kizingiti cha juu na miimo miwili ya mlango.  Bila damu, hakukuwa na wokovu.  [KUTOKA 12:5-7, 12-13, 22-23].  Katika Torati pia karibu vitu vyote husafishwa kwa damu, na pasipo kumwaga damu, hakuna ondoleo la dhambi [WAEBRANIA 9:22].  Sasa, kwa jinsi hiyo hiyo, hakuna kusamehewa dhambi na kupata wokovu nje ya damu ya Yesu.

MATHAYO 26:28:

Kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.”Amini sasa kwamba damu ya Yesu ikinyunyiziwa kwako leo, dhambi zote zitaondolewa na utawekwa huru mbali na dhambi.  Utakuwa na uwezo wa kuishinda dhambi.

5.         MKIRI YESU KUWA BWANA WAKO:

WARUMI 10:9:

“Kwa sababu ukimkiri Yesu kwa Kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.”

WARUMI 10:13:

“Kwa kuwa, kila atakayeliitia jina la Bwana ataokoka.”

Neno “BWANA” maana ya “MTAWALA”.  Kumkiri Yesu kuwa ni Bwana wako au kuliitia jina la BWANA wako; maana yake kukubali Yesu akutawale katika mambo yote.  Mtu mwenye dhambi anakuwa ni mtawala wa maisha yake.  Anafanya analolitaka.  Huu ni uasi.  Kulielezea jambo hili vizuri, ni kwamba mtu mwenye dhambi, amekalia kiti katika moyo wake na kuushika usukani wa moyo.  Yeye mwenyewe ndiye dereva.  Anakwenda popote anapotaka mwenyewe.  Iwe ni dansini, kwenye sinema, katika baa ya pombe n.k.  Sasa, kumkubali Yesu kuwa Bwana wako, ni kuwa tayari kuondoka katika kukikalia kiti cha moyo wako na kumpisha Yesu akikalie.  Yeye awe dereva wako.  Akupeleke anakotaka na wewe umfuate bila ubishi wowote.  Ukubali kwenda sawasawa na neno la Mungu.  Linakokupeleka, na wewe ulifuate mara moja.  Ukubali kuwa mtumwa na ukubali kuwa huna haki yoyote ya kujitawala.  Je uko tayari kumfanya Yesu awe BWANA wako?  Tazama, yuko katika mlango wa moyo wako leo anabisha.  Anataka kuingia akikalie kiti cha moyo wako.  Je uko tayari kumpokea na kumfungulia mlango wa moyo wako aingie?  Ukimfungulia, utakula pamoja naye katika Ufalme wa Mungu.

UFUNUO 3:20:

“Tazama, nasimama mlangoni, nabisha, mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.”

6.         CHUKUA MANENO PAMOJA NAWE, MWENDEE HAKIMU:

Hii ndiyo hatua ya mwisho:  Yesu Kristo ndiye Hakimu atakayeuhukumu ulimwengu

[SOMA YOHANA 5:22; MATENDO 17:31]. Hata kabla ya hukumu ya mwisho, mtu yeyote asiyemwamini Yesu katika hatua hizi ulizozifahamu, amekwisha hukumiwa tayari.  Ghadhabu ya Mungu inamkalia, na hata akifa sasa kabla ya kutubu, anakwenda Jehanum moja kwa moja.

YOHANA 3:18, 36:

Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.  Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia.”

Kwa hiyo ili ukwepe hukumu au uokolewe, njia ni rahisi tu!  Ukiwa umeyaamini na kuyakubali haya yote, chukua maneno yote haya kwa ufupi na mwendee Hakimu ukamwambie akuondolee maovu yako yote.  Unafanya hivi kwa kutoa sadaka ya mdomo wako au kinywa chako.  Kwa kinywa chako unakiri kwamba ni mwenye dhambi na kuhitaji kusamehewa na kumpokea Yesu awe BWANA wako.  Maneno haya tunayoyatamka katika sala kwa Hakimu, ndiyo yanayojulikana kwa jina “SALA YA TOBA”.

Ni muhtasari wa haya yote tuliyojifunza.  Siyo lazima yawe sawasawa kwa kila tunayemwabia ayatamke, maana yake ni kwamba hakuna sala maalum ya kukariri ambayo lazima itumike kwa kila mmoja.  Ila ni kwamba misingi ya sala hiyo inabidi iwe ni hatua hizi sita tulizojifunza.

HOSEA 14:2:

“Chukueni maneno pamoja nanyi, mkamrudie BWANA, mkamwambie Ondoa maovu yote, uyatakabali yaliyo mema; na hivyo ndivyo tutakavyotoa sadaka za midomo yetu kana kwamba ni ng’ombe.”

Ungeweza kuomba mwenyewe ingekuwa pia ni sawa, lakini kwa sababu hujui kuomba, fuatisha maneno haya na kuyatamka.  (Huu ni mfano wa sala ya toba inavyopasa kuwa).

S  E  M  A     M  A  N  E  N  O     H  A  Y  A

Mungu Baba, nakuja mbele zako na mbele ya Hakimu wa Ulimwengu, Yesu Kristo.  Nakiri kutoka moyoni kwamba mimi ni mwenye dhambi kwa kuzaliwa na kwa kutenda. Nimekutenda dhambi mno, nimeasi na kuwa mbali na mapenzi ya Mungu.  Mimi ni mchafu mno, kwa dhambi hizi nastahili ghadhabu au hukumu yako kali, lakini sasa nakusihi unisamehe dhambi hizi.  Narudi kwako na kughairi kabisa na sitaki tena kuyafanya yote yaliyo kinyume na mapenzi yako, lakini kwa  nguvu zangu na uwezo wangu siwezi.  Nahitaji kukupendeza lakini sina uwezo wangu mwenyewe wa kuweza jambo hili.  Nahitaji msaada wako.  Ninaamini maneno yako yote na kuwa tayari kuyatenda.  Ninaamini kuwa uliteswa na kufa kwa ajili ya dhambi zangu.  Naamini ulimwaga damu yako ili nipate ondoleo la dhambi.  Nahitaji damu sasa inisafishe na kuniosha uovu wangu wote.  Naamini kwamba katika damu yako kunanguvu ya kushinda dhambi.  Nipe nguvu hiyo sasa ili nikutii katika mambo yote.  Nizaliwe mara ya pili kwa Roho wako.  Nakukubali Yesu uwe BWANA wangu.  Karibu moyoni mwangu unitawale.  Niongoze popote kuanzia sasa.  Lifute jina langu katika kitabu cha hukumu, liandike katika kitabu cha uzima.  Asante kwa kunisamehe na kuniokoa.  Napokea wokovu huu kwa shukrani katika jina la Yesu.  AMINA.

Baada ya sala hii, omba kwa maneno machache ukimshukuru Mungu kwa kumuokoa mtu huyu.  Mpe maneno ya kumtia moyo  (YOHANA 6:37, YOHANA 1:12).  Baada ya kuokolewa ni muhimu kuwa pamoja na wenzio waliookolewa na kufundishwa ili uukulie wokovu [MITHALI 18:1, WAEBRANIA 10:25, 1 PETRO 2:2; 2 WAKORINTHO 5:17]

MSAADA KWA MTU ANAYEWALETA WATU KWA YESU

Unapokuwa unawashuhudia watu na kuwavuta watu kuokolewa kwa misingi uliyojifunza, utakutana na maswali au maneno yanayofanana na haya kutoka kwao.  Yafuatayo ni mifano ya mistari ya kuwajibu kutoka katika Biblia.

1.         Nimekusikia vizuri, lakini uamuzi wangu wa kuokoka nitautoa siku nyingine.

JIBU:  MITHALI 27:1; YAKOBO 4:14; 2 WAKORINTHO 6:2; MHUBIRI 9:12.

2.         Nitaokoka, ngoja kwanza nitengeneze pesa na nizidi kuifahamu dunia.

JIBU: LUKA 12:16 – 20; MARKO 8:36.

3.         Mimi bado kijana nitaokoka nikiwa mzee.

JIBU:  MHUBIRI 12:1, MHUBIRI 10:14; MATHAYO 24:42-44.

4.         Siwezi kuacha yale niliyofundishwa na baba zangu katika dini.

JIBU: EZEKIELI 20:18; MARKO 7:8 – 9.

5.         Lakini kwani kunywa pombe kidogo kunakatazwa?

JIBU: MITHALI 23:20

6.         Kwani kuvuta sigara, bangi, kula madawa ya kulevya, kula mirungi au ugolo

kumekatazwa wapi katika Biblia?  

JIBU: ISAYA 55:2

7.         Lakini mimi ni mkristo tangu utoto wangu na nilibatizwa tangu utoto.

JIBU: TITO 1:16; LUKA 6:46; WARUMI 10:13-14.

8.         Wote tunaamini kwamba Mungu ni mmoja tatizo tu tunahitilafiana katika

kumwelezea  Yesu.  Kwa hiyo kwa sababu ninaamini katika Mungu mmoja basi tutakwenda wote mbinguni, njia zetu tu tu ndiyo tofauti.

JIBU: YAKOBO 2:19; 1 TIMOTHEO 2:5; YOHANA 15:23; 1 YOHANA 2:23;

YOHANA 14:6; YOHANA 10:7, 9.

9.         Wokovu na utakatifu siyo hapa duniani ila ni huko mbinguni.  Haiwezekani mtu kuwa mtakatifu ukiwa duniani.

JIBU:Yesu alitoka mbinguni kuja duniani kuokoa.  Kama wokovu ungekuwa mbinguni asingekuwa na haja kuja huku duniani.  Alipokuwa duniani aliwaambia watu wokovu umefika nyumbani kwao.  Biblia inasema Mungu anapendezwa na watakatifu walioko duniani Yesu aliwahubiri watu waokoke duniani. LUKA 19:9-10; YOHANA 5:34; ZABURI 16:3; TITO 2:11-12; WAFILIPI 4:13; Watu waliokuwa duniani walishuhudia kwamba wameokoka wakati bado wako duniani [SOMA TITO 3:3-4]

10.       Mimi nakwenda Kanisani kila siku, naimba kwaya na tena ni Mzee wa Kanisa   

na ninatoa sadaka sana.

JIBU: MARKO 7:6; AMOSI 5:21- 22; EZEKIELI 33:31-32.

11.       Nikiokoka nitakuwa maskini.

JIBU: MATHAYO 27:57; 3 YOHANA 1:2; HAGAI 2:8

12.       Muziki wa dansi nao umekatazwa wapi katika Biblia?

JIBU: ISAYA 5:12 – 14.

13.       Niliwahi kuokoka nikaacha njia ya wokovu

JIBU: 2 PETRO 2:20-22; UFUNUO 2:4-5.

14.       Wamekwisha nieleza wengi habari ya kuokoka bado ninafikiria.

JIBU: MITHALI 29:1.

15.       Ngoja nikamuulize mume wangu na baba yangu ili wakikubali tuokoke wote.

JIBU: WAGALATIA 6:5; LUKA 20:34-36; MATHAYO 11:12; WAGALATIA 1:15-16.

16.       Mbona watu wengine waliookoka wanafanya mambo yaliyo kinyume na

wokovu? Wengine wao ni Wachungaji na nawajuwa kabisa. Nimesikia pia wengine wanagombana na wengine waasherati hata Radio imetangaza.

JIBU: WARUMI 14:12; ZABURI 37:37.

17.       Ngoja kwanza siku ikifika nitakuambia.  Saa hizi nikiamua kuokoka itakuwa

nusunusu.  Nitakapoamua mimi siku hiyo, ni moja kwa moja hakuna unafiki wala kurudi nyuma.

JIBU: WARUMI 9:16; ZEKARIA 4:6

18.       Maisha ya siku hizi unajua yalivyo, sasa nikiokoka nitaweza kweli kuishi kwa

mshahara na mapato mengine ya halali tu.

JIBU: MATHAYO 6:25-33; 1 PETRO 5:6 – 7.

19.       Lakini huku ndiyo kutangatanga.

JIBU:  MATHAYO 13:45; MATENDO 26:4-5, 9-18.

20.       Mimi ninauza pombe, na ndiyo tegemeo langu.  Nina watoto ninao

wasomesha kwa pombe hii hii sasa nikiokoka nitaishije?

JIBU: MARKO 9: 43-48.

21.       Mimi Baba yangu ni Mchungaji wa Kanisa linalohubiri wokovu na ni Mhubiri

mkubwa.

JIBU: EZEKIELI 14:14, 16, 20.

22.       Nyinyi ndiyo manabii wa uongo waliosema watatokea.

JIBU: Manabii wa kweli wa Mungu husema yaliyo ya Mungu yaani sawa na Neno la Mungu  2 NYAKATI 18:13; YOHANA 3:34; HESABU 22:18; EZEKIELI 2:7 nabii wa uongo humweleza mtu kwamba amani tu iko mbele yake wakati maagizo yanafuata bila kuokolewa, EZEKIELI 13:9-10. Hakuna amani kwa mabaya – ISAYA 48:22.

23.       Kuokoka ni kwa watu wenye shida ya pesa, mimi sina shida.  Kuokoka ni kwa watu wasiokuwa na mafanikio duniani.

JIBU: MATHAYO 27:57; MATENDO 17:12.

24.       Kanisa letu ndilo la kwanza na lina watu wengi zaidi kuliko yote duniani.

JIBU: Kanisa au dhehebu siyo Njia ya kwenda mbinguni YOHANA 14:6; YOHANA 10: 7,9. Ingia kwa kupitia mlango mwembamba.  Wengi wako katika njia pana iendayo upotevuni.MATHAYO 7:13-14; LUKA 13:24-25.

25.       Kweli inawezekana kuokoka katika hali hii ngumu ya uchumi?

JIBU:  MATHAYO 19:25-26.

UKIYAJUA HAYA, HERI WEWE UKIYATENDA – YOHANA 13:17;

MATHAYO 9:37; YOHANA 4:35; YOHANA 9:4; MARKO 16:15.

Kumbuka

(1)       Wale wanaokata shauri kuokoka waongoze katika Makanisa ya Nyumbani na Kanisa Kuu ili waukulie wokovu au siyo kaziyote itakuwa ni bure maana watajaribiwa na mjaribu na kuiacha imani ya wokovu [SOMA: 1 WATHESALONIKE 3:5].

(2)       Siyo lazima katika kushuhudia kutumia mistari mingi namna hii uliyojifunza,inakupasa tu kujifunz             a misingi yote na namna nzima ya ujumbe kamili wa Injili.  Ukiweza kutumia mistari kadha wa kadha tu inatosha.  Katika somo hili umepewa ufahamu kwa UPANA MNO na ni kazi yako kutumia muhtasri unaposhuhudia.  Hata hivyo inategemeana na mtu unayemshuhudia.  Wengine inabidi kwenda nao kwa maandiko mengi.  Ikiwa ni kwa machache au kwa mengi yote ni sawa [SOMA: MATENDO 26:29].

<><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><><>< s

 

Advertisements

One comment on “YANIPASA NIFANYE NINI NIPATE KUOKOKA?

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s